Na MUSSA YUSUPH
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema uraia wa nchi mbili kwenye katiba mpya ni suala muhimu linalohitaji kuwepo kwa manufaa ya Watanzania wote.
Alisema wao kama Wizara, wamejipanga kuhakikisha wanaitetea hoja hiyo pindi itakapojadiliwa kwenye bunge la Katiba linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma.
Membe alisema Watanzania wengi waliopo nje ya nchi wanashindwa kushiriki katika fursa za kimaendeleo nchini kutokana na kuwa na uraia wa nchi zingine, baada ya kuomba huko na kupewa.
Alisema watanzania hao hukataliwa pia kupata huduma za kiupendeleo kama mikopo ya nyumba, fedha na hata huduma za afya kutokana na kukosa uraia kamili wa nchi hizo.
“Tuwasaidie kupata Uraia wa Tanzania na tutapigania, ikiwa mgeni anayeishi nchini kwa muda wa miaka 10 anapewa uraia wa Tanzania. Je kuna tatizo gani Mtanzania mwenye uraia wa nje nayea akapewa uraia,” alihoji Membe.Alisema wamejipanga kutetea hoja hiyo, ili watanzania wenye uraia wa nchi za nje nao wapate uraia wa Tanzania ili waweze kushiriki katika fursa muhimu za kimaendeleo ndani na nje ya nchi.
Hivyo, alisema kuna umuhimu wa kuandaa utaratibu wa sheria na kanuni za kila mtanzania kupata haki hiyo pasipo kuasili usalama na maendeleo ya nchi.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru