Thursday, 3 April 2014

Kinana awaweka kikaangoni viongozi wa CCM Rukwa

NA SULEIMAN JONGO, KALAMBO

KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana amekiagiza Chama mkoa wa Rukwa kufanya uchunguzi wa fedha za CCM zilizopotea katika mazingira ya kutatanisha wilayani Kalambo.
Ametaka kuchukuliwa hatua za haraka dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na upotevu huo kwa kuwa unatoa sura mbaya kwa Chama na watendaji wake.
Kinana alitoa agizo hilo juzi wakati akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wilaya ya Kalambo, ambapo miongoni mwa mambo yaliyoibuliwa kwenye kikao hicho ni pamoja na upotevu wa sh milioni saba zilizokuwa mgawo wa Chama kwa wilaya mpya ya Kalambo.
Aliwataka viongozi wa CCM mkoa wa Rukwa wakiongozwa na Mwenyekiti wa mkoa huo, Polycatus Matete kuchunguza upotevu huo ili watakaobainika kuhusika kwa namna yoyote wachukuliwe hatua za kindhamu.

"Tumekuwa tukiibana serikali kuhakikisha inaondoa uwozo ikiwemo kusimamia fedha mbalimbali, hatuwezi kukubali ndani ya chama wawepo wajanja wachache wenye uroho watuharibie sifa nzuri. Yeyote atakayebainika ama awe ni wa kuchaguliwa au mtumishi wetu, tutamchukulia hatua stahili,"alisema.

Aliongeza: "Ndugu zangu fedha ni fedheha na katika hili, hatutamwacha mtu, yeyote atakayebainika tutamchukulia hatua za kinidhamu kulingana na kosa alilotenda."

Kinana yuko mkoani Rukwa kwa ziara ya kikazi, ambapo amekuwa akitembelea wilaya na majimbo yote ya uchaguzi yaliyoko mkoani humo.
Baada ya mkoa wa Rukwa, Kinana na ujumbe wake wanatarajia kuendelea na ziara hiyo mkoani Kigoma, ambako pia atakagua shughuli mbalimbali za maendeleo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru