Thursday, 20 February 2014

Nyongeza ya posho yazusha mjadala mkali

  • Bunge launda kamati kuivaa serikali
  • Wananchi wawajia juu, wadai ni walafi
  • Zitto: JK wapuuze wanaodai nyongeza

Na waandishi wetu, Dodoma na Dar

SAKATA la wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kudai nyongeza ya posho limeingia hatua mpya baada ya kuundwa kamati ili kufuatilia suala hilo.
Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hilo, Pandu Ameir Kificho, ameunda kamati ya watu sita kufuatilia posho hizo.
Kificho, ambaye pia ni Spika wa Baraza la Wawakilishi, alitangaza kamati hiyo jana asubuhi kabla ya kuanza semina maalumu ya wajumbe kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema ameunda kamati hiyo baada ya kupata mawazo ya wajumbe kadhaa kuhusu namna nzuri ya kuishi mjini Dodoma kutokana na ugumu wa kazi.

“Wajumbe, mawazo mliyoyatoa kuhusu jinsi gani tutaweza kuishi hapa na kuifanya kazi hii nimeyachukua lakini bado sijawa na jibu.
“Ili kuwa na majibu, nimeona ni vyema nikaunda kamati ya watu sita ili kwa pamoja tuone ni namna gani nzuri ya kuishauri serikali tuweze kufanya kazi kwa ufasaha tukiwa hapa Dodoma,’’ alisema.
Kificho aliwataja wajumbe wa kamati kuwa, William Lukuvi, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge).
Baada ya kutajwa jina la Lukuvi, baadhi ya wajumbe walizomea wakiashiria kutoridhika na uteuzi wake.
Hata hivyo, Kificho alisema Lukuvi hatafanya kazi peke yake na kwamba, ipo siku wajumbe hao watapiga kofi juu ya uteuzi wa mjumbe huyo.
Wajumbe wengine ni Mohammed Aboud Mohammed, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar na Freeman Mbowe, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani katika Bunge la Jamhuri ya Muungano na Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA.
Wamo pia mwanasiasa mkongwe nchini, ambaye amewahi kuwa mbunge na waziri, Paul Kimiti, Asha Bakar Makame na Jenista Mhagama, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Mwenyekiti aliwataka wajumbe wa kamati baada ya kumaliza kazi jana wakutane naye ili kujipanga katika timu hiyo itakayowashirikisha pia makatibu wa Bunge la Muungano na Baraza la Wawakilishi.
Kificho alisema anaamini watapata jibu litakalosaidia kupata suluhu.

Jukwaa la Katiba lawaponda
Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), limelaani madai hayo yaliyotolewa na baadhi ya wabunge ya kutaka nyongeza na kusema sh. 300,000 wanazolipwa zinakidhi mahitaji.
Kaimu Mwenyekiti wa JUKUTA, Hebron Mwakagenda, alisema jana kuwa wabunge wanapaswa kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya kujali matumbo.
Pia, alionya wabunge kuacha kulitumia Bunge la Katiba kama sehemu ya kujitajirisha kwa kutumia kodi za wananchi ambazo zinahitaji pia kutumika kwenye maendeleo ya taifa.
“Madai ya nyongeza ya posho yanaonyesha jinsi baadhi ya wabunge hawako makini na kazi waliyopewa na umma. Hawana uzalendo na nia ya dhati ya kuwapatia
Watanzania Katiba bora na yenye tija,’’ alisema.

Zitto: JK awapuuze wabunge

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, amemuomba Rais Jakaya Kikwete kuwapuuza wabunge kwa kukataa maombi ya kuongezewa posho kwani kilichopangwa na serikali kinatosha.
Pia, aliwataka wabunge wenzake kuacha kutanguliza mbele maslahi binafsi na badala yake waweke utaifa mbele ili kutimiza malengo ya wananchi.

“Namuomba rais asikubali kuongeza posho kama ilivyoombwa na baadhi ya wabunge. Binafsi sitapokea ongezeko lolote la posho licha ya kwamba uamuzi huu usisaidie kuzuia walafi wengine kupata posho kubwa,” alisema Zitto.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, Mrisho Gambo, aliwashangaa wabunge wanaodai ongezeko la posho.
Alisema wabunge hao wamekuwa wakilipwa posho ya chini ya sh. 300,000 katika vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano iweje kwenye Bunge la Katiba isitoshe.

“Haya madai ya ajabu kabisa, miaka yote Bunge linafanyika Dodoma na wabunge wanalipwa posho ya chini ya sh. 300,000 na inawatosha, iweje bunge hilo ambalo ni nyeti na la kihistoria watake malipo makubwa,’’ alihoji Gambo.
Mkazi wa Dar es Salaam, John Shayo alisema iwapo wabunge hao wanaona posho wanayolipwa ni ndogo ni vyema wakajiondoa na kutoa fursa kwa wazalendo kwenda kufanya kazi ya kutayarisha katiba.
Alisema walioomba kushiriki kwenye bunge hilo ni wengi, wengine wameachwa kutokana na ufinyu wa nafasi, waliokwenda kwa ajili ya matumbo yao wanaweza kutangaza kujiondoa.

“Serikali ya Rais Kikwete imetoa fursa kwa Watanzania kupata katiba mpya ambayo kwa kiasi fulani itakuwa suluhisho la kero na matatizo, lakini bado itaendelea kutoa huduma za kijamii na maendeleo kwa wananchi.
“Hawa wanataka posho kubwa fedha hizo zitatoka wapi, kama wamekwenda kushibisha matumbo yao wajiondoe,’’ alisema Subira Juma, mkazi wa Kiwalani.
Juzi, baadhi ya wajumbe walizua zogo kuhusu posho, wakidai ni ndogo ikilinganishwa na waliyolipwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Richard Ndassa, ambaye ni mbunge wa Sumve, alisema posho ya sh. 300,000 wanayolipwa hailingani na hadhi ya kazi wanayoifanya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Alisema inashangaza kuona wakilipwa posho ya sh. 220,000, ambayo ni ndogo ikilinganishwa na waliyolipwa madereva wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Wajumbe pia wanalipwa posho ya kujikimu ya sh. 80,000 kwa siku.
Pia, ili kupata posho hiyo, alisema ni lazima mjumbe ahudhurie vikao siku nzima na kwa Jumamosi na Jumapili hawalipwi zaidi ya posho ya kujikimu ya sh. 80,000, huku akilazimika kuwalipa wasaidizi wake, akiwemo dereva.

“Hebu tuangalie wajumbe wa Tume ya Katiba walikuwa wakilipwa sh. 500,000 kwa siku, dereva analipwa sh. 220,000, ambayo ndiyo posho ya siku. Mimi ninahangaika hivi nami nalipwa sh. 220,000,” alisema.
Ndassa pia alidai kuwa wajumbe kutoka Zanzibar wameongezwa posho ya vikao kutoka kwao, hivyo kutengeneza makundi.
Hata hivyo, mjumbe wa bunge hilo, ambaye ni mwakilishi wa Kwahani, Ali Salum Haji, akizungumzia hilo alisema si kweli kuwa wamelipwa ziada.
Kwa upande wake, Seleman Nchambi, alisema posho zinazolipwa kwa wajumbe ni sawa na mishahara ya vibarua wa mashambani.
Nchambi pia alitoa ombi maalumu kwa Mwenyekiti wa Muda Kificho, kuwanunulia wajumbe kitendea kazi cha mawasiliano cha ipadi (IPAD) ili kupunguza matumizi ya karatasi na gharama kwa bunge.
Kificho akijibu hilo, alisema ununuzi wa IPAD pia ni gharama, hivyo Bunge litaendelea kutumia karatasi katika kutoa nyaraka mbalimbali.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru