- Vifungu vya sheria vyawakwaza wajumbe
- Mwenyekiti Sitta aombwa kuongeza muda
NA WAANDISHI WETU, DODOMA
SHERIA ya Mabadiliko ya Katiba huenda ikarejeshwa tena katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho.
Hatua hiyo inatokana na Kifungu cha 26 (2) cha sheria hiyo kuonekana kuwakwaza wajumbe wengi wakati wa kujadili Rasimu ya Pili ya Katiba.
Tayari baadhi ya wajumbe wakiwemo wenyeviti wa kamati wamelalamikia kubanwa na kifungu hicho hivyo kushindwa kufikiwa kwa haraka kwa baadhi ya mambo.
Christopher Ole Sendeka, wakati wa kujadili kanuni, alikaririwa akilalamikia kifungu cha 26 (2) cha sheria hiyo kuwa ni kikwazo katika kuwapatia Watanzania katiba bora na itakayojali maslahi ya wengi.
Kifungu hicho ndicho kinachopendekeza kuwa, ili Katiba na ibara zake vipitishwe na Bunge Maalumu la Katiba, lazima viungwe mkono kwa kura na wajumbe wote wa Bunge Maalumu kwa theluthi mbili kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili kutoka Zanzibar.
Wenyeviti wa kamati tatu, ambao ni pamoja na Ummy Mwalimu, Mwenyekiti wa Kamati namba moja, amekiri kutokea kwa tatizo hilo, sambamba na Anna Abdallah, anayeongoza kamati namba 10. Pia Mwenyekiti wa Kamati namba 11, Hamad Rashid Mohammed alisema tatizo hilo lilijitokeza katika upigaji wa kura.
Hali hiyo inaashiria kuwa, kuna uwezekano mkubwa wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ikarejeshwa tena katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili ifanyiwe marekebisho.
Kipengele hicho ambacho kipo kwenye Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kinataka uamuzi wa Bunge Maalumu ufanyike kwa idadi ya kura, ambazo ni theluthi mbili kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili kutoka Zanzibar.
Hata hivyo, baadhi ya wenyeviti waliozungumza jana akiwemo Hamad, alisema katika Kamati yake, baadhi ya ibara walilazimika kuzipitisha kwa mfumo wa kura za wengi wape badala ya kura za theluthi mbili kila upande.
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati Namba Moja, Profesa Makame Mbarawa alisema hilo si tatizo kubwa kwa upande wa kura za kwenye kamati, ambako wanaweza kulirekebisha.
Hata hivyo, bado kuna hatari ya tatizo hilo kujitokeza katika kura za bungeni kama alivyoainisha Ole Sendeka.
“Kifungu hicho ndicho kinachopendekeza kuwa ili Katiba na ibara zake vipitishwe na Bunge Maalumu la Katiba, lazima viungwe mkono kwa kura na wajumbe wote wa Bunge Maalumu kwa theluthi mbili kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili kutoka Zanzibar,” alisema Ole Sendeka, ambaye anaongoza Kamati Namba Nne.Uwezekano wa kupata kura hizo katika masuala yanayobishaniwa, likiwemo suala la Muungano, imetajwa kuwa mgumu, hasa theluthi mbili kutoka Zanzibar.
Hali hiyo inatokana na ukweli kuwa, ili kupata theluthi mbili za wajumbe kutoka Zanzibar, CCM italazimika kuwashawishi wajumbe kutoka CUF au CUF kuwashawishi wajumbe kutoka CCM.
Mwenyekiti wa Kamati Namba Nane, ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri, Job Ndugai alikiri kuwa ibara nyingi za sura ya Kwanza na Sita, zimeshindwa kupitishwa kwa theluthi mbili kutoka Bara na Zanzibar.
Hata hivyo, Ndugai alisema tatizo hilo linaweza kuthibitishwa zaidi wakati wa majadiliano ya wajumbe wote, ambapo alionyesha hofu ya kutofanikiwa.
Mwenyekiti wa Kamati Namba 11, Anne Kilango Malicela alisema wajumbe wa Tanzania Bara na Wazanzibar wanakubali kuwepo kwa Muungano.
Alisema baadhi ya wajumbe wameendelea kuvutana kuhusu serikali mbili na serikali tatu na kwamba malumbano hayo yanafanyika kwa hoja.
Muda wa majadiliano watesa wenyeviti
Asilimia kubwa ya wenyeviti waliozungumza jana, waliendelea kulalamikia muda wa majadiliano wa siku mbili kutotosha.
Anna Abdallah alisema mpaka jana mchana walikuwa wamemaliza kujadili Sura ya Kwanza, hivyo amelazimika kumuandikia barua Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kuomba kuongezwa muda wa siku mbili zaidi ili wakamilishe kazi hiyo.
Naye Ummy alisema tayari wameshamwandikia barua mwenyekiti huyo, kuomba kuongezwa muda wa majadiliano.
Alitolea mfano wa siku ya kwanza ya majadiliano, ambapo alidai walitumia siku nzima kujadili kipengele cha ibara moja ya Sura ya Kwanza inayozungumzia muundo wa serikali ya shirikisho.
“Hapa ndipo tulitumia muda mwingi kwani kuna hoja za serikali mbili, tatu na shirikisho, kwa hiyo wajumbe walikuwa na hoja nyingi, ambapo kila mmoja alitakiwa kutumia dakika 10 kuchangia na kamati yangu ina wajumbe 53,” alisema Ummy.Mpaka kufikia jana jioni, kamati nyingi zilikuwa hazijamaliza kazi, isipokuwa kamati namba 11 inayoongozwa na Anne Kilango Malecela, ambayo ilkuwa imeshamaliza kuzijadili Sura zote mbili, na jioni walitaraijia kupiga kura.
Akizungumzia hali hiyo, Ummy alisema kwa mujibu wa Kanuni ya 32 (1), kila kamati itajadili Rasimu ya Katiba kwa wakati mmoja kwa kuzingatia mgawanyo wa sura mbili za Rasimu ya katiba kwa mujibu wa ratiba itakayopangwa na kamati ya uongozi.
Kwa maana nyingine, Ummy alisema kesho bunge litarejea kama kawaida na hivyo, Mwenyekiti kwa mujibu wa kanuni, anaweza akatengua kanuni hiyo ili muda uongezwe, ama viongozi wawasilishe taarifa walizonazo.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru