Tuesday, 1 April 2014

Watatu wadakwa na mabango ya uchochezi

NA MWANDISHI WETU

WATU watatu wamekamatwa na Polisi wakiwa katika mkusanyiko usio maalumu, huku wakiwa na mabango yanayodaiwa kuhamasisha uvunjifu wa amani, katika eneo la Manispaa ya Dodoma.
Watu hao wanadaiwa walikuwa wakiwasubiri Wajumbe wa Kamati za Bunge Maalum la Katiba ambao wako hapa kujadili rasimu ya Pili ya Katiba.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 3:30 asubuhi.
Misime aliwataja waliokamatwa kuwa ni pamoja na Augustino Pancras (60), mkazi wa Kilimani, Cosmas Katebelea (44), mkazi wa Kikuyu na Jotham Tarukundo (35) mkazi wa Chidachi.
Misime, alisema watu hao kwa pamoja, walikamatwa wakiwa na bango lenye ujumbe uliosomeka “Wajumbe Msijivunie wingi wenu humo ndani sisi wananchi tupo nje na ndiyo wengi maoni yetu yaheshimiwe’’
Alisema Polisi wanaendelea kuwahojiwa na upelelezi ukikamilika kulingana na ushahidi, watafikishwa mahakamani kwa kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukutwa na mabango ya kuhamasisha uvunjifu wa amani.

“Tunaendelea kuwasaka wengine ambao wamekimbia na wakikamatwa  tutawaunganisha na wenzao,’’ alisema Kamanda Misime.
Wakati watu hao wakikamatwa, katikati ya mji kulionekana watu wengine wawili wakiwa katika Hoteli ya Royal Village wakiwa wameshikilia mabango nayo yakiwa na ujumbe mbalimbali.
Watu hao walibeba mabango yaliyosomeka, ‘Bahati mbaya sana nyongeza ya wajumbe 201 inashindwa kutetea maoni ya wananchi wanaowawakilisha’.
Bango jingine lilisomeka ‘Katiba mpya wakina mama wenzetu mlioingia kwenye Bunge la Katiba msikubali maoni ya wananchi yachakachuliwe.’
Watu hao wawili walionekana pembeni mwa hoteli hiyo kati ya saa 2 na saa tatu asubuhi, wakati wajumbe wakiwasili katika ukumbi huo.
Walipohojiwa kwanini wako hapo, huku wakikwepa kupigwa picha, walidai kuwa nia yao ni njema na wanalengo la kufikisha ujumbe wao kwa Wajumbe hao wa Bunge la Katiba.
Mmoja wa Watu hao aliyejitambulisha kwa jina la Benadeta Mwaluko, alisema nia ni kuwakumbusha wajumbe kuwa wanawawakilisha wananchi na si wao binafsi.

“Tunawaoomba sana wajumbe ambao ni wawakilishi wetu wasichakachue rasimu aliyoiwasilisha Jaji Warioba, maoni yaliyomo wayaheshimu kwani ni ya wananchi,” alisema.
Kwa upande wake mtu aliyejitambulisha kwa jina la Kahumba Leula, alisema bado wanahofu kama mchakato huo utamalizika salama, ndiyo maana wameamua kuwafikishia ujumbe wajumbe hao kwa njia ya mabango.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru