NA SHAABAN MDOE, ARUSHA
HALI ni tete ndani ya CHADEMA mkoani Arusha, baada ya viongozi wake wane, wakiwemo wenyeviti wawili wa wilaya kutangaza kujiuzulu na kukihama chama hicho.
Hatua hiyo ya viongozi hao ni mwendelezo wa makada na wanachama kuendelea kujiondoa ndani ya CHADEMA kutokana na kutoridhishwa na uendeshaji wake pamoja na tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya zinazoelekezwa kwa baadhi ya viongozi wa kitaifa.
Viongozi waliotangaza kujiengua ndani ya chama hicho ni Mwenyekiti wa wilaya ya Monduli, Amani Silanga na Mwenyekiti wa wilaya ya Ngorongoro, Revocatus Parapara, ambao walisema wamechoshwa na uozo unaofukuta CHADEMA bila kupatiwa ufumbuzi.
Hata hivyo, wamesema kwa sasa bado wanatafakari mahali pa kwenda ili kuendeleza gurudumu la maendeleo.
Akizungumza baada ya kuachia wadhifa huo, Silanga alisema manyanyaso na uvunjaji wa katiba ndani ya CHADEMA vimeshika hatamu na kwamba mwanasiasa makini na mwenye kutaka maendeleo ya Watanzania, kamwe hawezi kuendelea kukaa.
Alisema baadhi ya viongozi wa juu wamejenga mtandao hatari wa kunyanyasa wanachama na viongozi wa chini kwa kuwatumia viongozi wa mikoa, ambao wengi wamewekwa na kazi yao kubwa ni kutii amri.
“Mambo si shwari kama wengi wanavyoona kwa nje, CHADEMA kumeoza na si taasisi inayoweza kuwakomboa Watanzania. Katibu wa Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa amenyanyaswa kwa sababu ya kupinga kusimamishwa kwa Zitto Kabwe na Dk. Kitilla Mkumbo,” alisema na kuongeza kuwa demokrasia ya kweli husikiliza na kuthamini mawazo ya pande zote.Alisema CHADEMA imekuwa ikiendeshwa kama SACCOS na maamuzi yanatolewa na wachache, jambo ambalo ni hatari na halipaswi kufumbiwa macho na wanachama wengine waliobaki.
Kwa upande wake, Parapara alisema amejiuzulu baada ya kutambua CHADEMA si chama cha ukombozi kwa Watanzania bali ni kikundi cha watu wanaolinda maslahi yao binafsi.
Alisema wanachama walio wengi na baadhi ya viongozi wamekata tamaa, lakini wanashindwa kuweka mambo hadharani kwa kuhofia yaliyowapata waliotangulia.
Alisema kwa muda aliokaa madarakani wilayani humo, aliweza kuanzisha matawi ya chama hicho katika kata 20 na kupata wanachama 15,000, ambao wako tayari kumuunga mkono chama chochote atakachokwenda.
Vigogo wengine waliotangaza kujiuzulu nafasi zao na uanachama ni Mwenyekiti wa chama hicho kata ya Terati, Gerald Majengo na Katibu Mwenezi wa kata ya Olorien, Prosper Mtinanga.
Viongozi hao wamedai kuchoshwa na siasa za kitapeli na ufisadi wa baadhi ya vigogo wa ngazi za juu na kwamba, kwa maslahi ya watanzania wataweka mambo hadharani.
Kwa pamoja walimshutumu Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema kwa madai amekuwa akifanya kazi za viongozi wa juu kwa kutangaza kuwafukuza na kuwadhibiti makada wanaozungumza ukweli.
Majengo alisema aliwahi kuhoji kiwanja kilichotolewa na mwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya akinamama, ambacho kwa sasa hakieleweki.
Habari za kuaminika zinasema kuwa, kuendelea kupasuka vipande vipande kwa CHADEMA ni laana ya Zitto, ambaye kwa sasa amefukuzwa uanachama kwa kile kilichodaiwa kutaka kufanya mapinduzi ya uongozi.
Kwa sasa Kabwe ameendelea kuwa mbunge kwa zuio la mahakama, ambapo uongozi wa CHADEMA umempiga marufuku kutumia bendera na vitu vingine vinavyokihusu chama hicho.
Mbali na kukimbiwa na viongozi na wanachama, CHADEMA pia kimeendelea kuwa dhaifu mbele ya CCM kutokana na kugaragazwa kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani na ubunge.
Katika uchaguzi mdogo wa madiwani uliohusisha kata 27 nchini, CCM ilizoa kata 23 huku CHADEMA kikiambulia tatu, licha ya kuzunguka nchi nzima kwa kutumia helkopta tatu, ambazo zilikodiwa kwa mamilioni ya shilingi na vigogo kulipwa posho.
CHADEMA pia kimeangukia pua kwenye uchaguzi mdogo wa majimbo mawili ya ubunge, ambapo CCM ilishinda Jimbo la Kalenga na Chalinze kwa zaidi ya asilimia 80 ya kura zote
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru