Taasisi zilizoagizwa kuwachunguza watuhumiwa wa Escrow zitende haki.....!
"HATIMAYE Rais Jakaya Kikwete ameweka hadharani mambo yote kuhusiana na sakata la akaunti ya Tegeta Escrow na kuchukua hatua kwa baadhi ya watendaji.
Akihutubia mkutano wa Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, Rais
Kikwete, alimvua uwaziri Profesa Anna Tibaijuka kutokana na kuhusishwa katika
kashfa hiyo na watendaji wengine wakiendelea kuchunguzwa.
Pia, aliagiza hatua kadhaa kuchukuliwa ili kuhakikisha
serikali inapata halali yake kwenye mambo ambayo yalizusha utata baada ya
sakata hilo kuibuka na kutikisa nchi.
Kabla ya hatua hiyo, sakata la akaunti ya Tegeta Escrow
lilifikishwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambaye
baada ya uchunguzi aliwasilisha ripoti iliyopelekwa bungeni na ambako maazimio
kadhaa yalifikiwa.
Ni ukweli usiopingika kuwa katika sakata hilo kuna baadhi ya
watu na wanasiasa ambao walitaka kulikuza na kuliongeza chumvi, lengo likiwa
kuwakomoa baadhi ya watendaji kwa kutaka wawajibishwe.
Walio katika kundi hilo, walihakikisha wanatumia mbinu na kila
aina ikiwemo kuvumisha na kusingizia wengine uongo huku wakijua wanafanya hivyo
kwa makosa, lakini walitaka kushinikiza malengo yao kutimia.
Wapo waliotetea na kutaka kuona haki inatendeka na ambao
baadhi yao walijitoa kimasomaso kuhakikisha waliotenda makosa wanaadhibiwa
badala ya kuwahusisha waliokuwemo na wasiokuwemo kwa mkumbo.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Jaji Frederick Werema, kwa
kutambua kuwa ushauri wake haukueleweka kiasi cha kusababisha mtafaruku kwa
busara aliamua kujiuzulu.
Hata hivyo, kutokana na sababu ambazo baadhi ya wahusika
wanazijua, walishinikiza kutaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri wa Nishati
na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, nao wajiuzulu kwa sababu walisema fedha
zile hazikuwa za umma.
Kauli ya Rais Kikwete kuwa fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya
Tegeta Escrow hazikuwa za umma bali za Kampuni ya Independent Power Tanzania
(IPTL) inamaliza utata ulioibuka kuhusiana na fedha hizo.
Kwa hiyo, suala hilo limewekwa hadharani na kila kitu
kimeelezwa, hivyo kilichobaki ni kuacha kuumiza vichwa kwa jambo ambalo
limeshapatiwa ufumbuzi kwani mwenye fedha ameshachukua na kinachotakiwa sasa ni
kuendelea kuumiza vichwa ili kuona ni kwa namna gani wananchi wengi watanufaika
na nishati ya umeme tena kwa bei nafuu.
Pia, utaratibu unaotaka kuota mizizi hivi sasa na hasa kwa
wafanyabiashara na wanasiasa kuviziana na ‘kuumizana’ kwa sababu za maslahi
binafsi unapaswa kuepukwa ili kuweza kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
Escrow imefungwa na watu wanapaswa kuacha nongwa na badala
yake kujikita katika jitihada za kujikwamua kiuchumi badala ya kuendelea
kulumbana kwa mambo ambayo hayana faida.
Kwa mamlaka zilizopewa majukumu ya uchunguzi, zinapaswa kukamilisha majukumu yake na kujendelea na taratibu nyingine ili kuona haki ikitendeka."
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru