Thursday, 17 April 2014

Kuwatukana waasisi ni kukosa adabu- JK



  • Askofu Mtetemela amshukia Prof. Lipumba
  • Lukuvi afyatuka bungeni, arusha kombora CUF
  • Mwigulu asimamisha posho kwa waliogoma
  • Wajumbe waliofuata mkumbo mikononi mwa JK

NA MWANDISHI WETU
RAIS Jakaya Kikwete amesema ni utovu wa nidhamu na ukosefu wa adabu kwa baadhi ya Watanzania kuwatukana, kuwadhihaki na kuwakejeli waasisi wa Taifa hayati Julius Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amaan Karume.

Amesema viongozi hao wawili wameifanyia Tanzania mambo mengi makubwa na ya kihistoria kiasi kwamba Watanzania wanao wajibu wa kudumisha na kuenzi heshima yao kwa namna ya kudumu.
Rais Kikwete alisema hayo juzi wakati akizungumza na wahariri wa baadhi ya vyombo vya habari nchini Ikulu mjini Dar es Salaam katika mahojiano maalumu ya kuadhimisha miaka 50 ya Muungano.
“Ni kukosa adabu na ni utovu mkubwa wa nidhamu kwa Mtanzania yeyote kuwatukana, kuwadhihaki ama kuwakejeli waasisi wa taifa letu. Hawa ni watu ambao wameifanyia nchi yetu mambo makubwa,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza : “Mzee Karume, yule aliongoza Mapinduzi yaliyoondoa dhuluma na uonevu pale Zanzibar. Waafrika walio wengi walikuwa wanaonewa sana pale, pengine watu wamesahau, lakini hata pale walipokuwa wanashinda uchaguzi, bado walikuwa hawapewi nafasi ya kuongoza maisha yao wenyewe.”
 “Ni ukosefu wa adabu kwa yeyote kumshutumu mtu aliyejitolea kiasi hicho ili kubadilisha mfumo dhalimu na kujenga maisha na mazingira ya maisha bora kwa wengi,” alisisitiza.
“Mzee Nyerere ametuachia taifa moja, lililoungana, lenye umoja, lenye amani na mshikamano. Misingi ambayo aliijenga yeye ndiyo imeendelea kuongoza taifa letu kwa miaka yote hii. Viongozi wengine wote ambao wamemfuata – Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa na sasa mimi mwenyewe, tumefuata na kuongozwa na misingi hiyo. Na siku nchi yetu inaamua kuipuuza misingi hiyo, tutaingia katika matatizo makubwa,”alionya.
Rais Kikwete alitoa msimamo huo baada ya kuulizwa swali kuhusu matusi, kejeli na dhihaka ambazo zimekuwa zikionyeshwa na wajumbe wachache wa Bunge Maalum la Katiba juu ya waasisi hao wa Tanzania na wabunifu wakuu wa Muungano wa Tanzania.
Miongoni mwa watu walitoa kauli dhidi ya waasisi hao hivi karibuni ni Tundu Lissu, kiasi cha kusababisha wabunge wenzake, viongozi wa dini na wananchi kumjia juu.

Askofu Mtetemela amshukia Lipumba
Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Donald Mtetemela, ameeleza kushangazwa na kuchukizwa na kitendo cha Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, kulifananisha bunge hilo na askari wa Itarahamwe.
Akichangia bungeni jana, Askofu Mtetemela alisema kitendo kilichofanywa na Profesa Lipumba hakikubaliki na si cha uungwana kwani, kinaweza kuleta uhasama baina ya Tanzania na Rwanda.
“Binafsi nilitaka kumuona Lipumba kumueleza haya, lakini sikufanikiwa mpaka sasa nilipopata nafasi ya kuchangia. Nimesikitishwa na kitendo hicho cha kufananisha wajumbe wa bunge na wauaji, sisi hatupo hapa kuua mtu,’’ alisema.   
Alisema kitendo hicho kinapaswa kukemewa kwa nguvu zote na Watanzania na kwamba hakikustahili kufanywa na kiongozi kama Lipumba.
“Hata kama kuna jambo limewaudhi wajumbe wa UKAWA, walikuwa na nafasi ya kukaa pamoja na kuridhiana. Kiongozi kama Lipumba ambaye anasifa kubwa ndani na nje ya nchi anadiriki kutoa kauli ya ajabu kisha kutoka ndani ya bunge kususia mchakato huo.
“Busara ya kiongozi si kukasirika au kuamua jambo kwa hasira, angetumia maridhiano kutatua hilo kwani wananchi wanataka kuona tunatoka na katiba, hatupo hapa kwa ajili ya vyama na wala vyama visitubomoe na kuacha kilichotuleta,’’ alisema.
Alisema pia kuwa mfumo wa serikali tatu unahitaji muda na matayarisho ya kutosha na si kukurupuka na kuamua mambo bila kutafakari.
Alisema kwa sasa mfumo uliopo ni wa Muungano wa serikali mbili, ambao umefanya mambo mengi katika kipindi cha miaka 50, ambayo yanastahili kupongezwa licha ya kuwepo changamoto.
‘’Wapo watu wanaosema hakuna kilichofanyika, lakini yapo mengi yenye mafanikio kwa taifa letu.
Cha msingi tufanye mambo yetu mazuri bila kujali kama tutasifiwa au la,’’ alisema.
Kuhusu mwenendo wa bunge, alisema: “Katika mila na desturi zetu, bunge hili ni kama baraza la wazee, ni lazima kuwe na utulivu, lakini pamoja na kuwepo kwa viongozi wetu wa kitaifa hapa ndani, tumeshindwa kutunza heshima yetu.
“Tunaitwa waheshimiwa, lakini sisi wenyewe hatuheshimiani na wala hatuheshimu viongozi wetu waliopo humu ndani, tusipoteze lengo lililotuleta hapa.’’
Kuhusu lugha za kejeli na kashfa bungeni, Askofu Mtetemela alisema, kauli zilizotolewa dhidi ya waasisi wa taifa zinastahili kulaaniwa.
“Wewe una kipimo cha kiasi gani cha kuwakosoa waasisi hawa, ambao wameweza kuliletea taifa amani na utulivu kutokana na maono yao.
“Wewe kama una nguvu, pambana na mtu mwenye nguvu na si mfu na hata kwenye misiba huwa tunasema mazuri ya marehemu na si mabaya kwani, mabaya anayeweza kuyahoji ni Mungu tu kwa wakati huo,’’ alisema.

Lukuvi afyatuka, arusha kombora CUF
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi jana aliwatolea uvivu viongozi wa UKAWA kutokana na kulazimisha hoja zao ili kupata fursa ya kuongoza dola.

Pia alifichua siri kuwa viongozi wa CUF na CHADEMA wameungana kwa mkataba wa kila upande kuunda serikali na ndio sababu wanashupalia serikali tatu licha ya kuwa na changamoto lukuki.
Alikituhumu CUF kuendesha siasa zake kupitia kivuli cha kikundi cha Uamsho, jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa taifa.
Lukuvi alitoa kauli hiyo baada ya kupewa nafasi ya kujibu tuhuma zilizoibuliwa na Profesa Lipumba kuwa alitumia sherehe za kumsimika Askofu wa Kanisa la Methodist la mjini hapa, kupigia chapuo muundo wa serikali mbili na kutoa vitisho kuhusu serikali tatu.
Alisema Uamsho wamekuwa wakiendesha siasa za CUF kwa kupitia kivuli cha dini, hivyo hakuna shaka kuwa hata kitakapopata madaraka ,utawala wake utakuwa wa kidini.
“Mambo mengi wanayoyasema wanachama wa CUF ndiyo yanayosemwa na taasisi hiyo, hivyo kwa hofu yangu binafsi, sina shaka Uamsho ni CUF kwani hata Wazanzibar wenyewe wanajua hilo,’’ alisema.
‘’ Hatujawahi kuona Chama kinachojitayarisha kuchukua madaraka kinatumia mgongo wa dini kufanya siasa. Hii si sahihi, kwanini nisiwe na hofu na kusema,’’ alisisitiza
Akizungumzia Jeshi kuchukua madaraka, Lukuvi alisema hofu yake hiyo imetokana na rasimu ya katiba, ambayo inapendekeza kuwepo kwa serikali tatu, jambo ambalo serikali moja ya Muungano vyanzo vyake vya mapato havikuwekwa wazi.
“Haya yalikuwa ni mawazo yangu binafsi na sikuwa na shida kuyaeleza na nitaendelea kuyaeleza na kisiwe chanzo cha wanachama wa UKAWA kudai kuwa hiyo ni lugha ya uchochezi.
“Hivi kati ya mimi na Maalim Seif (Katibu Mkuu wa CUF) nani ni mchochezi ? Mbona hawakugomea kauli yake aliyoitoa Kibanda Maiti kuwa Rais Kikwete atamtuma Mkuu wa Majeshi Mwamunyange kwenda kupindua nchi iwapo serikali tatu zitapita,’’ alisema lukuvi.
Aliwataka wajumbe wa Bunge hilo kufanya kazi waliyokabidhiwa ya kupitia rasimu iliyopendekezwa na si kutafuta visingizio kama inavyofanya UKAWA.
Juzi, Profesa Lipumba alisema Lukuvi alisikika akisema kuwa endapo serikali tatu zitapita, jeshi litachukua nchi.
Akizungumza jana asubuhi, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samwel Sitta alisema, wamelazimika kumuita Lukuvi ndani ya bunge ili aweze kutoa maelezo kuhusiana na kauli yake iliyodaiwa na Lipumba kuwa ni chanzo cha kususia bunge.
Alisema awali Lukuvi alitakiwa kusafiri kwenda nchini India kwa matibabu, lakini amemrudisha ili kutoa ufafanuzi wa tuhuma hizo kwanza.
Sitta alisema jambo la wajumbe hao wa UWAKA la kususia Bunge kwa madai ya kauli za uchochezi halikustahili kufanywa kwani, kila kero ina utaratibu wake wa kushughulikiwa.
Alisema kuteuliwa na Rais kuwa miongoni mwa watunga katiba ni jambo la heshima na ya kipekee kwani utungaji wa katiba si jambo ambalo hufanyika kila mara.
“Baadhi ya wajumbe wenzetu hawajatambua uzito wa jambo hilo, kwani wakati wote kumekuwa na mambo kadhaa hapa ndani, lakini yamevumiliwa kwa nia njema ili tufikie mwisho ulio salama,”alisema.
Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samia Suluhu Hassan, alisema kitendo kilichofanywa na wajumbe wa UKAWA hakiwatendei haki Watanzania.
Pia,alisema watakutana na Kamati ya Uongozi  kujadiliana hatua zaidi za kuchukua.

Mwigulu asimamisha posho
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Mchemba amesema serikali imesimamisha malipo ya posho ya wabunge wote waliosusia vikao vya bunge juzi.

Pia, amesema wajumbe ambao ni watumishi wa umma, wataripotiwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi kwa ajili ya hatua za kinidhamu.
Alisema licha ya kuwa wajumbe hao wameshalipwa posho hizo hadi Aprili 26, mwaka huu, tayari amesitisha malipo hayo ambayo yalikuwa yapitie benki.
“Huku kwa upande wa bunge taratibu za kuwalipa zilishakamilika, lakini kwa kuwa malipo hayo yanapitia benki, nimeagiza wasitishe,’’ alisema.
Alisema malipo kwa wajumbe hao yatafanyika pale tu watakaporejea ndani ya bunge kuendelea na mchakato huo wa Bunge.
“Watakaolipwa posho kwa sasa ni wale wanaohudhuria vikao, hatuko pikiniki hapa, tunawalipa watu halafu hawataki kufanya kazi,” alisema.

Juzi, Livingstone Lusinde alisema kilichokosewa ni uamuzi wa bunge kulipwa kwa fedha za sikukuu, jambo ambalo limewafanya kususa na kuondoka.
Naye Said Mkumba alielezea kushangazwa na wajumbe hao walioamua kutoka nje, akihoji kwamba kwa nini hawakutoka siku mbili zilizopita, mpaka wamesubiri walipwe posho hadi ya Aprili 26, ndio waondoke.

WASSIRA: SIJASHANGAZWA NA WALIOSUSA
Naye Stephen Wasira, amesema hakushangazwa na kitendo cha kutoka nje ya bunge wajumbe wa UKAWA kwani, ni matukio yaliyopangwa muda.

Wasira, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), alisema UKAWA walikuwa na mpango huo muda mrefu baada ya kuona hoja yao kuhusu kutokuwepo kwa hati ya muungano kukosa ukweli.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Wasira alisema sababu wanayosema kuwa wametukanwa ndipo wakaamua kutoka nje ya bunge, haina mashiko kwani UKAWA walitoa maneno ya kashfa dhidi ya waasisi wa Muungano.
“Hoja iliyotolewa na Kiongozi wa UKAWA kuwa wanatukanwa bungeni ni ya ajabu kwa kuwa UKAWA wamekuwa wakiwatolea maneno yasiyofaa waasisi wa muungano, kitendo ambacho hakikubaliki na Wananchi” alisema 
Aliongeza kuwa ni muhimu kwa wajumbe wa bunge hilo kushindana kwa hoja na sio kutoka nje ya bunge na kutafuta sababu zisizokuwa na msingi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru