Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Monday, 27 October 2014

CCM: Ndoa ya wapinzani ‘feki’  •  Yasema kuing’oa madarakani ni ndoto za alinacha
  •  Viongozi wa vyama vilivyoungana kila mmoja anatafuta ulaji
  •  Mangula awaonya viongozi wa wilaya kutowagawa wanachama

NA SELINA WILSON
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema  hakitishiwi nyau kuungana kwa vyama vinne vya upinzani kwa lengo la kuking’oa madarakani.

 Kimesema muungano huo wa wapinzani si halali na ni sawa na ndoa ya mkeka.
Pia kimesema ni ndoto za alinacha kwa wanandoa hao wa msimu, ambao kila mmoja anatafuta ulaji, kuing’oa CCM, ambayo imesimamia maendeleo ya nchi pamoja na kuifanya kuwa na amani na mshikamano.
Kauli hiyo imetolewa jana na Makamu Mwenyekiti wa CCM- Bara, Philip Mangula, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na ndoa hiyo ya wapinzani.
Ndoa hiyo ilifungwa juzi katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam, na viongozi wa vyama hivyo, Freeman Mbowe (CHADEMA), James Mbatia (NCCR-MAGEUZI), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na Emmanuel Makaidi (NLD).
Kwa mujibu wa viongozi hao, makubaliano hayo yanalenga kuhakikisha wanaing’oa CCM madarakani katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa na ule wa rais na wabunge. Pia kuungana na kuhamasisha wananchi kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa.
Hata hivyo, habari za kuaminika zinasema kuwa, vyama hivyo vimejificha chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ili kukwepa mawimbi makali kutokana na vyote kukabiliwa na migogoro mizito inayohatarisha uhai wake.
Mangula alisema takwimu zinaonyesha kuwa wapinzani hawana uwezo wa kuing’oa CCM, kwani wamekuwa wakipata asilimia 61 hadi 89 katika uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani na kuwaachia wapinzani asilimia chache.
Pia alisema Watanzania wamekuwa wakipigia kura CCM kutokana na kuvutiwa na sera zake za maendeleo, amani na mshikamano, tofauti na wapinzani ambao wamekuwa wakipiga kelele bila kuonyesha uwajibikaji kwa vitendo.
“Kwa takwimu hizo, maana yake CCM ikipata asilimia 89 ya kura, vyama vyote vya upinzani vinagawana asilimia ndogo, hivyo ndoa yao ni kama ya mkeka na hakuna uhusiano wowote wa kuishinda CCM,” alisema.
Alitoa mfano wa uchaguzi mkuu wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi, ambao CCM ilishinda kwa asilimia 80, mwaka 2000 asilimia 87 na mwaka 2005 ilishinda kwa asilimia  89 katika kura za wabunge.
Kwa upande wa kura za Rais, mwaka 1995 ilishinda kwa asilimia 61.8, 2000 ilishinda kwa asilimia 71 na mwaka 2005 CCM ilishinda kwa asilimia 80.2 huku vyama vyote vikigawana asilimia 38 mpaka 20.
“Kutokana na hali hiyo, nawatakia kila kheri na kwamba wakikosa mgombea katika uchaguzi mkuu wa mwakani, CCM inaweza kuwakopesha kwa kuwa inao wengi,” alisema.
Mangula alisema muungano huo wa wapinzani hautapunguza idadi ya mashina wala matawi ya CCM, hivyo ndoto zao kushika dola hazitatimia.
Chini ya ndoa hiyo ya mkeka, viongozi hao walisema watasimamisha mgombea mmoja wa urais katika uchaguzi wa mwakani na katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa Desemba 14, mwaka huu, pia vitaungana.
Muungano huo wa vyama vinne vya upinzani chini ya UKAWA, ulianzia katika Bunge Maalumu la Katiba, ambapo baadae walisusia vikao hivyo na hatimaye Bunge liliendelea na kupata theluthi mbili za wajumbe kwa Bara na Zanzibar na Katiba Inayopendekezwa kwa wananchi kupatikana kwa kishindo.
Mangula aonya
Katika hatua nyingine, Mangula amewaonya viongozi wa CCM wa ngazi za wilaya kutowagawa wanachama kwa lengo la kuimarisha makundi yao, badala yake waimarishe kundi moja la CCM.
Alisema viongozi wa Chama katika wilaya na mikoa, wakiwemo wabunge na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), wanapaswa kuhakikisha Chama kinafanya vizuri katika uchaguzi wa serikali za mitaa. 
Mangula alisema yapo maeneo wabunge na wajumbe wa NEC wanavutana kwa lengo la kupanga safu, jambo ambalo alisema kamwe  halitavumiliwa na watakaobainika wataadhibiwa.
“Wakati huu ni wa kuimarisha kundi moja la CCM ili iweze kushinda uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwakani, lakini si muda wa kuimarisha kundi la mtu fulani,” alisema.
Mangula alisema uzoefu unaonyesha kwamba maeneo ambayo CCM ilishindwa katika uchaguzi, sababu zilitokana na makundi ndani ya Chama, hivyo aliwaonya viongozi hao kuwaachia wanachama waamue.
Alisema amekuwa akifanya ziara na kufuatilia maendeleo ya Chama katika maeneo mbalimbali nchini, lakini yapo maeneo ambayo viongozi hawaelewani kwa sababu ya makundi yasio na tija kwa Chama.
Mangula alisema CCM inafuatilia kwa kina maelekezo yake wa viongozi wa mikoa, wilaya, kata, matawi na mashina na yeyote atakayebainika kuvuruga uchaguzi huo kwa sababu za kuimarisha kundi lake, Chama kitamchukulia hatua.
Akizungumzia mkakati wa Chama katika uchaguzi huo, Mangula alisema CCM ina mtandao wa uongozi hadi ngazi ya tawi, ambao unajisimamia katika mipango yao.
“Tutashinda uchaguzi wa serikali za mitaa na kwamba hakuna kiongozi wa kitaifa atakayekwenda kufanya kampeni kwenye uchaguzi huo. Katika vijiji na mitaa, CCM ina viongozi wanaoaminika kwa wananchi na ndio watakaofanya kampeni,” alisema.
00000

000000

00000

Kikwete aweka historia China


Na mwandishi wetu
RAIS Jakaya Kikwete amesababisha mageuzi makubwa kwa namna Jamhuri ya Watu wa China inavyowapokea viongozi wageni kutoka nje kwa kuwa kiongozi wa kwanza duniani kupokewa rasmi na pikipiki za polisi.

Mbali na kupokewa kwa pikipiki, msafara wa Kikwete pia uliongozwa na pikipiki hizo kwa muda wote wa ziara, tofauti na mapokezi ya viongozi wengine katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Rais Kikwete, ambaye aliwasili China wiki iliyopita kuanza ziara rasmi ya siku sita nchini humo, amekuwa kiongozi wa kwanza wa nje kupokewa na msafara wa pikipiki tokea Januari Mosi, mwaka 2004, miaka 10 iliyopita wakati China ilipofuta utaratibu wa misafara ya viongozi kusindikizwa na pikipiki za polisi.
Rais Kikwete na msafara wake alipokewa na msafara wa pikipiki wa polisi mara baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Beijing hadi kwenye Nyumba ya Kufikia Wageni wa Serikali ya Diaoyutai, katikati ya Jiji la Beijing na utaratibu huo kuendelea kwa siku zote alipokuwa China.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya China na kukaririwa na Shirika la Habari la nchi hiyo la Xinhua, haikutoa sababu zozote za mabadiliko ya sera hiyo.
Katika nchi karibu zote duniani, utaratibu wa viongozi wa nchi mbali mbali kupokewa kwa misafara ya pikipiki ni protokali ya juu kabisa, ambayo pia huongeza usalama wa kiongozi na ni utaratibu wa kawaida katika nchi nyingi duniani.
Tokea kuasisiwa kwake mwaka 1949, Jamhuri ya Watu wa China ilikuwa na utaratibu wa pikipiki za polisi kuongoza misafara ya viongozi, lakini utaratibu huo ulisimamishwa Januari Mosi, mwaka 2004, kwa sababu ambazo hazijapata kuelezwa.
Baada ya kuweka historia hiyo ya kuwa kiongozi wa kwanza wa nchi ya kigeni kupokewa na msafara wake kuongozwa na msururu wa pikipiki nane, Rais Kikwete amemaliza ziara yake nchini humo jana.
Kikwete alitarajiwa kuanza ziara rasmi ya siku mbili nchini Vietnam kwa mwaliko wa Truong Tan Sang, Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam, ambako miongoni mwa mambo mengine, nchi hizo mbili zitaadhimisha miaka 50 tokea kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya nchi hizo mbili.
Miongoni mwa shughuli zake kubwa, Rais Kikwete atakutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha Vietnam, Nguyen Phu Trong na Mwenyekiti wa Bunge la Vietnam, Nguyen Sinh Hung.
Aidha, Rais Kikwete atatembelea taasisi mbalimbali zenye uhusiano wa kiuchumi na Tanzania, ikiwemo Kampuni ya Viettel, inayotaka kuwekeza katika mawasiliano ya simu za maeneo ya vijijini katika Tanzania kwa bei nafuu zaidi.

Aliyejilipua kwa risasi aibua mambo mazito


NA LILIAN JOEL, ARUSHA
SAKATA la Mkurugenzi wa Kampuni ya Kitalii ya DAGT, Timoth Mroki, kujiua kwa kujilipua kwa risasi, limeibua mambo mapya kutokana na kuelezwa kuwa wivu wa kimapenzi.
Habari zilizopatikana jijini hapa, zinasema kuwa Mroki (36), alikuwa na vimada wawili ambao ni wake za watu na kuwa kabla ya kujilipua kwa risasi na kupoteza maisha, alitoa taarifa kwa wanawake hao (majina yanahifadhiwa).
Imeelezwa kuwa Mroki alikuwa akitoka na wanawake hao kila mmoja kwa muda wake, lakini baadaye siri hiyo ilianza kuvuja na hatimaye vimada kufahamiana, ikiwa ni pamoja na mkewe kuanza kupenyezewa taarifa hizo.
Mroki, ambaye pia ni Meneja wa Operesheni na Masoko wa Kampuni ya Tanzania Bush Camp, alijiua kwa kujipiga risasi Oktoba 25, mwaka huu, saa 1:00, baada ya kubaini kuwa vimada wake hao wamefahamiana.
Habari kutoka kwa mtu wa karibu zimesema kuwa, vimada hao baada ya kufahamiana, walikutana na kufanya mazungumzo kisha kupiga picha pamoja na kumrushia kupitia simu ya mkononi.
Kugundulika kwa siri hiyo, kulizusha taharuki kwa Mroki, hivyo kusababisha kuyumba kwa uhusiano baina yake na vimada hao, akiwemo mmoja ambaye pia ni mshirika wake kibiashara.
“Hawa wanawake wana siri nzito kuhusiana na kifo hiki kwa sababu kabla ya kufanya uamuzi, aliwasiliana nao…kikubwa awali walikuwa hawafahamiani ila baadaye walikutana na kuungana kuwa kitu kimoja.
“Haifahamiki ni kwa vipi walijenga urafiki, ila watu wa karibu wanasema walijipanga kumkomoa ili afilisike kwa kuwa kila mmoja alikuwa na malengo yake,” alisema mtoa habari wetu.
Kuungana kwa wanawake hao kumlichanganya Mroki, ambaye tayari uhusiano wake nyumbani pia ulianza kuwa tete baada ya mkewe kuhisi kuna mambo yanafanyika kinyume cha utaratibu.
Hata hivyo, habari zaidi zinasema kuwa miongoni mwa wanawake hao, yupo aliyejenga uswahiba na mke wa marehemu huku uhusiano wa kimapenzi ukifichwa chini ya mwamvuli wa biashara.
Chanzo chetu kimesema kuwa, kutokana na ukaribu huo, familia hizo zimekuwa na kawaida ya kutembeleana, ikiwa ni pamoja na watoto kukaa kwa siku kadhaa nyumbani kwa kimada mmoja.
Imeelezwa kuwa kutokana na kugundulika kwa siri hiyo, Mroki alichukua uamuzi wa kujimaliza ili kukwepa aibu mbele ya familia.
“Kugonga gari si sababu ya Mroki kujiua, ni kutokana na kutingwa na mambo mengi kichwani, hasa baada ya siri ya kimapenzi kuanza kubainika,” aliongeza mmoja wa rafiki wa marehemu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema Mroki alijiua kwa kujipiga risasi kifuani kwa kutumia bastola aina ya KEL –TEC yenye namba HCB21.
Katika taarifa yake, Kamanda Sabas alisema kabla ya tukio hilo, Mroki alikuwa na gari namba T222CMX, aina ya Isuzu Double Cabin, iliyokuwa ikitokea Mbauda kwenda katikati ya jiji.
Hata hivyo, taarifa hiyo iliongeza kuwa kutokana na msongamano wa magari, Mroki alitanua barabara kukwepa foleni huku akiwa katika mwendo kasi.
Alipofika maeneo ya Shams, aligongana na gari la mizigo, mali ya Kampuni ya Gupta, lenye namba T548 BRL.
Taarifa ilisema pamoja na kusababisha ajali hiyo, Mroki aliendelea na safari yake ndipo madereva wa bodaboda walipoamua kumfukuza na kumkamata eneo la kona ya Nairobi Ngarenaro.
Mroki aliporejea eneo la tukio na kuulizwa sababu za kusababisha ajali na kuendelea na safari, alitoa bastola na kufyatua risasi mbili hewani na ya tatu kumpiga kifuani.

‘Tuhuma dhidi ya Nyalandu ni uzushi’


NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imesema tuhuma zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya vyombo vya habari dhidi ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, hazina ukweli na zimelenga kumchafua binafsi pamoja na wizara.
Pia imetoa ufananuzi wa tuhuma hizo zilizokuwa zikielekezwa kwa Nyalandu na kuonya kuwa, kuanzia sasa itachukua hatua kali za kisheria dhidi ya wanaomchafua na kupaka matope utendaji kazi wake.
Hivi karibuni Nyalandu amekuwa akiandamwa na baadhi ya watu kwa kile kinachodaiwa kuwa ni hatua yake ya kudhibiti mtandao hatari wa ujangili na kuziba mianya ya ulaji ndani na nje ya wizara hiyo.
Taarifa ya Wizara ya Maliasili na Utalii, iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, ilisema tuhuma hizo zimelenga kuchafua utendaji kazi wa Nyalandu na watendaji wengine.
Ilisema baadhi ya vyombo hivyo vya habari (si Uhuru), vimekuwa vikichapisha habari ambazo hazina ukweli wala mashiko kwa jamii zaidi ya kuchochea chuki na uhasama.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, moja ya  habari hizo ni ile inayodaiwa kuwa Nyalandu ameuza hifadhi, kutoa leseni maalumu ya Rais kwa Familia ya Freidkin kwa ajili ya kuwinda idadi kubwa ya wanyama bure.
Taarifa hiyo ya wizara ilisema tuhuma hizo zimetolewa na watu wenye nia ovu na kumpunguzia dhamira, malengo na kasi ya kupambana na mtandao hatari wa ujangili nchini.
Ilisema Leseni ya Rais ya kuwinda kwa mujibu wa Kifungu cha 58 (1) cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 ikisomwa kwa pamoja na Tangazo la Serikali Na. 273 la mwaka 1974, inampa mamlaka Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori baada kupata ridhaa ya Waziri mwenye dhamana ya wanyamapori kutoa kibali maalumu kwa malipo au bure.
Aidha, kibali hicho hutolewa baada ya Waziri kuridhika kwamba kina maslahi kwa taifa na hakikinzani na sheria na mikataba ya kimataifa kama CITES.
Kufuatana na Kifungu hicho cha 58 (1) Leseni Maalum hutolewa kwa mtu yeyote kwa masilahi ya taifa ikiwemo utafiti wa kisayansi, makumbusho, elimu na utamaduni au chakula wakati wa dharura.
Maslahi ya taifa ni pamoja na leseni kutolewa kwa watu mashuhuri kama vile wakuu wa nchi,  wafalme, malkia, wakuu wa dini na watu ambao katika utendaji wao wametoa michango yenye manufaa kitaifa au katika shughuli za uhifadhi wa wanyamapori.
Imewataja baadhi ya waliowahi kupewa leseni hiyo ya Rais kwa mwaka 2013 hadi sasa kuwa ni H.H. Sheikh Abdullah Mohamed Buli Al Hamed kupitia kampuni za Kilombero North Safaris/Green Mile Safaris, ambayo ilitolewa bure.
Nyingine ni H. H Sheikh Mohamed Rashid Al Maktoum kupitia kampuni ya Ortello Business Corporation (OBC), ambacho pia kimetolewa bure.
Familia ya Freidkin ya watu wanane kupitia kampuni ya Tanzania Game Trackers Safaris Ltd, ambacho kimelipiwa ada pamoja na Kiongozi wa Bohora Duniani, kilichotolewa bure.
Taarifa hiyo imesema kuwa, familia ya Freidkin imekuwa na sifa ya kupewa Leseni ya Rais kutokana na mchango wake mkubwa kwa taifa katika shughuli za uhifadhi wa Wanyamapori kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20 iliyopita bila kukoma.
Imekuwa ikitoa mchango huo kupitia Kampuni ya Uwindaji wa Kitalii iitwayo Tanzania Game Trackers Safaris Ltd. Pamoja na Asasi yake iitwayo Freidkin Conservation Fund (FCF tangu miaka ya 1990).
FCF imekuwa ikitoa michango mikubwa hususan ya kukabiliana na ujangili pamoja na shughuli za kijamii.
Ilisema tuhuma ya kuwa Nyalandu amekiuka kifungu kinachoweka ukomo wa idadi ya vitalu ambavyo ni vitalu vitano kwa kampuni si za kweli.
Kwa kuzingatia maelezo hayo hapo juu, kutolewa kwa leseni ya Rais kwa familia ya Freidkin kulizingatia sheria, kanuni na taratibu zote za uwindaji.
Kuhusu tuhuma za Nyalandu kudaiwa kuuza hifadhi, taarifa hiyo ya serikali ilisema kuwa ni za uzushi na kuwa ukweli ni kwamba, waziri huyo alikwenda Afrika Kusini kwa kufuata taratibu rasmi na maagizo ya serikali kuhudhuria mkutano wa African Parks Network (APN) wa uhifadhi ulioandaliwa na asasi hiyo kwa lengo pia la kuhakiki uwepo, utendaji halisi wa taasisi hiyo na kufanya majadiliano kuhusiana na mapendekezo yao.
Imesema katika mkutano huo, hakukuwa na mikataba yoyote iliyowekwa na Nyalandu au maamuzi yoyote ya kukabidhi hifadhi za Taifa kama ilivyoelezwa katika baadhi ya vyombo vya habari husika.
Hata hivyo, taarifa hiyo imesema kuna mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kupambana na ujangili ikiwemo kupungua kwa kiasi kikubwa kwa mauaji ya tembo.

Bunge latishwa na madudu Ranchi ya Ruvu


NA KHADIJA MUSSA
MSAJILI wa Hazina kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, wametakiwa kupitia upya ripoti ya ukaguzi ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) na kuchukua uamuzi ndani ya wiki tatu.
Pia Bodi ya NARCO imeagizwa kufanya tathmini iwapo menejimenti ya NARCO na ya Ranchi ya Ruvu kama zinastahili kuendelea na kazi zao na kutoa majibu katika kipindi cha wiki tatu.
Msajili ya Hazina ametakiwa kutathmini na kubaini kama Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NARCO bado anastahili kuendelea kuwemo katika nafasi hiyo.
Maagizo hayo yalitolewa jana Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudunu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Deo Filikunjombe, baada ya kamati kutoridhishwa na utendaji wa kampuni hiyo.
Mbali na maagizo hayo, pia Filikunjombe alisema kamati yake haiwezi kukubali ombi la kampuni hiyo la kutaka serikali iwape sh. bilioni 17 kwa ajili ya kuongeza mtaji wake kwa kuwa utendaji wake hauridhishi.
Alisema kampuni hakuna sababu ya serikali kutoa fedha za walipakodi kwa ajili ya kampuni hiyo ambayo inajiendesha kwa hasara na katika kipindi cha miezi mitatu walipotea ng’ombe 376 katika ranchi moja ya Ruvu.
Pia alisema katika baadhi ya ranchi kuna watendaji ambao hawajui KKK (kusoma, kuandika na kuhesabu) na kuna taarifa zinaonyesha kuwa kwa miezi mitatu mfululizo, wachungaji wanapewa ng’ombe na hawahesabiwi wakati wa kutoka kwenda machungani na hata wa kurudi.
Aliongeza kuwa baadhi ya taarifa zao zinaonyesha kuwa asubuhi wametoka ng’ombe 300 na jioni wamerudi 400, huku baadhi ya vitabu takwimu zake si sahihi kwa kuwa zimefutwafutwa, jambo ambalo linashangaza.
Naye Dk. Hadji Mponda, mjumbe wa kamati hiyo, alisema licha ya NARCO kudai kuwa na mfumo wa kuandika idadi ya ng’ombe wanaotoka na kurudi machungani, imebainika mfumo huo si sahihi na ndiyo sababu kunakuwa na upotevu na wanazidi kupungua mwaka hadi mwaka badala ya kuongezeka.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya NARCO, Salum Shamte alisema anasikitikika na hatua hiyo kwa sababu athari yake si ndogo kwa kuwa kama suala la wizi hata wao haliwafurahishi na hatua zilichukuliwa na vyombo husika vinaendelea na uchunguzi.
Filikunjombe alisema wanatambua mchango wa shirika hilo lakini kwa sasa hawastahili kupewe hata shilingi moja kutoka kwa walipakodi kutokana na menejimenti waliyo nayo.
Katika hatua nyingine, Filikunjombe aliuliza kuhusu Machinjio ya Ruvu ambayo serikali ilitoa zaidi ya sh. bilioni tisa na hayajakamilika hadi sasa. Hata hivyo, Shamte alisema walipokea sh. bilioni 5.6 tu.
Filikunjombe alisema kamati ilifanya ziara katika machinjio hayo na kilichoonekana hakilingani ya kiasi hicho cha fedha na kusisitiza tena kuwa hakuna haja ya kampuni hiyo kupewa fedha.
“Nasikia uchungu. Ni wizi ujangili, tuko katika matatizo wengine wanafanya wizi. Tatizo ranchi hazina uzio na watu wanaingia na kutoka,” alisema Shamte.
Kuhusu ujenzi wa machinjio ya Ruvu, Shamte  alisema waliamua kusitisha baada ya mkandarasi waliyeingia naye mkataba kujenga chini ya kiwango na sasa wako katika mchakato kutafuta mkandarasi mwingine hivyo yatakamilika mwishoni mwa mwaka ujao.

PAC yataka mikataba ya gesi


NA MARIAM MZIWANDA
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imelitaka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuwasilisha mikataba yote ya gesi ambayo haijafanyiwa ukaguzi.
Pia imeagiza kuwasilishwa kwa taarifa za mapitio ya mikataba hiyo kesho kwa Katibu wa Bunge baada ya saa za kazi ili ifanyiwe ukaguzi kubaini utekelezaji wa miradi.
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, alisema hayo jana wakati wajumbe wa kamati hiyo walipokutana na uongozi wa TPDC.
Alisema TPDC lazima iwasilishe mikataba yake isiyokaguliwa na ofisi ya  Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za  Serikali (CAG), ambayo ni 19 na kuondoa saba iliyokaguliwa kati ya 26 ya gesi iliyopo.
Alisema shirika hilo limekuwa likipiga chenga kuwasilisha mikataba ya gesi na mapitio yake hivyo, kukiuka sheria katika kuiwezesha kamati kutekeleza kazi yake.
“Tunaiagiza TPDC kesho wawasilishe mikataba ya gesi na watapangiwa siku ya kuja ili ijadiliwe na kukaguliwa kwa kina. Kamati ndiyo wananchi hivyo inafanya kazi kisheria. Kuinyima taarifa za mikataba ni kuvunja sheria,“ alisema.
Akitolea ufafanuzi suala hilo, Katibu wa Kamati PAC, Eric Maseke, alisema sheria mama inayotoa mamlaka kwa kamati za Bunge inaelekeza ofisi yeyote ya umma  kupitia kwa maofisa wake wanapotakiwa kutoa nyaraka za serikali.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC, Michael Mwanda, aliomba radhi kwa kamati hiyo kutokana na kutokea kutofautiana kati ya uongozi wake na kamati hiyo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, James Andilile, aliieleza kamati hiyo kuwa iwapo wanahitaji nyaraka za mikataba wawasiliane na Wizara ya Nishati na Madini kwa kuwa imewasilishwa huko.

DK. SHENI ALIPOHUTUBIA MKUTANO WA CCM ZANZIBAR

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar), akionyesha rasimu ya Katiba iliyowaslishwa katika Bunge Maalum la Katiba, juzi alipohutubia mkutano wa hadhara wa CCM, Zanzibar.

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar), akionyesha rasimu ya Katiba iliyowaslishwa katika Bunge Maalum la Katiba, juzi alipohutubia mkutano wa hadhara wa CCM, Zanzibar.


WANANCHI waliohudhuria mkutano huo wakiungamkono kuipigiakura Katiba Inayopendekezwa.


VIONGOZI waliohudhuria mkutano huo wakiomba dua. (Picha zote na Othman Maulid).

Wanaokiuka kutoa taarifa waonywa


NA RACHEL KYALA
KIONGOZI yeyote atakayeshindwa kurejesha fomu za tamko la Rasilimali na Madeni ya Viongozi katika muda uliowekwa, anapaswa kutambua kuwa hilo ni kosa na ukiukwaji wa Maadili ya Viongozi wa Umma, imeelezwa.
Taarifa kwa Umma iliyotolewa na Kamishna wa Maadili, imesema  viongozi wa umma wanapaswa kujua kuwa si wajibu wa kisheria kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi kuwapelekea viongozi fomu hizo.
Aidha kupitia taarifa hiyo wametakiwa kuzingatia kuwa ni wajibu wa kiongozi husika kuzitafuta kwa wakati ili kutekeleza matakwa hayo ya kisheria.
Taarifa hiyo inasema fomu hizo tayari zimeanza kutolewa na zinapatikana katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Dar es Salaam na katika ofisi za kanda zilizoko Kibaha, Arusha, Dodoma, Tabora, Mwanza, Mbeya na Mtwara. 
Kamishna wa Maadili kupitia taarifa hiyo alisema kiongozi atakayeshindwa kurejesha kwa tarehe husika atachukuliwa hatua kama ambavyo kifungu cha 15 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995 kinavyoeleza.

Machangudoa Moro wanyooshewa kidole


NA LATIFA GANZEL, MOROGORO
HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro, imewataka wanawake wanaojihusisha na biashara ya ngono katika eneo la Msamvu  maarufu Itigi, kuacha mara moja.
Imeonya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wote watakaokaidi amri hiyo kwa kuwa ni kinyume cha sheria.
Agizo hilo lilitolewa juzi na Meya wa Manispaa ya Morogoro, Amiri Nondo, ambapo alisema biashara hiyo ni haramu na kamwe haitaachwa iendelee.
“Nilifanya ziara ya kushitukiza katika eneo la Itigi Msamvu.  Eneo  lile limechafuliwa sana na wanawake hao wanaofanya biashara za kuuza miili.  Kuna  magari makubwa yanasimama hapo ndiyo sababu ya kuwepo kwa baishara hiyo,’’ alisema.
Alisema  halmashauri hiyo imebaini kuwepo kwa matumizi mabaya ya vibanda vya mawakala wa simu za mkononi, ambavyo hutumika kama vyumba vya kufanyia bishara hiyo haramu.
“Tumeagiza wenye vibanda vilivyojengwa bila utaratibu kubomoa kabla ya halamshauri kuchukua hatua ya kuwabomolea. Wakisubiri tufanye hivyo itawagharimu,’’ alisema meya huyo.

Balozi Sefue atema cheche


NA WAANDISHI WETU, DODOMA
SERIKALI imewataka viongozi waandamizi wanaoendelea kutumia risiti za kuandikwa kwa mikono katika makusanyo ya serikali kuachia ngazi kwa kuwa wameshindwa kudhibiti mapato ya serikali.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alipokuwa akifungua mkutano wa faragha wa mwaka wa makatibu wakuu, manaibu na makatibu tawala wa mikoa.
Sefue alisema mfumo ya kukusanya mapato kwa kutumia risiti zilizoandikwa kwa mikono unasababisha uvujaji mkubwa wa mapato ya serikali.
Alisema katika sehemu nyingi ambazo wameacha kutumia mfumo huo na kutumia mfumo wa kieletroniki kumekuwa na mafaniko makubwa katika ukusanyaji wa mapato.
‘’Katika Hospitali ya Tumbi mapato yaliongezeka kutoka wastani wa sh. 380,000 hadi sh. milioni tatu kwa mwezi, baada ya kutumia mfumo wa kiletroniki,’’ alisema.
Alisema ni lazima kusimamia mifumo madhubuti ya ufuatiliaji na tathimini kwa upande mmoja, mfumo wa udhibiti wa ndani katika masuala ya fedha na rasilimali nyingine.
‘’Msiwe waoga kuchukua hatua za kinidhamu au kisheria kwa wale wanaochafua sura na sifa ya utumishi wa umma.
“Ukishindwa kufanya hivyo ama wewe mwenyewe ni tatizo au hukufaa kupewa mamlaka ya nidhamu yanayoambatana na cheo ulichopewa,’’ alisisitiza.
Sefue alisema kumekuwa na upungufu katika ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na mengine yanajirudia mwaka hadi mwaka.
Alisema katika hilo inaonyesha kutokuwa na dhamira ya ukweli katika kumaliza hoja za mkaguzi au mifumo ya udhibiti wa ndani kuwa hafifu.
‘’Sasa tunajua tatizo ni nini. Kinachotakiwa ni dhamira ya kweli miongoni mwetu tuliopo hapa na kusema sasa basi na wale watakaoshindwa kusema itabidi watupishe,‘’ alisema.
Katibu huyo alitolea mfano udanganyifu mkubwa uliogunduliwa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani alipohakiki madai ya walimu tangu wa elimu ya msingi hadi wa vyuo vikuu na kusema udanganyifu wa aina hiyo lazima ukomeshwe.
Alisema pia mradi hati punguzo kwenye vyandarua vilivyotiwa dawa ambao ulikuwa ukiokoa maisha ya kina mama na watoto wachanga, umesitishwa na wahisani kutokana na wizi mkubwa.
“Ni hapa juzi tu nimeambia asilimia 40 ya dawa kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) zinaibwa katikati zikisafirishwa kutoka MSD hadi kufika kwa wananchi. Wizi wa aina hii lazima ukome na wahusika washitakiwe ili liwe fundisho kwa wengine,’’ alisema.
Katibu Mkuu aliwataka makatibu wakuu hao kutekeleza vyema na kwa moyo thabiti majukumu yao na kutumia mkutano huo kutafakari na kujitathimini kisha kuazimia kuwa chachu ya kweli ya maendeleo. 

Prof. Mwandosya awapa somo viongozi wa dini


 Na Rhoda Ezekiel, Kigoma
MAASKOFU na viongozi wengine wa dini wametakiwa kusoma na kuelewa kipengele kinachohusu haki na uhuru wa kuabudu katika Katiba Inayopendekezwa.
Kufanya hivyo kutawawezesha kuwafahamisha waumini wao haki na uhuru huo kama inavyopendekezwa katika Katiba hiyo pasipo kuingiliwa na mtu yeyote.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Profesa Mark Mwandosya, katika sherehe ya kumsimika askofu wa nne wa Jimbo la Kigoma,  Askofu Joseph  Mlolwa.
Alisema katika rasimu iliyo pendekezwa imeweka uhuru kwa kila mtu kuchagua dini yoyote pasipo kuingiliwa.
Profesa Mwandosya alisema katika rasimu inayopendekezwa ibara ya 19 kifungu cha 41 kinaelezea uhuru wa mtu kuabudu na kuamini imani anayotaka mradi asikiuke sheria za nchi.
“Nchi yetu haina udini tangu ilipoanzishwa mpaka ilipofikia sasa , na tutaendelea kumuenzi Baba wa Taifa (Mwalimu Julius Nyerere)  kwa kukemea udini na ukabila katika nchi yetu,” alisema  Mwandosya.
Aidha alisema serikali inatambua umuhimu na mchango wa makanisa na misikiti kwa kuendelea kuisaidia serikali katika nyanja za kijamii kama shule, hospitali pamoja na vituo vya kuhifadhi watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Hata hivyo aliwaomba viongozi wadini kuendeleza umoja na mshikamano  na kuepukana na uchochezi utakaosababisha kuvurugika kwa amani.
Kwa upande wake Askofu Mlola, alimshukuru kiongozi huyo na kuahidi kushirikiana na serikali kuhakikisha amani inaendelea kuwepo nchini.

Manufaa zaidi ziara ya JK China


NA MWANDISHI MAALUM
SERIKALI na taasisi mbili kubwa za kimataifa zimetiliana saini hati ya makubaliano (MOU) ya kuendeleza kwa pamoja Eneo la Kiuchumi la Bagamoyo.
Katika uendelezaji huo, pia itajengwa bandari kubwa ya Bagamoyo ambayo inatarajiwa kutoa mchango mkubwa kwa uchumi wa Tanzania.
Pande hizo tatu ambazo ni pamoja na Kampuni ya Uendeshaji Bandari ya China Merchant Holding International (CMHI) ya Jamhuri ya Watu wa China na Mfuko wa Uwekezaji wa Oman, zimetilia saini hati hiyo kwenye sherehe iliyofanyika katika Hoteli ya Hilton Shenzhen Shekou Nahai,  Shenzhen, Kusini mwa China.
Rais Jakaya Kikwete, ambaye alitembelea Jimbo la Guang Dong ambako liko Eneo la Uwekezaji wa Kiuchumi la Shenzhen, alishuhudia utiaji saini huo ambao kwa upande wa Tanzania saini ilitiwa  na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servicus Likwelile.
Chini ya hati hiyo, ujenzi wa Eneo la Uwekezaji la Bagamoyo utaanza Julai Mosi, mwakani. 
Kabla ya sherehe hiyo ya kutiliana saini hati ya makubaliano, Rais Kikwete alitembelea eneo la Makontena la Bandari ya Shenzhen, ambako alionyeshwa vifaa vya kisasa vya kupakia na kupakulia makontena. Kazi hiyo inafanywa na  CMHI ambayo ina uzoefu wa miaka 140 wa uendeshaji wa bandari.
Akizungumza katika sherehe hiyo, Rais Kikwete alisema kuwa serikali yake imedhamiria kuhakikisha mradi huo wa mamilioni ya fedha wa Bangamoyo unaanza.
 “Tutafanya lolote linalowezekana kuhakikisha kuwa mradi huu unaanza kwa sababu utaleta neema kubwa ya kiuchumi kwa nchi nzima,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa CMHI, Li Jianhong, ameitaka serikali kuangalia uwezekano wa kumaliza vikwazo vyote ambavyo vimechelewesha kuanzishwa kwa mradi huo ili uweze kuanza Julai Mosi, mwakani, kama ilivyokubaliwa.
Mapema jana, akiwa Shenzhen, Rais Kikwete alitembelea makao makuu ya kampuni ya Teknolojia ya Mawasiliano ya Hauwei  inayoajiri maelfu ya watu duniani, ikiwemo Tanzania na kutengeneza mamilioni ya faida.
Rais pia alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Manispaa ya Shenzhen ambayo yalifanyika kwenye hoteli ambako alifikia ya  Shenzhen Wazhou Guest Hotel ambayo ni mali ya Serikali ya China.
Pia alitembelea makao makuu ya kampuni ya Teknolojia ya Mawasiliano ya ZTE iliyoko Shenzhen, ambayo inaendesha shughuli zake Tanzania na inaajiri wafanyakazi 60,000 dunia nzima.

Dk Bilal mgeni rasmi tamasha la MOWE leo


NA EMMANUEL MOHAMED
MAKAMU wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tamasha la wanawake wajasiriamali mali (MOWE), litakalofanyika leo katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es salaam.  

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa tamasha hilo, Helihaka Mrema, alisema tamasha hilo lina lengo la kuwakutanisha wajasiriamali hao na wadau mbalimbali ili kuboresha ubora wa bidhaa zao kwa lengo la kukidhi haja ya masoko ya ndani na nje.
Helihaka alisema tamasha hilo litawakutanisha wajasiriamali zaidi ya 158 na wadau mbalimbali, ikiwemo Wakala wa Vipimo Tanzania, Benki ya Wanawake (TWB), Shirika la Viwanda Vidogovidogo (SIDO) na Mamlaka ya Udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA).
Alisema wadau hao watasaidia kutoa elimu ili bidhaa zao ziweze kukidhi haja katika masoko yao, hususan wanaozalisha bidhaa za chakula, dawa na nguo.
"Changamoto ya masoko kwa wajasiriamali ni suala la muda mrefu na ufumbuzi wake ni elimu kutoka kwa wadau, wakiwemo wakala wa vipimo na TFDA ili bidhaa zetu ziweze kukidhi soko," alisema.

Serikali yasema hakuna mgonjwa wa ebola


NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imekanusha kuwepo kwa ugonjwa wa ebola nchini, huku ikithibitisha kuwa mtu aliyedhaniwa kuwa na ugonjwa huo, anasumbuliwa na malaria.
Pia, wanafamilia wa karibu wa mgonjwa huyo wamechunguzwa na kuonekana  hawana dalili za ugonjwa huo au magonjwa jamii ya ebola, kama dengue na chikungunya.
Kauli hiyo ya serikali imetolewa baada ya sampuli ya damu iliyochukuliwa kutoka kwa mgonjwa huyo na kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara, kuonyesha kuwa alikuwa akisumbuliwa na malaria. 
Kwa mujibu wa tamko lililotolewa na serikali jana na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Donan Mmbando, baada ya kupatikana kwa taarifa ya kuwepo kwa mtu wenye dalili za ebola, serikali ililazimika kumfanyia uchunguzi wa kina mgonjwa huyo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa mgonjwa huyo, ambaye ni mkazi wa Dar es salaam, eneo la Kimara, alifika mkoani Kilimanjaro, Oktoba 20, mwaka huu, katika kijiji cha Kirua kwa ajili ya kusalimia ndugu.
Baada ya kufika mkoani hapo, alifikishwa katika Kituo cha Afya cha Shirimatunda, akisumbuliwa na maumivu ya misuli, kichwa, maumivu ya koo na kupoteza hamu ya kula.  
Taarifa za mgonjwa huyo zilionyesha kuwa kikazi ni mtaalamu wa kupima ardhi (Land Surveyor) na katika siku za hivi karibuni, alikwenda nchini Senegal kwa kazi za mkataba na kurejea nchini mwezi huu.

Vyeti vilivyopotea kulipiwa sh. 100,000


NA RACHEL KYALA
BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA), limeanzisha utaratibu wa kutoa nakala za vyeti kwa watahiniwa waliopoteza vyeti vyao kwa gharama ya sh. 100,000.
Utaratibu huo utawanufaisha watahiniwa waliohitimu kuanzia mwaka 2008, ambao vyeti vyao viliwekwa picha.
Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde, akizungumza jijini Dar es Salaam jana, alisema hatua hiyo itapunguza changamoto zilizokuwa zikiwakabili watahiniwa waliopoteza vyeti vyao kwa sababu mbalimbali.
"Baraza limeweka utaratibu madhubuti ili kuhakikisha fursa hii haitumiwi vibaya, ikiwemo kufanya uchunguzi wa uhalali wa mwombaji, taarifa ya upotevu wa cheti katika kituo cha polisi na kutangaza gazetini, vielelezo husika vilivyoambatanishwa," alisema. 
Hata hivyo, alisema yeyote aliyepatiwa cheti mbadala, atatakiwa kurejesha cheti hicho iwapo cheti cha awali kitapatikana.
Aliongeza kuwa iwapo baraza litabaini udanganyifu wa aina yoyote katika maombi hayo, wahusika watachukuliwa hatua za kisheria.
Dk. Msonde aliwashauri waajiri kufuatilia NECTA uhalali wa vyeti vya watu wanaopita kwenye usaili kabla ya kuwaajiri ili kukomesha tatizo sugu la waajiriwa kughushi vyeti.
Alisema NECTA kwa kushirikiana na kamati za uendeshaji mitihani katika ngazi za mikoa, wilaya na wasamaria wema, wamefanikiwa kudhibiti wizi na udanganyifu wa mitihani ya taifa.
Alifafanua kuwa katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE), mwaka 2013 takwimu, zinaonyesha kuwa watahiniwa waliofutiwa matokeo kwa kufanya udanganyifu ni 13 tu, ikilinganishwa na watahiniwa 9,736, mwaka 2011 na 293 mwaka 2012.

Vigogo wa dawa za kulevya watoweka  • Wauza mahekalu, magari wakimbilia nje 
  • Mawakala wahaha, polisi wapigwa butwaa

LChikawe: Tutawanasa wote kimya kimya
NA MWANDISH WETU
SIKU chache baada ya kunaswa kwa watuhumiwa wanaotajwa kuwa ni vinara wa kusafirisha na kuingiza dawa za kulevya nchini, hali imeanza kuwa tete kwa vigogo wengine wa biashara hiyo.
Baadhi ya vigogo wakiwemo wafanyabiashara wakubwa nchini, wameanza kukimbia nje ya nchi kukwepa mkono wa sheria, huku wengine wakisubiri hali itulie ndipo wajitokeze.
Hatua hiyo inatokana na askari wa Kikosi Maalumu cha Kudhibiti Dawa za Kulevya kuendelea kuwasaka vinara wa biashara hiyo kimya kimya, ikiwa ni mkakati wa kusambaratisha mtandao wa biashara hiyo haramu nchini.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya kikosi hicho, zinasema kuwa operesheni hiyo imekuwa ikifanyika kwa usiri mkubwa, kiasi cha mamlaka zingine kutofahamu kinachoendelea.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, kikosi hicho kilivamia nyumbani kwa Muharani Abdallah  Chonji (44), na kumtia mbaroni akiwa na wenzake wanne kwa tuhuma za kudaiwa kuwa ni kinara wa dawa hizo.
Kukamatwa kwa Chonji, ambaye tayari amepandishwa kizimbani kujibu mashitaka, kumezusha taharuki kubwa huku vigogo wengine wakijificha kukwepa mkono wa sheria.
Habari za kuaminina zinasema kuwa, tangu kutokea kwa tukio hilo, vijiwe vingi vinavyotumika kuuza dawa za kulevya katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, vimesimama kuendelea na biashara hiyo na vingine mawakala wake wakihama.
Kwa sasa, biashara hiyo hususan ile ya uchuuzi kwa watumiaji wa hali ya chini kabisa (mateja), imekuwa ikifanyika kwa usiri mkubwa tofauti na hapo awali, ambapo ilikuwa ikifanyika hadharani bila woga.
“Hali imekuwa mbaya, matajiri hawaonekani na simu wamezima tangu wanene walipokamatwa… hakuna vijiwe ambavyo vinafanya kazi hadi hapo hali itakapotulia ndipo inaweza kurejea tena.
“Wakubwa wengine wameshapanda pipa (ndege), wamekwenda kusikilizia nchi za watu hali itakuwaje ndipo tutajua kinachoendelea,” kilisema chanzo kimoja.
Chanzo hicho kimesema kuwa operesheni iliyoanzishwa ni tofauti na zilizowahi kufanyika na kwamba, ya sasa imetawaliwa na usiri mkubwa.
Pia, kimesema kuwa askari wanaotumika ni wageni na wamekuwa wakisimamia maadili kwani, hata wanaporubuniwa kwa fedha, wamekuwa wakali.
Habari za kuaminika zinaeleza kuwa, kikosi kinachoendesha operesheni hiyo, kinahusisha askari maalumu wapya, wakiwemo maofisa usalama wa taifa.
Kimesema kuwa siku ya tukio la kwenda kukamatwa kwa Chonji na wenzake, kikosi hicho kiliweka mikakati yake kisha kuomba msaada wa askari polisi wa kituo kimoja.
Hata hivyo, askari wa kituo hicho waliokuwepo kwenye msafara huo hawakufahamu mhusika anayekwenda kukamatwa, badala yake walielezwa kuwa ni jambazi.
“Hawa makamanda walivamia pale bila askari ambao wamezoeleka kufahamu kinachofanyika. Walidai wanakwenda kukamata jambazi, lakini waliposimama nyumbani kwa mtuhumiwa, walishtuka na hawakuweza kufanya lolote zaidi ya kutoa ushirikiano ili kutimiza lengo hilo,” kilisema chanzo hicho.
Hatua hiyo inatokana na madai kuwa, askari polisi wengi wanafahamu mtandao wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya nchini na kwamba, inapopangwa mikakati ya kuwatia mbaroni, huwabonyeza ili kutoroka, hivyo kufanya kazi hiyo kuwa ngumu.
Chidi Benz kupanda kortini
Kukamatwa kwa msaani nyota wa hip hop, Rashid Benzino (Chid Benz), kumezidisha hali ya hatari kwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya.
Chid Benz anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia leo kujibu mashitaka ya kukutwa na dawa za kulevya.
Msaani huyo alikamatwa na dawa hizo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, ambapo alikutwa na kete 14 za heroin na misokoto miwili ya bangi.
Kamanda wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa, amewaonya vijana kuacha kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Alisema kukamatwa kwa Chid Benz, ambaye alikuwa na nafasi kubwa ya kuiepusha jamii na biashara hiyo haramu, ni fursa nyingine ya vijana kujifunza na kujiepusha na dawa za kulevya.
Serikali yaonya
Akizungumza na Uhuru jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, alisema hiyo ni operesheni maalumu na kamwe haitakuwa upepo wa mpito, hivyo itakuwa endelevu.
Alisema serikali imeibuka na mbinu mpya za kukabiliana na vinara wa dawa za kulevya na kwamba, vita hiyo itakuwa ya kudumu na hakuna atakayepona.
Aliwataka vijana kukaa mbali na kutojihusisha na vinara wa dawa za kulevya kwani kufanya hivyo ni kujitafutia matatizo.
“Hii mikakati dhidi ya hawa vinara wa dawa za kulevya haitasimama na tumekuja kivingine kabisa…miaka ya nyuma walikuwa wanawatumia vijana wetu kuwaibia taarifa, lakini sasa wataona vumbi tu,” alisema.
Hata hivyo, alionya kuwa vigogo wa dawa hizo  wanaokimbilia nje ya nchi ili kukwepa mkono wa sheria, kamwe hawatakuwa salama kwa kuwa watasakwa kimya kimya na kutiwa mbaroni popote walipo.
Bila kuweka hadharani mikakati hiyo, Chikawe alisema serikali imejipanga kikamilifu na itaendelea kubana njia zote zinazotumika kuingiza dawa hizo.

Mwandosya: Fedha si kigezo cha Urais


NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Profesa Mark Mwandosya, amesema fedha si kigezo cha mtu kuteuliwa kuwania nafasi ya urais na kwamba, imani iliyojenga haina mashiko.
Amesema suala hilo limekuwa likimtatanisha na kueleza kuwa kiongozi huchaguliwa kutokana na uadilifu na uwezo wake na si kigezo cha fedha kama baadhi ya makada walivyojenga imani hiyo.
Profesa Mwandosya, ambaye ni miongoni mwa makada wa CCM wanaotajwa kwenye kinyang’anyiro cha urais mwakani, alisema imani hiyo inakwenda kinyume na matarajio ya wananchi na misingi ambayo vyama vya siasa havikuichagua.
Aliyasema hayo mjini hapa jana wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Mbeya.
“Fedha ili iweje …kwamba utawanunua wajumbe, utawapa thamani wajumbe, utasema mjumbe wa mkutano mkuu wa Taifa thamani yake ni sh.200,000 wa NEC sh.500,000 na yule wa Kamati Kuu ni sh.milioni moja.
“Hicho ni kiburi na sifahamu makada wenye imani hiyo potofu wanaipata kutoka wapi… halafu inakuwaje baada ya kuteuliwa,” alihoji Profesa Mwandosya.
Alisema kwa mshahara wake tangu alipoteuliwa, posho za safari za ndani na nje ya nchi, kamwe hana uwezo wa kumpa kila mjumbe  sh. 200,000.
”Sasa hizi fedha zingine wenzetu hawa wanazipata wapi na kama wanazikopa, watazirudisha namna gani? Kama wanafanya biashara, watawezaje kuwatumikia wananchi wakati wana mambo yao mengine pembeni,” alisema.
Alisema vitabu vya dini vinasema kamwe mtu hawezi kuwatumikia mabwana wawili, hivyo kuchanganya siasa na mambo mengine ni tatizo na kuwanyima haki wananchi.
Alisema hao wenye uwezo huo kifedha, wamekuwa wanawaona wengine wanaohoji hali hiyo, kuwa wanasiasa za kizamani, lakini kwake ni afadhali kuendelea na siasa za kizamani, kuliko siasa za kumrubuni mwananchi kwa uongozi kupatikana kwa njia ya fedha.
“Fedha ambazo utazirudisha namna gani, zimetoka wapi na kwa sababu gani? Kwa kweli hili ni jambo, ambalo nitaendelea kulizungumza tu, kama Mwenyezi Mungu akinijalia kufika popote pale, nitakuwa kwa sababu nina upendo, nataka kuwatumikia wananchi, lakini si sababu nina fedha,” alisema Mwandosya. 

Urais ni zaidi ya hapo
Katika hatua nyingine, Profesa Mwandosya amesema ndani ya CCM, hawateui mtu kwa ajili ya kuwa rais tu, bali wanamtarajia kuwa Mwenyekiti wa Taifa.
Alisema makada wengi wamekuwa wakilisahau hilo na kwamba, lazima wajiulize mtu wanayemtaka anaweza kudumisha fikra za waasisi, Hayati Julius Nyerere na Amani Karume?
Alisema urais ni mfumo unaoendana na dhamana na heshima na jukumu kubwa, hasa ikichukuliwa kuwa kuna utaratibu ndani ya CCM.
Kwa mujibu wa Profesa Mwandosya, kumsaidia mwananchi kimaendeleo,  kwa kupiga hatua ni jukumu kubwa, ambalo analiona linatetemesha, lakini ni lazima mmoja wao aende akaifanye hiyo kazi.
Alisema Mwalimu Nyerere, aliwahi kusema viongozi wazuri na bora hawajitangazi kwa sababu wanaona uzito wa dhamana iliyopo mbele yao.
“Hawajitangazi ila kuna watu wanawajua viongozi wanaofaa kuwaongoza.
“Fulani tunamfahamu anaweza akatutoa hapa, na kutuongoza kupigania kijiji chetu. Kwa mfano ataongoza majeshi yetu kupigana na kijiji kingine na haiwezekani mtu ajitokeze na kusema atafanya kila njia ili achaguliwe,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa hilo ni suala gumu sana ambalo hata ndani ya Chama, ni lazima waanze kufikiria iwapo hii demokrasia waliyonayo (CCM), ifike kiasi ambacho kila mtu kwa sababu ana uhuru, basi anaweza akasema anataka kwenda Magogoni.
Alisema mwakani, taifa litaingia kwenye hatua ya kufanya mabadiliko ya uongozi, ambapo kila chama kina mchakato wake, na CCM nacho kina utaratibu wake.
“Mwakani ndio uchaguzi, lakini dira na maelekezo bado hayajatoka, basi ni dhahiri mwananchi na mwana-CCM ana ruksa ya kugombea nafasi yoyote ikiwemo urais,” alisema Profesa Mwandosya.

Sunday, 26 October 2014

Profesa Mwandosya alonga


NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA
ALIYEKUWA mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Profesa Mark Mwandosya, amesema suala la wabunge kuwajibishwa na wananchi, halipo katika katiba ya nchi yoyote duniani.
Imeelezwa wajumbe wa Bunge hilo waliangalia na kuzipitia katiba nyingi, lakini hawakuona hata moja  iliyowapa uwezo wananchi kumwajibisha mbunge.
Profesa Mwandosya aliyasema hayo, alipokuwa akijibu swali aliloulizwa kwanini katiba iliyopendekezwa haikuweka kifungu hicho kama wananchi walivyopendekeza katika tume ya Jaji Warioba.
Alisema maoni ya awali ya wananchi yalikuwa ni mwanzo wa utaratibu wa kupata katiba na si hatua ya mwisho. “ Ingekuwa hivyo kusingekuwa na haja ya kwenda kwenye kura ya maoni, hata Bunge kuketi,” alisema.
 “Tume ya Jaji Warioba  haikuwa kura ya maoni tafadhali sana, wale walioweza kutoa maoni walitoa, lakini wengi zaidi hawakutoa. Watu wengi zaidi watakuja kutoa maoni yao kwa kutoa uamuzi kusema ndiyo au hapana,” alisema Profesa Mwandosya.
Alisema anachojua, wananchi wanawawajibisha wabunge wakati wa uchaguzi, kama mbunge hakutekeleza ahadi, pale anaweza kuwajibishwa kwa kutochaguliwa tena.
Kwa mujibu wa Mwandosya, kila baada ya uchaguzi mkuu kufanyika, zaidi ya nusu ya wabunge wanaondoka, hivyo wananchi wanakuwa wamewawajibisha na kuwa huo ni mfumo tu na wabunge wabovu hawataendelea kubaki hata siku moja.

Alisema  mwaka 2010, zaidi ya asilimia 60 ya wabunge waliokuwepo mwaka 2005, waliwajibishwa na wananchi kwa kunyimwa kura.
Profesa Mwandosya alibainisha kuwa  hivi sasa idadi ya wabunge waliopo bungeni tangu mwaka 2000,  hawazidi 20 .

Dk. Sheni: Someni katiba na kuzielewa sheria


NA MWANDISHI MAALUMU, ZANZIBAR
WAKUU wa mikoa na wilaya wametakiwa kuisoma mara kwa mara na kuielewa katiba pamoja na sheria nyingine za nchi.
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Sheni, alitoa agizo na kusema wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku, wanapaswa kuzingatia katiba na sheria.
Alitoa agizo hilo jana, alipokuwa akifungua mkutano elekezi kwa wakuu wa mikoa na wilaya za Zanzibar.
Alizitaja baadhi ya sheria ambazo wakuu hao wanapaswa kuzielewa na kuzitekeleza kila siku ni pamoja na Sheria Namba 1 ya Mwaka 1998 ya Tawala za Mikoa, Sheria Namba 3 ya Baraza la Manispaa ya Mwaka 1995 na Sheria Namba 2 ya mwaka 2011 ya Utumishi wa Umma.
Aliwataka pia  kuheshimu kiapo cha uaminifu wanachokula kabla ya kukabidhiwa dhamana zao na kuwakumbusha kuwa kiapo hicho ni jukumu walilochukua katika maisha yao duniani na mbinguni.
Dk. Sheni aliwataka wakuu wa mikoa kuelewa kuwa  ndio watendaji wakuu katika mikoa yao na kuwakumbusha mabadiliko ya kumi ya katiba ya Zanzibar,  ambayo yanaeleza kuwa wakuu wa mikoa na wilaya ni watendaji wa serikali, tofauti na ilivyokuwa kabla ya mabadiliko hayo.
Alisema ni vigumu shughuli za serikali kutekelezwa katika ngazi hizo, bila ya kuwepo kwao, hivyo wanapaswa kuelewa uzito wa majukumu yao katika kuleta maendeleo ya nchi na ustawi wa wananchi katika mikoa na wilaya zao.
Hata hivyo, alibainisha kuwa kazi za mikoa na wilaya si za kuratibu shughuli za serikali kuu pekee, bali mikoa na wilaya inapaswa kuwa na dira na kupanga mipango yake ya maendeleo kwa kuzingatia changamoto, vipaumbele, mazingira na mahitaji ya mkoa na wilaya husika.

Sekta ya anga yakabiliwa na uhaba wa wafanyakazi


NA MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA),  imetoa wito kwa wanafunzi wote nchini kusoma masomo yatakayowawezesha kufanya kazi katika sekta ya anga.
Imeelezwa kuwa sekta hiyo hivi sasa inakabiliwa na uhaba mkubwa wa wataalam.
Rai hiyo ilitolewa jana na Mwanasheria Mkuu wa TAA, Wakili, Ramadhani Maleta alipokuwa akihutubia katika mahafali ya nne ya Shule ya Sekondari ya Lilian Kibo, Goba Matosa, Dar es Salaam.
Maleta alisema ni aibu kwa  mamlaka kuajiri wataalam kutoka nje ilhali wanafunzi wana uwezo wa kusoma na kufaulu vizuri.
 “Mamlaka ya Viwanja vya Ndege inategemea sana juhudi zenu ili tuweze kupata wataalam wakiwemo marubani, wahandisi, waongoza ndege, wanasheria na wahudumu wa kwenye ndege,” alisema.
 “Natoa rai kwa vijana mnaomaliza na hata ambao bado mpo katika vidato vya chini, mwongeze juhudi katika masomo yenu, kwani taifa na hata sisi tulio katika sekta ya usafiri wa anga tunawategemea muwe wataalam wetu hapo baadaye,” alisema na kuongeza kuwa sekta hiyo hivi sasa inakuwa kwa kasi nchini.
Aliupongeza uongozi wa shule hiyo kwa kazi nzuri ulioifanya ya kuwalea vijana kielimu na kufanikisha kupeleka vijana wote 22 wa kidato cha sita katika vyuo vikuu vya Mzumbe, Sokoine, SAUT, Dar es Salaam, Chuo cha Uhasibu (TIA), IFM baada ya kufaulu kwa daraja la kwanza na la pili tu katika masomo ya sayansi na sanaa mwaka 2013.
TAA imeahidi kuchangia sh. milioni tano kwa ajili ya kuvuta maji ya bomba shuleni hapo. Hata hivyo iliwataka wazazi kuchangia mfuko wa maji

Msiwaozeshe mabinti wadogo-Marombwa


Na Cecilia Jeremiah
WAZAZI na walezi wametakiwa kuacha kuwaozesha watoto wao kwa tamaa za fedha  mara wanapomaliza masomo yao.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mbunge wa Kibiti,  Abdul Marombwa, wakati akiwahutubia wazazi  na wanafunzi wahitimu wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Mtanga.
Alisema si sahihi kwa wazazi kupokea fedha na kuwaoza watoto wao, kwani  kufanya hivyo ni kukatisha malengo yao.
Mbunge  huyo alisema mbali na kuwaozesha wakiwa wamemaliza masomo yao, pia kuna wengine ambao wamekuwa wakifanya hivyo hata kwa wanafunzi wanaofeli mitihani yao.
“ Kuna baadhi ya wazazi, mtoto akifeli ndio tiketi ya kumwozesha, hapana… huyu ana uwezo wa kuendelea na masomo ya ziada na baadaye kufanya vizuri pia,” alisema.
Alisema hivi sasa hosteli kwa ajili ya wanafunzi wa kike inajengwa ili kuwasaidia wale wanaokaa mbali na shule kutopata shida.
Marombwa alibainisha wengi, wengi waliobainika kuwa na mimba walikuwa wakidanganywa njiani na wengine kutofika shule.
Hata hivyo alisema, jitihada zinafanywa kufikisha maji katika hosteli hiyo ili wanafunzi waanze kuitumia.
Aliahidi kulipa ada ya mhula wa kwanza kwa wanafunzi wote wanakaochaguliwa kwenda kidato cha tano shuleni hapo.
“Idadi ya wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne ni 18, wasichana wanne wavulana 14, hawakufika idadi ya kupewa kituo cha mtihani hapa Mtanga hivyo wataenda kufanya mitihani yao Muhoro, hawa nitawalipia gharama za malazi,” alisema.
Mkuu wa Shule ya Mtanga, Gynogret Nwakyambiki, alisema shule yake inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ya kutokuwa na maabara.

MSD yaidai serikali mabilioni


NA EPSON LUHWAGO 
UHABA mkubwa wa dawa na vifaa tiba umezikumba hospitali nyingi nchini, zikiwemo za Muhimbili na Ocean Road, kutokana na serikali kudaiwa zaidi ya sh. bilioni 90 na Bohari Kuu ya Dawa, (MSD).
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali linalofuatilia masuala ya afya nchini la SIKIKA, Irenei  Kiria, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa hali hiyo inahatarisha maisha ya wananchi kutokana na kukosa matibabu.
Irene alisema kutokana na madeni hayo, MSD imesimamisha usambazaji wa dawa katika hospitali za serikali, zikiwemo za rufani na za wilaya, hasa za Mpwapwa na Kiteto, ambazo zinadaiwa mamilioni ya shilingi. 
Alisema Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kwa mfano, inadaiwa sh. bilioni nane, huku Hospitali ya Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, ikidaiwa sh. milioni 38.
Kwa mujibu wa Kiria, ongezeko la deni hilo limekuwa likiathiri ufanisi na utendaji kazi wa MSD, kwakuwa taasisi hiyo haijiendeshi kwa faida.
Alisema kutolipwa kwa fedha hizo kwa wakati kunaifanya MSD kukosa fedha za kugomboa, kuhifadhi na kusambaza dawa na vifaa kutoka mahali vinakotengenezwa na katika matawi yake. 
Kutokana na hali hiyo, alisema afya za wananchi ambao wengi wao hawana uwezo wa kugharimia matibabu, ziko shakani kwa kuwa tegemeo lao kubwa ni hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya vilivyo chini ya serikali. 
“Nchini Tanzania, zaidi ya asilimia 80 ya wananchi hawako katika mfumo wowote wa bima za afya na inapotokea uhaba wa dawa na vifaa tiba, wananchi hawa wanakuwa ndio waathirika wakubwa zaidi,” alisema.
Pamoja na taarifa ya SIKIKA, uchunguzi uliofanywa na Uhuru katika baadhi ya hospitali za jijini Dar es Salaam,  kama Sinza Palestina na Mwananyamala, unaonyesha kuwa wagonjwa wengi wamekuwa wakiandikiwa dawa na kutakiwa wakazinunue kwenye maduka ya dawa.
Mmoja wa madaktari katika hospitali ya Sinza Palestina (jina linahifadhiwa) alikiri kuwepo kwa hali hiyo na kusema tatizo hilo limekuwepo kwa zaidi ya mwezi.
Katika hospitali ya Mwananyamala ambayo ina hadhi ya rufani katika Manispaa ya Kinondoni, baadhi ya wagonjwa walisema wanandikiwa dawa huku wakiambiwa haziko kwenye hifadhi na kutakiwa kwenda kwenye maduka yaliyoko jirani. 
Hata hivyo, sababu kubwa ya serikali kutoilipa MSD ni kutokana na ufinyu wa bajeti kwa kuwa fedha zilizopangwa kwa ajili ya afya zimetolewa kidogo kulinganisha na mahitaji. 

Tapeli latiwa mbaroni Mbeya


Innocent Ng’oko, Mbeya
MAKACHERO wa Jeshi la Polisi Nchini, wamemtia mbaroni mmiliki wa Kampuni ya KEAR Computer Training, Uttu Kingwande, kwa tuhuma za utapeli.
Kingwande anadaiwa  kuwatapeli wanafunzi lukuki waliokuwa wakipata mafunzo ya kompyuta katika kituo chake alichokuwa amekifungua katika Shule ya Sekondari ya Mbeya.
Inadaiwa kuwa kituo hicho hakikuwa kimesajiliwa na hivyo alikuwa akijipatia pesa kiujacha ujanja.
Mtuhumiwa huyo alikuwa akitafutwa kwa zaidi ya miezi mitatu sasa, ambapo taarifa za kiuchunguzi zinaeleza kuwa alitiwa mbaroni akiwa mafichoni wilayani  Handeni, katika mkoa waTanga.
Habari za kipolisi zinasema baada ya kutiwa mbaroni, mtuhumiwa  alisafirishwa hadi Mbeya akiwa chini ya ulinzi.
Inadaiwa kuwa kituo alichokuwa akikiendesha hakikuwa na usajili unaotambulika, hivyo wanafunzi waliokuwa wakisoma walijikuta wakikosa ajira na vyeti vyao kutotambulika popote.
Hadi jana, baadhi ya  wanafunzi waliopatwa na msukosuko  wanadai hawajarudishiwa pesa zao za ada tangu mmiliki huyo akimbie na kufunga kituo kwa miezi mitatu.
Julai mwaka huu, wanafunzi waliokuwa wakipata mafunzo kituoni hapo walielezwa kuwa mafunzo yamesitishwa kwa muda kutokana na polisi kuvamia. Kila mwanafunzi kituoni hapo alikuwa akilipa sh. 40,000.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Barakael Masaki, alikiri kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kusema anatarajiwa kufikishwa mahakamani.

Friday, 24 October 2014

Pata nakala yako


Risasi zarindima Dar  •  Polisi, genge la mihadarati wapimana ubavu 
  •  ‘Wazungu wa unga’ watano watiwa mbaroni 

NA MWANDISHI WETU
MILIO ya risasi ilirindima kwa dakika kadhaa wakati Polisi wa Kikosi cha Kuzuia Dawa za Kulevya, walipokuwa wakiwakamata watu wanaotuhumiwa kuwa vigogo wa dawa za kulevya.
Kundi kubwa la wananchi lililokuwa likishughudia tukio hilo, lililazimika kutawanyika baada ya polisi kufyatua risasi hewani huku watuhumiwa nao wakijibu kwa kufyatua risasi pia.
Habari za kuaminika zinasema polisi hao walikuwa kwenye operesheni maalumu ya kuwasaka vigogo wa dawa za kulevya, ambapo katika tukio hilo, watuhumiwa watano walitiwa mbaroni.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kuwa ni vinara wa kuingiza na kusafirisha dawa za kulevya nchini.
Hata hivyo, kabla ya kusalimu amri watuhumiwa hao walikaidi amri ya polisi kujisalimisha kwa madai ya kutaka kuzungumza kwanza na mtoto wa kigogo mmoja (jina linahifadhiwa).
Watuhumiwa waliotiwa mbaroni ni Muhalani Abdalla (Chonja), ambaye alidaiwa kugoma kutii amri ya polisi hivyo kuzusha tafrani kubwa iliyowafanya watu kujazana kutaka kujua kulikoni.
Mtuhumiwa huyo ambaye ni maarufu jijini Dar es Salaam na anayedaiwa kudaiwa kumiliki idadi kubwa ya nyumba kwenye mtaa mmoja, aliwaongoza wenzake kukaidi amri ya polisi.
Kutokana na kukaidi huko, polisi walitaka kutumia nguvu hivyo kusababisha wananchi kujongea ili kufahamu kinachoendelea, ndipo walipofyatua risasi hewani kwa lengo la kuwatawanya.
Wakati polisi wakifyatua risasi kuwatawanya wananchi, watuhumiwa hao nao walianza kufyatua risasi hewani kujibu mapigo.
Mabishano hayo ya risasi yalidumu kwa dakika kadhaa kisha hali ikatulia kidogo na hatimaye polisi kufanikiwa kuwadhibiti na kuwatia mbaroni.
Mtuhumiwa wa kwanza kutiwa mbaroni alikuwa Chonja, ambapo baada ya wenzake kuona amedhibitiwa na polisi, walijisalimisha na kupandishwa kwenye gari la polisi.
Kamanda wa Polisi wa Kikosi Maalumu cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kukamatwa kwa watuhumiwa hao.
Alisema watuhumiwa hao wanadaiwa kuwa vinara wa kusafisha dawa za kulevya ndani na nje ya nchi na kwamba walikuwa wakisakwa kwa muda mrefu.
Aliwataja watuhumiwa wengine waliokamatwa ni kuwa ni Maric Zuber, Tanaka Adam, Rehani Mursal na Abdu Abdallah, ambao kwa sasa wanashikiliwa na polisi.
Pia alisema watuhumiwa hao walikutwa na dawa za kulevya aina ya heroin kilo saba, ambazo zimechukuliwa kama uthibitisho.
“Oparesheni hii ni endelevu na ninawaasa wananchi watusaidie kwa kutupa taarifa sahihi ili kuwatia mbaroni hawa vinara. Tulikuwa  tunawasaka hawa kwa muda mrefu kutokana na kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi.
“Hii ni hatua muhimu na nzuri kwetu kwa kuwa itatusaidia kuubaini mtandao wote ili kuusambaratisha,” alisema Nzowa.
Habari zaidi zinadai kuwa, kuna mtandao mkubwa wa dawa za kulevya nchini ambao unahusisha wafanyabiashara wakubwa katika nchi za Pakistani, China na Falme za Kiarabu, ambapo husafirisha vijana wa Kitanzania kuwekwa rehani.
Vijana wa Kitanzania wanapowekwa rehani, wafanyabiashara hupewa kiasi kikubwa cha dawa za kulevya kwa ajili ya kusambaza na kuuza kisha kurejesha fedha na inapotokea wametoweka, vijana hao hupewa mateso makali.
Habari zaidi zinasema vijana wanaopelekwa kwenye nchi hizo kuwekwa rehani, hupata mgawo wa kati ya asilimia 20 na 25 katika kila mzigo, ambapo mkataba maalumu huriwa saini na wahusika.
Imeelezwa kuwa baadhi ya vigogo wa dawa hizo wamekuwa wakiwatosa vijana hao, hivyo wengine huuawa kwa mateso. Vijana kutoka Tanzania, Afrika Kusini na Nigeria ndio wamekuwa vinara wa kuwekwa rehani nchini Pakistan.

JK azungumzia Rais ajaye


NA MWANDISHI WETU, BEIJING
“NINGEPENDA Rais ajaye baada yangu awe bora kuliko mimi.” Ni kauli ya Rais Jakaya Kikwete kwa mabalozi wa Afrika wanaowakilisha nchi zao nchini.
Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya kikazi mjini hapa, alitoa kauli hiyo juzi alipozungumza na wawakilishi hao wa Afrika na kuwaeleza hali ilivyo Afrika kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Kilichomsukuma Rais kuzungumzia mustakabali huo wa uongozi wa taifa, ni swali aliloulizwa na mwakilishi wa Nigeria, Sola Onadije, ambaye mbali na kuupongeza utaratibu wa uongozi wa Tanzania, alitaka kujua kama  ana wazo la kuongeza muda wa kuendelea kuwa madarakani.
“Kipindi changu cha pili cha uongozi kinamalizika mwakani. Nafarijika  kusema nitastaafu nikiwa nimeridhika kabisa na nikijivunia pia juhudi zangu chanya nilizozifanya wakati wa uongozi wangu,” alisema. 
Aliwataka wawakilishi hao wa Afrika kuondoa mawazoni uwezekano wa yeye kuwania madaraka wakati muhula wake utakapomalizika na kusema atajisikia furaha sana atakapokuwa anakabidhi ‘kijiti’ kwa Rais ajaye.
“Urais ni kazi ngumu. Nawashangaa wenye misuli ya kuendelea nao kwa kipindi kirefu,” alisema na kuongeza kuwa kuna uzuri wa kuwa na ukomo wa madaraka.
Alisema ukomo huo unatoa fursa kwa nchi kupata kiongozi mpya, mwenye mawazo mapya na njia mpya za kufikiria kusukuma mbele ajenda za kitaifa.
“Wakati kipindi changu kitakapomalizika, nitapenda kubaki shambani nikilima na kumwachia mwingine aendeleze kazi tuliyokwishaianza. Natamani ajaye awe bora kuliko mimi,” alisema.
Naibu Kiongozi wa Mabalozi hao anayetoka Mauritius, Paul Chong Leung, aliupongeza uongozi wa JK na mchango wake katika kuleta amani na utulivu Tanznia na Afrika kwa jumla na kutolea mfano wa juhudi za hivi karibuni za upatanishi wa mahasimu wa Sudan Kusini.

Mgonjwa wa ebola azua taharuki


NA RODRICK MAKUNDI NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
WANANCHI wa Kata ya Shirimatunda katika Manispaa ya Moshi,  Kilimanjaro, wamepatwa na taharuki kutokana na taarifa za kuwepo  mgonjwa anayedhaniwa kuwa na ebola.
Mgonjwa huyo, ambaye amelazwa katika zahanati iliyoko kwenye kata hiyo, amesababisha huduma kusitishwa na zahanati kufungwa kwa muda huku wagonjwa waliokuwa wakipatiwa matibabu wakihamishiwa katika Ofisi ya Mtendaji wa Kata.
Habari zaidi zimeeleza kuwa mgonjwa huyo, aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), ambapo alisafirishwa hadi kwenye zahanati hiyo baada ya kudai kusikia maumivu makali ya kichwa.
Taarifa hizo zilisema mgonjwa huyo (jina halikufahamika), anayedaiwa ni mzaliwa wa Marangu wilayani Moshi, mwenye makazi yake Dar es Salaam, ameendelea kutibiwa hospitalini hapo na wataalamu wa afya walioko katika zahanati hiyo.
Tayari wataalamu wamechukua sampuli kutoka kwa mgonjwa huyo kwa ajili ya vipimo ili kujiridhisha huku huduma zingine za matibabu zikiendelea kutolewa kwa mgonjwa huyo anayedaiwa kusafiri kutoka nchini Senegal.
Hata hivyo, waandishi wa habari waliofika eneo la tukio walishuhudia watoa huduma za afya katika zahanati hiyo, wakiingia na kutoka ndani ya jengo alikolazwa mgonjwa huyo, ingawa baadhi yao hawakuwa na mavazi rasmi ya kujikinga.
Jopo la wataalamu wa afya likiongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk. Mtumwa Mwako, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Moshi, Dk. Christopher Mtamakaya, na watendaji wengine akiwemo Mkurugenzi wa Manispaa, Shaban Mtarambe, walikutana kwa dharura katika zahanati hiyo.
Mtarambe alipoulizwa kuhusu hali hiyo, alisema hawezi kuzungumza kwa maelezo kuwa suala hilo ni la kitaalamu zaidi linalohitaji wataalamu husika kulizungumzia.
Jitihada za kumpata Dk. Mwako, kutolea ufafanuzi suala hilo hazikuzaa matunda.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kigongoni, Juma Sambeke, alithibitisha kuwepo kwa mgonjwa huyo baada ya kupokea taarifa kutoka viongozi wa wenzake.
Alisema licha ya mgonjwa kufikishwa kwenye zahanati hiyo, uongozi wa kijiji haukuwa na taarifa huku akipokea majibu kutoka ngazi ya manispaa kuwa suala hilo linaratibiwa na mkoa.
Diwani wa Kata ya Shirimatunda, Felix Mushi, alilaumu uongozi wa manispaa kwa uamuzi wake wa kutenga eneo hilo kwa ajili ya wagonjwa wanaohisiwa kuwa na ebola.
Alisema eneo hilo limezungukwa na huduma zote za kijamii, ambapo baadhi ya wazazi wamekuwa na shaka na kuwazuia watoto wao kwenda shuleni.
Zahanati hiyo inakadiriwa kutoa huduma kwa zaidi ya wagonjwa 5,000 kwa mwezi, ambapo takribani wagonjwa 100 walihamishiwa katika ofisi za Ofisa Mtendaji Kata, wakiwemo wale wanaofika kwa ajili ya chanjo ya surua na rubella.

Walimu wagomea mafunzo wakidai posho


Walimu wagomea mafunzo wakidai posho 
NA CHIBURA MAKORONGO, SIMIYU
MAFUNZO kwa ajili ya walimu wa masomo ya sayansi mkoani Simiyu, yameingia dosari baada ya walimu kugoma wakidai posho.
Walimu 200 kutoka wilaya tano za mkoa huo, wanashiriki mafunzo hayo yenye lengo la kuwajengea uwezo, ambapo jana waligoma kuendelea wakitaka kufahamu mustakabali wa posho za kijikimu.
Habari za kuaminika zinasema walimu hao walifikia uamuzi huo baada ya kuhudhuria mafunzo hayo ya siku 10 kwa siku nne mfululizo bila kulipwa, hivyo kuwaweka kwenye mazingira magumu.
Jana, walimu 175 walisusa kuendelea na mafunzo hayo yanayofanyika katika Shule ya Sekondari ya Bariadi, wakitaka ufafanuzi kutoka kwa wakubwa walioandaa mafunzo.
Wakizungumza na waandishi wa habari, walimu hao walisema barua za mwaliko ziliwaeleza semina itakuwa ya siku 10, lakini walishangazwa kupunguzwa siku hizo hadi kufikia tano.
Walisema wamekuwa wakiishi maisha ya shida bila kulipwa posho za kujikimu tangu walipofika huku wahusika wakiwapiga change bila kuwaeleza kinachoendelea.
Mwalimu Masaga Sitta, alisema wanashangazwa na hatua ya uongozi wa mkoa kukataa kuwaona wala kusikiliza kilio chao kuhusiana na posho hizo.
“Tunashangazwa sana na uongozi wa idara ya elimu. Wamekuja  kututelekeza na kutuaibisha tu bila sababu. Ni semina gani isiyotoa mwongozo na maelekezo vizuri kwa washiriki. Wanatupa  shaka na hali hii inatufanya tufikirie fedha zetu zimechakachuliwa,” alisema.
Naye Mwalimu Mujo Meli alisema kitendo hicho si kizuri kwa kuwa kila wanapohoji kuhusu na posho hizo, hutolewa kauli za dharau na kejeli, jambo ambalo ameliita kuwa ni udhalilishaji.
“Tangu tumefika hapa tunadaiwa katika hoteli tunazoishi lakini tumeamua kutoendelea na mafunzo bila kukaidi ila hawatupi majibu ya msingi. Sasa hatushiriki tena mpaka kieleweke,” alisema Meli.
Akizungumza madai hayo, Ofisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Alois Kamamba, alikiri kuwepo kwa mgomo huo akisema umetokana na kuchelewa kwa mhasibu kutoka makao makuu ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
“Ni kweli walimu waligoma na walikuwa na haki kweli ya kugoma maana tangu wamefika katika semina siku ya nne sasa, hatujawalipa kweli na walikuwa wanadaiwa. Tatizo ni mhasibu alichelewa kufika, kwa sasa ameishafika tutawalipa,” alisema Kamamba.