Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Monday 30 June 2014

UOZA UWANJA WA NDEGE


Dk. Mwakyembe kulipua mtandao hatari wa vigogo

  • Ni baada ya kukabidhiwa  picha za CCTV
  •  Kuonyesha wanavyoshiriki michezo michafu

NA BAKARI MNKONDO
AGIZO lililotolewa na Waziri wa Uchukizi, Dk. Harrison Mwakyembe, kuhusu taarifa za uhalifu unaofanywa na baadhi ya watumishi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JKIA), zimekamilika.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa maofisa wa vikosi vya ulinzi na usalama uwanjani hapo wamekamilisha jukumu lao na kukabidhi taarifa husika kwa Dk. Mwakyembe.
Taarifa hizo zinahusisha picha zilizopigwa na kamera za siri (CCTV) ambazo hutumika kurekodi matukio yanayofanywa na baadhi ya vigogo katika utendaji wao wa kila siku.
Habari zilisema katika baadhi ya picha hizo wataonekana baadhi ya vigogo hao wakiwasumbua abiria kwa kuwatisha na wengine wakipokea mlungula au kutoa lugha chafu.
Hata hivyo, licha ya kupata uhakika wa kukabidhiwa kwa picha hizo, halikufanikiwa kupata majina ya vigogo waliorekodiwa wakijihusisha na vitendo vilivyo kinyume na maadili.
Kuwekwa hadharani kwa picha hizo, kunatokana na agizo lililotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Dk. Mwakyembe alipofanya ziara uwanjani hapo, kuwapongeza masofisa wa ulinzi na usalama.
Maofisa hao walifanikisha kukamatwa kwa raia wa Oman akiwa na dawa za kulevya na kutaka kuwahonga maofisa hao sh. milioni 20 na gari ili wamwachie.
Dk. Mwakyembe alisema anachukizwa na kuwepo kwa watumishi wasiokuwa na uadilifu ambao wamekuwa wakisumbua wageni pindi wanapowasili kwa kujivika majukumuambayo sio yao.
“Nafahamu kila kitu kinachoendelea. Nakuagizeni nipeni taarifa za picha zote zinazowaonyesha watumishi wakichukua rushwa na kuiba marashi ya wageni wakati wa ukaguzi na picha zao nitaziweka katika vyombo vya habari,” alikaririwa akisema
Aliongeza kuwa kuna maofisa wanaofanya ukaguzi wa kuangalia chanjo kwa wageni wanaowasili nchini au kuondoka na ambao wamekuwa wakichukua rushwa kwa raai hao huku wakijipa majukumu ya kuangalia hati za kusafiria.
Dk. Mwakyembe alisema hawezi kuvumilia kuona nchi ikiharibiwa sifa yake na watumishi wanaoendekeza rushwa na kusumbua wateja kutoka mataifa mbalimbali.

HELSB yatangaza kiama kwa waajiri


NA MWANDISHI WETU
BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB), imewatangazia kiama waajiri watakaoshindwa kuwasilisha taarifa za watumishi waliokopa katika bodi hiyo.
Imesema haitakuwa na huruma na waajiri hao na kwamba itawafikisha mahakamani.
Mkurugenzi Msaidizi Urejeshaji Mikopo wa HELSB, Robert Kibona, alisema hayo jana mjini Dodoma katika kutano mkuu wa mwaka wa wakurugenzi wa Utawala na Raslimali watu serikalini.
Alisema tayari waajiri watano wamechukuliwa hatua kutokana na kushindwa kuwasilisha taarifa za watumishi wanaodaiwa na bodi hiyo.
Kibona alisema mwajiri atakayeshindwa kutoa taarifa za wahitimu wa elimu ya juu kwenye bodi kwa wakati, atatakiwa kulipa faini ya sh. milioni saba au kutumikia kifungo kisichopungua miezi 12  jela au vyote kwa pamoja.
Alisema hadi sasa waajiriwa 18 wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kushindwa kurejesha mikopo hiyo.
Kibona alisema ili kufanikisha kazi ya urejeshaji  mikopo kutoka kwa wadaiwa,  HELSB iko mbioni kutunga  sheria na mifumo  mbalimbali ya kuwadhibiti wadaiwa hao.
ìTunatarajia sheria ambazo zitawazuia wadaiwa wa mikopo ya elimu ya juu kupata hati ya kusafiria nje ya nchi au kibali cha kusafiri hadi atakapowasiliana na bodi,” alisema.
Alisema mhitimu atakayeshindwa kulipa mkopo, taarifa zake zitatangazwa kwenye vyombo vya habari na kwenye taasisi za mikopo ili asipate huduma yoyote ya kifedha.
Naye, Msaidizi wa Mtendaji Mkuu Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Veronica Nyahende, aliwataka wahitimu wa elimu ya juu nchini kutumia elimu waliyonayo kujiajiri,  badala ya kusubiri kuajiriwa.
Alisema changamoto ya kurejesha mikopo  ni kubwa kwa upande wa wahitimu wa elimu ya juu ambao hawana kazi ama hawajajiajiri.
Veronica alisema Bodi imeingia mkataba na kampuni itakazokusanya mikopo kwa walionufaika lakini wakashinda kuirudisha.

Vikwazo vya kibiashara dhidi ya Czech kuondolewa


NA SUBIRA SAID, TSJ
SERIKALI imeandaa mpango wa kuondoa vikwazo vinavyokwamisha ukuaji wa biashara na Jamhuri ya Czech.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk. Mary Nagu, alisema hayo jana alipokuwa akifungua kongamano la kibiashara kati ya Tanzania na Jamhuri ya Czech.
Alisema mpango huo utawawezesha wawekezaji na wafanyabiashara kutumia fursa zilizopo ili kukuza uchumi na maendeleo ya nchi hizo.
Dk. Mary alisema tayari serikali imetayarisha mpango huo na inatarajia kuupeleka Czech ili iweze kuainisha vikwazo vilivyopo.
“Mpango huo ukikamilika tuna imani tutaweza kuondoa vikwazo vilivyopo na kuonyesha maeneo mbalimbali ya ushirikiano wa kibiashara,” alisema.
Alisema maendeleo katika sekta ya uwekezaji hayawezi kufikiwa bila ya kuondoa vikwazo vya utozwaji kodi mara mbili pamoja na ukiritimba.
Kwa upande wake, mwakilishi kutoka serikali ya Czech, Pavel Rezac, alisema kongamano hilo litasaidia kukuza na kutambua fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji.
Kongamano hilo ni la kwanza kufanyika nchini na linawashirikisha wadau mbalimbali wa kibiashara kutoka ndani na nje ya nchi.

Watoa huduma za afya wadhibitiwe-Balozi Mchumo


NA KHADIJA MUSSA
SERIKALI imeombwa kuharakisha utaratibu wa kudhibiti gharama za huduma za afya hususan upande wa dawa ili kuwapunguzia mzigo wananchi.
Hatua hiyo inatokana na baadhi ya watoa huduma za afya kupandisha gharama kila kukicha, jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa.
Pia, watoa huduma hao wametakiwa kuacha tabia ya kubagua wagonjwa wa kadi na kuthamini wale wanaotoa pesa taslimu.
Mwenyekiti wa bodi ya Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), Balozi Ali Mchumo, alitoa ombi hilo jana alipokuwa akizungumza na wadau wa mfuko wa afya, mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema wakati umefika wa kudhibiti watoa huduma za afya ili kuwaondolea gharama wananchi kwani wanapata shida katika upatikanaji wa huduma hiyo, kutokana na kutokuwepo kwa mfumo wa kudhibiti gharama.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo alisema ili kuweza kutatua tatizo la udanganyifu wa madai, uwepo utaratibu wa kutoa huduma kwa njia ya TEHAMA.
Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Ilala, Raymond Mushi, aliziagiza Manispaa za mkoa wa Dar es Salaam, kuharakiasha mchakato wa ukusanyaji maoni kuhusu utaratibu wa Tiba kwa Kadi (TIKA).
ìUlimwenguni kote kwa sasa matumizi ya kadi katika utoaji wa huduma za kijamii ndio mtindo unaotumika, kwa bahati mbaya  hapa nchini, baadhi ya watoa huduma huthamini wagonjwa wanaotoa fedha taslimu, tabia hii lazima ikome,î alisema.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Hamis Mdee, alisema katika mwaka ujao wa fedha, wanatarajia kuandikisha upya wanachama wao na kuanza kutumia teknolojia ya kisasa ili kuweza kuwatambua wanachama wao.

CCM Kibaha yaweka hadharani msimamo


NA MWANDISHI WETU
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Kibaha Mjini, kimesema wanachama wake watakaoongoza kura za maoni pasipo mizengwe, watateuliwa kuwania uongozi katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa.
Kimesema kitakabiliana na wagombea wote wasiokubali kushindwa, ambao mara nyingi wamekuwa chanzo cha kuendeleza makundi na kuleta matatizo kwenye uchaguzi.
Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Abdallah Mdimu, alisema hayo juzi kwa wenyeviti wa serikali za mitaa na madiwani alipokuwa akifunga mafunzo ya viongozi hao yaliyofanyika mjini hapa.
ìSuala la wagombea wanaokubalika halina mjadala kwa kuwa CCM imejipanga kuhakikisha wanachama wanaokubalika kwa wananchi wapewe nafasi ili kuondoa manung’uniko yasiyo ya lazima.
ìTunahitaji kushinda uchaguzi, hatufanyi majaribio, tunataka kuendelea kushika dola, dola inaanzia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, hivyo ni lazima tusikilize wananchi  wanahitaji nini,î alisema.
Naye Katibu wa Siasa na Uenezi wa Mkoa wa Pwani, Dk. Zainab Gama, aliwataka viongozi wa CCM kuhakikisha wanafanya kazi kwa karibu na wananchi.
Dk. Zainab aliwataka wana CCM kuacha tabia kuwalalamikia viongozi wanaofanya kazi zao vizuri kwani watakatishwa tamaa na mwisho wa siku CCM ndio itakayopata hasara.
Aliwashangaa wanaopiga kelele pale diwani au mbunge anapotekeleza majukumu yake ya kazi.

TPB yawapiga jeki Kyela


NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amepokea hundi ya sh. milioni 5 kutoka Benki ya Posta Tanzania (TPB) kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa Kyela walioathirika na mafuriko ya mvua za masika.
Mvua hizo zilitokea mwanzoni mwa mwaka huu na kusababisha madhara makubwa kwa wananchi na miundombinu.
Makabidhiano hayo yalifanyika jana katika Makao Makuu ya TPB, ambapo Dk. Mwakyembe, ambaye pia ni Mbunge wa Kyela, alishukuru kwa mchango huo na kueleza kuwa utatumika kama ilivyokusudiwa.
Alisema mvua ziliharibu miundombinu ya shule ikiwa ni pamoja na madarasa na vyoo, hivyo kuwafanya watoto kushindwa kupata elimu kwa kadri inavyotakiwa.
Mwakyembe alisema tathmini ya awali hadi kukamilika kwa ujenzi huo inaonyesha jumla ya sh. bilioni mbili zinatakiwa.
Naye Mtendaji Mkuu wa TPB, Sabasaba Moshingi, alisema msaada huo umelenga kusaidia ukarabati wa majengo ya shule zilizoathirika kwa kiasi kikubwa, ili watoto waweze kurejea darasani.
ìTunatambua uharibifu uliotokana na mvua hizo ni mkubwa na changamoto zinazoikabili wilaya hiyo bado ni nyingi, ili kurudisha hali ya maisha ya wakaazi hao kama zamani,  tunaahidi kuwa nanyi bega kwa bega kuwasaidia,” alisema.
Alisema Benki ya Posta ni taasisi ya fedha ya umma ambayo siku zote ipo katika mstari wa mbele kuisaidia serikali katika kutatua changamoto mbalimbali zinazotokea ndani ya jamii.

Wanawake 30 wapima kansa Sabasaba


NA WILLIAM SHECHAMBO
WANAWAKE 30 wamejitokeza kupima afya zao ikiwemo saratani za kizazi na matiti kwenye banda la Taasisi ya Kansa ya Ocean Road,  katika Maonyesho ya 38 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam. 
Mmoja wa madaktari wa taasisi hiyo, Dk. Rehema Ngomola, alisema kati ya kinamama hao, mmoja ndiye aliyekutwa na viashiria vya saratani ya kizazi.
Alisema kutokana na takwimu hizo, idadi ya kinamama wenye maradhi ya ya saratani ya matiti na kizazi, inapungua hivyo kuwataka kujitokeza kwa wingi ili kuweza kutambua afya zao.
Alisema lengo lakutoa huduma hiyo katika maonyesho hayo imetokana na kugundulika kuwa wanawake wengi kuwa na saratani ya shingo ya kizazi  na matiti.
“Tumeamua kuleta huduma hii hapa, kutokana na kwamba wakina mama wengi wamekuwa na magonjwa hayam, lakini kutokana na idadi hii tuliyopima tunaweza kupata matumaini kuwa kidogo inapungua,” alisema Dk. Rehema.
Aidha alisema kinamama wanatakiwa kupima afya zao mapema kwa ajili ya kupatiwa matibabu haraka ili kuepusha wadudu kuwashambulia zaidi jambo linaloweza kuharibu kizazi.
Alisema mbali na kupima saratani, pia wamegundulika kuwa na maradhi ambayo ni ya kuambukiza.

TCRA yapata ubora wa kimataifa


NA RACHEL KYALA
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imepata cheti cha kiwango cha ubora kutoka Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO), kutokana na  kukidhi vigezo vya utoaji huduma kwa jamii.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhiwa cheti hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma, alisema mamlaka hiyo imepata cheti hicho kutokana na utendaji kazi wake katika kudhibiti sekta ya mawasiliano ikiwemo kujulikana kimataifa.
“Tulikwenda shule chini ya Shirika la Viwango Nchini (TBS), wafanyakazi wetu waliingia darasani na baadaye alikuja mkaguzi wa kimataifa na kukagua yale tuliyoandika ambapo tulifaulu na leo ndiyo tunakabidhiwa cheti hiki,” alisema.
Alivitaja baadhi ya vigezo vinavyozingatiwa na ISO kuwa ni pamoja jinsi wanavyowashirikisha kila siku wafanyakazi wake katika utawala  wa mamlaka, namna wanavyotumia rasilimali watu katika kufanikisha utendaji mzuri wa kazi ndani na nje ya mamlaka.
Kwa upande wake Mkuu wa Maabara ya Vifaa wa TBS, Salvatory Rusimbi, alisema kigezo muhimu kinachotazamwa ni kuangalia iwapo wateja wanaridhika na huduma zinazotolewa na kampuni na taasisi zinazosimamiwa na mamlaka husika.

Serikali yatakiwa kusimamia gesi kwa maendeleo ya taifa


NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imeshauriwa kuwekeza mapato ya rasilimali zake hususan mafuta na gesi ili kuleta maendeleo endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.
Vile vile imetakiwa kuhaikisha matumizi ya ndani kwenda sambamba  na mapato hayo ikiwemo kuongeza tija katika matumizi ya sekta za umma katika ngazi zote.   
Mkurugenzi wa kampuni ya Pan African Energy, Patrick Rutabanzibwa, alisema hayo jijini Dar es Salaam jana kwenye mkutano wa kujadili mikakati ya kuhakikisha rasilimali zilizopo zinawanufaisha wananchi ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi.
Rutabanzibwa, ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu katika wizara kadhaa ikiwemo ya Nishati na Madini, alikuwa mwezeshaji wa mkutano huo ulioshirikisha nchi washirika wa maendeleo. 
Alisema ni muhimu serikali ikazingatia mapendekezo hayo kwani ipo siku raslimali hizo zitakwisha.
“Miongoni mwa mambo ya msingi yaliyojadiliwa ni umuhimu wa serikali kuweka wazi mikataba itakayoingia na kampuni mbalimbali katika sekta hiyo pamoja na kuhakikisha inapata mgawanyo mkubwa wa asilimia na wa haki ili utumike kuleta tija katika maendeleo ya taifa,” alisema.
Alisema jambo lingine la msingi lililojadiliwa ni kuwepo kwa uwazi wa mikataba hiyo kutoka mamlaka zinazohusika ili wananchi waweze kusimamia raslimali za nchi yao.

JK ateta na ujumbe toka Vietnam


NA MWANDISHI WETU
RAIS Jakaya Kikwete, jana alikutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka kampuni ya simu ya Viettel kutoka Vietnam, ukiongozwa na Le Dang Dung ambaye ni Makamu wa Rais wa Kundi la Kampuni za Viettel Group.
Kwenye mkutano huo uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Dung alifuatana na Tao Duc Thang ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Shughuli za Kimataifa za Kampuni hiyo – Viettel Global.
Dung amemwelezea Rais Kikwete kuhusu mipango ya Viettel kuwekeza katika shughuli ya mawasiliano ya simu hasa kwa maeneo ya vijijini.

Friday 27 June 2014

Ada elekezi sasa kupangwa vyuoni



SERIKALI imeanza kufanya utafiti wa kina kwa kushirikisha wadau mbalimbali ili kuweza kupanga ada elekezi kwa programu zote zinazofundishwa katika vyuo vikuu nchini.


Jenister Mhagama - Naibu Waziri, Elimu na Ufundi
Imesema mwongozo wa ada elekezi ulizinduliwa rasmi Machi 13, mwaka huu, na kwamba ada mpya zitaanza kutumika baada ya utaratibu wa mfumo huo mpya kukamilika.



Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenister Mhagama, alipokuwa akijibu swali la Ismail Rage (Tabora Mjini-CCM), aliyetaka kujua gharama za ada za masomo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vyuo vikuu vingine nchini.



Jenister alisema kwa sasa Tanzania inavyo jumla ya Vyuo Vikuu 53 na taasisi 21 zinazotoa shahada.



Alisema sera ya elimu ya juu ya mwaka 1999 kifungu cha 6.4.3 kinaruhusu taasisi za elimu ya juu kupanga na kusimamia vyanzo vya mapato, ikiwa ni pamoja na kutoza ada za masomo.



Naibu Waziri alisema gharama za ada ya masomo katika vyuo vikuu hutegemea chuo na programu ambayo mwanafunzi anasomea.



Akitoa mfano wa ada za kozi, Jenister alisema katika programu za uhandisi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinatoza sh. milioni 1.3 kwa mwaka wakati Chuo Kikuu cha Dodoma kinatoza sh. milioni 1.5.



Alisema katika programu za sayansi na elimu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinatoza sh. milioni 1.3 wakati Chuo Kikuu cha Dodoma kinatoza sh. milioni 1.2.



Aidha, alisema katika programu za elimu kwa masomo ya sayansi ya jamii, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kinatoza ada ya sh. milioni moja wakati Chuo Kikuu cha Dodoma kinatoza sh. 800,000.

Serikali yacharukia viwanda vya nyavu


WAZIRI wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kamani, amesema viwanda vyote vinavyotengeneza nyavu haramu zinazotumika katika shughuli za uvuvi vitachukuliwa hatua za kisheria.


Dk. Kamani amesema hatua hizo pia zitachukuliwa kwa wafanyabiashara wanaouza nyavu hizo na wale wanaozinunua na kuzitumia katika uvuvi kwa vile kufanya hivyo ni kosa kisheria.



Alikuwa akijibu swali la nyongeza la Jasson Rweikiza (Bukoba Vijijini-CCM), aliyetaka kujua kwa nini serikali inashindwa kuwachukulia hatua wamiliki wa viwanda vinavyotengeneza nyavu hizo na wanaoziuza kwa vile wanafahamika.



"Wanaotengeneza, wanaoziuza, wanaozinunua na kuzitumia katika uvuvi, wote wanafanya makosa kisheria na watashughulikiwa," alisema.



Akijibu swali la msingi la mbunge huyo, Naibu Waziri wa Maendeleo  ya Mifugo na Uvuvi, Kaika Ole Telele, alisema serikali imeendelea na jitihada za kuwawezesha wavuvi wadogo kwa kuhakikisha kuwa zana na vyombo vya uvuvi vinapatikana kwa bei nafuu.



Alisema katika jitihada hizo, serikali imefuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye injini za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu za uvuvi na vifungashio.



Telele alisema pia kuwa injini za uvuvi, malighafi zinazotumika kutengeneza zana mbalimbali za uvuvi na viambata vyake, hupewa punguzo la kodi ama kufutiwa kodi kabisa ili kuwawezesha wavuvi kumudu bei za vifaa hivyo.



Naibu Waziri alisema katika mwaka wa fedha 2013/2014, Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), kupitia Dirisha la Kilimo, imewezesha miradi minne ya uvuvi yenye thamani ya sh. bilioni 1.5 katika halmashauri za Sumbawanga, Ukerewe, Ilemela na Muleba.



Alisema miradi hiyo imewezesha upatikanaji wa boti nne za uvuvi na vifaa vya kuhifadhia samaki katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, boti sita za uvuvi Ukerewe, boti 28 za uvuvi, injini za boti 20 na boti moja ya doria Ilemela.

Viwango vya askari akiumia kazini vyatajwa


KIWANGO cha juu cha fidia kwa polisi aliyepoteza maisha akiwa kazini ni sh. milioni 15 wakati kiwango cha fidia kwa aliyeumia kazini ni kati ya sh. milioni moja na milioni tano.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Perreira Ame Silima, alisema hayo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Saidi Zuberi (Fuoni-CCM), aliyetaka kujua viwango vya fidia kwa polisi wanaopoteza maisha wakiwa kazini na wanaoumia.
Hata hivyo, Silima alisema viwango vinavyotolewa kwa polisi walioumia kazini hutegemea kiwango cha maumivu.
Naibu Waziri alisema pia kuwa likizo za uzazi na ugonjwa kwa watumishi wa Jeshi la Polisi hazina tofauti na watumishi wengine wa serikali.
Alisema sheria ya likizo ya uzazi kwa polisi wanaume wakati wake zao wanapojifungua, bado haijaanza kufanyakazi katika jeshi hilo na wizara yake inaendelea kulishughulikia suala hilo.
Akijibu swali la msingi la Jaku Hashim Ayoub (Kuteuliwa),  Silima alisema serikali huwalipa fidia askari wanaofariki wakiwa kazini kwa mujibu wa kanuni za fidia za askari polisi na magereza za mwaka 2010 iliyotangazwa kwenye gazeti la serikali GN. 270 ya 30/07/ 2010.
Alisema pia kuwa likizo za askari polisi zipo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za ajira ya polisi. Alisema utaratibu huo unazingatia masharti ya ajira ya askari, ambapo hupewa likizo ya siku 84 kwa kipindi cha miaka mitatu, sawa na siku 28 kwa kila mwaka.


"Hivyo si kweli kwamba taratibu za likizo za uzazi na za mwaka zinapingana na misingi ya haki za wafanyakazi. Lakini katika maboresho yanayoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi, taratibu mbalimbali zitaangaliwa upya, ikiwemo likizo," alisema.


Katika swali lake, Jaku alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kuwalipa fidia askari polisi wanapoumia kazini na pia katika kuangalia upya haki ya likizo ya uzazi na likizo ya mwaka oli zilingane na misingi ya haki za wafanyakazi.

Mabomu yaua 12, yajeruhi watu 137




WATU 12 wameuawa na wengine 137 kujeruhiwa katika matukio tisa ya ulipuaji mabomu yaliyotokea katika mikoa ya Arusha, Morogoro, Lindi, Dar es Salaam, Mwanza na Zanzibar.

Aidha, watu 25 wamekamatwa katika tukio la ulipuaji bomu lililofanyika hivi karibuni katika eneo la darajani kisiwani Zanzibar, ambapo mtu mmoja alifariki. Watano kati ya watu hao, wameshafikishwa mahakamani.

Hayo yalisemwa bungeni jana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Perreira Ame Silima, alipokuwa akijibu swali la Waride Bakari Jabu (Kiembesamaki-CCM), aliyetaka kujua kauli ya serikali kuhusu matukio ya uhalifu wa kutumia tindikali na ulipuaji mabomu yaliyotokea hivi karibuni.

Silima alisema katika juhudi za kukabiliana na matumizi haramu ya tindikali, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na Mkemia Mkuu wa Serikali ya  Muungano na  ya Zanzibar, liliendesha operesheni kubwa ili kupunguza matumizi holela ya tindikali. Alisema operesheni hiyo imeonyesha mafanikio makubwa.

Naibu Waziri alisema kwa sasa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa matukio yaliyotokea katika mikoa hiyo sita, ambapo wataalamu wamefanikiwa kubaini aina za mabomu yanayotumika na nchi yanakoundwa kama silaha za kivita.


"Kwa sasa timu hiyo inaendelea na uchunguzi wa kisayansi ili kubaini waingizaji na walipuaji wa mabomu hayo," alisema.


Silima alisema serikali imejidhatiti kukabiliana na vitendo vya uhalifu  wa aina zote na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu au kikundi chochote kitakachothibitika kuhusika na matukio ya uhalifu wa matumizi ya mabomu na tindikali.

Aliwataka wananchi kutoa taarifa mara kwa moja kwa jeshi hilo iwapo watawabaini watu au kikundi chochote kinachofanya vitendo vinavyoashiria uhalifi, hasa wa mabomu na tindikali.

Akijibu swali la nyongeza la mbunge huyo, Silima alisema upelelezi wa matukio hayo hauwezi kuwekwa hadharani, hasa katika hatua za awali kwa vile kufanya hivyo ni kuharibu upelelezi.

Mbaroni kwa kumbaka bintiye



NA DOROTHY CHAGULA, MUSOMA
MKAZI wa Musoma mkoani Mara, Emmanuel  Lucas, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumbaka kwa nyakati tofauti binti yake wa miaka 19 (jina linahifadhiwa) na kumwambukiza ukimwi.
Lucas (52), anatuhumiwa kufanya kitendo hicho kuanzia mwaka 2007 na  kumsababishia binti yake kupata maambukizi ya ukimwi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Paul Kasabago, alisema mtuhumiwa huyo alikuwa akimbaka binti yake huyo mara kwa mara hadi kupata ujauzito, ambapo mtoto aliyezaliwa alifariki dunia.
Alisema binti huyo baada ya kujifungua, alipimwa afya yake na kugundulika kuwa ni mwathirika wa virusi vya ukimwi, hivyo kutoa taarifa  polisi mjini hapa.
Wakati huo huo, mtoto Catherine Emmanuel (4) wa kijiji cha Masinono wilayani Butiama, amepotea katika mazingira ya kutatanisha tangu Juni 22, mwaka huu, akiwa mikononi mwa baba yake wa kufikia, Emmanuel Dinda.
Alisema  kabla ya kupotea, mtoto huyo alisindikizwa nyumbani kwao na mtoto mwenzake Nelea Emmanuel (9), ambaye alimkabidhi kwa baba yake huyo na wakati anaondoka kurudi kwao alisikia mwenzake akiwa analia.
Kwa mujibu wa Kamanda Kasabago, Nelea alimweleza bibi yake kuwa alimwacha mwenzake analia huku mlango ukiwa umefungwa, lakini bibi yake aliichukulia kuwa hali ya kawaida kwa mtoto kuadhibiwa.
Alisema baadaye mama mzazi wa Catherine, Anastazia Emmanuel, wakati akirejea kutoka kisimani alikutana na mumewe akiwa amebeba kiroba chenye kitu kizito ndani yake akienda kusikojulikana.
Alisema mama huyo, alipofika nyumbani alikuta mwanawe hayupo, huku kukiwa na kinyesi na ndala ndani ya nyumba, ndipo alipoanza kumtafuta.
Polisi inamshikilia Dinda ili aeleze mazingira ya kupotea kwa Catherine.