Wednesday, 19 February 2014

Mzee Makamba awapasha Lowassa, Membe

  • Awataka watumikie adhabu kwa uadilifu
  • Adai angekuwa yeye angekata rufani
  • Wasomi: CCM ni makini na imekomaa

Na Khadija Mussa

Yusuph Makamba - Katibu mkuu mstaafu wa CCM
ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba, amewataka makada sita waliopewa onyo kwa kukiuka utaratibu wa Chama kutumikia kwa uaminifu na uadilifu.
Pia, alisema adhabu iliyotolewa kwa makada hao haikupaswa kulingana na kwamba, kila mmoja angepewa adhabu kwa kuzingatia makosa aliyokutwa nayo.
Makada hao ni pamoja na Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na wabunge Edward Lowassa (Monduli) na William Ngeleja (Sengerema), walitiwa hatiani kwa kukiuka utaratibu wa CCM.
Walituhumiwa kuanza kampeni za urais katika uchaguzi mkuu ujao kinyume cha utaratibu hivyo, kuvuruga utaratibu wa Chama, ambapo Kamati Ndogo ya Maadili iliwaita kuwahoji.
Juzi, Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alitangaza kuwa makada hao wamepewa onyo kali na Chama kinaendelea kuchunguzwa mienendo yao kwa miezi 12 pamoja na kuzuiwa kugombea nafasi yoyote ya uongozi ndani ya Chama.
Hata hivyo, akizungumza na Uhuru jana kuhusiana na hatua zilizochukuliwa dhidi ya makada hayo, Makamba, alisema wanatakiwa kutumikia adhabu hiyo kwa uaminifu na uadilifu kama Nabii Ayoub.

“Nawaomba wawe wavumilivu kama Nabii Ayoub, na watumike adhabu hiyo kwa uaminifu na uadilifu.
“Wakifanya hivyo, watamaliza adhabu zao na watapata fursa ya kugombea tena nafasi za uongozi ndani ya Chama,’’ alisema Makamba.
Hata hivyo, alisema iwapo angekuwa yeye angekata rufani kwa kuwa adhabu hiyo imetolewa kwa ujumla huku makosa yaliyowatia hatiani makada hao yakitofautiana.
Alisema adhabu zilipaswa kuwa tofauti kulingana na makosa, kwani anasikia wapo waliotoa fedha kwa wanachama huku mafungu yanayotajwa yakitofautiana.
Naye Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema hatua zilizochukuliwa na CCM dhidi ya makada hao inaonyesha namna kinavyo jipambanua kuwa ni makini na hakikurupuki.
Alisema CCM imekuwa ikisimamia nidhamu na misingi iliyojiwekea jambo ambalo litaendelea kukifanya kiimarike zaidi tofauti na vyama vingine.

“Nidhamu ni jambo zuri, hatua zilizochukuliwa dhidi ya makada wake ambao ni maarufu na wameshika nyadhifa kubwa serikalini, itasaidia kukiimarisha Chama,” alisema Dk. Bana.
Pia, alisema kilichofanywa na CCM ni funzo kwa vyama vingine vya siasa nchini katika kusimamia kanuni badala ya kukurupuka na kufukuza wanachama ama viongozi bila utaratibu.
Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Mohammed Bakari, alisema suala la kufuata utaratibu na sheria ndani ya chama ni zuri na muhimu.
Pia, aliipongeza CCM kwa kutoa onyo kali kwa makada wake ambao wamethibitika kwenda kinyume na kuvuruga utaratibu.

“Napongeza hatua zilizochukuliwa, mwenendo waliokuwa wakienda nao makada hawa haukuwa sahihi kwa mustakabali wa kanuni, hivyo CCM ipo sahihi katika hili,” alisema.
Alisema ni lazima CCM iendelea kuimarisha na kusisitiza matumizi ya kanuni zake inazotumia katika kuwapata viongozi kwani mambo yalivyokuwa yalianza kuwavuruga wanachama.
“Chama kibaki na kanuni na utaratibu wake katika kuwapata viongozi, mambo yalivyokuwa yakipelekwa si sahihi na ingeachwa ingewavuruga wanachama na kusababisha mpasuko mkubwa,’’ alisema.
Akitangaza adhabu hizo mbele ya waandishi wa habari juzi, Nape alisema Kamati Kuu ya CCM, imeiagiza Kamati Ndogo ya Udhibiti kuendelea kuwachunguza na kuchukua hatua kali kwa makada hao iwapo watakiuka onyo hilo.
Pia, imeagiza mawakala na wapambe wa makada hao walioshiriki kukivuruga Chama nao wachunguzwe na kuchukuliwa hatua kali.
Kwa mujibu wa Nape, waliohojiwa walithibitika kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea urais kabla ya wakati kinyume na kanuni za uongozi na maadili za CCM toleo la Februari 2010, ibara 6 (7) (i).
Pia, walithibitika kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya Chama na baadhi yao kukiuka maadili ndani ya jamii, jambo ambalo ni kinyume.
Kosa hilo ni kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili za CCM toleo la Februari 2010, ibara kadhaa za kanuni.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru