Na Amina Athumani
WATANZANIA watatu wanaocheza soka wameombewa Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa ajili ya kucheza mpira wa kulipwa katika nchi za Thailand na Ujerumani.
Wachezaji hao ni Khamis Jamal, Said Nassor na Samuel Chuonyo ambao wanacheza soka katika klabu mbalimbali nchini.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema Mroki wa timu ya Polisi Dar es Salaam, ameombewa ITC Thailand (FAT) kujiunga na Kabinburi ya nchini humo.
Alisema Nassor na Chuonyo wanaocheza FC Turkey ya Zanzibar wameombewa ITC na Chama cha Mpira wa Miguu Ujerumani (DFB) kwa ajili ya kujiunga na klabu ya VfB Eichstatt.
Alisema TFF inafanyia kazi maombi hayo na baada ya utaratibu kukamilika ikiwemo ridhaa kutoka kwa klabu zao shirikisho hilo litatoa ITC hizo.
Wakati huo huo, timu ya Stand United ya Shinyanga imekata rufani TFF kupinga Kanembwa JKT ya Kigoma kuchezesha wachezaji waliosajiliwa katika dirisha dogo katika mchezo wao wa kiporo.
Mchezo huo namba 22 wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ulichezwa juzi kwenye Uwanja wa Ali Hassani Mwinyi mjini Tabora ambapo Kanembwa JKT iliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Boniface Wambura alisema Stand United inadai Kanembwa JKT iliwatumia wachezaji wanane kinyume na maelekezo kutoka TFF.
Wachezaji wanaodaiwa kusajiliwa katika dirisha dogo ni Hamidu Juma, Ibrahim Issa, Joseph Mlary, Lucas Karanga, Raji Ismail, Salvatory Raphael, Seif Zaidi na Yonathan Sabugowiga.
Alisema dirisha dogo lilifunguliwa Novemba 15 na kufungwa Desemba 15, mwaka jana, hivyo Stand United katika rufani yake inaombwa ipewe pointi tatu na mabao matatu.
Awali, mchezo huo ulichezwa Novemba 2, mwaka jana Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga kabla ya kuvunjwa na mwamuzi dakika ya 87 baada ya Kanembwa JKT kugomea mkwaju wa penalti.
Tuesday, 18 February 2014
MICHEZO - Watanzania waitwa Ujerumani kucheza Soka la kulipwa
21:01
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru