Thursday, 29 January 2015

Elimu ya msingi kuendelea kutolewa bure


SERIKALI imesema elimu ya msingi inaendelea kutolewa bure kwenye shule za serikali licha ya kwamba wazazi wanachangia kwa kiasi kidogo.
Hayo yalielezwa bungeni mjini hapa jana, na Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Adam Malima, wakati akijibu swali la Dk, Hamisi Kigwangwala (Nzega-CCM), aliyetaka kujua kwa nini serikali inakusanya kodi kwa wananchi na kisha kuchangiwa huduma za afya, elimu na maji badala ya kutoa huduma hizi bure.
Malima, alisema chanzo kikuu cha mapato ya serikali yoyote ni kodi, ambayo hukusanywa na serikali ili kugharamia matumizi yake, ikiwa ni pamoja na kulipa mishahara na mafao ya watumishi wa sekta ya umma, wakiwemo walimu, watabibu, mapolisi na watumishi kwenye taasisi  za ulinzi na usalama, kujenga miundombinu ya barabara, umeme, maji kuweka mingira bora ya kutoa elimu , afya na kadhalika.
«Ni kweli kuwa wananchi wanachangia malipo kwenye baadhi ya huduma hizi zinazotolewa na serikali kwa bei, ambayo sehemu kubwa ina ruzuku, yaani imefidiwa na mapato ya kodi na vyanzo vingine,» alisema.
Alisema hiyo hufanya huduma kupatikana kwa gharama ndogo, ikilinganishwa na gharama halisi za huduma hizo zinazotolewa na watu binafsi.
Malima alisema ukweli huu ulijitokeza miaka ya nyuma, kipindi hicho huduma hizo zikiwemo afya, elimu na maji zilikuwa zinatolewa bure, ambapo walishuhudia upungufu mkubwa, ikilinganishwa na mahitaji, kama vile upatikanaji wa dawa.
Alisema kwa kutambua hali hiyo na kwa kuzingatia uwezo wao mdogo kimapato, serikali imeanzisha utaratibu wa wananchi kuchangia upatikanaji wa huduma hizo, wakati serikali pia nayo ikiwa ni mmoja wa wanaochangia.
« Hivyo, bei zinazotozwa katika utoaji wa huduma hizo ni mchango wa serikali na wananchi, « alisema.
Aidha, alisema elimu ya sekondari inalipiwa ada kwa gharama ya chini, ikilinganishwa na gharama halisi za kutoa huduma husika.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru