Tuesday, 8 April 2014

Sitta: Bunge halitavunjwa

  • Asema wajumbe wanafikiri tofauti, wamepotoka
  • Alichozungumza na Pengo, Mufti Simba siri nzito
  • Bunge kuahirishwa Aprili 28, kupisha la bajeti
Na Hamis Shimye 
MWENYEKITI wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta amesema bunge hilo halitavunjwa na wale wajumbe wenye fikra za kuvunjwa kwa bunge hilo, watakuwa wamepotoka.
Mbali na hilo, pia amesema ifikapo Aprili 28, mwaka huu, bunge hilo litaahirishwa kwa ajili ya kupisha vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambalo litakuwa la bajeti na litarejea tena mwezi Agosti.
Sitta aliyasema hayo jana kwa nyakati tofauti alipokuwa katika vikao vya siri baada ya
kuwatembelea viongozi wa dini ya kiislamu na kikristo kwa upande wa dhehebu la Katoliki.
Katika ziara yake hiyo aliyosema itamfikisha katika madhehebu yote nchini, alianza kumtembelea Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycap Kardinali Pengo na Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Issa Shaaban Bin Simba.
Alisema Bunge Maalumu la Katiba limetumia fedha nyingi za umma na kwamba, serikali haipo tayari kuona fedha hizo zikipotea kwa vile kuna watu wana mawazo ya bunge hilo kuvunjwa. Alisema watu wenye mawazo hayo wanajidanganya.

Nimekutana na Rais Jakaya Kikwete juzi, nimemuona hana mpango wala mawazo ya kulivunja bunge hilo, kwani ana nia ya dhati ya kuhakikisha mchakato huu unafika salama na watanzania wanapata Katiba mpya. Wenye mawazo kwamba litavunjwa ni wapuuzi, alisema.
Sitta alisema katika kikao chake na Rais Kikwete,
alionekana kukubali bunge hilo kuahirishwa ifikapo Aprili 28 na kuitishwa tena Agosti baada ya vikao vya bajeti kumalizika, ingawa taarifa rasmi itatolewa na serikali.
Alisema kanuni na sheria zinamruhusu Rais Kikwete kuliahirisha bunge hilo pale siku zake 70 zitakapomalizika na kuona kazi haijamalizika na kuliitisha tena ili mchakato wote umalizike.

Nimekutana na Askofu Pengo na Mufti Simba. Hawa ni watu muhimu katika dini zetu.
Wamefurahishwa na mchakato mzima na nimewaomba watuombee ili tumalize mchakato wetu, alisema.
Mwenyekiti huyo alisema vikao hivyo atavifanya kwa madhehebu yote nchini bila kubagua na huo ndio mwanzo wake alioupanga kuhakikisha mchakato huo unashirikisha watu wote.
Sitta alisema katika vikao vyake na viongozi hao wa dini, aliwaeleza mchakato mzima unavyoendelea bungeni.


Sura mbili ndizo zilikuwa zinajadiliwa na Kamati zote 12. Wenyeviti wote watawasilisha taarifa zao kesho (leo) na baadae uchangiaji ndio utafuata, alisema.

Msimamo wa serikali mbili au tatu
Sitta alisema ziara yake haihusiani na upande wa serikali mbili au tatu, lakini katika suala hilo, anaunga mkono kauli ya mwanasiasa mkongwe Kingunge Ngombale Mwiru.

Niwe mkweli kabisa, namuunga mkono Kingunge. Rasimu ina mambo mengi zaidi ya serikali tatu. Katiba tuliyonayo ina mapengo na lazima tuyazibe ili kizazi kijacho kijivunie, alisema.
Alisema wanaopiga kelele juu ya hilo wapo katika kusaka nafasi za uongozi kwa kuwa wanaamini wakizikosa katika Tanganyika, wazitapata katika Muungano.

Tumeanza na sura ya namna muundo wa uongozi utakavyokuwa. Serikali tatu kwangu si kipaumbele na jambo la umuhimu ni kuhakikisha tunakuwa na Katiba itakayoziba mapengo na kuwashughulikia wabadhirifu wa fedha za umma, alisema.
Amewataka wajumbe wa bunge hilo
wajiandae kuchangia kwa makundi yote na hakuna atakayenyimwa nafasi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru