Tuesday, 18 February 2014

URAIS 2015 - Vigogo sita CCM hatiani

Katibu wa NEC -  CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Na Mohammed Issa

MAKADA sita wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliotuhumiwa kuvuruga utaratibu na kanuni kwa kujihusisha na kampeni za urais kabla ya wakati wametiwa hatiani.
Makada hao ambao ni pamoja na Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye, Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira, wamepewa onyo kali.
Pia, Chama kimewataka wajiepushe na vitendo vinavyokiuka maadili na iwapo wataendelea kitawachukulia hatua kali zaidi. Mbali na kupewa onyo kali, pia wametakiwa kutogombea uongozi wa aina yoyote ndani ya Chama kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Pia, Kamati Kuu ya CCM imeiagiza kamati ndogo ya udhibiti kuwachunguza na kuchukua hatua kwa mawakala na wapambe wa makada hao walioshiriki kufanya vitendo hivyo.
Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema hayo jana katika Ofisi Ndogo za Chama, Lumumba, Dar es Salaam.
Nape, alisema makada hao wataendelea kuchunguzwa mwenendo wao ili kuwasaidia waweze kujirekebisha.
Alisema kati ya Februari 13 na 18, mwaka huu, Chama kimekuwa na mfululizo wa vikao kadhaa vilivyoshughulikia maadili, ambapo makada hao waliitwa kuhojiwa na Kamati Ndogo ya Maadili.
Alisema vikao hivyo ni pamoja na kamati ndogo ya udhibiti iliyokutana Februari 13 na 14, mwaka huu, pamoja na tume ya udhibiti na nidhamu na kamati kuu, iliyokutana juzi.
Nape alisema baada ya kuwahoji, ilithibitika kuwa baadhi ya tuhuma dhidi yao zilikuwa za ukweli ikiwemo kujihusisha na kampeni za urais kabla ya wakati na kupendekeza adhabu.
Alisema mapendekezo hayo yalipelekwa kwenye tume ya udhibiti na nidhamu na kamati kuu ambayo ilitoa adhabu kwa wahusika.
Kwa mujibu wa Nape, waliohojiwa walithibitika kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea urais kabla ya wakati kinyume na kanuni za uongozi na maadili za CCM toleo la Februari 2010, ibara 6 (7) (i).
Alisema pia wamethibitika kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya Chama na baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii.
Nape alisema kosa hilo ni kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili za CCM toleo la Februari 2010, ibara kadhaa za kanuni.
Alisema kamati kuu imewaonya viongozi na watendaji wa Chama na imewataka kutojihusisha na matendo ya kuwania urais, ambayo yanavunja na kukiuka maadili ya Chama na wanatakiwa kuzingatia kanuni na utaratibu.


CHADEMA iwe na adabu kwa Kikwete
 

Katika hatua nyingine; Nape aliitaka CHADEMA kuwa na nidhamu kwa Rais Jakaya Kikwete na kuacha kuweweseka.
Alisema kamwe Rais Kikwete hawezi kufuta kauli yake na kwamba, itakuwa kali zaidi ili kukomesha vitendo vya vurugu vinavyofanywa na wafuasi wa CHADEMA.
Juzi, viongozi wa CHADEMA walimtaka Rais Kikwete kufuta kauli yake aliyoitoa kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, akiwataka wanachama na mashabiki wa Chama hicho kuacha unyonge.
Katika mkutano huo, Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, alisema kwa muda mrefu wana-CCM wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya vurugu na unyanyasaji na wafuasi wa CHADEMA,  wanapaswa kuwa ngangari.

“Mwenyekiti wetu hawezi kufuta kauli yake, CHADEMA wametufanyia unyama…tunawasubiri Kalenga waje wafanye hayo mambo yao tena.
“Kama wao ni jeshi la angani basi na sisi ni jeshi la nchi kavu na dawa ya moto ni moto, nina maanisha kuwa kama wao watatumia helkopta kufanya kampeni sisi tutatumia magari,” alisema Nape.
Hata hivyo, Nape alisema mchezo mchafu wa CHADEMA kuanza kuzitumia taasisi zisizo za kiserikali na wanaharakati kutoa matamko hayo umebainika.
“Tayari kuna taasisi ilishatoa taarifa, huu ni mpango endelevu, lakini ni mambo ambayo yanapaswa kutazamwa kwa umakini,” alisema mmoja wa viongozi wa Chama hicho makao makuu.
Utekelezaji wa matamko hayo yanafanywa na taasisi moja inayomilikiwa na chama hicho (jina linahifadhiwa), ambapo jana chama hicho pia kilitoa tamko la kumtaka Rais Kikwete aombe ardhi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru