Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Thursday 31 October 2013

Mfumo mbovu wa elimu wafumuliwa


NA SELINA WILSON
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imefuta mfumo wa zamani wa viwango vya upangaji wa alama za ufaulu kwa kidato cha sita na nne, ambapo kwa sasa hakutakuwa na daraja sifuri badala yake kutakuwa na daraja la tano.
Mfumo huo mpya ambao utaanza kutumika mwaka huu kwa kidato cha nne na mwakani kwa kidato cha sita pia watahiniwa wataanza kutumia alama za mitihani na kazi za mradi (project) kuanzia mtihani wa taifa wa kidato cha pili.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome aliwaambia hayo jana, waandishi wa habari kuhusu mabadiliko hayo  ambayo yanalenga kuimarisha mfumo wa elimu nchini na kuweka uwazi kwenye mitihani.
Alisema kuanzia mwaka huu mtihani wa taifa wa kidato cha nne utakuwa alama 60 na alama 40 zitapatikana katika mtihani wa taifa wa kidato cha pili, mitihani ya mitatu ya mihula ya kidato cha tatu na mazoezi ya vitendo.
Akifafanua katika alama hizo 40 za CA, Profesa Mchome alisema mtihani wa taifa wa kidato cha pili utakuwa na alama 15, matokeo ya mihula mitatu ya kidato cha tatu kila mmoja utakuwa na alama tano, mtihani wa majaribio wa kidato cha nne utakuwa na alama 10 na kazi za mradi itakuwa alama tano.
Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea ambao wanarudia mitihani, CA zao zitakazotumika ni zile zilizotoa matokeo ya mtihani wa awali na kwa watahiniwa waliopitia mfumo wa QT matokeo yao ya awali nayo yatatumika CA kwenye mtihani wa mwisho kuchangia alama 60.
Kuhusu viwango vya alama, Profesa Mchome, alisema kutakuwa na alama A, C, D, E na F yatakuwa kwenye kundi moja moja, lakini alama B itagawanywa kwenye makundi mawili kwenye alama B+ na B.
Profesa Mchome alisema mchanganuo wa alama na tafsiri yake utakuwa kama ifuatavyo: Alama A itakuwa na maana ya ufaulu uliojipambanua, B+ itakuwa ufaulu bora sana, B ufaulu mzuri sana.
Alisema alama D itakuwa ni ufaulu wa wastani, E itakuwa ni ufaulu hafifu (Very Low Perfomance) na F ni ufaulu usioridhisha (Unsatisfactory perfomance).
Katika uchambuzi wa matokeo kulingana na alama hizo, alisema A itakuwa na pointi 26 na kwa alama 75 hadi 100, B+ itakuwa na pointi 15 kwa alama  alama 60 hadi 74, B itakuwa na pointi 10 kwa alama 50 hadi 59, C itakuwa na alama 40 hadi 49 na D itakuwa na alama 30 hadi 39 na zote zitakuwa na pointi 10.
Profesa Mchome alisema E itakuwa na alama 20 hadi 29 nayo itakuwa na pointi 10 na F itakuwa na pointi 20 na alama 0 hadi 20, kwa maana ya ufaulu usioridhisha.
Kuhusu madaraja, alisema kuanzia mwaka huu kwa kidato cha nne hakutakuwa na daraja sifuri na badala yake mfumo wa madaraja utaanzia na daraja la kwanza ambalo litakuwa na kundi la ufaulu uliojipambanua na ufaulu bora sana, daraja la pili litakulokuwa na kundi la ufaulu mzuri sana.
Alisema daraja la tatu litakuwa na kundi la ufaulu mzuri na ufaulu wa wastani, daraja la nne litakuwa na kundi la ufaulu hafifu na daraja la tano litakuwa na kundi la ufaulu usioridhisha.
Katika hatu nyingine, Profesa Mchome alisema wizara inatarajia kuanza kutumia muundo wa wastani wa alama katika ufaulu (GPA) mwakani katika matokeo ya mitihani na kuondoa alama S katika mitihani ya kidato cha sita.
Alisema muundo huo mpya utatumika kwa mzunguko wa miaka minne kabla ya haujahuishwa tena ili kutoa muda wa kutosha kuona aina ya changamoto zinazojitokeza na jinsi ya kuzishughulikia.
“Aina hii ya muda itaruhusu vidato vinne vya elimu ya sekondari ya kawaida na nane ya elimu ya sekondari ya juu kupimwa,” alisema na kuongeza  kuwa uhuishaji wa masuala hayo ya mtihani unaweza ukafanyika iwapo matokeo ya kawaida ya uhuishaji wa mitaala, utahitaji pia eneo la mitihani liguswe na kuhuishwa.
Alisema kinachofanyika kwa sasa ni kuendelea kukusanya maoni ya wadau na kufanya maandalizi ili utaratibu huo wa GPA uanze mwakani.
Profesa Mchome alisema mabadiliko hayo ni mwendelezo wa mikakati ya wizara, na kwamba yapo mabadiliko ya mfumo wa mitaala, walimu, mazingira ya kufundishia na kujifunzia, vitabu na vifaa vingine muhimu katika elimu.

Mawaziri watoro walipuliwa bungeni


NA STEPHEN BALIGEYA, DODOMA
WABUNGE wamewajia juu mawaziri watoro kwa kueleza kuwa wanachangia kuzorota kwa mipango ya serikali, kwa kukosekana kwao kusikiliza maoni na ushauri unaotolewa na wabunge.
Hayo yalielezwa bungeni jana na wabunge mbalimbali walipokuwa wakichangia Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka 2014/2015, ambapo hadi inafika saa 12.08, walikuwemo mawaziri kamili saba tu kati ya 29.
Akichangia mpango huo, David Kafulila (Kigoma Kusini - NCCR-Mageuzi), alisema kuwa kitendo cha kukosekana kwa mawaziri bungeni kunachangia serikali kutojua na kufuatilia kwa kina kile kinachoelezwa na wabunge.
Kafulila alisema kitendo hicho husababisha serikali kushindwa kusimamia utekelezaji wa mipango yake kwa kuwa, watu wanaotakiwa kufuatilia utekelezaji huo, hawako makini.
Vilevile, James Mbatia (Kuteuliwa), alisema kitendo kinachofanywa na mawaziri hakikubaliki na kinaonyesha jinsi ambavyo uwajibikaji na umakini haupo katika kusimamia shughuli za serikali.
Mbatia ambaye wakati akichangia kulikuwa na wabunge kamili wanne kabla ya Waziri wa Uchukuzi,  Dk. Harrison Mwakyembe kuingia, alisema hali hiyo imechangia mambo mengi yanayofanywa na serikali kuchukuliwa yale ya miaka ya nyuma na kurudishwa kila mwaka, kwa kuwa watendaji wa serikali hawako makini kusikiliza maoni ya wabunge.
Aidha, Modestus Kilufi (Mbarali - CCM), alisema tabia ya mawaziri kutohudhuria vikao vya bunge kunachangia kutoratibu na kusikiliza maoni ya wabunge, hivyo ushauri mwingi ungeoweza kusaidia kuboresha mipango ya maendeleo kutofanikiwa.
ìKwa nini mawaziri kama wana safari zao wasiwe wanazipanga wakati ambao usio wa Bunge, kwa nini kila bunge linapofika ndipo wanakuwa na safari nyingi?î alihoji Kilufi.
Katika kutoa ufafanuzi wa utoro wa wabunge, Waziri wa Nchi, Ofsi ya Rais asiye na Wizara Maalum, Profesa Mark Mwandosya, kwa niaba ya waziri Mkuu, alisema serikali inachukua maoni yote yanayotolewa na wabunge hata kama mawaziri hawapo bungeni.
ìSerikali inafanya kazi zake kwa taarifa na kila kitu kinachozungumzwa humu hata kama hakuna mawaziri kinachukuliwa na hata sisi wachache tuliopo tunachukua na kuwapelekea mawaziri husika kwa ajili ya kujibu hoja zenu.
Kwa hiyo, naomba wabunge muelewe kuwa maoni na ushauri wenu unachukuliwa, na humu kuna watendaji wengine wa serikali wanachukua maoni hayo, na pia hata makatibu wakuu hawapo hapa, lakini katika ofisi zao kuna televisheni na hivyo wanasikiliza, alieleza.
Katika siku ya kwanza ya kikao cha bunge la mkutano wa 13 ulioanza Jumanne, Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliwataka mawaziri kuhudhuria katika majadiliano yanayofanywa na wabunge kwa kueleza kuwa mpango huo sio wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wasira, bali ni wa serikali nzima.
Nawaomba msije mkaacha kuja kusikiliza maoni na ushauri wa wabunge kwa kufikiri kuwa mpango huu ni wa Wasira, bali mawaziri wote mnahusika na hivyo mnatakiwa kuja kusikiliza na kila mmoja atajibu sehemu yake anayoguswa,î alieleza Makinda.
Lakini pamoja na ushauri huo wa spika katika kikao cha Jumanne wiki hii, mahudhurio ya mawaziri  yamekuwa hafifu kiasi cha wabunge kuona kuwa mipango mingi ya serikali inashindwa kufanikiwa kwa sababu watendaji wake wanakosa kusikiliza ushauri wa wabunge.

Watahiniwa kidato cha nne watajwa


NA SELINA WILSON
WATAHINIWA 427,906 wanatarajiwa kufanya mtihani wa taifa wa kidato cha nne, utakaoanza Novemba 4 hadi 21 mwaka huu.
Kiasi hicho ni pungufu ya watahiniwa 53,508 sawa na asilimia 11.1, ikilinganishwa na watahiniwa waliojiandikisha kufanya mtihani huo mwaka jana, waliokuwa 481,414.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, alisema kati watahiniwa hao, 367,399 ni wa shule za sekondari na 60,507 wanajitegemea.
Alisema kati ya watahiniwa hao, wamo 39 wasioona kati ya 309 wenye uono hafifu ambao wanahitaji maandishi makubwa, ingawa maandalizi yake yamekamilika.
Profesa Mchome alisema kati ya watahiniwa wa shule ya sekondari 198,257 sawa na asilimia 53.96 ni wavulana na wasichana ni 169,142 sawa na asilimia 46.04.
Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea, wasichana ni 30,051 sawa asilimia 49.67 na wanaume ni 30,456 sawa na asilimia 49.67, na kwamba kati yao watahiniwa 18,214 wamejiandikisha kufanya mtihani wa maarifa.
Alisema mtihani huo wa kidato cha nne utafanyika katika shule za sekondari 4,365, vituo 923 vya kujitegemea na vituo 636 vya watahiniwa wa Maarifa (QT).
Akizungumzia maandalizi ya jumla, Profesa Mchome alisema usafirishaji wa mitihani hiyo hadi kwenye ngazi ya mkoa yamekamilika, na kwamba mikoa inaendelea na utaratibu wa kuhakikisha kila kituo kinapata mitihani yake kwa kuzingatia muda ulipangwa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA).
Kuhusu usalama, katibu mkuu huyo alisema hadi sasa hali ni shwari, na kwamba hakuna mtihani uliovuja katika ngazi yoyote, hivyo aliipongeza NECTA kwa kufanikisha maandalizi hayo.
Profesa Mchome aliwataka walimu na wasimamizi wa mitihani kuzingatia utaratibu kama walivyoelekezwa katika semina bila kuwatisha watahiniwa, na kwamba watakaojihusisha na udanganyifu katika mitihani watachukuliwa hatua stahiki.
Aliwataka wazazi, viongozi na jamii kushirikiana  ili kuhakikisha mtihani huo unafanyika katika mazingira salama, tulivu na amani na wakuu wa shule wahakikishe mahitaji yote muhimu yanapatikana.

Lukuvi, Chiku ngoma nzito


SERIKALI imesema imeweka mpango kamambe kuhakikisha kuwa tatizo la maji katika Jimbo la Isimani mkoani Iringa linaondoka kabisa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, aliyasema hayo jana bungeni alipokuwa akitoa ufafanuzi wa tatizo hilo kufuatia swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Chiku Abwao (CHADEMA)
Chiku, alisema jimbo hilo limekuwa na matatizo makubwa ya maji kwa muda mrefu na hivyo, alitaka kujua mkakati wa serikali katika kulitatua tatizo hilo.
“Mimi ni msemaji wa serikali, naweza kujibu swali lolote kama hamjui na kwa taarifa tu, tatizo la maji katika jimbo hilo ambalo mimi ni mbunge wake linashughulikiwa kwa nguvu kubwa,’’ alisema Lukuvi baada ya kupewa nafasi.
Lukuvi, alisema serikali inalifahamu tatizo la maji katika Jimbo hilo na tayari mradi mkubwa wa maji katika Jimbo hilo wenye thamani ya sh. Bilioni 3 umeanza kutekelezwa.
“Mimi nikiwa kama mbunge wa Jimbo hilo la Isimani kwa kupitia vyanzo vyangu mbalimbali, nimesha chimba visima 25 katika jimbo hilo na tunaendelea kuchimba vingine 10,’’ alisema Lukuvi.
Alisema nia ni kuhakikisha kila kijiji katika jimbo hilo kinakuwa na kisima kitakachikuwa kikitoa maji muda wote.
Swali hilo la Chiku, lilikuwa ni la nyongeza kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, kuhusiana na miradi inayotekelezwa na TASAF.


Tanzania yaruka ‘kimanga’ EAC
SERIKALI imesema masuala yanayojadiliwa na kuamuliwa nje ya utaratibu wa Jumuia ya Afrika Mashariki, haiyatambui kama uamuzi wa jumuia na utekelezaji wake utazihusu nchi za Kenya, Rwanda na Uganda pekee.
Pia, imewataka wananchi watambue kuwa, serikali ipo makini katika kufuatilia masuala yanayotokea katika jumuia hiyo.
 Katika kuonyesha umakini huo wa serikali, kwa sasa, imesema ipo katika majadiliano na nchi za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Burundi, kuona namna ya kuanzishwa kwa ushirikiano kama nchi za Rwanda, Kenya na Uganda zikiendeleza mkakati wa kuzitenga baadhi ya nchi wanachama.
Msimamo huo wa serikali ulitolewa juzi na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, mjini hapa, alipomjibu Rukia Ahmed (Viti Maalum -CCM), aliyetaka kujua msimamo wa serikali juu ya mambo yanayohusu Jumuia ya Afrika Mashariki kujadiliwa na kutolewa uamuzi bila Tanzania kushirikishwa.
Rukia, alisema katika mkutano uliofanyika wakati wa ufunguzi wa Bandari ya Mombasa, masuala yaliyojadiliwa ni pamoja na biashara, miundombinu na Shirikisho la Afrika Mashariki kwa kuzihusisha Rwanda, Kenya na Uganda, huku Tanzania na Burundi zikitengwa.
Katika maelezo yake, Sitta alisema tayari Tanzania imeomba ufafanuzi kwa kumtaka Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri anayetoka Uganda, kutoa taarifa ya kina kuhusu mikutano hiyo ya utatu inayoendeshwa sambamba na mikutano ya kawaida ya kalenda ya jumuia.
Aidha, Sitta akijibu maswali ya Hamad Rashid Mohamed (Wawi - CUF) na John Komba (Mbinga Magharibi - CCM) waliotaka kujua kwa nini Tanzania isijitenge na jumuia hiyo na kuunda jumuia yake mpya, alisema wameshaanza majadiliano na DRC na Burundi.
“Mara nyingi matatizo ya Afrika yanachangiwa na viongozi, tunajua kwa nini Rwanda inatununia, lakini wakati ukifika tutachukua hatua, maana tuko makini kulinda maslahi ya taifa letu,” alisema Sitta.
Alisema si kwamba Tanzania imekaa kimya wakati Rwanda, Kenya na Uganda zikianza mchakato wa kuanzisha mambo yao, bali kwa sasa, serikali ipo katika majadiliano na DRC na Burundi wa kutaka kuanzisha ushirikiano.
Akijibu swali la Anne Kilango-Malecela (Same Mashariki - CCM), aliyetaka serikali kutoshiriki tena katika uamuzi wowote mpya katika jumuia mpaka pale mtengamano utakapopatikana, Sitta alisema kazi hiyo tayari imeanza.
“Si kwamba tumekaa kimya kwa utoto huu unaoendelea kufanywa, hatuwezi kuvumilia mchezo huu wa kuigiza, tayari tumeshamwagiza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimatiafa (Bernard Membe), kutoshiriki mkutano wa mawaziri hao watakaokutana kesho (jana) Kigali,” alisema.

Wednesday 30 October 2013

Mbunge CHADEMA ataka wananchi waiamini CCM


NA Stephen baligeya, DODOMA
MBUNGE wa Maswa Magharibi (CHADEMA), John Shibuda, amemwagia sifa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, kwa kumwelezea kuwa kiongozi mtendaji makini, mchapakazi na msikivu katika kushughulikia kero za wananchi.
Pia, alisema CCM ni chama sikivu katika kusikiliza kero za wananchi, hivyo kutakiwa kuwa na imani nacho ili matatizo mbalimbali yaweze kutatuliwa.
Kauli hiyo ya Shibuda, ambaye ni mwanasiasa makini na muwazi, alisema linapokuja suala la maendeleo na uzalendo kwa taifa, inadhihirisha namna CCM na serikali yake wanavyotimiza wajibu katika kuwatumikia Watanzania bila kujali itikadi.
Hayo aliyaeleza wakati wa mkutano wa pamoja kati ya wawakilishi wa wafugaji kutoka wilaya mbalimbali za mikoa ya Dodoma, Mbeya na Morogoro ulioandaliwa na Kinana katika kusikiliza kero zinazowakabili.
Alisema Kinana amekuwa kiongozi mchapakazi na makini katika kazi zake, hivyo kuwataka wafugaji hao kuwa na imani naye katika kushughulikia kero mbalimbali walizozieleza kwake, kwa kuwa ataziwasilisha katika sehemu husika.
ìMwamini huyu na kwa kuwa hata chama anachokiongoza ni sikivu kwa wananchi wake, matatizo yenu ya kukosa sehemu za malisho, migogoro kati yenu na wakulima itatatuliwa kwa haraka,î alieleza Shibuda.
Vilevile, aliwahakikishia kuwa, kwa kuwa katika mkutano huo alikuwepo Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, ambaye amekulia katika nyumba isiyojua dhuluma, basi matatizo yao yatashughulikiwa kwa haraka.
Katika kikao hicho, wafugaji hao walikuwa wakilalamikia ‘Operesheni Tokomeza’ ambayo inalenga kupambana na majangili wa meno ya tembo, ambapo katika operesheni hiyo wafugaji walieleza kunyanyaswa kwa kuchukuliwa mifugo yao, kulipishwa faini kwa kuitwa wahamiaji haramu.
Katika kulishughulikia tatizo hilo, Kinana alieleza kutokana na malalamiko hayo amegundua kuwa, tatizo kubwa lililopo ni kati ya wakulima na wafugaji, wafugaji na hifadhi za taifa na mchakato wa Operesheni Tokomeza.
ìMgogoro kati yenu na wafugaji ni kutokana na nyinyi kudaiwa kuingiza mifugo yenu katika mashamba, lakini pia wakulima kulima sehemu ya malisho ya mifugo. Vilevile, kumekuwa hakuna uhusiano wa karibu kati ya wafugaji na hifadhi, hivyo kuongeza migogoro,î alieleza.
Kinana alisema kuwa Operesheni Tokomeza ina nia njema ya kupambana na majangili wa meno ya tembo, lakini imepata changamoto kadhaa, ikiwemo baadhi ya wanaoiendesha kuvuka mipaka kwa kuonea watu.
Alisema kuhusu malalamiko ya suala hilo, tayari yameshamfikia Rais Jakaya Kikwete na ameshaagiza mawaziri wanaohusika kulishughulikia ili kuondoa kasoro ambazo zimeanza kujitokeza.
ìMimi nimesikia malalamiko na vilio vyenu, nitawasilisha serikalini na kuonana na Waziri Mkuu na nitawaita tena ili mje kusikia ni hatua gani zimechukuliwa katika kushuguklikia matatizo ya wafugaji.
ìBinafsi najua mkipata sehemu ya malisho, majosho na mabwawa hamtakuwa mnahamahama na kuitwa wahamiaji haramu, hivyo ni wajibu wa serikali kuhakikisha miundombinu ya maji, majosho na kutenga sehemu ya malisho,î alieleza.
Alisema Kamati Kuu ya CCM iliyopita iliona tatizo la wafugaji na wakulima na kuitaka serikali kulifanyia kazi na kwa kuwa yeye ni mtendaji wa Chama, atahakikisha anasimamia serikali kwa kuwa ndio wajibu wake kutekeleza Ilani ya Chama.
Dk. Nchimbi alieleza kuwa tayari mawaziri watatu wameshakutana ili kuona kasoro zilizoanza kujitokeza katika operesheni hiyo ili kuziondoa na kutoleta usumbufu kwa wananchi.

Shehena ya pembe za ndovu yanaswa


Na Tamimu Adam - Jeshi la Polisi
WAKATI taifa likiwa kwenye mjadala mkali na kampeni ya kusaka majangili nchini, polisi imekamata pembe 90 za ndovu zenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni moja.
Habari za kuaminika zinasema kuwa, pembe hizo zilikamatwa jana zikiwa kwenye gari aina ya Toyota Carina, iliyokuwa ikitokea Tunduru kwenda Masasi.
Hata hivyo, baada ya kunaswa, watuhumiwa walijaribu kumshawishi askari kumpa kiasi cha sh. milioni tatu ili aweze kuwaachia, jambo ambalo hakulifiaki, ndipo waliporuka kwenye gari na kukimbia. Pembe 90 ni sawa na tembo 45, ambao watakuwa wameuawa kwenye hifadhi za Taifa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen, alisema gari hiyo lilikamatwa katika Kata ya Maendeleo, baada ya polisi waliokuwa doria kuitilia shaka.
Alisema baada ya kuitilia shaka walimwamuru dereva kusimama na kuanza kufanya ukaguzi, ambapo kabla walimtaka kuonyesha leseni yake, ambayo hata hivyo hakuwa nayo.
Kutokana na hatua hiyo, askaru polisi hao waliamua kuchukua hatua zaidi ya kulikagua gari hilo, ndipo walipokuta shehena ya pembe hizo zikiwa zimehifadhiwa kwenye mifuko.
ìWatuhumiwwa hawa walijaribu kutaka kumuhonga askari aliyewakamata, lakini alikataa ushawishi huo na kuwafikisha kituoni. Huu ndio uzalendo na uadilifu,” alisema Kamanda Zelothe.
Alisema polisi inalishikilia gari hilo kwa hatua zaidi, huku wahusika wakiendelea kusakwa ili waweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Katika ukaguzi huo, gari hilo lilikutwa na vitu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na simu ya kiganjani, mizani na nyaraka mbalimbali za benki.
Hata hivyo, taarifa za awali zinasema kuwa dereva wa gari hilo amebainika kuwa Oliver Lucas mkazi wa Masasi, huku mwenzake akiwa bado hajatambulika.
Pia, Kamanda Zelothe alisema kuwa, kigogo mwenye mzigo huo ametambuliwa kwa jina la Hassan Koko maarufu kama Twalib Nyoni.
Mapema juzi, mvutano mkali uliibuka bungeni kutokana na Kangi Lugola (Mwibara - CCM), kuibana serikali akitaka iwataje vigogo wanaohusika na ujangili.
Katika majadiliano hayo bungeni, ilielezwa kuna taarifa kuwa baadhi ya mawaziri, wabunge na maofisa wa vyombo vya usalama nchini, wanadaiwa kuhusika kwenye vitendo vya ujangili wa wanyama, hususan tembo na faru, ambao kwa sasa wapo kwenye hatari ya kutoweka.

January awapigia debe walima chai


Na mwandishi wetu, Bumbuli
NAIBU Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, ametoa wito kwa viwanda vya chai vya Herkulu na Dindira kuongeza uzalishaji.
Lengo ni kutaka wanunue zao hilo kwa wingi toka kwa wakulima wa chai wa Bumbuli, ambao awali walikuwa wakihudumiwa na Kiwanda cha Mponde.
Kiwanda cha chai cha Mponde kimefungwa kufuatia mgogoro baina ya wakulima wa chai na Chama cha Wakulima wa Chai cha Usambara (UTEGA) na mwekezaji.
January, ambaye pia Mbunge wa Bumbuli alikuwa akizungumza na wakulima katika Kijiji cha Tamota hivi karibuni.
Alisema hivi sasa majani ya chai ni mengi, hivyo hatua ya viwanda hivyo kuongeza uzalishaji itawapatia unafuu wakulima.
Hata hivyo, alisema amekwisha zungumza na uongozi wa viwanda hivyo, ili viongeze uzalishaji na vifaa vya kusafirishia chai hiyo kutoka shambani hadi kwenye viwanda.
January, alitoa wito pia kwa wakulima, kuwa wavumilivu wakati huu ambapo kuna mpango wa kuweka menejimenti ya muda kama ilivyokubaliwa na serikali, ili kiwanda
hicho kianze kazi ya usindikaji.

Mama wa mtoto aliyeathirika akili adai kutishwa


NA RABIA BAKARI
SAKATA la mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Newala mkoani Mtwara, Salim Shamte, kudaiwa kuathirika akili kutokana na kipigo cha mwalimu wake, limechukua sura mpya.
Shamte anadaiwa kupigwa na mwalimu wake wa darasa, Fredrick Kapinga, kwa kile kilichoelezwa kuwa deni la sh. 300 alilotakiwa kulipa baada ya wanafunzi wa darasa hilo kupoteza vitabu viwili.
Hatua hiyo imetokana na mama wa Shamte, Vena Lupaso, kuanza kupokea vitisho kwa lengo la kumnyamazisha asiweze kupaza sauti kudai haki.
Kwa wiki kadhaa sasa, gazeti hili limekuwa likiripoti tukio hilo, ambapo juzi usiku, Vena alipokewa simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Akizungumza na gazeti hili jana, Vena alisema ofisa huyo wa TAKUKURU, alijitambulisha kwa jina la Eva Mushi na kumweleza kuwa, wamekuwa wakimuona akilalamika katika vyombo vya habari na kumtaka aache kufanya hivyo.
Alisema ofisa huyo alimtaka kwenda katika Bodi ya Shule ili aweze kupatiwa msaada badala ya kulalamika na kuahidi kuwa yeye na maofisa wenzake wa TAKUKURU watamtafuta ili kuzungumzia suala hilo na namna ya kulipatia ufumbuzi.
"Aliponipigia alijitambulisha kwa jina la Eva Mushi, hivyo alipokata simu niliangalia jina la mmiliki wa namba hiyo na kukuta imesajiliwa kama Suzana Kapinga, nikagundua kuna mchezo mchafu nimeanza kufanyiwa," alisema.
Alisema, baada ya kukumbwa na wasiwasi huo, akihofiwa mwanaye kuwa anaweza kudhurika zaidi, alikwena kutoa taarifa kituo cha polisi kwa hatua zaidi.
"Jana (juzi), nilienda Kituo cha Polisi Tabata, na kupewa RB namba TBT/RB/3068/2013, ikiwa kuna jambo lolote litaendelea," alisema.
Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara, Zelothe Steven alisema bado anafuatilia suala hilo na atalitoa tamko.

Mkono uliokuwa ukiuzwa mtaani


ni wa mwanafunzi
NA PETER KATULANDA, MWANZA
MKONO wa binadamu, ambao walikamatwa nao watu watatu, wakiwemo waganga wa kienyeji wawili na mfanyabiashara mmoja, umebainika kuwa wa kijana wa miaka 11 (jina linahifadhiwa), ambaye kwa sasa amelazwa akipatiwa matibabu.
Habari za kuaminika zimesema kuwa, kijana huyo alikatwa mkono wakati akijaribu kumuokoa mama yake mzazi walipovamiwa na watu wasiojulikana nyumbani kwao.
Oktoba 24, mwaka huu, watu wasiojulikana walimvamia mama wa kijana huyo, Dotto Luchagula (60) na kumshambulia kwa mapanga hadi kufa kwa kile kilichodaiwa imani za kishirikiana, ambapo mwanaye huyo alijaribu kupambana ili kumwokoa ndipo naye akakatwa kiungo hicho.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa, Joseph Konyo, alisema kijana huyo alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kongolo iliyopo wilayani Magu.
“Kijana huyu alikatwa mkono wake wa kulia wakati akijaribu kumuokoa mama yake aliyevamiwa na kuuawa kikatili kwa kucharangwa mapanga nyumbani kwake Kijiji cha Kongolo katika Kata ya Nyabusu wilayani Magu,” alisema.
Aliongeza kuwa hadi jana jioni, kijana huyo alikuwa bado amelazwa hospitalini (jina linahifadhiwa kwa usalama wake zaidi) akipatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri.
Watuhumiwa hao walitiwa mbaroni juzi, saa tisa alasiri, katika eneo la kati ya ufukwe wa Ziwa Victoria na Uwanja wa Ndege wa Mwanza, wakiwa kwenye harakati za kukiuza kiungo hicho kwa gharama ya sh. milioni 100.

Mtumishi KADCO apigwa risasi akidhaniwa jambazi


NA SHAABAN MDOE, ARUSHA
POLISI waliokuwa lindo katika benki ya CRDB tawi lililopo katika jengo la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), jijini hapa, wamemjeruhi kwa kumpiga risasi begani mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Violeth Mathias (33).
Inadaiwa kuwa walihisi mwanamke huyo mkazi wa Njiro, alitaka kutekeleza tukio la ujambazi katika benki hiyo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Alisema lilitokea jana saa 6.45 mchana, wakati mwanamke huyo ambaye ni mtumishi wa shirika la uwakala wa uendeshaji wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KADCO), alipofika katika eneo hilo akiwa na gari aina ya Toyoto Mark, lenye namba za usajili T888 BWW.
Kamanda Sabas, alisema Violeth alifika na gari hilo na kupaki mbele ya mlango mkuu wa kuingilia katika benki hiyo jambo lililowasababisha askari hao kumuamuru kulisogeza gari lake mbele ili kupisha njia, lakini aligoma.
Alisema baada ya kugoma, askari hao walimlazimisha kwa nguvu na ndipo  kulizuka zogo kubwa na kisha askari hao waliamua kutoa upepo katika magurudumu ya gari hilo ili kumdhibiti.
Kamanda huyo, alisema kufuatia kitendo hicho cha gari lake kutolewa upepo, Violeth alishuka kwenye gari na kuchomoa bastola yake katika pochi, huku akimuelekezea mmoja wa askari hao kwa lengo la kumdhuru.
Ndipo askari mwingine aliamua kujikinga kwa kumfyatulia risasi mwanamke iliyompata katika bega la mkono wa kushoto.
Kamanda Sabas, alisema baada ya risasi hiyo kumpata, alianguka chini na walimkamata na kumpeleka katika Kituo cha Polisi Kati, jirani kabisa na benki hiyo kwaajili ya kuandikisha maelezo na kisha alipelekwa Hospitali ya Mount Meru akiwa chini ya ulinzi kwaajili ya matibabu.
Kamanda Sabas, alisema kwa mujibu wa sheria, hairuhusiwi gari lolote kusimama mbele ya lango kuu la kuingilia benki, kitendo kilichofanywa na mwanamke huyo.
 “Na hata pale alipoelekezwa cha kufanya alikaidi,” alisema Kamanda huyo.
Hata hivyo, Kamanda Sabas alisema kufuatia tukio hilo, Polisi wanaendelea kumshikilia  mwanamke huyo pamoja na mwenzake aliyekua naye kwenye gari kwaajili ya upelelezi zaidi.
“Askari wamekueleza ondoa gari, hapo hairuhusiwi kuegesha halafu wewe unakaidi na kisha unataka kuwapiga askari kwa risasi kama kweli huna nia mbaya.
“Tunamshikilia yeye na mwenzake mmoja kwa upelelezi zaidi ili tujiridhishe na tujue dhamira yao ilikuwa nini,” alisema Kamanda Sabas.

Babu Seya, Papii waiangukia mahakama


NA FURAHA OMARY
WAKILI Mabere Marando, amedai Mahakama ya Rufani, iliteleza kisheria katika uamuzi wake ambao uliwatia hatiani  na kuwahukumu kifungo cha maisha mwanamuziki Nguza Vikings au 'Babu Seya' na mwanawe Johnson Nguza 'Papii Kocha'.
Marando alidai jana mbele ya jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani lililotoa hukumu hiyo, likiongozwa na Jaji Natharia Kimaro, kwamba mahakama iliteleza kwa kutozingatia miongozo ya kisheria ya nanma ya kuchukua ushahidi wa mtoto, kutoitwa kwa mashahidi muhimu. Mbali na Jaji Nathalia, Majaji wengine ni Mbarouk Mbarouk na Salum Massati.
Wakili huyo, alidai hayo wakati wa kusikilizwa kwa maombi ya mapitio ya hukumu hiyo, iliyotolewa Februari, 2010, Jopo hilo liliwatia hatiani Babu Seya na mwanawe Papii na kuwapa adhabu ya kifungo cha maisha. Jopo hilo liliwaachia huru watoto wengine wa Babu Seya, Nguza Mbangu na Francis Nguza.
Marando alidai mahakama hiyo ilijiridhisha kulikuwa na makosa katika kupokea ushahidi wa watoto na kwa sababu matakwa ya sheria hayakufuatwa hivyo ushahidi huo ulipaswa kufutwa na waleta maombi kuachiwa.
"Mlikubaliana na sisi kwamba Mahakama ya Kisutu ilikosea haikuzingatia uchukuaji wa ushahidi lakini mlisema ilimradi kuwe na ushahidi wa kuunga mkono. Sisi tulisema hapana,"alidai.
Pia, alidai mahakama hiyo, ilikosea katika hukumu yake kwa  kusema  kuna shahidi wa 13 aliyedai kwenye nyumba ya Babu Seya kuna mlango wa siri ambao mtu anaweza kuingia na asionekane, ushahidi ambayo haupo na wala shahidi huyo hakusema hivyo.
"Mashahidi walisema wao waliona katika nyumba ya Babu Seya kuna milango miwili wa mbele na nyuma na yote inainghia sebuleni, mtu huwezi kuingia katika chumba chochote bila kupitia sebuleni
"Sasa katika ukurasa wa 38 wa hukumu yenu, mmetamka kwamba shahidi wa 13 aliiambia mahakama kuna mlango fulani wa kuingia katika nyumba bila ya mtu mwingine kukuona. Ushahidi huo haupo katika ushahidi wa shahidi wa 13 hawakusema. Haya ndiyo mambo yanayojidhihirisha kuna kuteleza," alidai Marando.
Aidha, alidai katika ushahidi wa mashahidi wanaohusika na ushahidi uliowatia hatiani Babu Seya na Papii Kocha, walidai walikuwa wakiingia katika nyumba hiyo wakitokea dukani kwa Mangi ambaye alikuwa akijua kinachotokea.
Marando alidai kwa mujibu wa sheria, upande wa Jamhuri ulipaswa kumleta Mangi ambaye ni shahidi muhimu ili aje kuthibitisha, lakini katika hukumu yao walisema upande huo una hiari wa kumuita shahidi wanayemtaka, kauli ambayo ni kinyume cha sheria.
Alidai kuna kijana anaitwa Size ambaye anadaiwa alikuwa anawakusanya watoto wa kike na kuwapeleka kwa Babu Seya na kufanya kinachodaiwa kutendeka, lakini hakuitwa na wala mahakama hiyo katika hukumu haye haimkumzungumzia.
Hoja nyingine, Marando anadai mahakama hiyo, iliteleza kwa kutotoa maoni yake juu ya utetezi wao, kuhusu uwepo wa watu katika nyumba ya Babu Seya, ambao walidai ingekuwa si rahisi watoto kuingia bila ya wao kuwaona kwa kuwa kuna milango miwili ambayo inaingia sebuleni.
"Naomba mpitie tena hukumu yenu na kurekebisha mambo ninayoona yana makosa ya kiuterezi na mkikubaliana nasi mfute washitakiwa kutiwa hatiani na mfute adhabu zao," aliomba Marando.
Upande wa Jamhuri ulikuwa ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Jackson Bulashi, akishirikiana na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Mwangaza Mwipopo, Emmaculata Banzi, Joseph Pande na Wakili wa Serikali Apimaki Mabrouk.
Wakili Bulashi aliiomba mahakama hiyo, kutupilia mbali maombi hayo kwa sababu yalishatolewa uamuzi katika rufani waliyokata waleta maombi. Alidai kwa upande wao wanaona hakuna makosa yaliyofanywa katika kufikia uamuzi huo na kwamba kilichowasilishwa ni sababu za rufani ambazo tayari zilishatolewa uamuzi.

Jopo la Majaji lilisema kuwa limesikia hoja za pande zote na kwamba wataarifiwa tarehe ya kutolewa uamuzi. Awali, jopo hilo lilitupilia mbali maombi ya mapitio yaliyokuwa yamewasilishwa na Babu Seya na Papii Kocha mwenyewe kwa msaada kutoka gerezani, kwa kuwa hawakutumia vifungu sahihi kuyawasilisha.

Tuesday 29 October 2013

DARAJA LA KIKWETE LAKAMILIKA


WANANCHI wa mikoa ya Kigoma, Tabora na mingine ya jirani sasa watasafiri kwa raha mustarehe kutokana na kukamilika kwa sehemu kubwa ya barabara na Daraja la Kikwete, lililojengwa katika Mto Malagarasi, mkoani Kigoma. Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli, alifanya ziara kukagua ujenzi huo kama msafara wake unavyoonekana pichani. (Picha na Martin Ntemo).

CHADEMA yapasuka


Na waandishi wetu
HALI imezidi kuwa tete ndani ya CHADEMA kufuatia aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, kuanza kufichua madudu yaliyoota mizizi na udhaifu wa viongozi.
Mwigamba, ambaye mwishoni mwa wiki iliyopita alishushiwa kipigo na viongozi wenzake kisha kusimamishwa uanachama kwa tuhuma za usaliti, amesema baadhi ya wajumbe wa kamati kuu na wenyeviti wa mikoa 12 wametangaza kumuunga mkono.

Akizungumza na Uhuru kwa njia ya simu jana, Mwigamba amesema viongozi wenzake hao wamesema watamuunga mkono, na kwamba wamekuwa wakikerwa na uozo na madudu yanayofanyika ndani hya CHADEMA.
Bila kuwataja viongozi walimpigia simu na kumpongeza kwa uamuzi wa kuweka mambo hadharani na kutangaza kumuunga mkono, Mwigamba amesema wanachama na baadhi ya viongozi hawaridhishwi na mambo yanavyokwenda, lakini wanashindwa kusema kwa kuogopa kushughulikiwa.
Amesema wajumbe watano wa kamati kuu, wenyeviti wa mikoa 12 Bara na Zanzibar pamoja na wenyeviti wa wilaya zaidi ya 20 na makatibu wao, wamemweleza amechukua uamuzi sahihi wa kuwapsha viongozi kuhusu udhaifu, ikiwa ni pamoja kukifanya chama hicho kama taasisi binafsi.
“Ndio nimeanza kazi ya kukisafisha chama kwa maslahi ya wanachama wote na Watanzania, mambo yanayovyokwenda si sawa na tukiendelea hivi tukipewa nchi tutaiharibu na kuwafanya watu wajute.
“Viongozi wenzangu wametangaza kuniunga mkono na wako nyuma yangu licha ya wachache kuniita msaliti kwa kusema ukweli,’’ alisema Mwigamba.
Pia, alisema bado ana siri nyingi kuhusu madudu yanayoendelea ndani ya CHADEMA, na kwamba viongozi wakiendelea kumdhalilisha kwa kumwita msaliti licha ya kumshushia kipigo, ataweka hadharani yote.
“Kwa muda mrefu nimekuwa mwanachama na kiongozi mzalendo kwa chama changu, lakini viongozi wachache mamluki wameamua kunidhalilisha na kuniangamiza, kabla ya kunifukuza makao makuu nilikuwa mhasibu, hivyo uchafu wote naujua,’’ alionya Mwigamba.
Hata hivyo, Mwigamba amesema kuwa baadhi ya wanachama wachache ambao anaamini hawafahamu uchafu unaofanyika ndani ya CHADEMA, wamempigia simu na kumtuhumu kutaka kukisambaratisha chama.
Amesema viongozi na wanachama wa mikoa ya Arusha, Manyara, Singida, Shinyanga, Mara, Tabora na hata sehemu kubwa ya Zanzibar, wamempigia na kumweleza wako pamoja, lakini wachache wamemlaumu kwa uamuzi wake huo.
“Wengi wanaumia na mambo yanavyokwenda katika hiki chama, kwa nje kinaonekana kisafi, lakini ndani kimeoza. Kuna ukiukwaji mkubwa wa Katiba, hakuna uchaguzi na mbunge wa jimbo anatoka Arusha ila viti maalumu anapewa wa Kilimanjjaro,’’ alisema na kuongeza:

“Hawa si kosa lao, kwani hawaingii ndani ya vikao, wanachofahamu ni kutakiwa kukunja ngumi na kupiga kelele tu, vinginevyo wangenielewa hiki ninachokisema”.
Afichua madudu ya Lema Arusha
Mwigamba ameweka bayana kuwa kuna hatari kubwa ya CHADEMA kupoteza jimbo la Arusha kutokana na ahadi zilizotolewa na Mbunge wa Jimbo hilo Godbless Lema, kutotekelezwa huku kukiwa na visingizio mbalimbali.
Amesema Lema anadaiwa ahadi nyingi, ikiwemo ujenzi wa Machinga Complex alioliahidi kwa wafanyabiashara, hospitali ya kinamama na watoto, kuhamisha kituo cha mabasi ya mikoani kutoka Mjini kwenda Kisongo na mengine mengi.
Hata hivyo, amesema ahadi hizo haziwezi kutekelezwa kutokana na Lema kubeba ajenda za ubabe na fitina na kuacha maendeleo kwa wapigakura wake.

Asisitiza kumvaa Mbowe
Mwigamba, ambaye juzi alilalamika kuwa alishambuliwa na viongozi wenzake, huku Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, akishuhudia, amesema kamwe hatasita kumweleza udhaifu wake katika uongozi.
Amesema Mbowe alishuhudia mwanzo hadi mwisho wakati akishushiwa kipigo kabla ya kukabidhiwa kwa polisi, na kwamba kamwe hilo haliwezi kumfunga mdogo kueleza mfumo mbovu wa uongozi ndani ya chama hicho.

UVCCM yatoa siku 21 kwa Waziri Chiza


Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI wa Kilimo, Chakula na Ushiriki, Mhandisi Christopher Chiza, amepewa siku 21 kuwasilisha taarifa kwa umma kueleza hatua zilizochukuliwa na wizara yake kuwakomboa wakulima wa korosho dhidi ya walanguzi.
Pia, ametakiwa kueleza sababu za kuyumba kwa bei ya korosho, kuchelewa kwa malipo pamoja na tozo nyingi walizowekewa wakulima wa korosho kunakosababisha na udhaifu na ukosefu wa maadili ya baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika.
Agizo hilo limetolewa na Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), baada ya kukutana na kujadili kwa kina masuala yote yanayohusu korosho na changamoto zinazowakabili wakulima wa zao hilo nchini.
Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda, aliwaeleza waandishi wa habari mjini hapa, jana kuwa, kuyumba kwa bei ya korosho pamoja na kuchelewa kwa malipo kumekuwa kukirudisha nyuma maendeleo na harakati za wakulima nchini katika kupambana na umasikini.
Alisema kamwe UVCCM haiwezi kuvumilia mambo yanavyokwenda katika korosho kwa sasa, na kwamba watahakikisha kero hiyo ambayo inawakabili wakulima wengi inapatiwa ufumbuzi na serikali kupitia watendaji waliopewa jukumu la kusimamia.
“Baraza linamtaka Mhandisi Chiza kufanya uamuzi wa dharura wa kushughulikia matatizo hayo ndani ya siku 21 na kutoa taarifa kwa umma kuhusu hatua zilizochukuliwa ili kuwaokoa wakulima wa korosho na unyonyaji unaofanywa na walanguzi na pamoja wajanja wachache,’’ alisema Sixtus.  
Pia, alisema Baraza Kuu limeiagiza serikali kuachana na mipango isiyotekelezeka, ikiwa ni pamoja na kodi ya laini ya simu za mkononi ambayo inatozwa sh. 1,000 kwa mwezi, kwani itakuwa na madhara makubwa iwapo itatekelezwa kwa kuwa waathirika watakuwa watu wa kipato cha chini.
Katika kikao chake kilichoketi juzi, Baraza hilo limemteua Paul Makonda kuwa Mkuu wa Idara ya Chipukizi na Uhamasishaji, Zainab Athuman Katimba kuwa Mkuu wa Idara ya Organizesheni na Siasa na Omar Seleman kuwa Mkuu wa Idara ya Utawala, Uchumi na Fedha.

Watano wanaswa na mkono wa binadamu


Mwanza, waganga wa kienyeji
NA PETER KATULANDA, MWANZA
WATU watatu wakiwemo waganga wawili wa kienyeji, wametiwa mbaroni kwa kukutwa na kiungo cha mkono wa kulia wa binadamu, wakiwa kwenye harakati za kukiuza.
Watuhumiwa hao walikamatwa juzi, saa tisa alasiri, katika eneo la kati ya ufukwe wa Ziwa Victoria na Uwanja wa Ndege wa Mwanza, kutokana na taarifa za raia wema, ambapo polisi waliweka mtego kama wanunuzi na kufanikiwa kuwanasa.
Habari za kuaminika zinasema, miongoni mwa watuhumiwa hao yumo mfanyabiashara maarufu jijini hapa, ambaye amekuwa akishirikiana na waganga kufanya biashara hiyo haramu.
Habari zilizothibitishwa na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa, Joseph Konyo, watuhumiwa walipokuwa wakikinadi kiungo hicho waliwaeleza wanunuzi (polisi) kuwa wana kila aina ya viungo ambavyo watahitaji.
Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa, Ernest Mangu,, Konyo alivitaja baadhi ya viungo vya binadamu ambavyo watuhumiwa hao walidai wanavyo kuwa miguu, kichwa na sehemu za siri za mwanamke au mwanamme.
Alisema kabla ya kunaswa, mchakato wa biashara hiyo ulichukua takriban wiki mbili na wauzaji walitaka kupatiwa sh. milioni 100 kwa kiungo kimoja, ambapo walitakiwa kupunguza kidogo, ikiwa ni pamoja kuonyesha kiungo hicho na kupanga eneo mwafaka la kufanyika kwa biashara hiyo.
“Kiungo hicho kilikuwa bado kibichi kabisa na ni cha binadamu, walikihifadhi kwenye begi ambalo ndani yake ulikuwa umewekwa kwenye mfuko wa Rambo uliofungwa kwa ustadi mkubwa,’’ alisema Konyo.
Hata hivyo, polisi walipata wakati mgumu kudhibiti baadhi ya wananchi waliokuwa jirani na eneo hilo, ambao walishtushwa na tafrani ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao.
Wananchi hao walitaka kuwashambulia na kuwaua watuhumiwa hao baada ya kugundua walikuwa na kiungo cha binadamu.

Diwani CHADEMA kortini kwa wizi


Na Nathaniel Limu, Singida
DIWANI wa kata ya Iseke (CHADEMA), Emmanuel Jingu, amepandishwa kizimbani kujibu mashitaka ya kuvunja ofisi ya kijiji  cha Nkhoiree na kuiba vifaa mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya sh. 200,000.
Jingu alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya  Hakimu Mkazi Singida na kusomewa mashitaka na Wakili Petrida Muta, mbele ya Hakimu Asha Mwitendwa.
Muta alidai mshitakiwa alitenda makosa hayo, Septemba 20, mwaka huu, saa 8.30 mchana, ambapo alivunja nyumba kwa lengo la kuiba mali.
Ilidaiwa mshitakiwa huyo, baada ya kuvunja mlango wa nyumba inayotumiwa na serikali ya kijiji cha Nkhoiree, aliiba vifaa mbalimbali vyenye thamani ya sh. 298,000.
Mshitakiwa huyo alidaiwa kuiba vocha, vitabu vya risiti, kitabu cha malipo, risiti za ushuru, hati za malipo, vitabu vya ushuru, risiti za zahanati  na madumu matupu 100.
Jingu alikana mashitaka na alirudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Masharti ya dhamana ni kuwa na mdhamini mmoja atakayetia saini bondi ya sh. 500,000. Kesi hiyo itatajwa Novemba 11, mwaka huu.

Membe aongoza mamia kumuaga Balozi Sepetu


NA RACHEL KYALA
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, jana aliongoza mamia ya waombolezaji kuuaga mwili wa marehemu Balozi Isaac Sepetu unaotarajiwa kuzikwa leo kijijini kwao Mbuzini, Zanzibar.
Akizungumza wakati wa shughuli hiyo nyumbani kwa marehemu Sinza, Dar es Salaam, Waziri Membe alisema Taifa limepoteza kiongozi mzuri na mwenye uzoefu mkubwa katika kazi aliyewaheshimu, kuwapenda na kuwathamini watu wote.
“Marehemu ameacha majonzi kwa watu wake, kwani alikuwa kiongozi mchapakazi na mwadilifu, alikuwa mfano wa kuigwa, amefanya mengi mazuri kwa nchi yake na ameondoka bila dosari yoyote katika utumishi wake,” alisema.
Aidha, Waziri Membe aliongeza kuwa, marehemu alikuwa mtu aliyekataa mabaya kwa nguvu zake zote, hususan suala la rushwa na atakumbukwa daima na watu wote.
“Natoa pole kwa familia na ninawaombea ndugu, jamaa na marafiki wote Mwenyezi Mungu awape nguvu haraka ili kuweza kuendelea na ujenzi wa taifa,” alisema.
Viongiozi wengine walioeleza jinsi walivyomfahamu marehemu ni Mama Getrude Mongela, ambaye alisema kuwa katika maisha yake ya siasa alikuwa mtu mwadilifu na aliyechukia majungu.
Marehemu Balozi Sepetu alizaliwa Oktoba 16, 1943 wilayani Sikonge, Tabora na baadaye alichukuliwa na baba yake mkubwa mareheu Said Sepetu Kilanga na kuhamia visiwani Zanzibar alikokulia na kusoma shule.
Mwaka 1952 hadi 1963, marehemu alisoma elimu ya msingi na sekondari katika shule ya St. Joseph’s (Tumekuja), Zanzibar ambapo mwaka 1964 hadi 1970 alipata Shahada ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Berlin, Ujerumani.
Mwaka 1971 hadi 1972 aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi, Zanzibar.

Askofu Mkude atia neno Katiba Mpya


na mwandishi wetu
ASKOFU wa Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro, Mhashamu Telesphory Mkude, amemsifia na kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuanzisha, kusimamia na kuongoza vizuri mchakato wa kutungwa kwa Katiba mpya nchini.
Pia, amewataka wananchi badala ya kukaa na kulalamika, wajitokeze kutoa maoni yao ili kuboresha mchakato huo utakao iwezesha Tanzania kupata Katiba nzuri itakayoiongoza kwa miaka mingine 50 ijayo.
Aidha, Askofu Mkude, amemwelezea Rais Kikwete kama kiongozi wa mfano ambaye anawajali wananchi na kushirikiana  nao katika kujitafutia maendeleo.
Aliyasema hayo katika sherehe za Jubilee ya miaka 100 ya Parokia ya Lugoba, iliyopo Bagamoyo mkoa wa Pwani.
Sherehe hizo zilifanyika mwishoni mwa juma lililopita katika Kanisa la Msalaba Mtukuka.
Askofu Mkude, aliwaambia mamia ya waamini na wakazi waliojitokeza kuhudhuria sherehe hizo kuwa, katika eneo hilo, kuna shule ambayo Rais Kikwete alisoma mwanzoni mwa miaka ya 1960.
“Umefanya mengi sana wakati wa kipindi cha uongozi, lakini moja ya mambo hayo makubwa ni kuanzisha, kusimamia na kuongoza mageuzi makubwa ya kutungwa kwa Katiba mpya katika nchi yetu. “Tunakupa heko sana kwa kusimamia jambo hili ambalo litatuwezesha sote kupata Katiba inayotokana na ridhaa ya wananchi,” alisema.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria sherehe hizo ni Askofu Anthony Banzi wa Jimbo Katoliki la Tanga.
Akizungumzia nafasi ya wananchi katika mchakato huo, Askofu Mkude alisema: “Tuache kunung’unika. Tutoe maoni ya kuiboresha. Si viongozi wengi wanatoa nafasi kama hii duniani kwa wananchi wao kushiriki katika kujadili Katiba yao wenyewe. Kama asingependa, Rais Kikwete angeweza kubakia na Katiba ya sasa ambayo ni nzuri pia.”
Kuhusu suala la amani, alisema ni muhimu kwa Watanzania kumuunga mkono Rais Kikwete kwa kuilinda na kuitetea badala ya kuivuruga.
Hata hivyo, alisema wapo miongoni mwa Watanzania ambao pengine hawaelewi maana ya amani, wameamua kuanzisha harakati za kutaka kuisambaratisha.
Aliwaonya watu hao kuacha mara moja mchezo huo, kwani ni hatari kwa maisha yao nay a Watanzania wote.
Mbali na kusoma katika Shule ya Kati ya Lugoba kati ya mwaka 1962 na 1965 wakati huo ikiitwa ‘St. John Bosco’s Lugoba Middle School’ iliyokuwa inamilikiwa na Kanisa Katoliki, Rais Kikwete amekuwa akichangia maendeleo ya shule na Parokia hiyo ya Lugoba mara kwa mara.
Kabla ya kilele cha sherehe hizo, Rais Kikwete alizindua rasmi zahanati ya Kanisa ambayo aliifanyia ukarabati na aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa ukumbi ambao unajengwa na Parokia hiyo kwa gharama ya sh. milioni 200.
Parokia ya Lugoba ilianzishwa miaka 100 na Mapadri wa Cornel na Herman, kwa kushirikiana na wenyeji akiwemo mtawala wa eneo hilo wakati huo, Mzee Kinogile.

Ngeleja azamisha jahazi la CHADEMA


NA PETER KATULANDA, SENGEREMA
VIJANA 38 wakiwemo wapiga debe wa daladala wa Kamanga Ferry, Kata ya Nyamatogo wilayani Sengerema, wametimka kutoka vyama vya CHADEMA na CUF na kujiunga na CCM.
Wamedai kuvutiwa na sera za Chama zilizotangazwa na Mbunge wa Jimbo la Sengerema, William Ngeleja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Anthon Diallo.
Walivihama vyama hivyo hivi karibuni na kuanzisha kikundi cha ujasiriamali cha Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), tawi la Kamanga, kwa madai kuwa wamechoshwa kutumiwa katika maandamano yasiyokuwa na tija, yenye lengo la kuwagawa Watanzania.
Wakizungumza katika kikao maalum cha maandalizi ya uzinduzi wa kikundi hicho juzi, walisema vyama hivyo vya upinzani vimejaa unafiki, ubinafsi na ubabaishaji ambao hautaweza kuwakomboa wananchi katika umaskini.
Walisema wanaimani kubwa na CCM kutokana na sera zake nzuri zikiwemo za kuwawezesha kiuchumi vijana, hivyo wamemuomba Ngeleja na Diallo wawawezesha kupata ‘boda boda’(pikipiki) za mikopo.
“Umaskini ndio unaotufanya tutange tange na kutumiwa hovyo kisiasa, lakini sasa tumejiunga na Chama Mama, kupitia UVCCM, tunaamini maisha yetu yataboreka.
“Tunamuomba mheshimiwa Diallo na Mbunge wetu Ngeleja, watusaidie kupata mikopo ya pikipiki,” alisema Nuhu Maulid, Mwenyekiti wa vijana hao.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Nyamatongo, Adam Yusuph, akiwapongeza vijana hao kwa kujiunga na CCM, alisema Chama kitahakikisha wanafikia maendeleo makubwa ya kiuchumi na kisiasa ili wawe mfano wa kuigwa na wengine waliosalia upinzani.
Katibu Mwenezi wa CCM wa Kata hiyo, Said Manyasi, alisema vijana waliokikimbia CHADEMA na kujiunga na CCM katika tawi hilo, wanafikia 38.
Alisema sera ya CCM ni kulinda vijana na kuwapatia maendeleo, siyo kuwatumikisha.
Manyasi, aliwataka wakitumikie Chama kwa bidii na moyo mkunjufu na kuahidi kufikisha kilio chao kwa Ngeleja na Diallo na kutoa wito kwa UVCCM kuzingatia vikao vya kikatiba na kuhamasisha vijana wachape kazi na kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali ili wapewe mikopo.
Ngeleja, akizungumza na UHuru juzi, alisema anawapongeza vijana hao kujiunga na CCM.
Aliahidi kuwapa ushirikiana na viongozi wengine wa Chama, ili vijana hao na wajasiriamali wengine waliojiunga katika vikundi, wapate mikopo ya kuwakwamua kiuchumi.

Sunday 27 October 2013

Tamati ya CHADEMA imewadia


Na waandishi wetu
BAADA ya viongozi wa CHADEMA kumshushia kipigo aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, hali imezidi kuwa tete na viongozi waandamizi ndani ya chama hicho wamesema muda wa kusambaratika umewadia.
Pia, wamesema ubabe wa baadhi ya viongozi na kunajisiwa kwa demokrasia kamwe hakuwezi kuwa mwarobaini wa kukinusuru chama hicho zaidi ya kuongeza kasi ya kukitafuna kwa kasi.
Mwigamba, ambaye anatajwa kuwa mhimili mkubwa na muhimu katika chama hicho mkoani Arusha, alishambuliwa na viongozi wenzake pamoja na walinzi wa Red Brigade kwa madai ya kuwa msaliti, huku kiongozi mmoja akidaiwa kumtolea bastola.
Kiongozi huyo alishambuliwa na wenzake wakati wa kikao cha Baraza la Uongozi wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, kwa kile kilichoelezwa na baadhi ya viongozi waandamizi kuwa hatua ya kuwapasha viongozi wa juu kuhusu mgawanyo wa ruzuku na ukomo wao wa kukaa madarakani.
Katika taarifa yake, Mwigamba alilipua bomu akiwatuhumu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Wilboard Slaa, kuwa wamechakachua katiba ili waendelee kukaa madarakani.
Hata hivyo, Mwigamba ambaye kwa sasa amesimamishwa uanachama na kuvuliwa uongozi, amesema ataeleza chanzo cha tukio zima na jinsi alivyotaka kuuawa ndani ya ukumbi wa mkutano.
Pia, amesema amewasiliana na mwanasheria wake kwa ajili ya kufungua kesi, na kwamba chanzo cha yeye kupigwa na kudhalilishwa ni kiongozi mmoja ambaye ni mamluki na mwenye maslahi binafsi ndani ya chama hicho.
Akizungumza na UHURU jijini hapa jana, Mwigamba amesema kwa muda mrefu amekuwa muwazi na mzalendo kwa CHADEMA na kwamba, amekuwa masikini na fukara kwa ajili ya kutumia rasilimali zake kwa ajili ya chama hicho.
‘’Siku zote nimekuwa muwazi na mzalendo kwa ajili ya chama, lakini leo nimedhalilishwa na kupigwa kwa ajili ya mtu mmoja mamluki ambaye ana maslahi binafsi ndani ya chama. Lakini mwisho wake umefika, leo nitaeleza kila kitu tangu mwanzo,’’ alisema Mwigamba.
Wakizungumza na UHURU kwa nyakati tofauti, baadhi ya viongozi waandamizi wa CHADEMA (majina yanahifadhiwa), walisema suala la matumizi mabaya ya fedha za ruzuku litakizamisha chama hicho.
Wamesema viongozi walipaswa kuwaeleza wanachama ukweli, lakini kila wanapoulizwa au kuhojiwa katika vikao huwa wakali na kuwaziba midomo kwa ubabe kama walivyofanya kwa Mwigamba.
Walisema kilichozungumzwa na Mwigamba ni jambo la msingi na ambalo limekuwa likipigiwa kelele kwa muda mrefu tangu enzi za marehamu Chacha Wangwe (mbunge wa Tarime). Wangwe alifariki dunia kwa ajali yenye utata eneo la Pandambili wilayani Kongwa, Dodoma, ambapo aliwahi kuingia kwenye mzozo mzito na uongozi wa juu wa CHADEMA kuhusu suala la matumizi ya ruzuku.
‘’Kilio cha Mwigamba hakina tofauti na cha marehemu Wangwe na viongozi wengine wa chini, lakini wachache ndio wana uwezo wa kusimama na kuhoji, japo hushambuliwa. Lakini mambo si mazuri na CHADEMA imefikia njiapanda ya kusambaratika,’’ alisema kiongozi mmoja.
Licha ya kuwepo kwa mpasuko wa muda mrefu ndani ya CHADEMA kutokana na kuwepo kwa upendeleo, hali imekuwa mbaya zaidi pale Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, kutaka vyama ambavyo hesabu zake hazikaguliwa kufutiwa ruzuku.
Zitto, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, alisema vyama vichache ndio hesabu zake zimekaguliwa, huku vingine ikiwemo CHADEMA vikiwa havijawasilisha taarifa za ukaguzi wa hesabu kwa muda mrefu.
Kauli hiyo ilipokewa kwa shangwe na baadhi ya viongozi waandamizi ndani ya CHADEMA wakidai itasaidia kurejesha nidhamu ya fedha za ruzuku.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa CHADEMA, Anthon Komu, aliibuka na kudai hesabu za chama hicho zimekaguliwa na kuishambulia kamati ya Zitto kuwa imedanganya umma.

HUU NDIO WARAKA UNAODAIWA KUSAMBAZWA NA
MWIGAMBA NA KUZUSHA TAFRANI KUBWA CHADEMA
KUFUATIA malumbano yanayoendelea kwenye vyombo vya habari na udhaifu mwingine ambao tumeushuhudia kwenye chama kwa sasa, natoa wito kwa wana-CHADEMA wote nchini kwamba, wakati umefika tubadilishe uongozi wa juu wa chama.
Kihistoria, CHADEMA kati ya mwaka 2005 na 2010, ajenda zetu kwa wananchi zilikuwa mbili. Kupiga vita ufisadi, iliyosukumwa sana na Dk. Slaa na ile ya utetezi wa rasilimali zetu iliyobebwa na Zitto. Lakini sasa hivi chama kinaenda kwa matukio.

Naandika nikiwa mwana-CHADEMA safi na nataka kila mwanachama atakayesoma atulie na kutafakari. Hili siyo jambo la ushabiki. Ni mawasiliano baina yetu wana-CHADEMA na tunahitaji tutulie na kutafakari.
Nimekuwa mwanachama wa siku nyingi na nimebahatika pia kuwa kiongozi ndani ya chama kwa nyakati tofauti, kwa hiyo naelewa ninachokiandika. Nadiriki kusema kwamba kwa sasa chama kinakwenda kwa matukio na ni bahati tu kwamba CCM inaendelea kutupatia matukio, lakini CCM na serikali yake wakitunyima matukio, CHADEMA chini ya Mbowe, Katibu Mkuu Slaa na Naibu Zitto utakuwa ndo mwisho wake.
CHADEMA iliyopiga kelele sana dhidi ya ufisadi, CHADEMA iliyopiga kelele hadi sheria ya vyama vya siasa ikabadilishwa na vyama kutakiwa kukaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), eti leo inaungana na CCM kumshambulia Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kwa kutamka kwamba vyama havijawasilisha ripoti zake za fedha zilizokaguliwa.
Kwa nini? Muungano huu wa CHADEMA na CCM maana yake nini? Kama chama kinajiamini ni kisafi kwenye hesabu zake hofu ni ya nini? Si wasubiri kikao na kamati ya bunge. Katibu mkuu aende na hizo ripoti na nyaraka zinazoonyesha kweli wamewasilisha hesabu hizo?
Napenda kabla sijaendelea mbele kuwapongeza wenyeviti wetu wawili wa kwanza, ambao kimsingi waliweka msingi mzuri sana wa kutong’ang’ania madaraka na badala yake kuachia mapema na kumwachia mwingine kidemokrasia bila vurugu.
Hawakuwa madikteta na nawapongeza sana. Walijitahidi sana kutokuwa wapenda madaraka na kimsingi walituwekea utamaduni ambao walitaka wote tuufuate na kujenga taasisi imara inayojali demokrasia na haki ya kila mwanachama.
Ni kwa msingi huo, waliamua kuandika kabisa katika katiba yetu kwamba kiongozi yeyote katika ngazi yoyote ya kuchaguliwa atakapogombea na kushinda ataongoza kwa kipindi kimoja cha miaka mitano na kisha ataweza kugombea na kuongoza kwa kipindi cha pili cha miaka mitano baada yapo hawezi kugombea tena katika nafasi ile ile aliyoitumikia kwa vipindi viwili.
Ili kuonyesha kwamba walimaanisha kile walichokisema, wote wawili hawakuwahi kukaa madarakani kwa vipindi viwili vilivyoruhusiwa katika katiba, bali wote wawili walikaa kipindi kimoja kimoja tu.
Napenda pia kumpongeza mwenyekiti aliyepo madarakani, Mbowe. Kuna mengi amekifanyia chama. Kakitoa kutoka kwenye chama cha tatu ama nne kwa upinzani hadi kuwa cha kwanza na kustahili kuitwa chama kikuu cha upinzani. Kakichukua kikiwa na wabunge watano (5) bungeni na leo katika kipindi chake cha miaka 10 kina wabunge 49.
Ni ‘achievement’ kubwa! Si hivyo tu, ni wakati wake CHADEMA imebeba ajenda nzito za kitaifa kama vile vita dhidi ya ufisadi, utetezi wa rasilimali, katiba mpya, nk.
Lakini kuna matatizo yameanza kujitokeza na tusipochukua hatua haraka huko mbele tunaweza kupata shida kubwa. Ni muhimu kwa Mbowe kuelewa kwamba uwezo wake umefikia hapo asitake kulazimisha kusonga mbele akidhani bila yeye hakuna CHADEMA. Akiache chama kikiwa salama, abaki kama mwenyekiti mstaafu na awaachie wengine awamu inayofuata ya kuingia madarakani.
Kama hataki kuwa mwelewa na kuachia ngazi, wanachama tumsaidie kwa kumpiga chini uchaguzi ujao. Leo nitaainisha mambo machache tu yanayohusiana na fedha za chama na uaminifu ili wana-CHADEMA muelewe kwa nini viongozi wakuu wa chama wamehamaki sana kusikia wanatakiwa kuwasilisha ripoti za fedha wakajikuta wanapambana na mwenyekiti wa kamati ya bunge badala ya kamati na hata kufikia kusahau kwamba huyo mwenyekiti wa kamati ya bunge ni mwenzao, ni naibu katibu mkuu wa chama. Mengine nitaendelea kuyadondoa siku nyingine nitakapopata fursa:

Mabadiliko ya Katiba ya CHADEMA
Wakati tukifanya mabadiliko ya katiba mwaka 2006 hatukugusa kipengele kinachomzuia kiongozi kuongoza kwenye nafasi moja kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano mitano.
Lakini wakati katiba inachapwa chini ya uongozi uliopo, kipengele hicho kiliondolewa kinyemela. Mambo yanayotokea hivi leo yanaonyesha dhahiri kipengele hicho kiliondolewa kwa makusudi kwa maslahi na kwa faida ya viongozi waliopo madarakani kwa sasa.
Hiki kinaweza kuchukuliwa kama kitendo kidogo, lakini kama viongozi wetu wanaweza kutokuwa waaminifu katika jambo kama hili, ni dhahiri hawawezi kuaminika na wanaweza kufanya mambo mengine makubwa na yenye athari zisizomithilika kwa chama.
Ni muhimu wana-CHADEMA mkafahamu kwamba kitendo cha kuondolewa kwa kipengele hicho ndicho kinacholeta mpasuko leo kwenye chama unaotokana na Mbowe na Zitto kupigania uenyekiti. Kama kingekuwepo leo Mbowe alikuwa anakatazwa na katiba kugombea kipindi cha tatu na hivyo vita iliyopo kati yake na Zitto isingekuwepo na chama kingekuwa imara zaidi.
Ni dhahiri Mbowe aliondoa kipengele hicho kwa makusudi ili aweze kuendelea kugombea bila mwisho na huu ni udikteta kama ule tu wa kina Lyatonga Mrema, John Cheyo na wengineo, na wana-CHADEMA hatupaswi kuuruhusu si kwa Mbowe tu, bali kwa yeyote atakayepata nafasi ya kuwa mwenyekiti wa chama chetu.
2. Matumizi ya fedha za chama:
Hakuna mtu anayejua hivi sasa fedha za chama zinatumikaje zaidi ya kakikundi ka watu watatu. Maamuzi ya vikao hayaheshimiki tena na mabwana hawa. Baada ya uchaguzi wa 2010, vikao halali vilielekeza kiasi na aina ya fedha ambazo hazitaguswa, bali zitunzwe kwenye akaunti maalumu kwa ajili ya uchaguzi wa 2015.
Lakini leo si tu akaunti hiyo haina fedha, bali hakuna akaunti yoyote yenye fedha. Watu watatu ndo wanaamua fedha zitumikeje. Mfano mwingine ni maamuzi ya kikao cha Baraza Kuu cha Januari kilichoamua kwamba kiasi cha fedha kinachotoka serikalini kipelekwe kwenye mikoa, wilaya na majimbo na kiasi kingine kipelekwe kwenye kanda. Leo ni mwezi wa 10 maamuzi hayo hayajatekelezwa ipasavyo.
Nyinyi viongozi wa kanda, mikoa, wilaya na majimbo ni mashahidi wa hili. Lakini kuna michango ya watu binafsi kama Mzee Sabodo, hizo nazo hazijulikani zimechukuliwa lini kwa mfumo gani, zikatunzwa wapi na hatimaye zimetumikaje. Hapo sijataja fedha zinazopatikana kutoka kwenye ‘Fund-Raising Events’ mbalimbali kama ile ya Dar es Salaam na Mwanza. Hizo nazo hazijawahi kuonekana na walioendesha hizo ‘Fund-Raising’, uaminifu wao kwenye masuala ya fedha ni ‘questionable’ (unatia wasiwasi).
3. Taarifa za fedha
Tokea baada ya uchaguzi wa 2010 mpaka leo, hakuna kikao chochote kilichowahi kupokea na kujadili hadi mwisho ripoti ya mapato na matumizi ya fedha za chama. Kila kikao ajenda hiyo inarushwa kiaina.
Wanaojua mchezo huo ni watu watatu hawa na malengo ya kurusha hiyo ajenda kila wakati na kukwepesha isijadiliwe pia wanayajua wao.
Ni dhahiri tukiendelea na hawa watatufikisha mwaka 2015 tukiwa hatuna pesa hata ya kuweka mawakala kwenye vituo na tutapigwa tukiwa tumesimama.
4. Mipango ya kukipatia chama mapato ya ziada kutoka nje ya chama
Wakuu waliopo hawana hata ndoto ya namna ya kupata fedha za ziada. Wanachokijua ni kukusanya ‘sadaka’ kwenye mikutano ya hadhara na kuwapatia kazi watu eti waendeshe harambee za kuchangisha fedha kwa njia ya matukio.
Mawazo mazuri kama ya kuanzisha kampuni ya uwekezaji ya chama itakayowekeza kwenye miradi mbalimbali, haijawahi kufanyiwa kazi, na hivyo uanzishaji wa miradi mbalimbali ya kuiingizia taasisi fedha imebaki ndoto ya mchana.
Hatuwezi kufika hata siku moja bila fedha. Hata uchaguzi wa wenzetu wa Kenya juzi juzi wakuu wetu ingawa walishiriki, lakini hawaonekani kama wamejifunza chochote.
5. Matumizi mabaya ya madaraka yanayoweza kuhusishwa na ufisadi
Chama chetu kinayo kamati ya tenda ambayo iko chini ya sekretariati, lakini kamati hii haifanyi kazi imezimwa kimya kimya na wajumbe wote wa kamati ya tenda kwa kuwa ni dhaifu na wamekubali kuzimwa.
Leo ikidaiwa kamati hiyo ilete nyaraka za mchakato wa manunuzi ya magari, pikipiki, kadi za uanachama, seti ya televisheni iliyofungwa ofisini kwa katibu mkuu, hawana. Manunuzi haya yote yanafanywa na wakuu bila utaratibu wowote, jambo ambalo ni hatari.
Hivi tunavyoongea, ni mwenyekiti taifa mwenyewe ndiye aliyenunua magari na pikipiki zote za M4C.
Hivi tunavyoongea kuna sh. milioni 80 ambazo alizichukua na kuagiza kadi za uanachama tangu mwaka jana mpaka leo hizo kadi hazijawahi kuonekana.

6. Makubaliano ya kifisadi na mtu binafsi anayeuza vifaa vya uenezi vya chama
Hakuna kikao chochote cha juu kilichojadili au kilichowahi hata kupewa taarifa tu kwamba sasa kuna mtu binafsi amepewa tenda ya kuuza vifaa vya chama na chama kinanufaika vipi na mauzo hayo na kwa nini vifaa muhimu vya chama kama bendera vinauzwa na mtu binafsi.
Napenda kwanza kuipongeza kamati ya bunge kwa kuvikomalia vyama vinavyopokea ruzuku bila kujali ni chama tawala au upinzani.
Pili, namshauri CAG unaweza kutumia kampuni binafsi kwenye wizara, idara, taasisi, wakala na asasi zote za kiserikali na serikali za mitaa kwenye ukaguzi, lakini kamwe usiruhusu vyama vya siasa vikaguliwe na kampuni hizo.
Hapo nenda mwenyewe ndio utajionea mwenyewe. Kampuni binafsi kwenye vyama huko zinafundishwa ziandikeje maoni yao. Nenda mwenyewe ujionee.

Pia, kuna mkakati unaendeshwa na CHADEMA kwa sasa wa kuwapigia simu viongozi wa mikoa, hasa hapa Dar es Salaam na mikoa mikubwa kama Mwanza, Arusha, Mbeya nk, wakiwataka watoe matamko kumpinga Zitto. Kataeni ushenzi huu. Hili si jambo la Zitto ni la kamati ya bunge na kimsingi ni la uadilifu ndani ya serikali na vyama.
Hata kama jambo lenyewe lingekuwa limeagizwa na Mwigulu Nchemba msingetoa matamko ya kupinga zaidi ya kuwaacha viongozi wetu wakuu watoe ripoti kuthibitisha uadilifu wao, japo kidogo maana ni ukweli pia kwamba kwenye ripoti wanaweza kuzuga zikawa safi, lakini ufisadi umefanyika.
Kama ni matamko toeni matamko ya kuutaka uongozi wetu utoe hizo ripoti, na hapo ndipo mtakapojua kwa nini hampati ruzuku. Kuna matumizi mengi sana ya hovyo na ufisadi mkubwa unafanyika hapo Makao Makuu.
Nitaendelea kuwadondolea ili muone kwa nini napendekeza tuung’oe uongozi huu chini ya Mbowe.
Ahsanteni kwa kunisoma

Thursday 24 October 2013

Mganga mbaroni kwa wizi wa dawa


Na Ahmed Makongo, Bunda
MGANGA Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk. Rainer Kapinga, anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za wizi wa sh. milioni 16 ambazo zilitengwa kwa ajili ya ununuzi wa dawa za binadamu.
Mbali na Dk. Kapinga, pia mtunza stoo wa halmashauri ya wilaya hiyo, aliyetajwa kwa jina la Mashini, naye anashikiliwa kwa tuhuma za kusababisha hospitali, vituo vya afya na zahanati kukosa dawa.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Mirumbe, alisema Dk. Kapinga na Mashini walitiwa mbaroni juzi na wanahojiwa na polisi kuhusiana na wizi huo na watafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.
Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Bunda, Mika Nyange, alisema baada ya jeshi lake kupitia vielelezo vyote wahusika watafikishwa mahakamani.
Nyange alisema kukamatwa kwa Dk. Kapinga na Mashini, kunatokana na kutuhumiwa kuiba fedha hizo zilizotengwa kwa ajili ya kununua dawa za binadamu, lakini walizichukua kisha kuandika vielelezo bandia kuwa dawa hizo zimenunuliwa.
ìPamoja na maofisa hawa wawili ambao wanashikiliwa, lakini uchunguzi zaidi unafanyika katika taarifa ya mkaguzi wa hesabu za serikali, ili kuwakamata wote waliohusika katika mlolongo huo,îalisema OCD Nyange.
Naye Mirumbe alisema maofisa hao wanatuhumiwa kwa wizi wa fedha hizo ambapo inadaiwa walifanya uchakachuaji huo kati ya Machi hadi Juni, mwaka huu, na kwamba fedha hizo zinaonyesha kununua dawa hewa kupitia kwa mzabuni mmoja wa mjini hapa.
Kubainika kwa uchakachuaji huo ni kunatokana na Kamati ya Ulinzi na Usalama kubaini kuwepo kwa hali mbaya kwenye hospitali na kusababisha wagonjwa kukosa dawa.
Alisema wahusika wa uchakachuaji huo ni wengi na uchunguzi unaendelea kuwabaini wengine.
ìNi maeneo mengi kwenye vituo vya afya kuna ubadhirifu mkubwa wa fedha na usimamizi mbaya wa idara ya afya...tutawakamata wote na kuwafikisha mahakamani, hatuwezi kuvumilia hali hii wakati wananchi wetu wanakosa dawa kwa tamaa ya watu wachacheî alisema.

Kampuni yakamatwa ikisambaza mbolea feki


Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), imekamata zaidi ya tani 2,700 za mbolea feki ya kupandia aina ya CAN yenye thamani ya zaidi ya sh.bilioni mbili.
Mbolea hiyo, iliyoelezwa na TFRA kuwa ilimaliza muda wake wa matumizi tangu mwaka jana, ilikuwa ikisafirishwa kinyemela kwenda katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, ambayo ni maarufu kwa kilimo cha mazao ya chakula.
Aidha, TFRA imechukua uamuzi mzito wa kuinyangíanya kampuni ya Swiss Singapore Overseas Enterprises PTE Limited, leseni ya  kufanya biashara hiyo, sanjari na kulifunga ghala lake lililopo eneo la Tabata Matumbi, Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa TFRA Dk.Susan Ikerra, alisema katika eneo la tukio wakaguzi wake walifanikiwa kupata taarifa kuhusu hujuma zinazofanywa na kampuni hiyo, kwa kusambaza mbolea feki kwa wakulima.
Dk. Suzan alisema wamiliki wa kampuni hiyo walikutwa wakisimamia uchekechaji wa mbolea hiyo ambayo haifai kwa matumizi ya kilimo na iliyoganda kama mawe ya kujengea nyumba na kuitenganisha.
Alisema mmoja wa maofisa wa kampuni hiyo waliihadaa mamlaka yake kwa kuandika barua na kuomba kibali cha kutaka kubadilisha mifuko ya mbolea hiyo kutokana na kupata dhoruba na hivyo kuchanika ikisafirishwa kutoka bandarini.
“Lakini kumbe nia yao haikuwa njema kwa TFRA, bali walitaka kutumia kibali chetu ili kuhalalisha madhambi haya ya kutenganisha mbolea iliyoganda na kuichekecha na kisha kuiweka tena kwenye mifuko na kuisambaza,î alisema Dk. Suzan.
Mkurugenzi huyo wa TFRA aliwaoonyesha waandishi wa habari waliokuwa eneo la tukio moja ya magari lenye namba T723 AXR na T247 AWG mali ya Abinel Mahepela wa Njombe, yaliyokuwa tayari yamepakiwa mbolea hiyo kupelekwa kwa wakulima wa mkoa wa Njombe.
Hata hivyo, wakijitetea mbele na Mkurugenzi wa TFRA na maofisa waandamizi wa idara ya Ukaguzi, wakiongozwa na Samson Mussa, wawakilishi wa kampuni hiyo Manish Kothari na Santosh Reddy, walidai tatizo s

Mwanafunzi apata ulemavu kwa kipigo


NA RABIA BAKARI
MWANAFUNZI wa Kidato cha Pili katika Sekondari Newala, mkoani Mtwara, Salim Shamte, amepata ulemavu wa akili kwa madai ya kipigo kutoka kwa mwalimu wake.
Mateso kwa mwanafunzi huyo, ambaye alikuwa na ndoto nyingi katika maisha yake, yametokana na deni la sh. 300, ambazo alitakiwa kulipa kufuatia kupotea kwa vitabu darasani kwao.
Tukio hilo, lilitokea Oktoba Mosi, mwaka huu, ambapo mwalimu huyo Fredrick Kapinga, alikuwa akikusanya sh.300 kwa wanafunzi wa darasa analosoma Salim, kama adhabu ya kupoteza vitabu viwili vya shule.
“Alipofika kwa Salim, alimjibu kuwa hakuwepo siku ambayo vitabu vinapotea, na mwalimu alimjibu kuwa anafahamu waliopoteza ni wachache, lakini adhabu hiyo italikumba darasa zima.
“Alimjibu ‘haya mwalimu nitalipa’, na ndipo mwalimu alipomkunja na kuanza kumpiga kwa nguvu na kumvutia nyuma ya darasa ambapo, alimbamiza ukutani mara mbili kisha kumweleza arudi akapige magoti na wenzake mbele ya darasa,” alisema mlezi wa mwanafunzi huyo, Neema Solo.
Baada ya tukio hilo, mwanafunzi huyo alianza kuumwa kichwa na kupiga kelele, walipokwenda shuleni kufahamu kilichompata, Mwalimu Kapinga, alikiri na kuomba samahani, kwamba alipandwa na hasira baada ya kujibiwa ‘haya’ badala ya sawa, ambapo aliona amedharauliwa.
“Nilipata taarifa kuwa hali ya mtoto wangu ni mbaya, nikapanda basi na kwenda Newala, ambako nilimkuta mahututi, tuliandikiwa fomu namba tatu ya matibabu kutoka Polisi (PF3), na mwalimu alishikiliwa na polisi,” aliongeza mama wa mtoto huyo, Vena Lupaso mkazi wa jijini Dar es Salaam.
Alisema kutokana na hali ya mtoto kuzidi kuwa mbaya, waliandikiwa rufani kumpeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili, kitengo cha wagonjwa wa mifupa, ambapo aliendelea na matibabu.
“Cha kushangaza tukiwa kule Newala hospitali, kuna taarifa ilienda kwa polisi kwamba mtoto anaendelea vizuri na mwalimu Kapinga akaachiwa ndani ya siku moja, na hata PF3 ya mwanzo ilipotezwa, ndipo tukaandikiwa nyingine baada ya kuomba,” alisema Vena.
Kwa mujibu wa Vena, hata mwalimu huyo kukamatwa na polisi ni kwa msukumo wa wanafunzi ambao, walishuhudia tukio hilo, na kutoa ushirikiano mkubwa kwa mwenzao.
Mtoto huyo kwa sasa hawezi kuzungumza vizuri na pia amepoteza kumbukumbu.
“Hapa unapomuona ni afadhali, kwani amepoteza kumbukumbu na madaktari walisema ni kilema cha muda mrefu kwani, hata kama atapona bado kunaweza kuwa na tatizo kwenye akili,” alisema Vena.
Ripoti za hospitali, zinaonyesha kuwa ubongo wa mtoto huyo umetikisika na itachukua muda mrefu kurudi katika hali ya kawaida.
Daktari kutoka Newala, ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake, alikiri kumpokea mtoto huyo katika hali mbaya, ambapo mwanzo walidhani amepasuka kichwani au ubongo umeingiliana na damu.
“Lakini baada ya vipimo, tulimshukuru Mungu, hatukuona matatizo tuliyodhani, lakini kutokana na ufinyu wa vipimo na ukubwa wa tatizo, tukaona wenzetu wa Muhimbili, watasaidia zaidi,” aliongeza.
Jana, gazeti hili lilikutana na jopo la madaktari wanaomtibu mtoto huyo, ambapo waliotoa maelekezo ya kuendelea na matumizi ya dawa mfululizo na kumpumzisha ili matibabu yawe rahisi.
Hata hivyo, walikataa kuzungumzia lolote na kwamba, ripoti itatoka kwa vibali maalum ama kwa kutakiwa na mahakama au polisi.
Mkuu wa Sekondari ya Newala, Babu Mshamu, alikiri kutokea kwa tukio hilo, lakini alisema limeshafika kwa Ofisa Elimu wa Newala, Alice Msemwa, ambaye alipotafutwa alidai yupo safarini.
Vena aliomba mamlaka zinazohusika kumsaidia ili sheria ichukue mkondo wake ikiwa ni pamoja na Mwalimu Kapinga kulipia gharama za matibabu, na mtoto arejee shuleni pindi atakapopata nafuu.
“Yeye alikuwa akidai sh. 300, lakini amesababisha madhara makubwa kwa mwanangu, hapa nilipo ni mjane, mtoto huyu nalea mwenyewe, nimesimamisha kazi zangu zote za kuniingizia kipato kumuangalia mgonjwa,” alilalama Vena.

Dk. Sheni hakuna linaloshindikana


Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Sheni, amesema hakuna lisilowezekana katika kuleta maendeleo lakini jambo la msingi ni wananchi kujiamini na kuwa na dhamira ya kweli ya kuendeleza nchi yao.
Aliyasema hayo jana wakati akizungumza katika mahojiano maalum na Kamati ya Uandishi wa Taarifa za Serikali kuhusu Miaka 50 ya Mapinduzi yaliyofanyika ofisini kwake Ikulu.
ìHakuna lisilowezekana katika kubadili maendeleo yetu kuwa bora zaidi lakini kwanza tunapaswa kujiamini kuwa tunaweza kufanya hivyo na kudhamiria,î alisema Dk.Sheni.
Aliongeza kuwa Wazanzibari wanapaswa kubadilika kwa kufanya mambo yao kwa malengo na kwa wakati na kunukuu kauli ya Rais wa kwanza wa Zanzibar, Marehemu Abeid Amani Karume kuwa la leo ni lazima lifanywe leo.
ìTumezoea kusubiri kuhimizwa na wakati mwingine mawizarani hatupendi hata kuona wengine wanafanyakazi. Nchi za wenzetu wanafanyakazi kwa dhamira na wanapata maendeleo. Tukibadilika nasi tutakuwa kama wenzetu,î alisema Dk. Sheni.
Alibainisha kuwa jitihada zimekuwa zikifanywa na serikali kuwapeleka watumishi wake nchi mbalimbali kujifunza ili kutumia uzoefu wa nchi hizo kusukuma maendeleo ya nchi.
Kuhusu mafanikio ya miaka 50 ya Mapinduzi, Dk. Sheni, alisema wananchi wa Zanzibar wameshuhudia mafanikio katika sekta mbalimbali ambapo huko nyuma baadhi walibeza lakini hivi sasa wamekubali.
ìTumepata mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali za maendeleo wako waliokuwa wakiyabeza lakini sasa wamekubali kuwa Zanzibar tumepiga hatua kubwa katika maendeleo,î alisema.

Vigogo Namtumbo wabanwa mbavu


NA KHADIJA MUSSA
MWENYEKITI wa Kamati ya Hesabu za Serikali (LAAC), Rajab Mohammed Mbarouk, amemtaka Mwenyekiti wa Halmashauri ya Namtumbo mkoani Ruvuma kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kuacha kukidhoofisha Chama.
Pia, kamati hiyo imekataa taarifa ya hesabu ya halmashauri hiyo na kuiagiza kuifanyia marekebisho na kuirudisha tena mbele ya kamati Desemba mwaka huu.
Amesema kitendo cha kutosimamia fedha za maendeleo ya wanawake na vijana kinadhalilisha Chama chake (CCM) na kuhujumu jitihada za serikali.
Aliyasema hayo jana katika Ofisi Ndogo ya Bunge, Dar es Salaam wakati kamati hiyo ilipowahoji viongozi wa halmashauri hiyo ambapo, ilibaini kwa muda wa miaka mitatu mfululizo haijapeleka fedha hizo kwa wahusika hivyo kusababisha malalamiko makubwa.
Mbarouk alisema ni aibu kwa halmashauri hiyo kushindwa kufikisha fedha hizo kwa wahusika wakati serikali inazipeleka na wao kuzitumia kwa matumizi mengine.
Naye Azza Hamad (Viti Maalumu CCM), alisema hayupo tayari kuona CCM kikidhalilishwa hivyo, aliomba kamati ya nidhamu kulishughulikia suala hilo.
Alisema wamechoshwa na vitendo vya baadhi ya halamashauri kushindwa kusimamia ipasavyo fedha za maendeleo zinazotolewa na serikali na badala yake kuishia katika matumizi ya posho za wataalamu.
Kutokana na hilo, Mwenyekiti wa kamati hiyo alimuagiza mwenyekiti wa halmashauri hiyo kuhakikisha anasimamia ulipaji wa madeni hayo na suala la maendeleo ya vijana na wanawake linakuwa moja ya ajenda katika vikao vyao.

Pinda apigia debe safari za Dar-China


Na Mwandishi Wetu, China
KAMPUNI ya Ndege ya Hainan ya China imekubali kufanya safari za ndege za moja kwa moja kutoka China hadi Tanzania ili kukuza sekta ya biashara na utalii baina ya nchi hizo mbili.
Ahadi hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Shirika la Ndege la Hainan, Chen Feng, baada ya kuombwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ambaye katika mazungumzo yao alimwomba akubali ndege za shirika lake ziwe zinatua Tanzania. Ndege za shirika hilo zinafanya safari kati ya China na Angola kupitia anga la Tanzania.
Waziri Mkuu Pinda, ambaye yuko ziara ya kikazi nchini hapa, moja ya eneo ambalo amekuwa anaziomba kampuni za ndege za China ni kufikiria kufanya safari ya moja kwa moja kati ya nchi hizo mbili ili kukuza biashara pamoja na utalii pamoja na kuja kuweza katika ujenzi wa hoteli za kitalii.
Pia alisema kuna Watanzania wengi ambao wanakuja China kuchukua bidhaa, lakini wanalazimika kuunganisha safari mara tatu hadi nne kabla hawajafika China jambo ambalo linawaongezea gharama.
Akijibu maombi hayo ya Waziri Mkuu,Chen alisema kutokana na urafiki uliopo baina ya nchi hizo mbili, maombi yake watayafanyia kazi na mojawapo ni hilo la kufungua safari za moja kwa moja za ndege kutoka China kwenda Tanzania.
Lakini alishauri kuwa ili njia hiyo iendelezwe ni lazima kuwepo na utaratibu wa kuhakikisha njia hiyo inakuwa ya kudumu kwa kuwa na abiria wengi na ikiwezekana Tanzania kiwe kitovu cha usafiri wa anga kwa abiria wanaotoka nchi jirani wanaokwenda na kutoka China.
Alisema ili kuweza kuwa kitovu cha usafiri wa China, ni lazima abiria kutoka nchi jirani wapate usafiri wa uhakika wa kuwafikisha katika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam ambako wataunganisha safari yao wakitokea katika nchi zao.
Alisema dawa pekee ya kufanikisha hilo ni kuwa na shirika la ndege lenye nguvu la taifa ambalo litashirikiana na Hainan kuhakikisha safari hizo zinakuwa zenye tija na faida kwa kuwafikisha abiria hao kwenye kitovu cha usafiri wa kuunganisha kwenda China.
Pia, alisema ili Dar es Salaam iwe kitovu cha usafiri wa anga ni lazima kuwe na uwanja wa ndege mkubwa na wa kisasa zaidi kuliko ilivyo sasa wenye kukidhi mahitaji ya kimataifa.
Alisema kampuni yake iko tayari kuja nchini kushiriki katika kupanua uwanja wa ndege utakaotumiwa na shirika hilo ili uwe wa kisasa.
“Tuna wataaalam waliobobea katika eneo hilo, maana sisi wenyewe tu tunamiliki viwanja vya ndege vipatavyo 16, hivyo mkitushirikisha mtakuwa na uwanja ambao kila aina ya ndege inaweza kutua,” alisema mwenyekiti huyo wa Hainan Airlines.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu alimweleza mwenyekiti huyo kuwa Tanzania inafanya juhudi za kujikomboa kiuchumi; lakini bado inahitaji msaada wa China hasa katika masuala ya usafiri wa anga ili iweze kupiga hatua kutoka hapo ilipo.
Alisema Tanzania kuna shirika la ndege lakini liko taabani licha ya kuwa lina njia nyingi na akatumia muda huo kumwomba mwenyekiti huyo wa Hainan kufikiria pia namna ya kuweza kufufua ATC ili iweze kufanya kazi pamoja na Hainan

Madudu yafichuka daraja la Rusumo



Na Alphonce Kabilondo, Ngara
UJENZI wa daraja la mto Rusumo linalounganisha Tanzania na Rwanda, umeghubikwa na madudu baada ya kubainika kutokuwa na mlinganyo wa viwango vya miundombinu kati ya nchi hizo mbili.
Hilo lilibainika wakati Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli, alipotembelea mradi huo unaofadhiliwa na serikali ya Japan kwa lengo la kukuza uchumi katika nchi wanachama wa Afrika Mashariki.
Katika ziara hiyo ya ukaguzi ya Dk. Magufuli iliyowahusisha pia Mwakilishi wa Waziri wa Ujenzi wa Rwanda pamoja na Balozi wa Japan nchini, Masaki Okada, ilibainika kuwepo kwa mapungufu ambayo yametokana na baadhi ya wataalamu wa serikali ya Tanzania kushindwa kutoa ushauri wenye manufaa kwa nchi.
Ilibainika kuwa ofisi za idara, urefu wa barabara ya lami kufika kwenye daraja,, kituo kikubwa cha kupaki magari na mizigo vikiwa upande wa Rwanda huku Tanzania ikiwa na miundombinu michache, hatua inayotajwa inaweza kuathiri uchumi wa taifa huku ule wa Rwanda ukinyanyuka.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Magufuli, alisema licha ya ujenzi huo kugharamiwa na Japan kwa aslimia 100, hakuna mlinganyo wa miundombinu na kwamba, hilo lazima liangaliwe kwa umakini wake.
Awali, akitoa taarifa ya ujenzi huo, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kagera, John Kalupale, alisema ujenzi huo umekamilika kwa asilimia 60, ambapo upande wa Tanzania umetekelezwa kwa asilimia 25 huku Rwanda ukiwa umefikia asilimia 35 na uko chini ya Kampuni ya Daiho Corporations ya nchini Japan.
Kwa upande wake Balozi Okada, aliwatupia lawama baadhi ya watendaji wa serikali ya Tanzania kwa kushindwa kuishauri serikali yao mapema juu ya ujenzi wa daraja hilo na kwamba, walipaswa kuwasilisha maoni kabla ya ujenzi kuanza


Spika amwaga siri za wabunge





Na Mwandishi Wetu
SPIKA wa Bunge, Anne Makinda, amemwaga hadharani kuwa baadhi ya wabunge waliomaliza muda wao, wana hali ngumu kimaisha na wengine huenda ofisi za Bunge kulia hali ili wapatiwe msaada.
Alisema kufuatia hali hiyo, Bunge linajipanga kuanzisha na kutekeleza mikakati mbalimbali ili wawezesha kuondokana na fedheha hiyo mbele ya jamii.
Spika Anne, alisema miongoni mwa mikakati hiyo ni kuanzisha mafunzo maalumu ya ujasiriamali kwa wabunge waliopo madarakani kwa lengo la kuwanusuru ili wasikumbane na hali kama za watangulizi wao.
Alisema karibu kila siku anapata ugeni wa wabunge wa zamani wanaofika ofisini kwake kuomba msaada.
Spika Anne, ambaye ni mbunge wa Njombe Kaskazini (CCM), aliyasema hayo jana, Ofisi Ndogo za Bunge mjini Dar es Salaam, alipokutana na Spika wa Bunge la Uswisi, Maya Graf, aliyefika kumtembelea.
Alisema baada ya kuwa Spika wa Bunge, amebaini wabunge wengi wanaomaliza muda wao wana maisha magumu huku wachache ndio wenye uwezo wa kujikimu.
“Nilipochaguliwa kuwa Spika nimeona mambo mengi, baadhi ya wabunge wanaomaliza muda wao wanakuwa na hali mbaya ya kimaisha.
“Kuna siku ofisini kwangu walikuja wabunge watano kutaka msaada na sikuwa na uwezo wa kuwasaidia wote kwa wakati huo, nikalazimika kuwapa nusu wengine walilalamika,” alisema.
Kwa mujibu wa Spika Anne, kutokana na hali hiyo, Bunge limedhamiria kuandaa mafunzo maalumu ya ujasiriamali na kwamba, yatatolewa kwa wabunge waliopo bungeni hivi sasa.
Alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo ili watakapomaliza vipindi vyao vya ubunge, wasiyumbe kimaisha na yatakuwa ya hiari.
Alisema wakati wa mfumo wa chama kimoja, kulikuwa na utaratibu wa kuwapa pensheni wabunge, lakini baada ya mfumo wa vyama vingi, utaratibu huo ulifutwa.
Alisema ifike wakati, jamii isiigeuze siasa kuwa kazi ya kudumu na kwamba, hali hiyo inasababisha uchaguzi wa Tanzania kuwa mgumu.
Aliongeza kuwa mishahara ya wabunge wa Tanzania ni midogo ukilinganisha na ya nchi zingine.
Kwa upande wake, Maya, alisema lengo la ziara hiyo ni kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali ya Uswisi hapa nchini.



Serikali yaibana Barrick




NA SELINA WILSON
SERIKALI imeiagiza Kampuni ya uchimbaji madini ya African Barrick, kutekeleza ahadi zake kwa wananchi, ikiwemo ujenzi wa barabara katika eneo la Nyamongo wilayani Tarime.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele, alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua mkutano wa pamoja kati ya wachimbaji wadodo, wakubwa na serikali, mjini Dar es Salaam.
Masele, alisema kuna ahadi nyingi zilizoahidiwa na kampuni hiyo ambazo baadhi zimetekelezwa na zingine hazijatekelezwa.
Hivyo, aliitaka kampuni hiyo kuhakikisha inazitekeleza haraka iwezekanavyo.
Alitaja baadhi ya ahadi hizo kuwa ni ujenzi wa shule, ununuzi wa madawati kwa shule za msingi, kuchimba visima katika vijiji saba na kusomesha vijana hadi chuo kikuu, ambazo alisema baadhi zimetekelezwa na zingine bado.
Masele, aliwahakikishia wakazi wa eneo hilo, kuwa serikali itafuatilia na kusimamia kikamilifu ili ahadi za barabara na maji zitekelezwe kwa lengo la kuboresha huduma za jamii kwa wananchi walioko jirani na migodi.
Kuhusu mkutano huo wa mkakati wa pamoja (MSP), alisema unalenga kuanza utekelezaji wa mradi wa kuwezesha wachimbaji wadogo katika maeneo ya Mgusu mkoani Geita na Tarime mkoani Mara.
Alisema chini ya mradi huo wenye lengo la kuondoa migogoro, wachimbaji wadogo watawezeshwa kwa kupatiwa utaalamu na vifaa vya uchimbaji wa kisasa badala ya kuchimba kiholela.
Masele, alisema wachimbaji wadogo watakaonufaika na mradi huo ni wale waliopatiwa leseni za uchimbaji.
Pia, watanufaika na mradi mkakati mwingine wa serikali wa kuwawezesha kwa mikopo kwa ajili ya vifaa na mitaji itakayotolewa na benki ya TIB.
Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa shirikisho la wachimbaji wadogo, John Bina, alisema haipendezi kuona kampuni kubwa zikichimba madini na kuondoka huku jamii ikibaki bila kunufaika.
Alisema utaratibu huu wa wachimbaji wadogo ambao ndio wenyeji, wataanza kuona matunda.
Bina, alisema serikali imefanikiwa kuondoa migogoro kati ya pande hizo mbili, kwa kuunda ushirikiano na kuhusisha Benki ya Dunia (WB) pamoja na wadau wengine muhimu, kukaa pamoja na kutoka na mkakati huo.
Kwa upande wake Meneja wa Uendelezaji Endelevu wa Kampuni ya Anglo Gold Ashanti, Rebecca Steven, alisema mradi huo utatoa matokeo chanya na manufaa makubwa.
Rebecca alisema pia mkutano huo utatoka na mpango wa utekelezaji wa namna kampuni zitakavyowasaidia wachimbaji wadogo.
Migogoro baina ya wachimbaji wakubwa na wadogo wa madini hapa nchini, imedumu kwa muda mrefu, ambapo kilio cha wachimbaji wadogo ni kutokuthaminiwa na wakubwa na kuondolewa katika maeneo yao.


Pinda ainadi Tanzania kwenye maonyesho



na mwandishi wetu, China
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amewaeleza washiriki wa Maonyesho ya 14 ya Kimataifa ya China Magharibi, kuwa Tanzania ni nchi ya pili duniani na ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kuwa na vituo vingi vya utalii na akawataka waanze kumininika kwa wingi kuja nchini kutalii.
Alitoa mwaliko huo jana wakati akihutubia kwenye maonyesho hayo yanayojulikana kama ‘14th Western China International Fair’ yaliyoanza jana jijini Chengdu kwenye jimbo la Sichuan, China na kuhudhuriwa na mataifa mbalimbali.
Waziri Mkuu Pinda, ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa mataifa 11 waliopata fursa ya kuhutubia maonyesho hayo makubwa, aliziomba kampuni za China kuja nchini kuwekeza kwa kujenga viwanda vya nguo zinazotokana na zao la pamba lilimwalo nchini.
Alitumia fursa hiyo pia kuinadi Tanzania kuwa ni nchi yenye ardhi kubwa tena yenye rutuba ambayo inafaa kwa kilimo, na kuzisihi kampuni za Kichina ambazo zinataka kuwekeza kwenye sekta ya kilimo, zije nchini.
Katika hotuba yake, Waziri Mkuu Pinda aliwaambia wawakilishi wa kampuni mbalimbali za kimataifa zinazoshiriki kwenye maonyesho hayo kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazolima pamba kwa wingi wakati China ni taifa ambalo limebobea kwa viwanda.
“Sisi tuna pamba na ninyi mna viwanda, nawaomba mje nchini kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya nguo kwani malighafi ipo ya kutosha,” alisema Pinda. Maonyesho hayo yanashirikisha kampuni 4,000 kutoka nchi 72 ulimwenguni na majimbo mengine ya China.
Ufunguzi wa  maonesho hayo ulihudhuriwa na wakuu wa nchi saba, mawaziri wakuu wanne akiwemo Pinda, mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi 25, wakuu wa mashirika ya kimataifa tisa na mabalozi wanane wanaoziwakilisha nchi zao nchini China.
Akizungumzia kuhusu utalii,  Waziri mkuu alisema Tanzania ni nchi ya pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki yenye vivutio vingi vya utalii vikiwemo vitatu vilivyoko kwenye maajabu saba ya Afrika.
“Kati ya maajabu saba mapya ya asili barani  Afrika yaliyotangazwa Februari, mwaka huu, maajabu matatu yako nchini kwetu, ambayo ni mlima Kilimanjaro, hifadhi ya Serengeti na Bonde la Ngorongoro,” alisema na kuongeza kuwa pamoja na vivutio hivyo lukuki, bado idadi ya watalii wanaofika nchini kutoka China haijawa ya kuridhisha.
Alisema licha ya maajabu hayo matatu, pia kuna hifadhi nyingine za wanyama, hifadhi za mambo ya kale na kisiwa maarufu cha Zanzibar.
Alisema hata takwimu za kimataifa zinaitaja Tanzania kama nchi ya pili duniani yenye vivutio vingi kuliko nchi zingine ikiifuatia Brazil ambayo inaongoza kwa vivutio duniani.

Mpango maendeleo elimu ya juu waja


Na Hamis Shimye
SERIKALI imesema ipo katika mchakato wa kuanzisha mpango wa maendeleo ya elimu ya juu ili kusaidia kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ya juu nchini.
Pia, imewataka wazazi na walezi nchini, kuwatilia mkazo watoto wao kusoma masomo ya sayansi ili kusaidia harakati za serikali katika kuboresha kiwango cha elimu.
Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, aliyasema hayo jana alipokuwa akizindua mradi wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu (STHEP), katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).
Alisema mradi huo ni sehemu ya mikakati ya kuboresha sayansi nchini.
Dk. Bilal, alisema serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB), imetekeleza mradi huo kwa dhumuni la kuongeza idadi ya wahitimu na kuwapa uwezo walimu katika ufundishaji wa masomo ya sayansi na teknolojia.
“Sayansi na teknolojia ni muhimu, wazazi, na walezi wanapaswa kuwapa moyo watoto wao wa kusoma masomo haya kwa kuwa ni muhimu katika ustawi wa maisha ya dunia ya sasa,” alisema.
Dk. Bilal, alisema utekelezaji wa mradi huo, ni moja ya vipaumbele ambavyo serikali imejiwekea katika kuhakikisha inatekeleza dira ya maendeleo ya mwaka 2025 kwa kujenga mazingira bora ya ufundishaji masomo ya sayansi.
Pia, alisema serikali imepanga kutekeleza sera mbalimbali ikiwemo ya kuhakikisha ina maliza tatizo la uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi na hesabu.
Alisema mradi huo utakuwa chachu ya ongezeko la ukuaji wa masomo ya sayansi nchini yatakayosaidia kupatikana kwa walimu wengi wenye uwezo katika  masomo hayo.
Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alisema utekelezaji wa mradi huo ni moja ya mipango ya wizara ya kuhakikisha ina maliza matatizo katika masomo ya sayansi hasa kwa kupata walimu.
Mradi wa STHEP umefadhiliwa na WB na umeegemea katika mambo mbalimbali, ikiwemo kuwasomesha walimu katika viwango vya shahada ya uzamili na uzamivu katika masomo ya sayansi na kujenga maabara, kununua vitendea kazi na ofisi.
STHEP umeshaanza kutekelezwa katika vyuo mbalimbali kikiwemo DUCE, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu Huria cha Dar es Salaam (UDSM).

000

Tuesday 22 October 2013

JK: Ni fedheha serikali kudaiwa


na mwandishi wetu, njombe
RAIS Jakaya Kikwete, amesema ni aibu kwa serikali kudaiwa na wakulima.
Hivyo, amewahakikishia wakulima wilayani Ludewa, mkoa wa Njombe, kuwa watalipwa madai yao haraka iwezekanavyo.
Wakulima hao wanaidai serikali baada ya kuiuzia mahindi.
Aidha, Rais Kikwete, amethibitisha kuwa meli ambazo serikali yake iliahidi kununua kwa ajili ya usafiri katika maziwa makuu ya Tanzania, zinajengwa na zitazinduliwa kabla ya mwaka 2015.
Alisema meli hizo zitakuwa sita na zitagawiwa mbili mbli kwa maziwa matatu ya Nyasa, Tanganyika na Victoria.
Rais Kikwete aliyasema hayo juzi alipozungumza kwa nyakati tofauti katika mikutano ya hadhara.
Rais yuko katika ziara ya kikazi ya siku saba mkoani Njombe, ambapo pamoja na kukagua shughuli za maendeleo, amezindua miradi kadhaa na kuweka mawe ya msingi.
Rais Kikwete alikiri kuwa serikali inadaiwa sh. bilioni 17, na wakulima wa mikoa mbali mbali nchini, ambao waliiuzia mahindi msimu uliopita kupitia kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).
Rais Kikwete, aliambiwa hayo jana, alipokuwa akipokea ripoti ya Maendeleo ya wilaya ya Ludewa.
Katika ripoti aliyosomewa, ilidaiwa kuwa  wakulima wa wilaya hiyo pekee, wanaidai serikali sh.bilioni 3.115, ambayo ni thamani ya mahindi tani 6,231, ambayo wakulima hao waliiuzia NFRA.
Rais Kikwete aliambiwa kuwa mpaka sasa wakulima hao wamelipwa sh.bilioni 2.839 za tani 5,679 za mahindi.
NFRA ilikuwa imelenga kununua mahindi tani 13,000 toka kwa wakulima wa wilaya hiyo.
Hata hivyo, mpaka sasa imeweza kununua kununua tani 11,911, ingawa sehemu kubwa ya kiasi hicho hakijalipiwa na serikali.
“Hii ni aibu. Serikali haiwezi kudaiwa na wakulima. Hizi fedha zitalipwa tu,” alisema Rais Kikwete na kuelezea hatua ambazo amezichukua binafsi, katika siku mbili akiwa wilayani humo, kuhakikisha wakulima hao wanalipwa.
Rais Kikwete pia alisema Serikali itaangalia uwezekano wa kununua tani 2,972 za mahindi ya msimu uliopita zilizobakia mikononi mwa wakulima wa wilaya hiyo.
“Naambiwa kuwa bado NFRA inahitaji kiasi cha tani 40,000 hivi, ili kukamilisha shehena ya tani 250,000 za mahindi kwa ajili ya Hifadhi ya Taifa mwaka huu.
“Nitawaambia waangalie kama wanaweza kununua kiasi hiki kilichobakia mikononi mwa wakulima wa Ludewa.”
Kuhusu maombi ya wakazi wa Ludewa kununuliwa meli nyingine baada ya kuzama kwa Mv. Mbeya Ziwa Nyasa, Rais alisema meli hiyo iko njiani, wavute subira.
“Tunajua kuwa meli ya Mv. Mbeya ilizama, hata hivyo, meli hizi zimezama katika maziwa mengine makubwa ya Tanganyika na Victoria, na mimi kwenye kampeni niliahidi kuwa nitanunua meli moja kwa kila ziwa,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Tumeagiza meli tatu kutoka Korea Kusini. Zinajengwa. Tumeagiza meli nyingine tatu kutoka Denmark. Nazo zinajengwa. Hivyo, tunaweza kupata siyo meli moja bali meli mbili katika maziwa yote matatu.
“Ni matumaini yangu kuwa nitaweza kuzizindua meli hizo kabla ya kumaliza kipindi changu cha uongozi, mwaka 2015.”
Rais Kikwete pia alifafanua kuhusu kero nyingine zilizoibuliwa na wakazi hao, ikiwa ni pamoja na ya ujenzi wa daraja kwenye Mto Ruhuhu, ambapo aliahidi kuwa litajengwa.

Kodi ya ving’amuzi kuangaliwa-January


NA LILIAN JOEL, ARUSHA
WIZARA ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, inakusudia kuwasilisha mapendekezo serikalini ya kupunguza au kuondoa kodi kwenye ving’amuzi ili kuwapunguzia gharama wananchi.
Hayo yalisemwa jijini Arusha jana na Naibu Waziri wa wizara hiyo, January Makamba, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano wa 21 wa Umoja wa Taasisi za Utangazaji za Nchi za Kusini mwa Afrika (SABA), unaoendelea jijini hapa.
Alisema sababu ya kupunguza ama kuondoa kabisa kodi hiyo inalenga kuwawezesha Watanzania wengi kumudu kununua vifaa hivyo na kupata huduma ya utangazaji wa runinga bila usumbufu.
Naibu Waziri huyo, alisema ili kufanikisha lengo hilo, wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, inawasiliana na Wizara ya Fedha na wadau wengine, kuangalia njia muafaka wa kufikia malengo hayo yatakayoleta nafuu kubwa kwa wananchi.
Alisema kwa sasa, wanatumia kiasi kikubwa cha fedha kununua ving’amuzi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Profesa John Nkoma, alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa malengo ya kimataifa ya kuhamia katika mfumo wa dijitali kutoka analojia.
“Ni faraja kubwa kwamba nchi zingine zinakuja kujifunza kwetu jinsi tulivyofanikiwa kutekeleza mipango ya kuhamia dijitali kutoka analojia. Ingawa tuna safari ndefu, lakini tunajivunia maendeleo tuliyoyafikia,” alisema Profesa Mkoma.
Serikali inatekeleza mpango wa kuzima mitambo yote ya analojia kuanzia mapema mwaka huu, huku ikikusudia kuwa ifikapo mwaka 2015, matangazo yote ya televisheni na radio yatarushwa kwa dijitali.

Kanisa lachomwa, muumini auawa


Na waandishi wetu, Dar na Mwanza
WATU wasiojulikana wamevamia na kulichoma moto Kanisa la Baptist lililopo Vingunguti, Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 8.20 usiku, eneo la Faru, mtaa wa Mtambani na watu ambao mpaka sasa hawajafahamika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Marietha Minangi, alithibitisha jana kutokea kwa tukio hilo.
Alisema watu wasiofahamika walionekana katika eneo hilo ambapo inadaiwa ndiyo waliowasha moto huo uliounguza mazabahu ya kanisa hilo.
Marietha, alisema nyuma ya kanisa kuna nyumba ya Mchungaji, Hezron Mwaisemba na binti wa nyumba ya jirani aliyekuwa ametoka nje usiku huo kujisaidia, ndiye aliyewaona vijana hao wakitokomea.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, moto ulizimwa na wakazi wa eneo hilo na haukuwa na madhara kwa binadamu.
Alisema vijana hao wanadaiwa walikuwa na chupa ya mafuta ya petroli ambayo waliyatumia kuchoma kanisa hilo.
Katika tukio lingine, muumini wa Kanisa la Gilgal Christian Worship Centre lililopo Ilemela jijini Mwanza, ameuawa kwa kucharangwa na mapanga na wengine wawili kujeruhiwa.
Tukio hilo lilitokea baada ya watu wasiofahamika kuvamia kanisani hapo wakati wa mkesha wa maombi saa 7:00 usiku wa kuamkia jana.
Askofu wa Kanisa hilo, Eliabu Sentoz, alimtaja aliyeuawa kuwa ni Elia Meshack na waliojeruhiwa ni Elias Msakuzi na Tumsifu Pungu, ambaye amelazwa Hospitali ya Rufani Bugando.
“Ni kweli waumini wetu watatu waliokuwa kwenye mkesha wa maombi, walivamiwa, mwenzao mmoja aliyekuwa mlango wa nyuma akiwalinda wenzake wakati wanaendelea na maombi ameuawa,’’ alisema.

Fastjet bado yang’ang’aniwa



NA MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Viwaja vya Ndege Tanzania (TCAA), imeiagiza kampuni ya ndege ya Fastjet kukutana leo na mfanyabiashara Majaliwa Mbasa ili wamalize mgogoro wao.
Kwa mujibu wa barua ya TCCA iliyosainiwa na James Mabala kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, iliitaka Fastjet kukutana na Mbasa kwa lengo la kupata suluhu kutokana na kusudio la kushitakiwa mahakamani kwa kukatisha mkataba baina yake na mteja huyo (Mbasa).
Mabala, ameutaka uongozi wa Fastjet kufika katika Ukumbi wa Mamlaka hiyo uliopo katika Jengo la Mamlaka ya Anga, saa tatu asubuhi.
Mbasa anakusudia kuifikisha Fastjet mahakamani kufuatia kushindwa kumsafirisha kutoka Dar es Salaam hadi Johannesburg, Afrika Kusini.
Kampuni hiyo iliahirisha safari muda mfupi kabla ya kuondoka, kitendo ambacho Mbasa amedai kimevuruga mipango yake na kumsababishia hasara.
Anataka arejeshewe gharama za tiketi ya safari ambazo ni sh. 521,560 pamoja na dola za Marekani 5,000 (sh. milioni nane), kama fidia kutokana na usumbufu.
Oktoba 9, mwaka huu, TCAA iliitaka kampuni hiyo kumaliza mgogoro huo ndani ya siku saba, lakini ilishindwa kufanya hivyo na sasa imeamua kuingilia kati kwa lengo la kupata suluhu.