NA WAANDISHI WETU, DODOMA
HATI za Muungano na muundo wa serikali vimeendelea kuzua mjadala mkubwa miongoni mwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, ambapo baadhi wamesema hayo ndio masuala ya msingi.
Wajumbe wengi wameendelea kupinga hadharani mapendekezo ya serikali tatu huku wakitaka kuwasilishwa kwa Hati za Muungano halisi kwa madai kuwa ndizo zitamaliza sintofahamu iliyopo kwa sasa.
Hayo yalijitokeza jana wakati baadhi ya Wenyeviti wa Kamati za Bunge walipowasilisha taarifa za kamati zao, ambapo Assumpter Mshama alisema kamati yake imekataa mapendekezo ya serikali tatu na wajumbe wametaka mfumo wa serikali mbili uendelee.
Assumpter, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati namba 5, alisema muundo wa serikali tatu umekataliwa na theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na kutoa mapendekezo.
“Muundo wa serikali mbili ndiyo ulioafikiwa na wajumbe wengi kuwa unalifaa taifa letu kwa kuzingatia maslahi ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiusalama kwa wananchi wa pande zote,’’ alisema.
Alisema muundo huo umedumu kwa miaka 50 na zimekuwepo changamoto mbalimbali ambazo nazo zimekuwa zikitatuliwa na serikali za pande zote mbili.
Aliongeza kuwa mchakato unaoendelea sasa ni fursa kubwa na ya pekee kuzishughulikia changamoto hizo kwa mapana yake.
“Mapendekezo yaliyotolewa na walio wengi yanalenga kuzipa jitihada hizi kinga za kikatiba na kisheria ili ufumbuzi wake uwe endelevu," alisema.
Alisema endapo muundo utakuwa wa serikali tatu, serikali hiyo ya tatu itakuwa inayoelea, iliyo mbali na wananchi, tegemezi na yenye gharama kubwa kiuendeshaji.
Akizungumzia sababu ya kufanya mapendekezo ya marekebisho hayo, Assupter alisema ni ukweli kuwa hati ya makubaliano ya Muungano ndiyo msingi wa muundo wa serikali mbili uliopo sasa.
Mwenyekiti wa Kamati Namba Mbili, Shamsi Vuai Nahodha, akiwasilisha mapendekezo ya kamati yake, alisema shirikisho la serikali tatu linalopendekezwa katika rasimu, litakuwa dhaifu kiasi cha kushindwa kudhibiti ulinzi wa eneo la Bahari ya Hindi.
Alisema udhaifu huo utayapa mwanya mataifa hayo kuzirubuni nchi washirika zisichangie gharama za uendeshaji wa Serikali ya Shirikisho, hasa kwa kuwa halitakuwa na vyanzo vya uhakika vya mapato.
HATI ZA MUUNGANO MOTO
Baadhi ya wajumbe wa Kamati za Bunge Maalumu la Katiba wamesisitiza kuwasilishwa kwa Hati ya Muungano halisi ili kumaliza utata uliojengeka miongoni mwa wajumbe.
Wamesema maelezo ya aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika wakati nchi mbili za Tanganyika na Serikali ya Watu wa Zanzibar zikiungana, kwamba Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliifuta Tanganyika, yanatia shaka.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Dk. Emmanuel Makaidi, aliyekuwa akitoa ufafanuzi kuhusu hoja za wachache wasiokubaliana na mfumo wa serikali mbili.
Alitoa ufafanuzi huo baada ya Mwenyekiti wa Kamati namba mbili, Shamsi Vuai Nahodha kusoma taarifa ya kamati hiyo.
"Kama hati hiyo ipo, tunaomba iletwe hapa wajumbe waione. Hati ya mashaka mashaka haiwezi kujenga katiba mpya," alisema na kuongeza hati ya muungano ndio msingi wa katiba.
Awali, akisoma maoni ya wajumbe wachache wa kamati hiyo juu ya utata wa uwepo wa uhalali wa hati ya muungano, Shamsi alisema wajumbe hao wanasema pamoja na ujio wa Msekwa, alishindwa kuwathibitishia uwepo wa uhalali wa hati hiyo pamoja na ile ya maridhiano, badala yake aliwaambia anaikumbuka siku ile ya Muungano na anazo picha, vitu ambavyo haviondoi utata uliopo.
"Ukweli ni kwamba mpaka sasa wajumbe wa Bunge hili wameshindwa kupata nyaraka hizi mbili zenye saini zinazothibitisha kuwa pande zote mbili ziliridhia uwepo wa Muungano. Hati ya maridhiano, ambayo iliwasilishwa kwa wajumbe wa kamati, ilikuwa ni batili kwa sababu mbalimbali, ikiwemo ya kughushiwa kwa saini ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Msekwa," walisema wajumbe hao katika maoni yao.
Kwa mujibu wa wajumbe hao, makosa hayo pamoja na mengine mengi yamechochea utata juu ya Muungano na kumekuwepo kwa malumbano ya viongozi mbalimbali juu ya uhalali wa nyaraka ambazo walipewa huku kukiwa na shaka ya kughushiwa kwa saini hizo.
Wajumbe hao wanasema Aprili 22, 1964, Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, Mwalimu Nyerere na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, inasemekana walitia saini Hati ya Makubaliano ya Muungano kati ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.
"Wakati wa mjadala wa Sura ya Kwanza na ya Sita, wajumbe wa kamati kama ilivyokuwa kwa wajumbe wa kamati nyingine, waliletewa nakala ya Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano, Sheria Namba 22 ya 1964, ilitolewa baada ya baadhi ya wajumbe kuomba kupatiwa nakala halisi ya kweli ya Hati ya Makubaliano ya Muungano iliyotiwa saini na Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume.
"Japokuwa nakala ya sheria ya kuthibitisha mapatano ya muungano iliyogawiwa kwa wajumbe imeambatanishwa na Hati ya Makubaliano ya Muungano kati ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kama nyongeza ya sheria hiyo, hicho sicho walichoomba wajumbe wa Bunge Maalumu," walisema wajumbe hao.
Wajumbe hao walisema pia kuwa nakala ya Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano haiwezi kuwa mbadala wa nakala halisi ya hati hiyo kwa sababu nyongeza ya sheria waliyogawiwa wajumbe, ambayo inadaiwa kuwa ndio hati ya makubaliano ya muungano, haina saini za Mwalimu Nyerere na Hayati Karume.
Kwa mujibu wa wajumbe hao, ni vigumu katika hali hiyo kuthibitisha kama kweli kile kilichodaiwa kuwa ni hati ya makubaliano ya muungano, ndicho hicho walichokubaliana waasisi hao wa Muungano kwa kutia saini zao.
"Suala la kushindwa kupatikana kwa nakala halisi ya Hati ya Makubaliano ya Muungano sio jambo dogo. Suala hili ndio ufunguo wa kuelewa mgogoro mkubwa wa kikatiba na kisiasa, ambao umegubika Muungano katika nusu karne ya maisha yake,” alisema.
Katika majadiliano ya awali ya kamati hiyo, wajumbe hao wachache walidai kuwa saini ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Julius Nyerere iligushiwa.
Mbali na saini hiyo, pia saini ya aliyekuwa Spika wa Bunge wakati huo, Pius Msekwa nayo ilidaiwa kughushiwa na hivyo kumtaka Msekwa kwenda katika kamati kuthibitisha saini hizo.
David Kafulila, akitoa maoni ya walio wachache kupitia kamati namba tano, alisema nia ya kuwepo kwa serikali tatu si kuulegeza Muungano. Alisema watu wachache katika kamati hiyo waliona jina la shirikisho ndio sahihi.
"Hatutaki serikali tatu zitakazolegeza muungano, tunataka serikali tatu zitakazokuza muungano,” alisema na kuongeza kuwa hakuna shaka juu ya uendeshaji wa serikali ya muungano huku akitoa hoja kuwa Tanzania Bara itapaswa kuchangia zaidi kutokana na ukubwa wake.
MAKONDA: ACHENI KUSHUPALIA HATI
Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Paul Makonda amewaasa wajumbe wenzake kujadili mambo yaliyoko kwenye Muungano badala ya kushupalia hati halisi.
Kauli hiyo ya mjumbe huyo, ilikuja baada ya baadhi ya wajumbe wa bunge hilo, akiwemo John Mnyika, kushinikiza Hati ya Muungano iwepo, hoja iliyozua malumbano miongoni mwao.
Japokuwa hoja ya Mnyika ya kutaka wapewe kinga ya kuitumia ili waboreshe michango yao watakayoiwasilisha bungeni ilikubaliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Othuman Masoud, mjumbe Christopher Ole Sendeka aliipinga kwa utetezi kuwa ina kinga na haipaswi kutumiwa na wajumbe hao.
Katika taarifa yake aliyoituma kwenye vyombo vya habari jana, Makonda aliwaasa wajumbe wenzake waendelee kujadili rasimu ya Katiba Mpya kwa kutumia rasimu badala ya kutaka hati.
"Kama kuna hoja ya msingi kuhusu mchakato huu, basi iwekwe mezani, si kuweka viashiria vya sababu," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Makonda, ambaye pia ni Katibu Uhamasishaji na Chipukizi wa UVCCM, alikumbusha kuwa kila kilichoafikiwa katika Muungano, kilikuwa cha kikanuni na kisheria, hivyo kilicholeta uhai wa muungano huo ni ukamilishwaji wa taratibu za kuutangaza Aprili 26, 1964.
"Sote tumeapa kwa huo Muungano na kwa tafsiri tu kuwa Muungano upo na ulikuwepo. Tunayoweza kujadili ni mambo yaliyoko katika Muungano na si kujadili makaratasi ya muungano," iliongeza sehemu ya taarifa hiyo.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru