NA SHAABAN MDOE, LONGIDO
KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, amesema
serikali ya Rais Jakaya Kikwete imejipanga kuhakikisha inaongeza ajira na
kudhibiti watumishi.
Amesema kurejeshwa kwa mamlaka za ajira ndogo ndogo
katika ngazi za halmashauri kutasaidia kuongeza ajira kwa jamii.
Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu CCM |
Aliyasema hayo juzi wakati akizungumza kwenye semina
ya siku mbili kuhusu ardhi kwa viongozi wa mila wa Kimasai katika Mji wa
Namanga wilayani Longido mkoani Arusha.
Kinana yuko mkoani hapa akiendelea kuzungumza na
wananchi na viongozi wa kimila kuhusiana na migogoro ya ardhi.
Akijibu swali la kiongozi wa kimila Tina Timani,
alihoji kuwa pamoja na Hifadhi ya Ngorongoro kuwa katika makazi ya watu wa
kabila la Wamasai, bado nafasi za ajira kwa watu hao zimekuwa chache.
Alimuomba Kinana kuhakikisha kuwa mbali na ajira, pia
asilimia 50 ya mapato yote ya hifadhi hiyo yanarejeshwa kwa jamii kama faida
kwa kuwa ndio walinzi hifadhi hiyo na wanyama waliomo ndani.
Kufuatia kilio hicho ndipo, Kinana alipotolea
ufafanuzi suala hilo la ajira ambalo hapo awali hata watumishi wa kada ya chini
ya serikali wakiwemo maafisa watendaji wa kata, vijiji na udereva zilikua
zikitolewa na tume ya ajira taifa jambo ambalo lilikua likiwanyima fursa wakazi
wa eneo husika wenye vigezo.
Pia, alitolea mfano wa nafasi za udereva katika
halmashauri mbalimbali nchini ambapo mtumishi huyo utakuta anaajiriwa kutoka
mikoa na wilaya za mbali huku wale wenye sifa zinazohitajika kutoka halmashauri
husika wakiachwa.
Alisema kwasasa ajira hizo zitakua zikitolewa kwa
watu wa eneo husika wenye vigezo na italazimika kwenda kwa watu wa mbali
watakaopelekwa katika maeneo hayo iwapo tu hakutakua na mtu mwenye sifa
zinazohitajika.
“Napongeza uamuzi huo ile ya zamani hapana hata mtendaji wa kata au dereva anatolewa wilaya za mbali Tunduru au Newala huko analetwa hapa Longido wakati wapo wenye vigezo vinavyohitajika hii nasema hapana tuombe utekelezaji wa maagizo hayo uanze mara moja,” alisema Kinana.
Alisema kigezo anachokifahamu kilichokua kikitumika
kuwapata watumishi hao kutoka maeneo
mbalimbali ilikua ni kulinda utaifa zaidi lakini
alishauri kigezo hicho kibaki kwa watumishi wa ngazi za juu kuanzia makatibu
tawala wa wilaya,wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa wilaya na wengine lakini
siyo kwa wale wa kada za chini za uongozi.
Alieleza kuwa kuajiriwa kwa watumishi hao kutoka
maeneo wanayoishi kutasaidia mambo mengi ikiwemo gharama za malazi,likizo na
hata kuwezesha halmashauri husika kumuwajibisha pindi atakapokua hatimizi
majukumu yake ipasavyo.
“Sasa utakuta mtendaji anatoka huko Newala au Tunduma halafu unao kama kumi na mbili hivi je serikali itakua na uwezo wa kuwasafirisha kwenda likizo kila mwaka wao na familia zao hapana ila hii itasaidia,” alisema Kinana.
Kuhusu masuala ya ajira katika hifadhi ya Ngorongoro
na hifadhi nyingine aliahidi kulifikisha jambo hilo kwa viongozi wakuu wa
serikali ili liweze kufanyiwa kazi na kamwe hapendi kuona jambo moja
likizungumzwa zaidi ya mara tatu huku likikosa majibu yake.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru