Na Ahmed Makongo, Bunda
MFANYABIASHARA
wa samaki ameuawa kwa kupigwa risasi na mwingine kujeruhiwa kwa risasi katika
matukio mawili tofauti, yaliyotokea wilayani Bunda mkoani Mara.
Kamanda
wa Polisi mkoani Mara, Philpo Kalangi, alithibitisha jana kutokea kwa matukio
hayo alipozungumza na Uhuru kwa njia ya simu.
Alisema
tukio la kwanza lilitokea juzi saa 3:00 usiku, katika eneo la Nyasura mjini
hapa.
Alisema
mfanyabiashara huyo, Mkome Marwa (39), akiwa na mke wake, wakati wakirejea
nyumbani kwao, alipigwa risasi na mtu au watu wasiofahamika.
Kilangi
alisema katika tukio hilo, muuaji hakupora kitu chochote na kwamba ofisi yake
imetuma askari katika wilaya ya Bunda kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo na
kumsaka muuaji.
Kamanda
Kalangi alisema Marwa, ambaye ni mkazi wa mtaa wa Nyasura mjini Bunda,
alipoteza maisha usiku huo huo wakati akipewa matibabu katika Hospitali ya Rufani
ya Bugando jijini Mwanza.
Akisimulia
tukio hilo, Kalangi alisema baada ya kupigwa risasi, mfanyabiashara huyo na mkewee
walikimbilia katika nyumba ya jirani kuomba msaada, lakini wenye nyumba
walifunga geti.
Katika
tukio la pili, Kamanda Kalangi, alisema lilitokea eneo la Bunda Day, ambapo Ndaro Malemi (25), alijeruhiwa kwa
risasi na mtu asiyefahamika wakati
akielekea nyumbani kwake.
Akisimulia
mkasa huo akiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bunda, Malemi alisema alimuona mwanaume
huyo, aliyekuwa amevaa koti jeusi, ambaye alimvizia njiani na kumwamuru ampatie
kila kitu alichokuwa nacho.
Alisema
alipoona hivyo, aliamua kukimbia na ndipo alipopigwa risasi mbili na mtu huyo, ambaye alitokomea kusikojulikana
bila kuchukua kitu chochote.
“Aliniweka chini ya ulinzi na kuniambia nitowe kila kitu, mimi niliposikia hivyo na kuona bastola, niliiacha baiskeli yangu, nikatimua mbio, ndipo akanipiga risasi mbili,”alisema.
Akizungumza
na Uhuru, daktari wa zamu, Dk. Amosi Manya, alisema walipokea majeruhi wawili hospitalini hapo,
ambapo mmoja alikuwa na hali mbaya na kupelekwa Bugando, lakini alifariki dunia
wakati akipatiwa matibabu.
Dk.
Amosi alisema hali ya Maleni inaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu
hospitalini hapo. Maleni alipigwa risasi kifuani.
Kwa
mujibu wa Kamanda Kilengi, hakuna aliyekamatwa na polisi kuhusu matukio hayo na
bado wanaendelea na uchunguzi.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru