Na mwandishi wetu, Tarime
MAKADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Tarime, wameanza kutengeneza makundi hatari kutokana na kuanza harakati za kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu ujao.
Makundi hayo, ambayo baadhi yamekuwa yakiungwa mkono na viongozi, yameanza kuwagawa wanachama, hivyo kuhatarisha jimbo hilo kuanza kunyemelewa tena na upinzani.
Habari za kuaminika zimesema makundi hayo ni ya wanachama walioshindwa kwenye kura za maoni ndani ya CCM mwaka 2010, ambayo yameanza kuendesha kampeni za chini kwa chini.
Kutokana na hatua hiyo, baadhi ya wananchi hususan wanachama wa CCM, wamelalamikia hali hiyo na kuomba uongozi wa mkoa kuwadhibiti makada hao ili kuzuia mpasuko.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti juzi, baadhi ya wanachama wakiwemo madiwani, wamesema harakati zinazofanywa kwa sasa ni hatari na hazina nia njema kwa CCM.
Mwita Wambura, ambaye ni kada maarufu wilayani hapa, alisema fitina zinazoanza kufanywa na makada wenzake zinalenga kusababisha makundi na mwisho ni kupoteza jimbo hilo kwa upinzani.
“Tarime ilikuwa mikononi mwa upinzani kwa miaka 10, sasa imerejea CCM na hali imekuwa shwari na maendeleo ya haraka yanaonekana. Lakini hizi kampeni za chini kwa chini zinazoendelea na wengine wanafanya kwa uwazi na kuchinja ng’ombe, haziwezi kuwa na tija kwa mustakabali wa Chama chetu,” alisema.Aliongeza kuwa makada walioshindwa kwenye kura za maoni wanapaswa kumsaidia mbunge wa sasa, Nyambari Nyangwine ili aweze kutimiza ahadi na kutekeleza Ilani ya CCM badala ya kumvuruga kwa lengo la kumkwamisha.
Naye Chacha Mroni alisema uongozi wa CCM unapaswa kuchukua hatua za haraka kuwadhibiti makada walioanza kufanya kampeni mapema.
Alisema iwapo makada maarufu wa CCM walioanza kukivuruga Chama kwa kufanya kampeni za urais walidhibitiwa na kuchukuliwa hatua kali, haoni kwanini wanaovuruga majimbo wanaachwa.
“Tunakipenda Chama chetu na tutaendelea kuwa na imani nacho, wapo makada tena wazito na viongozi wa juu wamechukuliwa hatua kwa kuanza kampeni mapema, hawa wengine kwanini wanafumbiwa macho.“Tunataka kuona hatua zikichukuliwa na kama kuna watu wanataka ubunge, wasubiri muda mwafaka ufike waanze kujiuza kwa wanachama,” alisema huku akionyesha kukerwa na hatua hiyo.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tarime, Rashid Bogomba alipotafutwa kuzungumzia taarifa hizo, hakuweza kupatikana na hata alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi, haikupokewa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Tarime, Nyambari Nyangweni alipoulizwa, alikiri kuwepo kwa makada wanaozunguka kwa lengo la kuwania ubunge mwaka 2015.
Alisema baadhi ya makada hao wanaendesha kampeni chafu za ukabila na kuwagawa wanachama, jambo ambalo ni hatari na linapaswa kukemewa.
Alisema si vibaya kwa wana-CCM kuwania nafasi za uongozi, ikiwemo ya ubunge katika jimbo hilo, lakini suala la msingi ni kufuata taratibu za Chama badala ya kumvuruga na kumwekea vikwazo katika kuwatumikia wapiga kura wake.
“Nafahamu kuna wenzangu wanazunguka kila mahali kueneza fitina na kupanga mikakati kwa ajili ya uchaguzi wa mwakani. Si vibaya, lakini wanapaswa kufuata taratibu na kusubiri muda mwafaka na si kuvuruga utendaji kazi wangu.
“Kazi niliyoifanya wananchi wanaiona na kamwe sina shaka, lakini nasikitishwa na hila za wenzangu kuwagawa wanachama na kutumia ukabila kusaka uongozi. Kwa maslahi ya wananchi wa Tarime, nitawasilisha malalamiko mahali husika,” alisema Nyangwine
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru