- Mkakati mchafu waliopanga wagonga mwamba, Mgimwa apeta Kalenga
Na Tumaini Msowoya Iringa, IRINGA
MCHEZO mchafu na fitina zilizoanza kufanywa na uongozi wa CHADEMA kuihujumu CCM zimegonga mwamba baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kutupilia mbali pingamizi lao.
Walikuwa wakidai kuwa mgombea ubunge katika Jimbo la Kalenga, Godfrey Mgimwa si raia na waliomdhamini si wakazi wa Kalenga.
Harakati hizo ambazo wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanadai kuwa ni mwanzo wa chama hicho kuanza kutafuta visingizio, zilisukwa na baadhi ya viongozi kwa kushirikianana na mgombea wa ubunge wa CHADEMA, Grace Tendeka.
Hata hivyo, CHADEMA na mgombea wake wameshindwa kuwasilisha vielelezo kuthibitisha madai hayo, hivyo NEC kuamua kulitupilia mbali pingamizi hilo kwa kuwa halina mashiko.
Akizungumza na Uhuru jana, Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Kalenga, Pudensiana Kisaka, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, alisema NEC ilitumia muda uliopangwa kisheria kutaka pande zote mbili, kupeleka vielelezo vyake ili kujiridhisha na pingamizi hilo.
“CHADEMA walishindwa kuleta uthibitisho wa pingamizi lao kwa muda uliopangwa, badala yake walipeleka barua ya kusisitiza pingamizi hilo.
“Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, barua hiyo haikutosha kuthibitisha pingamizi lao la kwamba, Mgimwa sio raia wa Tanzania,” alisema.Alisema mgombea wa CHADEMA, aliwasilisha pingamizi lake likiwa na vipengele vingi, hivyo ikatumika sheria ya uchaguzi kuwataka mlalamikiwa kuwasilisha utetezi wake haraka iwezekanavyo na mlalamikaji kuwasilisha ushahidi wao ili tume ijiridhishe.
Pingamizi liliwasilishwa ofisini kwake juzi (Jumatano) na upande wa mlalamikiwa ulileta utetezi wao kama walivyoagizwa, huku CHADEMA wakiwasilisha barua. Mpaka jana mchana, hakukuwa na ushahidi kutoka kwa walalamikaji, hivyo Tume ikatoa ruksa ya kampeni kuanza kama ilivyopangwa.
“Hatuwezi kufanyia kazi vitu ambavyo havina ushahidi wa kutosha,” alisema Pudenciana.Katibu wa CCM wilaya ya Iringa, Amina Imbo, alisema Mgimwa ni raia wa kuzaliwa wa Tanzania na kwamba, pingamizi hilo halina maana na kamwe halitaweza kuvuruga kampeni za Chama hicho.
Amina alisema CCM ilisimamia kikamilifu kuhakikisha fomu za mgombea zinadhaminiwa na wananchi wa jimbo husika ambao waliambatanisha shahada za kupigia kura kutoka jimboni na si vinginevyo.
Alisema kilichofanyika ni kuwapotezea muda wao wa kampeni, kwa kuwa malalamiko hayo hayana ukweli wowote na kamwe hayataweza kuvuruga jambo lolote.
“Hatutaogopa hata kidogo, CCM ipo makini na mgombea wetu yupo makini, Mgimwa ni mzaliwa wa Tanzania na raia mwenye haki ndani ya nchi yake, ikiwemo haki ya kuchagua na kuchaguliwa kuwa kiongozi,” alisema Amina.Uhuru iliamua kuwatafuta ndugu wa karibu wa Mgimwa ili kupata ukweli wa maisha ya Godfrey ambao walidai kushangazwa na madai hayo ambayo hawakuyatarajia.
Baba mdogo wa Godfrey, Joachim Mgimwa, alisema mwanaye ni raia wa Tanzania wa kuzaliwa na sio kuomba.
“Jambo hili ni la ajabu, mwanagu alizaliwa katika hospitali ya Mkoa wa Iringa, baba yake ni mzaliwa wa kijiji cha Magunga wilaya ya Iringa vijijini, mama yake ni mzaliwa wa kijiji cha Kinyanambo ‘B’, wilayani Mufindi, uraia wake sio wa kuomba ni wa kuzaliwa,” alisema.Alisema baada ya Godfrey kuzaliwa, alipata elimu ya msingi katika shule ya msingi Wilolesi, iliyopo katika Manispaa ya Iringa, baadaye alijiunga na shule ya sekondari ya Njombe (NJOSS) ambako alisoma kwa muda mfupi kabla ya kuhamia Dar es Salaam.
Alisema Godfrey alienda nchini Uingereza kwa ajili ya masomo ya juu na mara zote amekuwa akitumia hati yake ya kusafiria inayoonyesha yeye ni raia wa Tanzania.
Pia alisema Godfrey anacheti cha kuzaliwa kinachoonyesha kuwa ni raia wa Tanzania.
“Hivi mtu asiye raia anaweza kuwa na cheti cha kuzaliwa? Jambo hili lisiwachanganye wapiga kura wa Kalenga, huyu ni mtoto wa nyumbani mwenye sifa na uwezo wa kuwa mbunge,” alisema Joachim.Alisema hati yake ya kusafiria ameitumia mpaka mwezi Desemba, mwaka jana wakati akienda nchini Afrika Kusini.
Akizungumza na Uhuru, Godfrey alikiri kuwepo kwa pingamizi dhidi, hata hivyo alisema anashangazwa na jambo hilo kwa kuwa tangu azaliwe hajawahi kuukana uraia wa Tanzania, nchi aliyozaliwa na ambayo anaipenda kwa moyo wake wote.
Alisema ataendelea kusimamia ukweli na kuwataka CHADEMA kutumia muda wao kwa ajili ya kuhangaikia mambo yao badala ya kuchokonoa masuala ambayo hayana msingi.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru