Tuesday, 18 February 2014

Meno ya tembo yanaswa Singida

Na Nathaniel Limu, Singida

JESHI Polisi mkoani hapa, limekamata vipande 16  vya meno ya tembo vyenye thamani ya sh. milioni 17.
Vipande hivyo ni sawa na tembo wakubwa wanne na tembo watano wadogo waliouawa na majangili.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Cordula Lyimo, alisema meno hayo yalikamatwa Jumapili iliyopita, saa tano usiku katika kizuizi cha mazao kilichoko kijiji cha Ukimbu, Itigi wilayani Manyoni.
Alisema askari wakiwa katika kizuizi hicho, walifanya ukaguzi kwenye gari  lenye namba za usajili T.288 AJF aina ya Scania, mali ya Kampuni ya Super Service likiendeshwa na Ally Hamadi akitokea Makogolosi, Chunya kwenda Itigi.
"Baada ya upekuzi huo, walikuta meno hayo yakiwa yamehifadhiwa ndani ya begi la nguo na kuwekwa kwenye keria za ndani ya basi. Mtuhumiwa aliweza kupatikana wakati akiwa katika juhudi za kutaka kutoka ndani ya basi ili akimbie,” alisema.
Kaimu Kamanda huyo alisema uchuguzi zaidi unaendelea ili kubaini na kuupata mtandao kamili unaojihusisha na kuwinda na kununua nyara hizo.
Idadi hiyo inafanya kufikisha vipande 37 vilivyokamatwa ndani ya wiki moja kwenye kizuzi cha mazao cha Ukimbu, mkoani Singida.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru