Tuesday, 1 April 2014

UKAWA wagonga mwamba


Na WAANDISHI WETU, Dodoma

NJAMA za Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kutaka kuvuruga mchakato wa katiba zimegonga mwamba.
UKAWA kupitia kwa wajumbe wa umoja huo, Tundu Lissu na Jussa Ismail Ladhu, juzi walikituhumu Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwa kimepenyeza rasimu mbadala kwenye kamati za bunge hilo.
Lissu na Jussa ambao ni wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, kwa nyakati tofauti walidai kuwa CCM imeandaa rasimu mbadala na kuipenyeza kwenye Kamati za Bunge Maalumu ili zijadiliwe badala ya rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kupitia kwa aliyekuwa Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba.
Madai ya UKAWA yameonekana ni hila za dhahiri za kutaka kuvuruga mawazo na malengo ya wajumbe wa kamati za Bunge hilo Maalumu la Katiba.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana, baadhi ya Wenyeviti wa Kamati walisema hakuna rasimu mbadala iliyowasilishwa bali wajumbe walijadili Rasimu ya Pili iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Mwenyekiti wa Kamati namba 11, Anne Kilango Malecela, alisema madai hayo hayana ukweli wowote na kwenye kamati yake hakuna rasimu mbadala iliyowasilishwa.
Alisema kamati hiyo ina wajumbe 53 kati yao 18 wanatoka Zanzibar na wote hawajaona rasimu mbadala iliyodaiwa kupenyezwa kwenye kamati hiyo.
Anne, alisema wajumbe wote wa kamati hiyo walikuwa wakishindana kwa hoja na hakuna malumbano yoyote yaliyojitokeza.

“Kamati yangu iliendesha mijada vizuri kila mjumbe alipata nafasi ya kuchangia rasimu tuliyokabidhiwa na Tume na si nyingine,” alisema Anne.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati namba moja, Ummy Mwalimu, alisema katika kamati yake hakuna rasimu ya mafichoni iliyowasilishwa kwenye kamati yake.
Alisema wajumbe wa kamati hiyo kila mmoja alipata nafasi ya kutoa mchango wake na hakuna aliyedai kuwa kuna rasimu mbadala iliyowasilishwa.

“Tuhuma hizo si za kweli, kila mjumbe alijadili kile kilichotakiwa kujadiliwa. Kamati zote zina mchanganyiko wa wajumbe kutoka makundi mbalimbali wakiwemo wanasiasa sasa kama kulikuwa na rasimu mbadala si wangeongea,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati namba tisa, Kidawa Hamis Salehe, alikana pia kuwepo kwa rasimu hiyo iliyokuwa ikidaiwa na kina Jussa na Lissu.
“Hiyo rasimu mbadala sisi hatujaiona, kila mjumbe kwenye kamati yangu alikuwa na rasimu hii tunayoijadili,” alisema Kidawa.

UTULIVU WATAWALA
Hali ya utulivu ilitawala katika kamati zote, na ilielezwa kuwa wajumbe wote walishindana kwa hoja, mivutano na mabishano ambayo hayakuwa na tija hayakupewa nafasi kwa mujibu wa wenyeviti wote waliozungumza na Waandishi wa Habari.

Wajumbe waomba nyaraka za Muungano
Sakata la Muungano limeendelea kuchukua nafasi kwenye kamati mbalimbali zilizoanza kazi ya kujadili Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu hiyo.
Sura hizo mbili zilizoanza kujadiliwa, zote zina vipengele vinavyozungumzia masuala ya Muungano, ambapo Sura ya Kwanza ina kipengele kinachozungumzia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na alama na sikukuu za Taifa, lugha ya taifa na lugha za alama na tunu za taifa.
Wakati Sura ya Sita nayo ina kipengele kinachozungumzia  muundo wa Muungano, vyombo vya utendaji vya Jamhuri ya Muungano, mamlaka ya serikali ya Muungano, mambo ya Muungano, nchi  washirika, mamlaka ya nchi washirika na mahusiano kati ya nchi washirika.
Pia sura hiyo inazungumzia mahusiano kati ya nchi washirika, mawaziri wakaazi, mamlaka ya wananchi na wajibu wa kulinda muungano.
Ilielezwa na Wenyeviti hao wa kamati kuwa, baadhi ya wajumbe, walidataka kupatiwa nyaraka za Muungano ili waweze kuona saini zilizowekwa na waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Aman Karume, kama zilikuwa sahihi.

“Hapa kwenye kamati yangu wajumbe wengi walitaka kuziona nyaraka za Muungano ambazo walipatiwa na walihoji saini kama zilikuwa halali,” alisema Anne ambaye ni mwenyekiti wa kamati namba 11.
Alisema baada ya kujitokeza mjadala huo, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Masoud Othmani Masoud, alilazimika kutoa ufafanuzi na kusema saini zilizowekwa na waasisi hao ni sahihi.
“Na nyaraka yenyewe hii hapa, Jaji Warioba ametuwekea kabisa kwa ushahidi katika bando kitita hiki,” aliionyesha Anne kwa waandishi wa habari.
Katika kamati namba tisa inayoongozwa na Kidawa, alisema wajumbe nao waliomba kupatiwa nyaraka hizo za ili wajiridhishe kabla ya kuendelea na mjadala.
Hata hivyo, alisema kila mjumbe anahaki ya kuomba kuona nyaraka hizo ili kujiridhisha na si dhambi wala kosa.
Mwenyekiti Ummy, alisema katika kamati yake namba moja, suala hilo lilijitokeza ambapo kila mjumbe alipatiwa na kutoa mchango wake.
Naye Mwenyekiti wa Kamati Namba Tano, Hamad Rashid Mohammed, alisema katika kamati hiyo, mvutano ulikuwa ni wa serikali tatu na mbili, ambapo wajumbe walishindana kwa hoja na hakutarajia kama kungekuwa na utulivu katika kipengele hicho. Alisema nguvu za hoja zilitawala katika mjadala mzima.

MUDA WATISHIA MCHAKATO
Wakati huo huo, muda uliopangwa kwa ajili ya majadiliano umezua hofu kwa wenyeviti, ambapo kila mmoja alisema ni mdogo na anahofia kuwa usitoshe kumaliza kazi hiyo.
Anne Kilango, alisema mpaka jana mchana, walikuwa bado hawajamaliza kuijadili Sura ya kwanza, ambayo ina vipengele vitano.

“Mpaka sasa tunahangaika na Sura ya Kwanza, kwakweli muda ni tatizo, itabidi tumuandikie mwenyekiti ili aweze kuliona hili na namna ya kulitatua,” alisema Anne.
Wenyeviti waliozungumza na waandishi jana, wote walionyesha hofu ya muda kuwa ni mdogo, na huenda Mwenyekiti Samuel Sitta, akalazimika kuuongeza.
Muda uliotengwa kwa ajili ya kujadili sura hizo mbili ni wa siku mbili tu, yaani jana na leo, na kesho itatumika kwa kuandika kile walichokubaliana kabla ya kuwasilishwa bungeni kesho kutwa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru