- Wajumbe warushiana vijembe, kashfa
- Kambi za serikali mbili, tatu zachuana
- Maalim Seif naye arushiwa makombora
Jane Mihanji na Furaha Omary, Dodoma
VIJEMBE, kebehi, kashfa na mipasho jana viliendelea kutawala katika Bunge Maalumu la Katiba wakati kila upande ukijinadi na kujinasibu kwanini unataka muundo wa serikali mbili au tatu.
Wakati hayo yakiendelea, baadhi ya wajumbe walimshukia Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad kwa kumtaka aache kuchochea vurugu, badala yake ashirikiane na viongozi wenzake kuimarisha umoja na amani miongoni mwa Wazanzibar.
Panya Ali Abdallah, akichangia sura ya kwanza na ya sita ya Rasimu ya Katiba, alisema Maalim Seif ndiye chanzo cha vurugu kutokana na kauli zake za kebehi na dharau kwa viongozi wenzake.
Alimtuhumu Maalim Seif kwamba amekuwa akipigia chapuo kurejea kwa utawala wa kisultani visiwani Zanzibar.
“Kuna watu wanayabeza na wanadai hawataki muungano, lakini wanatafuta njia ya kurudi mkoloni. Kwa hatua tuliyofikia, mkoloni harudi tena, wakati wa hewala bwana umekwisha, tunajinafasi na tutaendelea kulinda muungano huo,” alisema Panya.
Alisema wananchi wa Zanzibar wana wasiwasi mkubwa wa kuja Sultan. “Tuliambiwa mbele ya kadamnasi, hatatawala mweusi, atakuja mwenye ndevu zaidi. Mapinduzi ndio mkombozi wetu, tunamwomba Maalim Seif akae na Dk. Sheni asimamie amani na utulivu,” alisema.
Panya alisisitiza kuwa, ilifika mahali Wazanzibar waliomba serikali ya umoja wa kitaifa na walifanikiwa, hivyo wasilete chokochoko kutaka kuvuruga Muungano na kwamba kamwe hawawezi kukubali muundo wa serikali tatu.
Alikiri kuwepo kwa kero za Muungano, ambazo alisema zinaweza kurekebishwa na sio kuongeza serikali nyingine, ambayo inakuwa mzigo kwa wananchi.
Naye Haji Omar Heri akichangia hoja hiyo, alisema yupo tayari kusimama hadharani katika eneo lolote Zanzibar na kuwaeleza wananchi umuhimu wa muundo wa serikali mbili na kuimarisha Muungano.
Kauli hizo zilikuja baada ya baadhi ya wajumbe kukataa muundo wa serikali mbili walizokuwa wakidai zinawakandamiza na kuwanyima haki Wazanzibar.
“Msitikise kiberiti, kimejaa, Karume aliingia makubaliano ya muungano kwa kutekeleza ilani ya chama chake cha Afro Shirazi, kwamba kuwepo na umoja, elimu, makazi bora ndani ya serikali ya muungano na kwa dhamana ya serikali hiyo, Tumbatu tulipata umeme,” alisema.
Mawaziri SMZ washukiwa
Awali, Hija Hassan Hija, ambaye alikuwa akiunga mkono muundo wa serikali tatu, aliwashutumu mawaziri katika serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwamba wamekuwa na maslahi binafsi.
“Mawaziri wa Zanzibar ukiwanyang’anya madaraka, kesho watadai serikali tatu, hawa walibadilisha katiba, leo wamesahu wanatia ulimi puani,” alisema na kuwaita mawaziri hao kuwa ni wasaka tonge.
Kauli hizo za kuudhi ziliamsha ari kwa wajumbe kurushiana maneno, ambapo ilimlazimu Mwenyekiti, Samuel Sitta kuangalia lugha wanazotumia. “Tujihadhari, mipasho inazidi kipimo,” alisema Sitta.
Mbaruku Salim Ali alisema Wazanzibar wamechoshwa na muundo wa muungano na kero za muungano zimekuwa tatizo kubwa.
Asiyetaka serikali
mbili aondoke Z’bar
Hoja hiyo ilitupiliwa mbali na mjumbe Mwinyi Haji Makame, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Utawala Bora Zanzibar, aliyesema muundo wa serikali tatu hautekelezeki.
“Ukiona mtu anaanza kutukana, ujue kafilisika, hana ajenda. Sultani ametawala miaka 300, katuachia nini? Mwinyi alishawahi kusema Zanzibar njema, atakaye aje,” alisema na kuongeza: “ Asiyetaka mfumo wa serikali mbili, njia nyeupe.”
Alisema kuna watu wanataka kuuvunja muungano kwa gharama yoyote jambo ambalo haliwezi kuvumiliwa.
Aliwashangaa wajumbe wengi wa Zanzibar kubadilika kwani hoja yao ilikuwa serikali ya mkataba na sio serikali tatu ambayo wameikuta Dodoma.
Abwao awashangaza wajumbe
Katika hali ambayo kila mtu alibaki mdomo wazi, Chiku Abwao alisimama na kuidai Tanganyika kwa kusema ni heri Muungano uvunjike na Tanganyika ipatikane kwa gharama yoyote.
Chiku alisema licha ya kuwa muumini wa serikali ya shirikisho, hoja ya muungano isiwe mbinu ya kuzima uwepo wa Tanganyika.
Mjumbe Pereila Silima alisema mfumo wa serikali mbili, ambao umekuwepo kwa miaka 50 sasa umewasaidia Watanzania katika nyanja zote na kinachotakiwa ni kukabiliana na changamoto zilizopo.
“Sikubaliani na serikali tatu kutokana na hoja ya kwamba serikali mbili tumekaa nazo kwa miaka 50, siamini mawazo ya kutoka katika serikali mbili twende kwenye tatu,” alisema.
“Jambo linalonitisha ni kusema tuna serikali ya Tanganyika na ya Zanzibar na juu iwepo ya Muungano. Nawaomba wabunge tusijaribu kutoa nafasi mambo yakuwe na yatudhuru, utaifa utaibuka na tutasambaratika,” alisema.
Alisema anapendekeza serikali mbili zitakazofanyiwa marekebisho kwa kuwa kukiwa na serikali tatu, gharama zitaongezeka.
Mjumbe Assumpter Mshana alisema anaamini katika serikali mbili kwa sababu nchi ina amani na utulivu, hivyo kilichopo ni kurekebisha.
“Tulichukua udongo wa Tanganyika na Zanzibar na kuuchanganya na kupata serikali mbili. Hatuwezi leo kuchukua udongo wa Tanzania na Zanzibar na kupata serikali tatu. Hatuko tayari kwenda kinyume na mambo yaliyofanywa na waasisi wetu,” alisema.
Alisema hakuna mtu atakayetenganisha udongo huo, ambao uliunganishwa na waasisi wa nchi. “Hatuko tayari kuweka watu juu ili waning’inie na kula fedha za Watanzania. Kodi za wananchi wanataka barabara, miundombinu, masoko na sio serikali tatu. Hatutaki serikali tatu, tunataka mbili zenye manufaa kwa pande zote mbili,” alisema.
Naye Waridi Bakari Jabu, ambaye ni muumini wa wanaounga serikali mbili, alishangaa kauli za viongozi wa Zanzibar wanaotaka serikali tatu, kwamba wanataka kuwagombanisha Wazanzibar na Tanzania Bara.
“Viongozi wa CUF wamekusudia kutugombanisha kati ya Tanzania Bara na Zanzibar. Watuambie hati ya makubaliano kati ya Unguja na Pemba ililetwa hapa tuione. Hati ya Muungano tumeiona,” alisema.
Waridi alisema viongozi wanaojiita Wazanzibar, ambao ni wa CUF, sio wote wanataka kuvunja Muungano, kwa kuwa wengi wanataka Zanzibar iendelee na muungano wa serikali mbili.
Maige awashangaa wanaolalamika
Naye Ezekiel Maige alisema haoni sababu kwa nini Zanzibar inalalamika kunyonywa, ilhali inanufaika zaidi kiuchumi, chini ya mwamvuli wa Serikali ya Muungano.
Alisema hivi sasa Zanzibar imekuwa ikipata huduma za jamii nyingi bure, ikilinganishwa na Tanzania Bara, na kwamba licha ya maisha magumu watu wanayoishi, hawakuwahi kuilalamikia Zanzibar.
“Bara tumekuwa wavumilivu sana, lakini hakuna asiyejua kwamba wilaya zote za Zanzibar zina lami, huduma za hospitali bure pamoja na shule,” alisema.
Maige alishauri wakati umefika kutatua kero za muungano, ikiwa ni pamoja na muungano usiwe kwenye hadhi ya vyama vya siasa, badala yake usimamiwe kwa utaratibu utakaowekwa kisheria.
Pindi Chana alisema serikali mbili hazikwepeki na suala la serikali tatu lisifanyiwe majaribio kwa Watanzania.
“Watanzania wengi wanataka serikali mbili, japo kuwa ina changamoto, lakini serikali tatu ndiyo zenye changamoto nyingi zaidi. Leo watu wameufyata, nchi haiendeshwi kienyeji.
Serikali mbili hazikwepeki, hiyo habari ya serikali tatu, ambayo hatujawahi kuiona, tunataka kuitesti, basi tusitesti kwa Watanzania ambao hawajatutuma,” alisema.
Vijembe vyatawala bungeni
Katika hali ya kushangaza, wajumbe wa bunge hilo kutoka Zanzibar waliamua kurushiana vijembe, ambapo Salehe Nassoro Juma, ambaye ni muumini wa serikali tatu, alimshambulia Asha Bakari Makame.
Salehe alisema: “Namshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kuanzisha mchakato na anastahili kutunukiwa nishani aliyopewa hivi karibuni. Nyerere na Karumeru wamezeeka na wamazo yao yamezeeka,” alisema.
Mjumbe huyo alisema anataka kumsaidia mama huyo kutokana na kumtukana mwanaume, kwa kuwa wamefanya utafiti na kutambua kuwa naye hana mume.
“Baba yake Jusa (mjumbe wa bunge hilo), alipata usingizi hapo, tunataka tushirikiane, Jusa tumposee mke,” alisema mjumbe huyo
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru