Na Hamis Shimye
WATANZANIA na vijana wasomi nchini wametakiwa kuwashughulikia wale wote wasioutaka Muungano wa serikali mbili kwa kuwa watu hao hawaitakii mema nchi.
Pia wametakiwa kuhakikisha wanazilinda na kuzitetea fikra za mwasisi wa muungano huo, Sheikh Abeid Aman Karume, aliyekuwa analilia na kuulinda muungano, wakati wanapoadhimisha kumbukumbu ya kifo chake.
Msimamo huo ulitolewa jana katika kongamano la wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini la kumbukumbu ya miaka 42 ya kifo cha Sheikh Karume.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Katibu wa CCM wa Mkoa wa Vyuo vya Elimu ya Juu, Christopher Ngubiagai, ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema Muungano uliopo wa serikali mbili ni muhimu kuendelezwa na kudumishwa.
Alisema vijana wasomi wanapokusanyika na kumkumbuka Sheikh Karume ni muhimu kuhakikisha wanatekeleza misingi yake ya kuulinda na kuudumisha Muungano.
“Ni kweli muungano uliopo una matatizo, lakini matatizo yake hayamalizwi kwa kuongeza serikali. Wanaotaka serikali tatu, vijana wenzangu tunapaswa kuwashughulikia, wanaleta hatari ndani ya nchi yetu,’’ alisema.Alisema nchini Marekani kuna baadhi ya majimbo yalianza kuleta chokochoko ya kutaka kutoka katika muungano wao, lakini walichokifanya ni kuwadhibiti watu kutoka ndani ya majimbo ya Hawaii, Texas na Alaska.
“Nchi ilifikia uamuzi wa kuanzisha kambi za kijeshi katika majimbo hayo. Lengo ni kuhakikisha kulinda utaifa wa Marekani, lakini kwetu tuwashughulikie hawa watu maana wanataka kutugawanya na si kutuunganisha,’’ alisema na kuamsha shangwe.Ngubiagai alisema kinachotakiwa kufanywa na Watanzania ni kuhakikisha Muungano wa serikali mbili unalindwa na pia kuwashughulikia wasioutaka udumu na kuendelea zaidi.
Alisema Sheikh Karume na Mwalimu Julius Nyerere waliona kuna umuhimu mkubwa wa kuungana na ndio maana walifikia uamuzi wa kuijenga Tanzania mpya yenye matumaini kwao.
“Mzee wetu (Karume) alikuwa na matumaini mengi na Wazanzibar na watanzania kwa ujumla.Ingawa walimuua na kushindwa kutekeleza azma hiyo, sisi vijana tuitekeleze azma hiyo kwa kuulinda muungano kwa gharama yeyote ile,’’ alisema.Aliwataka vijana kutumia kongamano hilo kumkumbuka Sheikh Karume katika kulinda na kudumisha muungano kwa kuwa Utanzania ni muhimu katika kuijenga nchi na si vyama.
Tangu kutolewa kwa rasimu ya Katiba Mpya na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kupendekeza kuwepo kwa mfumo wa serikali tatu, kumekuwepo na kauli tofauti juu ya serikali hizo kuwa si nzuri na zitaleta mpasuko.
Hali hiyo ni pamoja na kauli aliyoitoa Rais Jakaya Kikwete bungeni Dodoma, wakati wa uzinduzi wa bunge hilo, ambapo alisema serikali tatu si mwarobaini wa kumaliza matatizo ya muungano.
Alisema wabunge wanapaswa kufikiri kwa umakini na kuhakikisha wanaisoma rasimu sentesi kwa sentesi, kurasa kwa kurasa ili kuhakikisha wanaipatia Tanzania katiba bora na imara.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema muungano wa serikali mbili ni muhimu na aliwatahadharisha wajumbe kutojadili rasimu hiyo katika misingi ya Utanganyika na Uzanzibar ili kusaidia kupatikana kwa katiba bora.
Baada ya kutolewa kwa hotuba ya Rais Kikwete, baadhi ya wasomi walimpongeza na wengine kutoa mihadhara yenye lengo la kudumisha muungano wa serikali mbili uliopo sasa.
Mihadhara hiyo ni pamoja na hotuba ya mwanazuoni maarufu, Profesa Issa Shivji alioutoa katika kongamano la vijana nchini, ambapo alisema taarifa ya mwisho ya tume inaweza ikawa na hatari.
Alisema hilo linatokana na kuamsha na kushawishi hisia za Utanganyika na, pili ni kufanya watu wa Tanzania Bara wawachukie wenzao wa Zanzibar.
“Muungano wowote hauwezi kudumu, au kudumu kwa amani, kama hauna mizizi katika watu na hisia zao na sisemi kwamba muundo wa serikali au dola mbili tulionao hauna matatizo, unayo,’’alisema Profesa Shivji.Alisema Watanzania hawapaswi kuuangalia muungano kwa jicho la idadi ya serikali bali uangaliwe katika mtazamo wa demokrasia na wakifanya hivyo, watabuni muundo utaokidhi mahitaji ya watanzania bila kuhatarisha uhai wa Muungano
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru