Tuesday, 1 April 2014

Kinana awaingiza mawaziri mtegoni


NA SULEIMAN JONGO, NKASI

KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, amewataka wabunge wa CCM kutokubali kila kitu kinachowasilishwa na mawaziri kwa kuwa baadhi havina manufaa kwa jamii.
Amesema kufanya hivyo ni kwa ajili ya kuwasaidia wananchi na jamii na mawaziri husika kupanga hoja na kuwasilisha mambo yenye tija.
Akizungumza kwenye kikao cha Halmashauri  Kuu ya CCM wilaya ya Nkasi, kilichofanyika kwenye mji mdogo wa Namanyere, Kinana alisema hata kama mawaziri wanatokana na CCM, haina maana kila wanachokiwasilisha kinafaa kupitishwa kama kilivyo.
Kinana alisema wabunge wa CCM wanapaswa kuongeza ukali katika kuisimamia serikali pale inapowasilisha bungeni mambo mbalimbali ambayo hayana msaada kwa taifa.
Akitoa mfano, Katibu Mkuu Kinana alisema anashangaa kuona wananchi, hasa wakulima wa mkoa wa Rukwa wakiendelea kulazimishwa kutumia mbolea ya Minjingu, ambayo imekuwa ikilalamikiwa kila kona ya nchi.

“Nitakwenda kukaa na wabunge wote wa CCM na kuwapa maelekezo, si kila kitu kinacholetwa na waziri kiko sawa, yako baadhi ya mambo hayaisaidii nchi wala CCM.
“Kuweni wakali endapo waziri atakuleteeni jambo la hovyo lisilo na maslahi kwa jamii, likataeni na wekeni msimamo wa pamoja kulipinga,” alisema.
Kwa mujibu wa Kinana, ili kukijenga Chama na serikali imara, ataendelea kuwa mkali kwa viongozi wa CCM waliopewa dhamana ili watimize majukumu na kusimamia utekelezaji wa ahadi mbalimbali zilizotolewa.
Wakati huohuo, Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Iddi Kamanta, alijikuta katika wakati mgumu baada ya umati wa wananchi wa mji mdogo wa Kirando kumpinga hadharani.
Wakazi hao waliohudhuria mkutano huo, walimpinga mkuu huyo wa wilaya aliyekuwa akitoa maelezo kuhusu matumizi ya sh. milioni 200 kwa ajili ya utandazaji mabomba yatakayosambaza maji kwenye mji huo.
Akitoa maelezo kuhusu fedha hizo kama alivyotakiwa na Kinana, Kamanta alisema zilitumika kuchimba mitaro ambayo hata hivyo mabomba yake hayakutandazwa.

“Ni kweli fedha hizo zilitumika kuchimba mitaro ya kulaza mabomba, hamkuyaona wananch?” Alihoji Kamanta.
Hata hivyo, swali hilo lilijibiwa na mlipuko wa miguno kutoka uwanjani hapo huku wengine wakiangua kicheko cha kuashiria kupinga maelezo ya mkuu huyo wa wilaya.
Awali mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keisy, alisema halmashauri imeshindwa kujenga kwa wakati mradi wa usambazaji mabomba hayo ili kusambaza maji na kusaidia wananchi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru