Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Friday 25 April 2014

Tuenzi mawazo ya waasisi - Pinda


NA THEODOS MGOMBA, DODOMA
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amewataka Watanzania kuendelea kuenzi mawazo ya waasisi wa taifa, katika kudumisha Muungano wa serikali mbili, uliopo hivi sasa.
Pinda alisema, hayo jana alipokuwa akichangia katika mkutano wa Bunge Maalumu la Katiba.

Pinda alisema, Muungano uliopo wa Nchi mbili za Zanzibar na Tanganyika ni muungano tofauti na wa kipekee.
Alisema, hata waasisi wa serikali hizo walifikiri kwa kina ndiyo maaana wakaamua kuweka Muungano uliokuwa unafanana na mazingira ya Watanzania.
Huu ni Muungano tofauti na mingine iliyopo na ndiyo maana unasifiwa na nchi mbalimbali hivyo ni vyema ukalindwa,alisema.
Aliongeza kuwa ingawa Muungano una kero mbalimbali, lakini bado ni muhimu kuwepo na wala muundo wa serikali tatu hauwezi kupunguza kero hizo.
Pinda alisema suala ya kero za Muungano kwa kiasi kikubwa limeshughulikiwa, kwani kwa sasa kero hizo zimepunguzwa kutoka 31 hadi kufikia sita.
"Mimi naamini vyovyote mtakavyosema, kama ni serikali tatu au nne, lakini kero hazitakwisha kwani kila siku kero zinajitokeza kutokana na mazingira yaliyopo,íí alisema .
Alisema, binafsi anashangwaza na watu wanaodai uwepo wa Tanganyika na kuhoji kuwa hiyo Tanganyika imetoka wapi.
Akizungumzia katiba, Waziri Mkuu alisema ni vyema wajumbe wa UKAWA wakarudi bungeni ili kuendelea na utungaji wa katiba hiyo kwani wananchi wanategemea kupata katiba hiyo.

Kingunge alonga
Akizungumzia katiba,  Mjumbe wa bunge hilo, Kingunge Ngombale Mwiru, alisema ni lazima katiba ijayo ilinde mafanikio ya Muungano yaliyopatokana katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.
Alisema, katika kipindi hicho chini ya muungano wa serikali mbili kumekuwa na mafanikio mengi katika nchi hizo mbili.
Kingunge alisema katika katiba ya sasa kuna mambo ambayo hayamo nayo ni vyema yakaangaliwa ili yawepo katika katiba mpya ijayo.
Alisema jambo la msingi  ni kuhakikisha kuwa mambo ya msingi yanaingizwa katika katiba mpya ijayo jambo kubwa likiwa, ni jinsi gani Watanzania wataondokana na umasikini.
Kwa mujibu wa Kingunge, hivi sasa zaidi ya Watanzania milioni 15 wanaishi chini ya dola moja kwa siku na wengine chini ya hapo.
"Ni lazima katiba ijayo ikazingatia pia makundi yote wakiemo wafugaji, wakulima na wavuvi kwani nao katika katiba ya sasa wamesahaulika,íí alisema.
Hata hivyo,  alisema ni vyema kukafanyika mazungumzo kati ya viongozi wakubwa na wengine  ili kuhakikisha kuwa kunapatikana maelewano na maridhiano ili katiba iweze kupatikana.
Pia mjumbe huyo alisema, si vyema kumtusi aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, Jaji Joseph warioba.
Alisema kitendo cha baadhi ya wajumbe kumshambulia mwenyekiti huyo si  chema kwani hakuwa pekee yake.
Alisema baadhi ya wajumbe wamekuwa wakimshambulia Jaji Warioba kwa kutumia msimamo wa chama jambo ambalo ni sawa na kuwatukanisha wanachama wote.
 Kwa upande wa Makamu wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi wa Zanzibar, balozi Seif Ali Idd, alisema Muungano wa sasa unafaida kubwa kwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano.
Alisema hivi sasa wananchi wa pande hizo mbili wamekuwa ndugu huku wakiishi kila upande wa Muungano bila tatizo. Bunge hilo Maalumu la Katiba limeahirishwa hadi Agosti 5, mwaka huu ambako litaendelea na vikao vyake kwa muda wa siku 60.

Wednesday 23 April 2014

Hamad awafyatukia Maalim Seif, Lipumba



  • Awaita wasaliti wakubwa wa Watanzania
  • Afichua michezo michafu ya CUF bungeni
  • Kigwangala aeleza hatma ya Tanganyika
  • UKAWA wawakera Wazanzibar, walaani

NA THEODOS MGOMBA, DODODMA
MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba, Hamad Rashid Mohamed juzi alimshukia Makamu wa Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad huku akimtuhumu ni kiongozi msaliti kwa Watanzania.

Maalim Seif, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alielezwa kuwa ni kiongozi kigeugeu kwani sasa amegeuka na kutaka serikali ya Muungano wa mkataba wakati awali alikuwa muumini mkubwa wa serikali mbili.
“Tuwe macho na viongozi wanaobadilika badilika kama kinyonga kwani, mwaka 1992,  CUF walikuwa na msimamo wa  serikali tatu, juzi serikali ya mkataba, kila siku anabadilika,  ni kiongozi wa aina gani huyu?’’Alihoji.
Kwa mujibu wa Hamad, katika kipindi cha kudai katiba mpya,  CUF na vyama vingine viliandamana na kuleta machafuko Zanzibar.
“Watu waliingia katika maandamano na  kusababishiwa ulemavu na  wajane, na hata sehemu zingine  wanafunzi walikosa masomo na leo badala ya kuhakikisha katiba inapatikana, wanahatarisha amani na kutaka mapinduzi tena,”alisema.
“Hivi kati yangu na yeye, msaliti ni nani kwani wakati wakiwa wanatafuta serikali ya umoja wa kitaifa, walikutana sehemu mbalimbali ikiwemo Dodoma na kuafikiana namna ya kufanya serikali hiyo.

“Lakini nilishangaa wenzake watano, akiwemo Maalim Seif, walijifungia ndani, wakaja na masuala ya mkataba, kama ni usaliti, nani msaliti wa wenzake?’’ Alihoji Hamad.
Alisema walipokwenda kwenye kikao cha Halmashauri Kuu, ikapendekezwa Mwinyi (Rais Ali Hassan) agombee Urais na kwa vyovyote Maalim Seif awe Waziri Mkuu.
Huku akishangiliwa na wajumbe, Hamad alisema waliwahi kwenda kwa Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1992 wakiwa saba, na aliwaambia kama kuna makosa amefanya ni kuitambua Biafra na kuwatambua wao, na aliwaagiza wahakikishe kuwa Muungano unabaki hai.
“Tushukuru tunaye Rais mstaarabu, mvumulivu, watu wanampa shinikizo siku saba, lakini anacheka tu, kwa wenzetu hili halitokei, utakuwa jela,” alisema  Hamad.


Akisisitiza zaidi, alisema Bunge linapaswa kufanya uamuzi kwamba ni theluthi mbili ya wajumbe kutoka Bara na kutoka Zanzibar wakutane ili kuweza kupata katiba.
“Theluthi mbili pande zote tukae tutafute katiba, lakini inashangaza  leo, katiba inapatikana, hutaki, tukae tuhakikishe katiba inapatikana,” alisistiza Hamad.
“Hakuna sababu ya kutoka hapa bila katiba.
Wananchi wanasubiri, hapa hakuna UKAWA wala Upawa,’’ alisema.
Alisema tangu mwaka 1982, amekuwa akiishi 
Tanzania Bara na kwamba uhusiano wake na Bara si wa kawaida, ni wa kindugu wa damu.
“Wanashangaa nyie Watanzania ndio walimu wetu, lakini leo mmepata kichaa gani mnamsema vibaya Nyerere na Karume, kama ingekuwa ni kwetu, mgeipata habari yenu,” alisema.
Alisema kuna watu wanajinadi kuwatetea Wazanzibar kuwa wao ndio Wazanzibar  wa kweli bila wanzanzibar wenyewe kutaka, na kusema ni vyema  Watanzania kuwa macho na watu wa aina hiyo.

Naye Dk. Hamis Kigwangala amesema hakuna sababu kwa Bunge Maalumu la Katiba kuendelea kujadili mambo ya Muungano kwani hayakuwepo kwenye mabadiliko ya tume ya katiba.
Amesema mchakato wa kupata katiba mpya unaoendelea bungeni mjini Dodoma, si wa kuifufua Tanganyika.
Alisema baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wameugeuza mchakato huo na kuufanya kuwa wa kujadili Muungano.
Ameonya kuwa mchakato huo wa katiba si wa kubadilisha muundo wa Muungano na kwamba kuna mambo mengi yanapaswa kujadiliwa.
Dk. Kigwangala alisema hayo jana mjini Dar es Salaam kwenye mdahalo wa utafiti ulioandaliwa na Taasisi ya Twaweza.
Alisema mchakato wa katiba umegeuzwa na kuwa wa kubadili muundo wa Muungano, jambo ambalo halikuwemo kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Dk. Kigwangala, ambaye alimuwakilisha Katibu Mkuu wa CCM, alisema iwapo suala hilo litaendelea, ni vyema likarejeshwa kwa wananchi.
Alisema pamoja na UKAWA kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, mchakato huo utaendelea mpaka mwisho.
“Ni bora UKAWA warejee bungeni tuendelee na mchakato, waonyeshe kutokerwa na lazima wafuate sheria,” alisema na kuongeza:“Muundo wa Muungano si ugali, sio maji na wala sio dawa kwa wananchi.” 
Alisema katika mchakato huo, si rahisi kukwepa makundi yenye mitazamo tofauti na jambo la busara ni kuvumiliana.

Jaji Warioba afunguka tena
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amesema wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wameacha kuzungumzia maoni ya wananchi, badala yake wanazungumzia suala la serikali tatu.

Alisema kuna mambo ya msingi ndani ya rasimu ya katiba mpya, yanayowahusu wananchi moja kwa moja, lakini hadi sasa hayajazungumzwa.
“Badala ya kujadili mambo muhimu ya wananchi, wameng’ang’ania serikali tatu, kila kundi linaonyesha dhahiri linataka nini ndani ya rasimu ile.
“Waliowengi wanataka wapitishe katiba yao na wachache wanataka kuwakwamisha wengi ili katiba isipite,” alisema.
Alisema iwapo wajumbe wa Bunge Maalumu wataendelea kuvutana, upo uwezekano mkubwa wa kupata katiba, ambayo haitadumu miaka mingi kama iliyopo sasa.

Mtatiro ataka kura ya maoni
Naye mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Julius Mtatiro alisema ni vyema ikapigwa kura ya maoni ili wananchi waamue wanataka serikali ngapi.

Wanzanzibar waijia juu UKAWA
Mwenyekiti wa Umoja wa Wazanzibar waishio Dar es Salaam, Swalehe Omary amesema wameshitushwa na kuhuzunishwa na kitendo cha wabunge wa vyama vya upinzani kutoka NCCR, CUF na Chadema kutoka nje ya Bunge na kususia vikao bila ya sababu maalumu.
Alisema inashangaza kuona wabunge wanaacha kutumia fursa ya kutunga katiba ndani ya bunge,
badala yake wanatoka na kuzurura mitaani na wakiwa wameshilipwa mamilioni ya fedha.
Omary alisema kitendo cha UKAWA kutoka ndani ya Bunge ni usaliti na kwamba, wanakilaani na wanawataka wananchi wasiwaunge mkono.
“Tunaamini kuwa katiba mpya haiwezi kupatikana kwa maandamano na mikutano ya hadhara, tunawataka UKAWA warejee bungeni kuendelea na mchakato, waache visingizio,” alisema.

Vigogo nishati na madini matatani


Na Latifa Ganzel, Morogoro
WATENDAJI na watumishi wa Wizara ya Nishati na Madini, waliojilimbikizia vitalu vya madini wako kwenye wakati mgumu kutokana na serikali kuagiza wachunguzwe.
Pia, imeagiza wachukuliwe hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Agizo hilo lilitolewa jana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipokuwa akifungua  Baraza la Wafanyakazi wa wizara hiyo mjini Morogoro, ambapo alisema baadhi ya watumishi wanadaiwa kujilimbikizia vitalu.
Alisema tatizo hilo limekuwa sugu kwa watumishi wa wizara yake huku baadhi wakitumia majina tofauti kwa lengo la kuficha ukweli, jambo ambalo limekuwa likiwakwaza wachimbaji wadogo na watanzania kwa ujumla.
Alisema baadhi ya watumishi wamejilimbikizia maeneo makubwa ya vitalu vya madini na kuagiza waanze kuchukuliwa hatua ili kupunguza malalamiko ya wananchi.
Pia, aliagiza suala la upatikanaji wa leseni za uchimbaji kutolewa kwa haraka na zile zilizoombwa bila kufuata utaratibu, zichunguzwe kisha zifutwe haraka.
Profesa Muhongo alisema kwa sasa sekta ya madini imekuwa kwa asilimia 15, ambazo hajaridhika nazo na kutaka hatua za haraka zichukuliwe ili kufikia malengo waliyojiwekea.
Naye Kamishna wa Madini, Mhandisi Paul Masanja alisema wameanza kuchambua maombi yote ya vitalu na ifikapo Julai Mosi, mwaka huu, utoaji wa leseni utakuwa umekamilika.
Alisema uchambuzi huo utasaidia kuwabaini watumishi wote waliokwapua maeneo makubwa ya vitalu vya madini na kwamba, watanyang’anywa bila kujali wadhifa wao.

Hata hivyo, alisema leseni 184 zimefutwa, 80 zikiwa zimesitishwa na leseni 150 za utafutaji madini zilifutwa na hii ni kutokana na agizo la  bunge la kuitaka wizara kufanya marekebisho.

Bulembo amshukia Jaji Warioba


NA THEODOS MGOMBA, DODOMA
MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba, Abdalah Bulembo, jana alimshukia aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya marekebisho ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, kuwa hana nia nzuri na taifa kutokana na kusimamia mapendekezo ya kutaka nchi iwe na serikali tatu.

Akichangia bungeni jana katika mjadala wa Rasimu, Bulembo alisema hali hiyo imejionyesha kutokana na shinikizo lake, la kutaka serikali tatu kwa madai kuwa ni mapendekezo ya wananchi walio wengi.
“Dhambi hii ya kutaka uwepo wa serikali tatu au shirikisho ni ya kutaka kuuwa muungano na haita mmaliza Maalim Seif Hamadi tu, bali hata baadhi ya viongozi,’’ alisema Bulembo.
Alisema kama kuna watu wanafikiria serikali ya tatu ndiyo moja ya njia ya waarabu kurudi Zanzibar, hiyo haitawezekana chini ya Serikali ya CCM.
“Mimi imenishangaza kuona Waziri wa Sheria wa Zanzibar, naye anainuka na kutaka serikali ya shirikisho je, kama siyo muungano ambao umeleta serikali ya maridhiano angepata wapi uwaziri,” alihoji Bulembo.
Mjumbe huyo, alisema Zanzibar kudai kuvunjika kwa muungano ili wapate serikali kamili sasa haitawezekana, na muungano utaimarishwa zaidi ya sasa.
“Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti, sisi tunasema tukimaliza hapa, mimi nitaanza safari ya kwenda Lindi, Mtwara na hata Njombe, kwenye majukwaa kuwaeleza wananchi nini wao wamefanya,’’ alisema.
Aidha, alisema ni muhimu kwa sasa Bunge likaweka sheria juu ya watu wanaowasema viongozi waasisi walioliunda taifa.
Alisema kuanzia sasa ni vyema watu wa aina hiyo wakashitakiwa au kutolewa ndani ya Bunge na askari wa bunge.

Komba: Serikali tatu ni uasi
Naye Kapteni mstaafu John Komba, alisema kitendo cha mapendekezo ya Tume ya Jaji Warioba kupendekeza serikali tatu, ni sawa na binadamu wa kwanza waliomuasi Mungu.
“Mimi nitakuwa wa mwisho kukubaliana na pendekezo hilo na kama litapita, nitaingia msituni kwenda kupigania serikali mbili,’’ alisema Komba.
Alisema pamoja na binadamu hao wa kwanza kupewa adidu za rejea, bado walimuasi Mungu na kisha kufukuzwa katika bustani ya Edeni
“Alichofanya Warioba ni sawa na binadamu hawa wa kwanza, kwani walipewa adidu za rejea lakini wao wamekuja na kitu chao, kwani awali Rais Kikwete aliwapa adidu kuwa pamoja na mambo mengine, suala la muungano lisiguswe, lakini wao wameligusa.
“Katika Tume ile kulikuwa na watu muhimu sana ambao walikuwa karibu sana na Hayati Mwalimu Julius Nyerere na walikuwa wakinywa chai na mikate pamoja na hata mambo mengine huwezi kuyapata toka kwa Nyerere bila ya wao,’’ alisema.

Walimu watakiwa kuacha ushabiki


na mwandishi wetu, dodoma
WALIMU na watumishi wengine nchini, wameshauriwa kutoshabikia serikali tatu huku wao wakiwa na madai na wanashindwa kulipwa kutokana na serikali zilizopo hivi sasa kukosa fedha.
Mmoja wa wajumbe wa Bunge la Maalumu la Katiba, Menrad Kigola, alisema inashangaza kusikia kuwa hata kundi la baadhi ya walimu nao wanapendekeza uwepo wa muundo wa serikali tatu.
“Kila siku tunasikia walimu hao hao wakilalamikia mshahara kuwa ni mdogo waongezwe, lakini bado ndiyo hao hao wanataka serikali tatu, ambazo ni kuongeza gharama za uendeshaji,’’ alisema
Alisema wafanyakazi wengi pia wamekuwa wakilalamikia kodi kubwa wanayokatwa, lakini nao pia wamekuwa wakipendekeza muundo wa serikali tatu.
“Kumbukeni kama serikali ya tatu itapita, lazima na kodi itaongezeka, sasa hapo mmetatua matatizo au umeongeza matatizo kwa kuongeza kodi,’’ alisema Kigola.
Alisema ni muhimu sasa kwa Watanzania kuelewa kuwa serikali inayotakiwa na kupendekezwa na walio wengi ni ile ambayo itabana matumizi bila kutegemea misaada.
Naye Paulo Kimiti; alisema ni muhimu kwa Watanzania kujua ni mfumo upi ambao utawasaidia kupunguza kero zao.
Alisema ni muhimu kwa wajumbe kuhakikisha kuwa katiba inayoendelea kutungwa hivi sasa inawagusa wananchi wengi na si kwa manufaa ya wachache.
Kimiti alisema, Bunge Maalumu la Katiba ni la kihistoria na endapo wajumbe wake watayumbishwa na watu wachache watahukumiwa na wananchi.
Alilalamikia kitendo cha UKAWA kutoka ndani ya bunge na kueleza kuwa kitendo hicho ni cha uwoga.
Alisema, yeye binafsi alishaambiwa kuwa  asili ya uongozi ni mbili ikiwemo kuheshimu watu kwa maana ya waliokutuma na kuwatendea haki wananchi hao jambo ambalo UKAWA hawajalifanya.
“Nchi hii imejengwa kwa miaka mingi zaidi ya 50, lakini leo tunataka kuvunja muungano wetu kwa siku moja tu, hilo ni jambo la hatari sana kwani mengi yatatokea,’’ alisema.
Hata hivyo, mjumbe huyo ambaye ni mkongwe katika siasa, alisema tabia ya kuwakejeli waasisi wa Taifa si nzuri.
Alisema, hata kutoka nje kwa UKAWA  ni moja ya kazi ya mizimu ya waasisi hao kutokana na kuwatusi pasipo sababu na  wasipo jirekebisha katika hilo, hawawezi kurudi.

‘Tutunge katiba tusijadilili watu’


WAJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba wameshauriwa kurejea katika kutunga katiba badala ya kujadili watu kwa majina yao.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mjumbe mmoja wapo wa Bunge Maalum la Katiba, Dk. Tulia Akson, alipokuwa akichangia rasimu ya katiba mjini hapa.
Alisema wajumbe wengi hivi sasa wameacha kujadili Katiba, wanajadili watu, jambo ambalio si lililowaleta bungeni.
“Katiba ndiyo iliyotuleta hapa, kwahiyo kama tunajadili, tujadili rasimu siyo kuchukua muda mwingi kuwajadili watu ndani ya Bunge,’’ alisema.
Alisema kitakacho kwenda kwa wananchi baada ya Bunge Maalumu kukamilisha kazi yake ni rasimu ya katiba na siyo majina ya watu.
Naye Velonica Sophu; alisema inashangaza kuona mjadala wa mchakato wa rasimu umeshikiliwa zaidi na wanasiasa kuliko wajumbe wengine wa kundi la 201.
Alisema, hivi sasa makundi makubwa wakiwemo wanasiasa, wameuteka mjadala huo na kuwafanya wajumbe wengine kushindwa kuchangia yale waliyotumwa na makundi yao.
Mjumbe huyo alisema awali, Tume hiyo ilipopita kwa wananchi kulikuwa na matatizo machache makuu lakini kila kukicha yanaongezeka.
“Malalamiko ya wananchi walio wengi kwanza tulisikia ni kupunguza madaraka kwa serikali, halafu tukaja hapa tukasikia masuala la muungano na sasa tunasikia masuala ya serikali tatu, sasa hata yale tuliyotumwa na wananchi wetu hayajasikilizwa,’’
Mjumbe huyo anayewakilisha kundi la wakulima, alisema wao wametumwa kuwasilisha masuala ya wakulima katika katiba ikiwemo masuala ya ardhi.
“Wakulima wetu kule wanalalamikia masuala ya ardhi, wafugaji na watu wengine, lakini hapa tunasikia masuala mbalimbali ya serikali tatu, muungano hakuna, masuala ya wakulima hebu na haya yasikilizwe basi,’’ alisema.

Thursday 17 April 2014

Kuwatukana waasisi ni kukosa adabu- JK



  • Askofu Mtetemela amshukia Prof. Lipumba
  • Lukuvi afyatuka bungeni, arusha kombora CUF
  • Mwigulu asimamisha posho kwa waliogoma
  • Wajumbe waliofuata mkumbo mikononi mwa JK

NA MWANDISHI WETU
RAIS Jakaya Kikwete amesema ni utovu wa nidhamu na ukosefu wa adabu kwa baadhi ya Watanzania kuwatukana, kuwadhihaki na kuwakejeli waasisi wa Taifa hayati Julius Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amaan Karume.

Amesema viongozi hao wawili wameifanyia Tanzania mambo mengi makubwa na ya kihistoria kiasi kwamba Watanzania wanao wajibu wa kudumisha na kuenzi heshima yao kwa namna ya kudumu.
Rais Kikwete alisema hayo juzi wakati akizungumza na wahariri wa baadhi ya vyombo vya habari nchini Ikulu mjini Dar es Salaam katika mahojiano maalumu ya kuadhimisha miaka 50 ya Muungano.
“Ni kukosa adabu na ni utovu mkubwa wa nidhamu kwa Mtanzania yeyote kuwatukana, kuwadhihaki ama kuwakejeli waasisi wa taifa letu. Hawa ni watu ambao wameifanyia nchi yetu mambo makubwa,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza : “Mzee Karume, yule aliongoza Mapinduzi yaliyoondoa dhuluma na uonevu pale Zanzibar. Waafrika walio wengi walikuwa wanaonewa sana pale, pengine watu wamesahau, lakini hata pale walipokuwa wanashinda uchaguzi, bado walikuwa hawapewi nafasi ya kuongoza maisha yao wenyewe.”
 “Ni ukosefu wa adabu kwa yeyote kumshutumu mtu aliyejitolea kiasi hicho ili kubadilisha mfumo dhalimu na kujenga maisha na mazingira ya maisha bora kwa wengi,” alisisitiza.
“Mzee Nyerere ametuachia taifa moja, lililoungana, lenye umoja, lenye amani na mshikamano. Misingi ambayo aliijenga yeye ndiyo imeendelea kuongoza taifa letu kwa miaka yote hii. Viongozi wengine wote ambao wamemfuata – Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa na sasa mimi mwenyewe, tumefuata na kuongozwa na misingi hiyo. Na siku nchi yetu inaamua kuipuuza misingi hiyo, tutaingia katika matatizo makubwa,”alionya.
Rais Kikwete alitoa msimamo huo baada ya kuulizwa swali kuhusu matusi, kejeli na dhihaka ambazo zimekuwa zikionyeshwa na wajumbe wachache wa Bunge Maalum la Katiba juu ya waasisi hao wa Tanzania na wabunifu wakuu wa Muungano wa Tanzania.
Miongoni mwa watu walitoa kauli dhidi ya waasisi hao hivi karibuni ni Tundu Lissu, kiasi cha kusababisha wabunge wenzake, viongozi wa dini na wananchi kumjia juu.

Askofu Mtetemela amshukia Lipumba
Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Donald Mtetemela, ameeleza kushangazwa na kuchukizwa na kitendo cha Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, kulifananisha bunge hilo na askari wa Itarahamwe.
Akichangia bungeni jana, Askofu Mtetemela alisema kitendo kilichofanywa na Profesa Lipumba hakikubaliki na si cha uungwana kwani, kinaweza kuleta uhasama baina ya Tanzania na Rwanda.
“Binafsi nilitaka kumuona Lipumba kumueleza haya, lakini sikufanikiwa mpaka sasa nilipopata nafasi ya kuchangia. Nimesikitishwa na kitendo hicho cha kufananisha wajumbe wa bunge na wauaji, sisi hatupo hapa kuua mtu,’’ alisema.   
Alisema kitendo hicho kinapaswa kukemewa kwa nguvu zote na Watanzania na kwamba hakikustahili kufanywa na kiongozi kama Lipumba.
“Hata kama kuna jambo limewaudhi wajumbe wa UKAWA, walikuwa na nafasi ya kukaa pamoja na kuridhiana. Kiongozi kama Lipumba ambaye anasifa kubwa ndani na nje ya nchi anadiriki kutoa kauli ya ajabu kisha kutoka ndani ya bunge kususia mchakato huo.
“Busara ya kiongozi si kukasirika au kuamua jambo kwa hasira, angetumia maridhiano kutatua hilo kwani wananchi wanataka kuona tunatoka na katiba, hatupo hapa kwa ajili ya vyama na wala vyama visitubomoe na kuacha kilichotuleta,’’ alisema.
Alisema pia kuwa mfumo wa serikali tatu unahitaji muda na matayarisho ya kutosha na si kukurupuka na kuamua mambo bila kutafakari.
Alisema kwa sasa mfumo uliopo ni wa Muungano wa serikali mbili, ambao umefanya mambo mengi katika kipindi cha miaka 50, ambayo yanastahili kupongezwa licha ya kuwepo changamoto.
‘’Wapo watu wanaosema hakuna kilichofanyika, lakini yapo mengi yenye mafanikio kwa taifa letu.
Cha msingi tufanye mambo yetu mazuri bila kujali kama tutasifiwa au la,’’ alisema.
Kuhusu mwenendo wa bunge, alisema: “Katika mila na desturi zetu, bunge hili ni kama baraza la wazee, ni lazima kuwe na utulivu, lakini pamoja na kuwepo kwa viongozi wetu wa kitaifa hapa ndani, tumeshindwa kutunza heshima yetu.
“Tunaitwa waheshimiwa, lakini sisi wenyewe hatuheshimiani na wala hatuheshimu viongozi wetu waliopo humu ndani, tusipoteze lengo lililotuleta hapa.’’
Kuhusu lugha za kejeli na kashfa bungeni, Askofu Mtetemela alisema, kauli zilizotolewa dhidi ya waasisi wa taifa zinastahili kulaaniwa.
“Wewe una kipimo cha kiasi gani cha kuwakosoa waasisi hawa, ambao wameweza kuliletea taifa amani na utulivu kutokana na maono yao.
“Wewe kama una nguvu, pambana na mtu mwenye nguvu na si mfu na hata kwenye misiba huwa tunasema mazuri ya marehemu na si mabaya kwani, mabaya anayeweza kuyahoji ni Mungu tu kwa wakati huo,’’ alisema.

Lukuvi afyatuka, arusha kombora CUF
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi jana aliwatolea uvivu viongozi wa UKAWA kutokana na kulazimisha hoja zao ili kupata fursa ya kuongoza dola.

Pia alifichua siri kuwa viongozi wa CUF na CHADEMA wameungana kwa mkataba wa kila upande kuunda serikali na ndio sababu wanashupalia serikali tatu licha ya kuwa na changamoto lukuki.
Alikituhumu CUF kuendesha siasa zake kupitia kivuli cha kikundi cha Uamsho, jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa taifa.
Lukuvi alitoa kauli hiyo baada ya kupewa nafasi ya kujibu tuhuma zilizoibuliwa na Profesa Lipumba kuwa alitumia sherehe za kumsimika Askofu wa Kanisa la Methodist la mjini hapa, kupigia chapuo muundo wa serikali mbili na kutoa vitisho kuhusu serikali tatu.
Alisema Uamsho wamekuwa wakiendesha siasa za CUF kwa kupitia kivuli cha dini, hivyo hakuna shaka kuwa hata kitakapopata madaraka ,utawala wake utakuwa wa kidini.
“Mambo mengi wanayoyasema wanachama wa CUF ndiyo yanayosemwa na taasisi hiyo, hivyo kwa hofu yangu binafsi, sina shaka Uamsho ni CUF kwani hata Wazanzibar wenyewe wanajua hilo,’’ alisema.
‘’ Hatujawahi kuona Chama kinachojitayarisha kuchukua madaraka kinatumia mgongo wa dini kufanya siasa. Hii si sahihi, kwanini nisiwe na hofu na kusema,’’ alisisitiza
Akizungumzia Jeshi kuchukua madaraka, Lukuvi alisema hofu yake hiyo imetokana na rasimu ya katiba, ambayo inapendekeza kuwepo kwa serikali tatu, jambo ambalo serikali moja ya Muungano vyanzo vyake vya mapato havikuwekwa wazi.
“Haya yalikuwa ni mawazo yangu binafsi na sikuwa na shida kuyaeleza na nitaendelea kuyaeleza na kisiwe chanzo cha wanachama wa UKAWA kudai kuwa hiyo ni lugha ya uchochezi.
“Hivi kati ya mimi na Maalim Seif (Katibu Mkuu wa CUF) nani ni mchochezi ? Mbona hawakugomea kauli yake aliyoitoa Kibanda Maiti kuwa Rais Kikwete atamtuma Mkuu wa Majeshi Mwamunyange kwenda kupindua nchi iwapo serikali tatu zitapita,’’ alisema lukuvi.
Aliwataka wajumbe wa Bunge hilo kufanya kazi waliyokabidhiwa ya kupitia rasimu iliyopendekezwa na si kutafuta visingizio kama inavyofanya UKAWA.
Juzi, Profesa Lipumba alisema Lukuvi alisikika akisema kuwa endapo serikali tatu zitapita, jeshi litachukua nchi.
Akizungumza jana asubuhi, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samwel Sitta alisema, wamelazimika kumuita Lukuvi ndani ya bunge ili aweze kutoa maelezo kuhusiana na kauli yake iliyodaiwa na Lipumba kuwa ni chanzo cha kususia bunge.
Alisema awali Lukuvi alitakiwa kusafiri kwenda nchini India kwa matibabu, lakini amemrudisha ili kutoa ufafanuzi wa tuhuma hizo kwanza.
Sitta alisema jambo la wajumbe hao wa UWAKA la kususia Bunge kwa madai ya kauli za uchochezi halikustahili kufanywa kwani, kila kero ina utaratibu wake wa kushughulikiwa.
Alisema kuteuliwa na Rais kuwa miongoni mwa watunga katiba ni jambo la heshima na ya kipekee kwani utungaji wa katiba si jambo ambalo hufanyika kila mara.
“Baadhi ya wajumbe wenzetu hawajatambua uzito wa jambo hilo, kwani wakati wote kumekuwa na mambo kadhaa hapa ndani, lakini yamevumiliwa kwa nia njema ili tufikie mwisho ulio salama,”alisema.
Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samia Suluhu Hassan, alisema kitendo kilichofanywa na wajumbe wa UKAWA hakiwatendei haki Watanzania.
Pia,alisema watakutana na Kamati ya Uongozi  kujadiliana hatua zaidi za kuchukua.

Mwigulu asimamisha posho
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Mchemba amesema serikali imesimamisha malipo ya posho ya wabunge wote waliosusia vikao vya bunge juzi.

Pia, amesema wajumbe ambao ni watumishi wa umma, wataripotiwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi kwa ajili ya hatua za kinidhamu.
Alisema licha ya kuwa wajumbe hao wameshalipwa posho hizo hadi Aprili 26, mwaka huu, tayari amesitisha malipo hayo ambayo yalikuwa yapitie benki.
“Huku kwa upande wa bunge taratibu za kuwalipa zilishakamilika, lakini kwa kuwa malipo hayo yanapitia benki, nimeagiza wasitishe,’’ alisema.
Alisema malipo kwa wajumbe hao yatafanyika pale tu watakaporejea ndani ya bunge kuendelea na mchakato huo wa Bunge.
“Watakaolipwa posho kwa sasa ni wale wanaohudhuria vikao, hatuko pikiniki hapa, tunawalipa watu halafu hawataki kufanya kazi,” alisema.

Juzi, Livingstone Lusinde alisema kilichokosewa ni uamuzi wa bunge kulipwa kwa fedha za sikukuu, jambo ambalo limewafanya kususa na kuondoka.
Naye Said Mkumba alielezea kushangazwa na wajumbe hao walioamua kutoka nje, akihoji kwamba kwa nini hawakutoka siku mbili zilizopita, mpaka wamesubiri walipwe posho hadi ya Aprili 26, ndio waondoke.

WASSIRA: SIJASHANGAZWA NA WALIOSUSA
Naye Stephen Wasira, amesema hakushangazwa na kitendo cha kutoka nje ya bunge wajumbe wa UKAWA kwani, ni matukio yaliyopangwa muda.

Wasira, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), alisema UKAWA walikuwa na mpango huo muda mrefu baada ya kuona hoja yao kuhusu kutokuwepo kwa hati ya muungano kukosa ukweli.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Wasira alisema sababu wanayosema kuwa wametukanwa ndipo wakaamua kutoka nje ya bunge, haina mashiko kwani UKAWA walitoa maneno ya kashfa dhidi ya waasisi wa Muungano.
“Hoja iliyotolewa na Kiongozi wa UKAWA kuwa wanatukanwa bungeni ni ya ajabu kwa kuwa UKAWA wamekuwa wakiwatolea maneno yasiyofaa waasisi wa muungano, kitendo ambacho hakikubaliki na Wananchi” alisema 
Aliongeza kuwa ni muhimu kwa wajumbe wa bunge hilo kushindana kwa hoja na sio kutoka nje ya bunge na kutafuta sababu zisizokuwa na msingi.

Uchaguzi serikali za mitaa kuahirishwa


NA MWANDISHI WETU
UCHAGUZI wa serikali za mitaa, ambao hufanyika mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu, huenda usifanyike mwaka huu, imeelezwa.

Hatua hiyo inatokana na uchaguzi huo kuingiliana na masuala ya kupata Katiba mpya, ambayo mchakato wake bado unaendelea.
“Nikiri nafasi ni finyu sana ila tutalizungumza serikalini,” alisema Rais Jakaya Kikwete, alipozungumza na baadhi ya wahariri Ikulu mjini Dar es Salaam juzi.
Rais Kikwete alisema atakutana na viongozi wengine wa serikali ili kuamua kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa kama ufanyike mwishoni mwa mwaka huu kama ilivyo kawaida au la.
Alisema ni kweli nafasi ya kufanyika kwa uchaguzi huo ni finyu sana kwa kuwa suala la Katiba mpya litaendelea hadi mwishoni mwa mwaka huu kipindi ambacho uchaguzi huo huwa ukifanyika.
Iwapo uchaguzi huo utaahirishwa, huenda ukafanyika mwakani na uchaguzi mkuu, lakini tofauti na ilivyozoeleka, upigaji kura utakuwa nne kwa Tanzania Bara.
Kwa kawaida upigaji kura kwenye uchaguzi mkuu unahusisha kura ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kura kwa ajili ya mbunge na kura ya diwani.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete imekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kueleza wasiwasi wake kuhusu kuahirishwa kwa uchaguzi huo.
Pinda aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma hivi karibuni kuwa, muda uliopangwa kwa ajili ya Bunge Maalum ni siku 70, lakini kazi ilikuwa ikienda kwa kusuasua.
“Hatari ya kusogeza mbele uchaguzi wa serikali za mitaa ninaiona dhahiri, nadhani itabidi tu tumuombe Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, tusogeze mbele uchaguzi huu, ili kutoa nafasi kwa kazi zingine kuendelea hususan ya kutengeneza katiba,” alisema Pinda.
Pinda alisema pia kuwa iwapo kazi ya bunge hilo itakuwa haijamalizika ifikapo mwishoni mwa Aprili mwaka huu, watamuomba Rais Kikwete aliahirishe ili lipishe Bunge la Bajeti liendelee na kazi zake.
“Hatuwezi kuacha kazi zingine za serikali zikasimama, lazima ziendelee, na zitaendelea kama bajeti za wizara zitapitishwa, nadhani kama hatutakwenda sawa, tutamuomba tu Rais aahirishe bunge hili la Katiba, tufanye kazi hii nyingine iliyo mbele yetu,” alisema Pinda.

Kinana amshangaa Lipumba


Na Suleiman Jongo, Mpanda
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimemshangaa Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Profesa Ibrahim Lipumba kutokana na madai yake kuwa CCM imekuwa ikitumia lugha za matusi katika kutetea hoja mbalimbali ndani ya bunge hilo.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Mpanda jana, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema wajumbe wa Bunge hilo wanaotokana na CCM si chanzo cha matusi bali wapinzani ndio wenye kuanzisha matusi bungeni.
“Prefesa Lipumba amewashutumu wajumbe wa CCM akidai wamekuwa wakitumia lugha za matusi. Namshangaa kwa kuangalia upande mmoja wakati wapinzani ndio walioanza lugha chafu, sasa lawama za nini,” alisema.
Kinana aliwataka Watanzania kutoghiribiwa na vitendo vitendo vya wajumbe wa bunge hilo, hususan wanaoshinikiza mfumo wa serikali tatu kwa kuwa si ajenda itakayowaletea maendeleo ya moja kwa moja.
Alisema jambo la muhimu kwa wananchi kufanya kazi kwa bidii kwa kuwa ndio kitu pekee kitakachowaletea maendeleo wakiwa kwenye mfumo wa katiba yoyote.
“Msisikilize propaganda za watu waliokata tamaa, wananchi fanyeni kazi ndiyo itakayokuwekeni kwenye maisha mazuri, katiba mpya haiwezi kukuleteeni chakula cha kila siku. Hata ikipitishwa leo, maisha yatabaki kuwa ni yale yale,” alisema.
Katika hatua nyingine, Kinana aliwataka wanachama wa CCM kuwa wa kwanza katika kuikosoa serikali badala ya kusubiri wapinzani kwa kuwa sio wenye ilani ya uchaguzi inayotekelezwa.
Aidha aliitaka serikali kuondoa urasimu wa kodi kama njia ya kuimarisha uchumi wa wananchi.
“Maisha ya Watanzania hayataweza kubadilika na kupambana na umaskini endapo tutaendelea kuwa na vikwazo vingi vya kodi,” alisema.
Naye Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema kutoka ndani ya bunge kulikofanywa na wajumbe wa upinzani, kunatokana na kulipwa posho wiki nzima za vikao vya Bunge hilo.
“Kama UKAWA wana msimamo wasirudi tena bungeni. Endapo watarudi, ni wazi Watanzania tutawaona wanafanya mchezo wa kitoto,” alisema.
Juzi wajumbe wanaounda UKAWA walisusia na kutoka bungeni kwa madai ya kuchoshwa na lugha za matusi zinazotumika ndani ya Bunge hilo.

Profesa Kayumbo: Lipumba amekosa hekima


NA HAMIS SHIMYE
ALIYEKUWA Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Hosea Kayumbo amesema kitendo kilichofanywa na Profesa Ibrahimu Lipumba kuwahamisha wajumbe wa bunge maalumu kutoka ndani ya bunge ni ukosefu wa hekima na uadilifu.
Pia amesema kitendo cha Profesa huyo kuwafananisha wabunge wa bunge hilo, kutoka Chama Cha Mapinduzi ni waauji wa Intarahamwe ni jambo baya linalopaswa kukemewa na siyo siasa.
Profesa Kayumbo aliyasema hayo jana katika mahojiano na Uhuru, ambapo alisema Profesa Lipumba anapaswa kuzungumza na wenzake na kurudi ndani ya bunge kwa kuwa wanachofanya si demokrasia.
“Imenisikitisha kwa mtu kama Profesa Lipumba kukosa uadilifu na hekima na hata kuwafananisha wabunge kutoka CCM ni wauaji wa Rwanda. Akiwa kama mnyamwezi wa Tabora, alipaswa kuvumilia na hata kutambua kauli yake ina madhara gani kwa jamii,’’ alisema.
Profesa Kayumbo alisema wanasiasa hawagombani bali wanatofautiana kihoja  na kinachofanywa na wajumbe hao kutoka Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (UKAWA) si kitendo cha kiungwana.
Alisema kususua bunge ni kuonyesha kutokomaa kisiasa na ‘poor judgment of events’. Alisema pamoja na kuonyesha uwezo wa kutoa hoja kipindi cha awali, wanapaswa kurudi bungeni.
“Waache hila na warudi bungeni kutetea hoja zao,ambazo awali walikuwa wanazitoa kuhusiana na mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya kama inavyotarajiwa na wananchi,’’alisema.
Profesa Kayumbo alisema kinachofanywa na watu wa UKAWA ni jambo baya na linalotoa taswira mfu katika kujenga mtazamo wa hoja juu ya mchakato mzima wa Katiba Mpya,ambayo watanzania wanaitegemea.

Kilimo kiwe cha tija-Serikali


NA SHAABAN MDOE, ARUSHA 
SERIKALI imewataka  wakulima nchini kuhakikisha kilimo chao kinakuwa chenye tija na kuondokana na kilimo cha mazoea ili kuwezesha sekta hiyo ya kilimo kukua kutoka asilimia nne ya sasa na kufikia asilimia sita inayotakiwa kitaifa.
Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Nkuvililwa Simkanga alitoa wito huo jana alipokuwa akizungumza na wakulima wa mbogamboga, matunda na viungo wa kikundi cha Umoja cha Midawe wakati wa uzinduzi wa kituo cha kuhifadhia mazao kilichopo kijiji cha Midawe kata ya Bang’ata wilayani Arumeru.
Alisema sekta ya kilimo inachangia asilimia 24 ya pato zima la taifa huku ikiwa inatoa ajira kwa zaidi ya asilimia 75, hivyo ili kuongeza pato zaidi, kilimo cha tija kinahitajika ili kuweza kufikia aslimia sita itakayowezesha nchi kupata chakula cha kutosheleza.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya  Chama cha
Wakulima wa Mbogamboga, Maua, Matunda na Viungo (TAHA) , Erick Ng’umanyo alisema  wakulima wengi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto, lakini hawana chombo maalumu cha kuwasemea ,hivyo wao kama TAHA ndio wasemaji wakubwa wa wakulima hao.
Alisema uwepo wa kituo hicho ni baada ya kuchukua jukumu la kwenda wizara ya viwanda na biashara kutokana na wakulima hao kupeleka ombi hilo la changamoto ya ukosefu wa sehemu ya kuhifadhia mazao yao .
Alifafanua kuwa, baada ya wao kuwasemea wizarani, ndipo wizara ya viwanda na biashara ilipochukua jukumu la ufadhili wa jengo hilo kwa kushirikiana na TAHA na hatimaye kuweza kuwasaidia wakulima hao kuondokana na changamoto hiyo.

Wednesday 16 April 2014

Mtikisiko Bungeni



  •  Wajumbe warushiana vijembe, kashfa 
  • Kambi za serikali mbili, tatu zachuana
  • Maalim Seif naye arushiwa makombora

Jane Mihanji na Furaha Omary, Dodoma
VIJEMBE, kebehi, kashfa na mipasho jana viliendelea kutawala katika Bunge Maalumu la Katiba wakati kila upande ukijinadi na kujinasibu kwanini unataka muundo wa serikali mbili au tatu.
Wakati hayo yakiendelea, baadhi ya wajumbe  walimshukia Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad kwa kumtaka aache kuchochea vurugu, badala yake ashirikiane na viongozi wenzake kuimarisha umoja na amani miongoni mwa Wazanzibar.
Panya Ali Abdallah, akichangia sura ya kwanza na ya sita ya Rasimu ya Katiba, alisema Maalim Seif ndiye chanzo cha vurugu kutokana na kauli zake za  kebehi na dharau kwa viongozi wenzake.
Alimtuhumu Maalim Seif kwamba amekuwa akipigia chapuo kurejea kwa utawala wa kisultani visiwani Zanzibar.
“Kuna watu wanayabeza na wanadai hawataki muungano, lakini wanatafuta njia ya kurudi mkoloni. Kwa hatua tuliyofikia, mkoloni harudi tena, wakati wa hewala bwana umekwisha, tunajinafasi na tutaendelea kulinda muungano huo,” alisema Panya.
Alisema wananchi wa Zanzibar wana wasiwasi mkubwa wa kuja  Sultan. “Tuliambiwa mbele ya kadamnasi, hatatawala mweusi, atakuja mwenye ndevu zaidi. Mapinduzi ndio mkombozi wetu, tunamwomba Maalim Seif akae na Dk. Sheni asimamie amani na utulivu,” alisema.
Panya alisisitiza kuwa, ilifika mahali Wazanzibar waliomba serikali ya umoja wa kitaifa na walifanikiwa, hivyo wasilete chokochoko kutaka kuvuruga Muungano na kwamba kamwe hawawezi kukubali muundo wa serikali tatu.
Alikiri kuwepo kwa kero za Muungano, ambazo alisema zinaweza kurekebishwa na sio kuongeza serikali nyingine, ambayo inakuwa mzigo kwa wananchi.
Naye Haji Omar Heri akichangia hoja hiyo, alisema yupo tayari kusimama hadharani katika eneo lolote Zanzibar na kuwaeleza wananchi umuhimu wa muundo wa serikali mbili na kuimarisha Muungano.
Kauli hizo zilikuja baada ya baadhi ya wajumbe kukataa muundo wa serikali mbili walizokuwa wakidai zinawakandamiza na kuwanyima haki Wazanzibar.
“Msitikise kiberiti, kimejaa, Karume aliingia makubaliano ya muungano kwa kutekeleza ilani ya chama chake cha Afro Shirazi, kwamba kuwepo na umoja, elimu, makazi bora ndani ya serikali ya muungano na kwa dhamana ya serikali hiyo, Tumbatu tulipata umeme,” alisema.
Mawaziri SMZ washukiwa
Awali, Hija Hassan Hija, ambaye alikuwa akiunga mkono muundo wa serikali tatu, aliwashutumu mawaziri katika serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwamba wamekuwa na maslahi binafsi.
“Mawaziri wa Zanzibar ukiwanyang’anya madaraka, kesho watadai serikali tatu, hawa walibadilisha katiba, leo wamesahu wanatia ulimi puani,” alisema na kuwaita mawaziri hao kuwa ni wasaka tonge.
Kauli hizo za kuudhi ziliamsha ari kwa wajumbe  kurushiana maneno, ambapo ilimlazimu Mwenyekiti, Samuel Sitta kuangalia lugha wanazotumia. “Tujihadhari, mipasho inazidi kipimo,” alisema Sitta.
Mbaruku Salim Ali alisema Wazanzibar wamechoshwa na muundo wa muungano na kero za muungano zimekuwa tatizo kubwa.
Asiyetaka serikali
mbili aondoke Z’bar
Hoja hiyo ilitupiliwa mbali na mjumbe Mwinyi Haji Makame, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Utawala Bora Zanzibar, aliyesema muundo wa serikali tatu hautekelezeki.
“Ukiona mtu anaanza kutukana, ujue kafilisika, hana ajenda. Sultani ametawala miaka 300, katuachia nini? Mwinyi alishawahi kusema Zanzibar njema, atakaye aje,” alisema na kuongeza: “ Asiyetaka mfumo wa serikali mbili, njia nyeupe.”
Alisema kuna watu wanataka kuuvunja muungano kwa gharama yoyote jambo ambalo haliwezi kuvumiliwa.
Aliwashangaa wajumbe wengi wa Zanzibar kubadilika kwani hoja yao ilikuwa serikali ya mkataba na sio serikali tatu ambayo wameikuta Dodoma.
Abwao awashangaza wajumbe
Katika hali ambayo kila mtu alibaki mdomo wazi,  Chiku Abwao alisimama na kuidai Tanganyika kwa kusema ni heri Muungano uvunjike na Tanganyika ipatikane kwa gharama yoyote.
Chiku alisema licha ya kuwa muumini wa serikali ya shirikisho, hoja ya muungano isiwe mbinu ya kuzima uwepo wa Tanganyika.
Mjumbe Pereila Silima alisema mfumo wa serikali mbili, ambao umekuwepo kwa miaka 50 sasa umewasaidia Watanzania katika nyanja zote na kinachotakiwa ni kukabiliana na changamoto zilizopo.
“Sikubaliani na serikali tatu kutokana na hoja ya kwamba serikali mbili tumekaa nazo kwa miaka 50, siamini mawazo ya kutoka katika serikali mbili twende kwenye tatu,” alisema.
“Jambo linalonitisha ni kusema tuna serikali ya Tanganyika na ya Zanzibar na juu iwepo ya Muungano. Nawaomba wabunge tusijaribu kutoa nafasi mambo yakuwe na yatudhuru, utaifa utaibuka na tutasambaratika,” alisema.
Alisema anapendekeza serikali mbili zitakazofanyiwa marekebisho kwa kuwa kukiwa na serikali tatu, gharama zitaongezeka.
Mjumbe Assumpter Mshana alisema anaamini katika serikali mbili kwa sababu nchi ina amani na utulivu, hivyo kilichopo ni kurekebisha.
“Tulichukua udongo wa Tanganyika na Zanzibar na kuuchanganya na kupata serikali mbili. Hatuwezi leo kuchukua udongo wa Tanzania na Zanzibar na kupata serikali tatu. Hatuko tayari kwenda kinyume na mambo yaliyofanywa na waasisi wetu,” alisema.
Alisema hakuna mtu atakayetenganisha udongo huo, ambao uliunganishwa na waasisi wa nchi. “Hatuko tayari kuweka watu juu ili waning’inie na kula fedha za Watanzania. Kodi za wananchi wanataka barabara, miundombinu, masoko na sio serikali tatu. Hatutaki serikali tatu, tunataka mbili zenye manufaa kwa pande zote mbili,” alisema.
Naye Waridi Bakari Jabu, ambaye ni muumini wa wanaounga serikali mbili, alishangaa kauli za viongozi wa Zanzibar wanaotaka serikali tatu, kwamba wanataka kuwagombanisha Wazanzibar na Tanzania Bara.
“Viongozi wa CUF wamekusudia kutugombanisha kati ya Tanzania Bara na Zanzibar. Watuambie hati ya makubaliano kati ya Unguja na Pemba ililetwa hapa tuione. Hati ya Muungano tumeiona,” alisema.
Waridi alisema viongozi wanaojiita Wazanzibar, ambao ni wa CUF, sio wote wanataka kuvunja Muungano, kwa kuwa wengi wanataka Zanzibar iendelee na muungano wa serikali mbili.
Maige awashangaa wanaolalamika
Naye Ezekiel Maige alisema haoni sababu kwa nini Zanzibar inalalamika kunyonywa, ilhali inanufaika zaidi kiuchumi, chini ya mwamvuli wa Serikali ya Muungano.
Alisema hivi sasa Zanzibar imekuwa ikipata huduma za jamii nyingi bure, ikilinganishwa na Tanzania Bara, na kwamba licha ya maisha magumu watu wanayoishi, hawakuwahi kuilalamikia Zanzibar.
“Bara tumekuwa wavumilivu sana, lakini hakuna asiyejua kwamba wilaya zote za Zanzibar zina lami, huduma za hospitali bure pamoja na shule,” alisema.
Maige alishauri wakati umefika kutatua kero za muungano, ikiwa ni pamoja na muungano usiwe kwenye hadhi ya vyama vya siasa, badala yake usimamiwe kwa utaratibu utakaowekwa kisheria.
Pindi Chana alisema serikali mbili hazikwepeki na suala la serikali tatu lisifanyiwe majaribio kwa Watanzania.
“Watanzania wengi wanataka serikali mbili, japo kuwa ina changamoto, lakini serikali tatu ndiyo zenye changamoto nyingi zaidi. Leo watu wameufyata, nchi haiendeshwi kienyeji.
Serikali mbili hazikwepeki, hiyo habari ya serikali tatu, ambayo hatujawahi kuiona, tunataka kuitesti, basi tusitesti kwa Watanzania ambao hawajatutuma,” alisema.
Vijembe vyatawala bungeni
Katika hali ya kushangaza, wajumbe wa bunge hilo kutoka Zanzibar waliamua kurushiana vijembe, ambapo Salehe Nassoro Juma, ambaye ni muumini wa serikali tatu, alimshambulia Asha Bakari Makame.
Salehe alisema: “Namshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kuanzisha mchakato na anastahili kutunukiwa nishani aliyopewa hivi karibuni. Nyerere na Karumeru wamezeeka na wamazo yao yamezeeka,” alisema.
Mjumbe huyo alisema anataka kumsaidia mama huyo kutokana na kumtukana mwanaume, kwa kuwa wamefanya utafiti na kutambua kuwa naye hana mume.
“Baba yake Jusa (mjumbe wa bunge hilo), alipata usingizi hapo, tunataka tushirikiane, Jusa tumposee mke,” alisema mjumbe huyo

Seif: Hakuna anayetaka Muungano uvunjike


WILLIAM SHECHAMBO NA MUSSA YUSUPH
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad amewataka wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutopuuzia mawazo ya makundi yaliyopo katika bunge hilo kuhusu mfumo wa Serikali utakaofaa kuwemo kwenye katiba mpya.

Alisema mawazo ya muundo upi wa Serikali utakaofaa kuwepo kwenye katiba hiyo ni lazima ulenge katika kuimarisha Muungano uliopo baina ya Tanyanyika na Zanzibar.
Makamu huyo wa kwanza wa Rais alisema ni lazima wajumbe wafahamu kuwa, hakuna Mtanzania anayependa Muungano uliopo uvunjike baada ya kudumu kwa takribani miaka 50 ya mafanikio na kwamba rasimu ya pili ya katiba imethibitisha hilo kwa kuonyesha kuna idadi ndogo ya watu wasiopenda kabisa kuwepo kwa Muungano.
Maalim Seif alisema hayo jana alipokuwa akifungua Maonyesho ya Miaka 50 ya Muungano kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja,
Dar es Salaam jana, ambayo yamehusisha taasisi na idara za serikali zinazohusika na mambo ya Muungano.
Alisema ni vizuri kuepuka maamuzi yatakayovunja Muungano.
Maalim Seif alisema pia kuwa, ili kupata katiba bora, wajumbe wa bunge hilo wanapaswa kusikilizana kila mmoja na hoja yake, ambayo inatetea muundo wa serikali anayotaka na kisha kuichuja kwa kuzingatia maslahi ya Muungano kwa kuwa kuwepo kwa fikra tofauti katika eneo fulani ndio chanzo cha maendeleo.
Makamu wa Kwanza wa Rais alitumia nafasi hiyo kuwasihi wananchi kufuatilia kwa ukaribu mijadala inayoendelea Bungeni na kuhakikisha wanatumia nafasi yao muhimu ya kupiga kura ya kupitisha katiba kwa kusimamia uwepo wa Muungano na si vinginevyo.
“Watanzania tunapaswa kuhakikisha tunaulinda na kuudumisha Muungano kwenye katiba ijayo kwa kupiga kura baada ya kutathmini mafanikio yake tuliyoyapata tangu mwaka 1964 mpaka sasa,” alisema.
Alisema hatua ya Rais Jakaya Kikwete kuridhia kuwepo kwa mchakato wa katiba mpya, ikiwa ni kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano, ni busara iliyojaa nia ya kizalendo, kwa kuwa alitoa nafasi ya kutathmini mustakabali wa Taifa kwa kipindi cha miaka 50 mingine ijayo ya Muungano.

Tembo wazusha balaaNa Chibura Makorongo, Bariadi


KUNDI la tembo wapatao 46 kutoka katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, wamevamia makazi ya watu na kufanya uharibifu mkubwa wa mazao na vyakula vilivyokuwa vimehifadhiwa katika kijiji cha Mwachumu kata ya Girya, wilayani Bariadi.
Diwani wa kata hiyo, Safari Lewa, alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 10:00 jioni.
Alisema  tembo hao wameharibu mazao mbalimbali yakiwemo mahindi na pamba katika mashamba ya wananchi.
Lewa, alisema zaidi ya hekari 60 za mazao ya mahindi na pamba zimeharibiwa vibaya na wakazi wa kijiji hicho wanahofia kushambuliwa na tembo hao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Abdallah, alikiri wanyama hao kuvamia maeneo hayo.
Alitoa rai kwa wakazi na viongozi wa maeneo hayo kutoa taarifa mapema pindi wawaona tena ili hatua za kuwarudisha hifadhini zichukuliwe haraka

Dk. Magufuli, we acha tu


NA WILLIAM SHECHAMBO
MKUTANO wa Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), uliopangwa kufanyika jana, mkoani Tanga, umesitishwa kwa agizo la  Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli.

Inadaiwa kuwa kafanya hivyo ili kutoa fursa kwa wahandisi kuongeza nguvu kwenye ukarabati wa miundombinu iliyoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha nchini.
Agizo hilo lilisababisha ratiba ya taasisi hiyo ya serikali ya kuendelea na mkutano mkoani Tanga kupigwa kalenda.
Akizungumzia hatua hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Alhaj Mussa Iyombe, alisema mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu nchini, hali inayowalazimu watendaji kufanya kazi kadri inavyowezekana ili kurudisha huduma katika hali ya kawaida.
Awali, Waziri Magufuli alipokuwa akikagua uharibifu uliotokea katika daraja la Mpiji Bagamoyo, mkoani Pwani, alisema TANROADS wanatakiwa kuhakikisha wanafanyakazi mchana na usiku ili barabara hiyo muhimu na yenye kupitisha magari mengi ifunguliwe haraka iwezekanavyo.
Dk. Magufuli, alisema shughuli za uchimbaji wa mchanga zinazofanywa karibu au chini ya madaraja na maeneo ya karibu na barabara, ndicho chanzo cha mito kuhama kutoka katika njia yake ya asili na kuharibu miundombinu ya barabara.
Aliwatahadharisha wananchi kuepuka tabia hiyo.
Mvua kubwa zilizonyesha katika maeneo mbali mbali nchini toka wiki iliyopita, zimesababisha madhara makubwa kwa upande wa miundombinu ya barabara kwa kusomba madaraja na kuvunja kingo za mitaro.
TANROADS kwa kushirikiana na kampuni za ujenzi za SKOL na Estim Construction Company Ltd zote za Dar es Salaam, tayari wameanza kazi za kurekebisha sehemu kadhaa ikiwemo daraja la Mpiji

TPB yajidhatiti kutoa huduma bora


NA RABIA BAKARI
BENKI ya Posta Tanzania (TPB), imejidhatiti kuendelea kutoa huduma za kisasa kwa mfumo wa teknolojia.
Pia, imesema imepata mafanikio kwa kuongezeka mapato kutoka bilioni 31 hadi kufikia bilioni 38 kwa mwaka jana.
Hayo yalielezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TPB, Sabasaba Moshingi, alipokuwa  akizungumza na waandishi wa habari jana, Dar es Salaam kuhusu mafanikio na changamoto za uendeshaji wa benki hiyo.
Alisema mpaka sasa kuna huduma mbalimbali za kielektroniki, ikiwemo ya huduma za fedha kwa mtandao, pamoja na huduma ya TPB Popote, na mwaka huu kunamipango madhubuti ya kuiboresha.
Alisema benki hiyo ina wateja zaidi ya 670,000, ikiwa ni ongezeko la wateja 70,000 kutoka mwaka jana mpaka mwaka huu.
Kwa upande wa faida, Moshingi alisema TPB imepata sh. bilioni 6.99 ambazo ni kodi kutoka  bilioni 5.6, mwaka juzi.
Aliongeza kuwa, mapato kwa ujumla yameongezeka na kufikia sh. bilioni 38.8 mwaka huu kutoka sh. bilioni 31 mwaka jana, sawa na ukuaji wa asilimia 24.
Alisema amana za wateja ziliongezeka na kufikia bilioni 170 kutoka bilioni 138 kwa mwaka 2012 sawa na asilimia 22.
Pia alisema faida iliyotokana na mikopo imeongezeka hadi kufikia bilioni 119.7 kutoka bilioni 100.8 sawa na ongezeko la asilimia 18.7

Friday 11 April 2014


Hati za Muungano, serikali mbili moto


NA WAANDISHI WETU, DODOMA

HATI za Muungano na muundo wa serikali vimeendelea kuzua mjadala mkubwa miongoni mwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, ambapo baadhi wamesema hayo ndio masuala ya msingi. 
Wajumbe wengi wameendelea kupinga hadharani mapendekezo ya serikali tatu huku wakitaka kuwasilishwa kwa Hati za Muungano halisi kwa madai kuwa ndizo zitamaliza sintofahamu iliyopo kwa sasa.
Hayo yalijitokeza jana wakati baadhi ya Wenyeviti wa Kamati za Bunge walipowasilisha taarifa za kamati zao, ambapo Assumpter Mshama alisema kamati yake imekataa mapendekezo ya serikali tatu na wajumbe wametaka mfumo wa serikali mbili uendelee.
Assumpter, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati namba 5, alisema muundo wa serikali tatu umekataliwa na theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na kutoa mapendekezo.

“Muundo wa serikali mbili ndiyo ulioafikiwa na wajumbe wengi kuwa unalifaa taifa letu kwa kuzingatia maslahi ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiusalama kwa wananchi wa pande zote,’’ alisema.

Alisema muundo huo umedumu kwa miaka 50 na zimekuwepo changamoto mbalimbali ambazo nazo zimekuwa zikitatuliwa na serikali za pande zote mbili.

Aliongeza kuwa mchakato unaoendelea sasa ni fursa kubwa na ya pekee kuzishughulikia changamoto hizo kwa mapana yake.

“Mapendekezo yaliyotolewa na walio wengi yanalenga kuzipa jitihada hizi kinga za kikatiba na kisheria ili ufumbuzi wake uwe endelevu," alisema.

Alisema endapo muundo utakuwa wa serikali tatu, serikali hiyo ya tatu itakuwa inayoelea, iliyo mbali na wananchi, tegemezi na yenye gharama kubwa kiuendeshaji.

Akizungumzia sababu ya kufanya mapendekezo ya marekebisho hayo, Assupter alisema ni ukweli kuwa hati ya makubaliano ya Muungano ndiyo msingi wa muundo wa serikali mbili uliopo sasa.
Mwenyekiti wa Kamati Namba Mbili, Shamsi Vuai Nahodha, akiwasilisha mapendekezo ya kamati yake, alisema shirikisho la serikali tatu linalopendekezwa katika rasimu, litakuwa dhaifu kiasi cha kushindwa kudhibiti ulinzi wa eneo la Bahari ya Hindi.
Alisema udhaifu huo utayapa mwanya mataifa hayo kuzirubuni nchi washirika zisichangie gharama za uendeshaji wa Serikali ya Shirikisho, hasa kwa kuwa halitakuwa na vyanzo vya uhakika vya mapato.

HATI ZA MUUNGANO MOTO
Baadhi ya wajumbe wa Kamati za Bunge Maalumu la Katiba wamesisitiza kuwasilishwa kwa Hati ya Muungano halisi ili kumaliza utata uliojengeka miongoni mwa wajumbe.

Wamesema maelezo ya aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika wakati nchi mbili za Tanganyika na Serikali ya Watu wa Zanzibar zikiungana, kwamba Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliifuta Tanganyika, yanatia shaka.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Dk. Emmanuel Makaidi, aliyekuwa akitoa ufafanuzi kuhusu hoja za wachache wasiokubaliana na mfumo wa serikali mbili.
Alitoa ufafanuzi huo baada ya Mwenyekiti wa Kamati namba mbili, Shamsi Vuai Nahodha kusoma taarifa ya kamati hiyo.

"Kama hati hiyo ipo, tunaomba iletwe hapa wajumbe waione. Hati ya mashaka mashaka haiwezi kujenga katiba mpya," alisema na kuongeza hati ya muungano ndio msingi wa katiba.

Awali, akisoma maoni ya wajumbe wachache wa kamati hiyo juu ya utata wa uwepo wa uhalali wa hati ya muungano, Shamsi alisema wajumbe hao wanasema pamoja na ujio wa Msekwa, alishindwa kuwathibitishia uwepo wa uhalali wa hati hiyo pamoja na ile ya maridhiano, badala yake aliwaambia anaikumbuka siku ile ya Muungano na anazo picha, vitu ambavyo haviondoi utata uliopo.

"Ukweli ni kwamba mpaka sasa wajumbe wa Bunge hili wameshindwa kupata nyaraka hizi mbili zenye saini zinazothibitisha kuwa pande zote mbili ziliridhia uwepo wa Muungano. Hati ya maridhiano, ambayo iliwasilishwa kwa wajumbe wa kamati, ilikuwa ni batili kwa sababu mbalimbali, ikiwemo ya kughushiwa kwa saini ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Msekwa," walisema wajumbe hao katika maoni yao.

Kwa mujibu wa wajumbe hao, makosa hayo pamoja na mengine mengi yamechochea utata juu ya Muungano na kumekuwepo kwa malumbano ya viongozi mbalimbali juu ya uhalali wa nyaraka ambazo walipewa huku kukiwa na shaka ya kughushiwa kwa saini hizo.

Wajumbe hao wanasema Aprili 22, 1964, Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, Mwalimu Nyerere na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, inasemekana walitia saini Hati ya Makubaliano ya Muungano kati ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.

"Wakati wa mjadala wa Sura ya Kwanza na ya Sita, wajumbe wa kamati kama ilivyokuwa kwa wajumbe wa kamati nyingine, waliletewa nakala ya Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano, Sheria Namba 22 ya 1964, ilitolewa baada ya baadhi ya wajumbe kuomba kupatiwa nakala halisi ya kweli ya Hati ya Makubaliano ya Muungano iliyotiwa saini na Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume.

"Japokuwa nakala ya sheria ya kuthibitisha mapatano ya muungano iliyogawiwa kwa wajumbe imeambatanishwa na Hati ya Makubaliano ya Muungano kati ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kama nyongeza ya sheria hiyo, hicho sicho walichoomba wajumbe wa Bunge Maalumu,"  walisema wajumbe hao.

Wajumbe hao walisema pia kuwa nakala ya Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano haiwezi kuwa mbadala wa nakala halisi ya hati hiyo kwa sababu nyongeza ya sheria waliyogawiwa wajumbe, ambayo inadaiwa kuwa ndio hati ya makubaliano ya muungano, haina saini za Mwalimu Nyerere na Hayati Karume.

Kwa mujibu wa wajumbe hao, ni vigumu katika hali hiyo kuthibitisha kama kweli kile kilichodaiwa kuwa ni hati ya makubaliano ya muungano, ndicho hicho walichokubaliana waasisi hao wa Muungano kwa kutia saini zao.

"Suala la kushindwa kupatikana kwa nakala halisi ya Hati ya Makubaliano ya Muungano sio jambo dogo. Suala hili ndio ufunguo wa kuelewa mgogoro mkubwa wa kikatiba na kisiasa, ambao umegubika Muungano katika nusu karne ya maisha yake,” alisema.

Katika majadiliano ya awali ya kamati hiyo, wajumbe hao wachache walidai kuwa saini ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Julius Nyerere iligushiwa.
Mbali na saini hiyo, pia saini ya aliyekuwa Spika wa Bunge wakati huo, Pius Msekwa nayo ilidaiwa kughushiwa na hivyo kumtaka Msekwa kwenda katika kamati kuthibitisha saini hizo.

David Kafulila, akitoa maoni ya walio wachache kupitia kamati namba tano, alisema nia ya kuwepo kwa serikali tatu si kuulegeza Muungano. Alisema watu wachache katika kamati hiyo waliona jina la shirikisho ndio sahihi.

"Hatutaki serikali tatu zitakazolegeza muungano, tunataka serikali tatu zitakazokuza muungano,” alisema na kuongeza kuwa hakuna shaka juu ya uendeshaji wa serikali ya muungano huku akitoa hoja kuwa Tanzania Bara itapaswa kuchangia zaidi kutokana na ukubwa wake.

MAKONDA: ACHENI KUSHUPALIA HATI

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Paul Makonda amewaasa wajumbe wenzake kujadili mambo yaliyoko kwenye Muungano badala ya kushupalia hati halisi.

Kauli hiyo ya mjumbe huyo, ilikuja baada ya baadhi ya wajumbe wa bunge hilo, akiwemo John Mnyika, kushinikiza Hati ya Muungano iwepo, hoja iliyozua malumbano miongoni mwao.
Japokuwa hoja ya Mnyika ya kutaka wapewe kinga ya kuitumia ili waboreshe michango yao watakayoiwasilisha bungeni ilikubaliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Othuman Masoud, mjumbe Christopher Ole Sendeka aliipinga kwa utetezi kuwa ina kinga na haipaswi kutumiwa na wajumbe hao.
Katika taarifa yake aliyoituma kwenye vyombo vya habari jana, Makonda aliwaasa wajumbe wenzake waendelee kujadili rasimu ya Katiba Mpya kwa kutumia rasimu badala ya kutaka hati.

"Kama kuna hoja ya msingi kuhusu mchakato huu, basi iwekwe mezani, si kuweka viashiria vya sababu," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Makonda, ambaye pia ni Katibu Uhamasishaji na Chipukizi wa UVCCM, alikumbusha kuwa kila kilichoafikiwa katika Muungano, kilikuwa cha kikanuni na kisheria, hivyo kilicholeta uhai wa muungano huo ni ukamilishwaji wa taratibu za kuutangaza Aprili 26, 1964.

"Sote tumeapa kwa huo Muungano na kwa tafsiri tu kuwa Muungano upo na ulikuwepo. Tunayoweza kujadili ni mambo yaliyoko katika Muungano na si kujadili makaratasi ya muungano," iliongeza sehemu ya taarifa hiyo.

Bilionea akufuru Maliasili

  • Ni Howard Buffet aliyetoa helkopta kwa JK
  • Amwaga Bil. 8.5/= kupambana na majangili
  • Jangili aliyeua faru, askari auawa kwa risasi
Na waandishi wetu
BILIONEA wa Marekani, Howard Buffet ameahidi kutoa zaidi ya sh. Bilioni 8.5 kusaidia harakati za serikali katika kupambana na ujangili nchini.
Sehemu ya fedha hizo zitakwenda kusaidia shughuli za uhifadhi wa wanyamapori katika hifadhi na mapori ya akiba.
Buffet, ambaye ni mtoto wa bilionea anayeshika nafasi ya pili kwa utajiri nchini Marekani, Warren Buffet, alitangaza neema hiyo jana, ambapo fedha hizo zitatumika kununua helkopta, magari ya doria, mafunzo kwa askari wa wanyamapori na kujenga mabweni katika Chuo cha Wanyamapori cha Pansiasi.
Mpango huo ni kuunga mkono hatua madhubuti zinazochukuliwa na serikali ya Rais Jakaya Kikwete kushinda vita dhidi ya ujangili. 
Akizungumza na watumishi na askari wa wanyamapori katika Chuo cha Pansiansi jijini Mwanza jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ambaye aliambatana na Buffett na ujumbe wake kutoka Marekani, alisema huo ni mkakati wa kutekeleza mpango wa kutokomeza ujangili alioutangaza Machi 13, mwaka huu.

Serikali imechukua hatua madhubuti kuongeza vitendea kazi, rasilimali watu na miundombinu muhimu kwa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN). Tunashirikiana na wadau wa uhifadhi na jumuia za kimataifa kuhakikisha taifa linashinda vita dhidi ya ujangili,  alisema.
Alisema Buffett ni mdau mkubwa wa masuala ya uhifadhi na kwamba hatua yake ya kuunga mkono jitihada za serikali ni ushirikiano mpya baina ya Tanzania na Taasisi ya Howard G Buffett Foundation (HGBF).

Taasisi ya Buffet imetoa helkopita kwa ajili ya Pori la Akiba la Selous na kutoa mafunzo kwa marubani wane. Serikali pia imeagiza helkopita zingine, alisema Nyalandu.
Alisema taasisi hiyo pia itakodi helkopta zingine kwa ajili ya doria, ambazo zitakuwa chini ya usimamizi wa Idara ya Wanyamapori kwa kipindi cha miezi sita kusubiri mpya ambayo inaendelea kutengenezwa kiwandani.
Pia ameahidi kuboresha miundombinu katika Chuo cha Pansiansi pamoja na kuimarisha mafunzo kwa askari wanyamapori nchini.
Misaada mingine iliyotolewa na Buffet ni magari matano ya doria, kujenga mabweni sita kwa ajili ya wanafunzi, jiko la kisasa pamoja na karakana kwenye chuo hicho.
Pia itahusisha ununuzi wa mabasi mawili aina ya Scania, malori, mahema na vifaa vingine ambavyo vitatumiwa na wanafunzi wa chuo hicho, lengo likiwa ni kuboresha taaluma hiyo na kuwajengea ari ya kulinda maliasili askari wa wanyamapori.

Jangili aliyeua faru auawa
Katika hatua nyingine, Polisi mkoani Simiyu kwa kushirikiana na askari wa Idara ya Wanyamapori
katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, wamemuua jangili sugu Majadiga Makabajinga au Mashaka Sai, kwa kumchapa risasi ya mgongo.
Sai, ambaye alikuwa akisakwa kwa muda mrefu, anatuhumiwa kuwa kinara wa ujangili na aliuawa wakati akipambana na polisi alipojaribu kuwatoroka baada ya kutiwa mbaroni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo, alisema Sai aliuawa juzi saa 3:00 usiku katika kijiji cha Mwasinansi wilayani Bariadi.
Alisema mtuhumiwa huyo alitiwa mbaroni na baada ya kuhojiwa alikiri kuhusika kwenye matukio mbalimbali ya ujangili pamoja na kifo cha askari wa wanyamapori.
Mbali na kuhusika kwenye matukio hayo, Sai alikuwa akiwafanyia ukatili ikiwa ni pamoja na kuwaua raia aliowahisi wanatoa taarifa zake kwa vyombo vya usalama.

Alibanwa na kukiri kuhusika na ujangili na siku nyingi tulikuwa tunamsaka. Ndiye alihusika na mauaji ya faru katika Hifadhi ya Serengeti (Mama Serengeti), alisema Kamanda Mkombo.
Hata hivyo, alisema baada ya mahojiano hayo, askari walimtaka awapeleke mahali anapohifadhi silaha, ndipo alipowapeleka katika kijiji cha Mwasinasi, ambapo awalionyesha sehemu ya kichaka.
Wakati askari wakifanya upekuzi kutoa silaha hizo, Sai alichukua mti na kumshambulia askari wa wanyamapori Christian Mlema kichwani kisha  kumpora silaha na kuanza kufyatua risasi hewani.
Polisi walianza kujibu na kufanikiwa kumpiga risasi mgongoni na kudondoka.
Katika kichaka hicho, polisi walikuta bunduki mbili SMG iliyokuwa na magazine mbili na SR moja, zote zikiwa na risasi 50 pamoja na meno ya tembo.

Viongozi wa dini wawajia juu watendaji wa serikali


NA SULEIMAN JONGO, KASULU

VIONGOZI wa madhehemu mbalimbali ya dini wilayani Kasulu mkoani Kigoma, wamewajia juu watendaji wa serikali kwa kuendekeza rushwa, hali inayosababisha kukosekana kwa haki miongoni mwa jamii.

Wamemuomba Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kuisimamia serikali katika vita dhidi ya tatizo hilo ili kutoa fursa kwa wananchi kupata huduma bila mizengwe.

Akizungumza katika mkutano kati ya Kinana na viongozi wa dini uliofanyika wilayani humo, Mchungaji wa Kanisa la Assembly of God (EAGT) wilayani humo, Edward Bakana alisema rushwa imesababisha hali ya upatikanaji huduma kuwa ya hovyo ikilinganshwa na malengo ya serikali.

“Rushwa katika Kasulu yetu imekuwa mbaya, kitu ambacho hakimpendezi Mungu.
Ili mwananchi apate huduma, lazima atoe rushwa. Hali hii haipaswi kufumbiwa macho," alisema.

Alisema rushwa imesababisha baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wilayani humo kupitishia bidhaa zao katika nchi za Kenya, Rwanda na Burundi badala ya Kasulu ambayo ni rahisi zaidi.

“Kama kweli tunataka maendeleo, hali hii lazima ifanyiwe kazi kuhakikisha huduma zinapatikana kwa urahisi kisheria bila kuwepo urasimu," alisema.

Mchungaji huyo alisema anaishangaa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kuelemewa na kutofuatilia vitendo vya rushwa vilivyoko wilayani humo.

Naye Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) wilaya ya Kasulu, Sheikh Kabaka Athuman alimuomba Kinana kuitazama polisi wilayani humo, kutokana na kukithiri kwa madai ya askari wake kuongoza kwa kuomba na kupokea rushwa.

“Sisi viongozi wa dini tunaomba tatizo hili la rushwa lishughulikiwe kwa kuwa ni miongoni mwa mambo makubwa yanayosababisha wananchi kuichukia serikali, ambayo imekuwa ikijitahidi kutafuta huduma mbalimbali na kuwaletea wananchi, hasa huduma za afya bure kwa wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano," alisema.

Akizungumza kuhusu hoja ziliziotolewa, Kinana aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanashirikiana na serikali ili kutatua changamoto za wananchi na kuepusha mgawanyiko wa kiimani ambao ni hatari kuliko kitu chochote.

Kuhusu tuhuma za rushwa kwa taasisi za serikali, Kinana alimuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo, Dani Makanga kuzifanyia kazi na kuondoa kero hiyo.

Mbio za Mwenge kuzinduliwa Kagera


NA KHADIJA MUSSA

MKOA wa Kagera unatarajia kuzindua miradi ya maendeleo yenye thamani ya sh. bilioni 14 katika hafla ya uzinduzi wa mbio za mwenge, itakayofanyika Mei 2, mwaka huu.

Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, ambapo wananchi zaidi ya 30, 000 wanatarajiwa kuhudhuria, wakiwemo viongozi wa ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkuu wa mkoa huo, Kanali Mstaafu Fabian Massawe alisema miradi ikayozinduliwa ni ya sekta za afya, elimu na uchumi.

Alisema baada ya kuzinduliwa kwa mwenge huo, utakimbizwa katika halmashauri nane za mkoa huo, ambako utazindulia miradi hiyo ya maendeleo.

Massawe alitumia fursa hiyo kuwaomba wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, kujitokeza kwenda kuwekeza katika mkoa huo, ambao una fursa nyingi.

Alisema kauli mbiu ya mbio hizo kwa mwaka huu ni 'Katiba ni sheria kuu ya nchi, watanzania wajitokeze kupiga kura ili wapate katiba bora.

Mvua kuongezeka nchini- TMA


NA MWANDISHI WETU

MAMLAKA ya Hali ya Hewa nchini (TMA), imetoa tahadhari ya uwepo wa mvua kubwa inayozidi milimita 50 kuanzia leo hadi Jumatatu.

Kufuatia kuwepo kwa mvua hiyo, mamlaka imewataka wakazi wa maeneo hatarishi, watumiaji wa bahari pamoja na mamlaka zinazohusika na maafa, kuchukua tahadhari stahiki.

Mikoa inayotarajiwa kupata mvua hiyo ni ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Visiwa vya  Unguja na Pemba na uwezekano wa kusambaa katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Morogoro.

“Hali hii inatokana na kuimarika zaidi kwa ukanda wa mvua 'Inter-tropical convergence zone (ITCZ)', ambao umeambatana na ongezeko la unyevunyevu katika eneo la bahari ya Hindi,” ilisema taarifa hiyo.

Mvua hiyo inatarajiwa kuambatana na upepo mkali unaozidi kilometa 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayofikia mita mbili katika ukanda wa pwani.

Moto wateketeza bweni la wanafunzi Dar

NA JESSICA KILEO

MOTO umezuka ghafla kwenye bweni la shule ya sekondari ya Father  Andrew  Memorial na kuliteketeza lote pamoja na mali zilizokuwemo ndani yake.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 6.00 usiku katika shule hiyo iliyoko katika
maeneo ya Salasala IPTL, Kinondoni, Dar es Salaam.

Wambura alisema moto huo ulizuka ghafla kwenye bweni la wavulana, mali ya shule hiyo na kulitekeleza lote, ikiwa ni pamoja kuharibu mali zilizokuwamo ndani yake.

Alisema hakuna madhara yoyote yaliyotokea kwa binadamu na kwamba tukio hilo lilitokea wakati wanafunzi wakiwa likizo.

Kamanda Wambura alisema chanzo cha moto huo bado hakijafahamika na upelelezi unaendelea.

Wakati huohuo, watu sita wamekamatwa katika maeneo ya Kariakoo wakiwa na dawa za kulevya pamoja na pombe haramu aina ya gongo.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alisema jana kuwa watu hao walikamatwa juzi saa 12.00 jioni maeneo ya Livingstone, Kariakoo.

Marietha alisema kukamatwa kwa watu hao kumetokana na msako maalumu uliofanywa na jeshi hilo.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Ashrafu Bashiri (32), Japhet Komba (40) na wenzao wanne.

Alivitaja vitu walivyokamatwa navyo kuwa ni bunda moja la mirungi pamoja na lita mbili za pombe haramu aina ya gongo.