Thursday 29 January 2015

Mtanzania afanyiwa unyama wa kutisha ‘Sauzi’



  •  Akatwa sehemu za siri, ajeruhiwa vibaya mgongoni, tumboni na kwenye jicho

NA MWANDISHI WETU
MFANYABIASHARA aliyefahamika kwa jina la Jumanne Tevez, mkazi wa Dar es Salaam, amefanyiwa unyama baada ya kudaiwa kukatwa uume wake na wenzake.
Habari za uhakika kutoka chanzo chetu cha habari zilisema kuwa Tevez, amelazwa katika hospitali moja nchini Afrika Kusini akipatiwa matibabu.

Chanzo chetu hicho ambacho kipo karibu na familia ya mfanyabiashara huyo, kilieleza kuwa taratibu zinafanywa ili mke wake pamoja na kaka yake waweze kusafiri kwa ajili ya kwenda kumchukua.
“Hizo taarifa ni za kweli kabisa na hivi ninavyokuambia mke wake na kaka yake wanatarajia kuondoka kesho ili wakamchukue. Amelazwa katika hospitali moja huko Afrika Kusini na hali yake si mbaya sana.
“Yule jamaa kama unavyojua alikuwa mtu wa dili wa muda mrefu, hivyo inawezekana alitofautina na wenzake ndio maana wakamfanyia kitu mbaya, si unajua hawa jama wa poda (dawa za kulevya), humalizana wenyewe tu,” kilisema chanzo hicho kilipozungumza na Uhuru, jana.
Habari zilizoandikwa kwenye mitandao ya kijamii, zilimuonyesha mfanyabiashara huyo akiwa amevuliwa nguo zote huku akiwa amefungwa kamba mikononi na miguuni.
Tevez, anadaiwa kufanyiwa unyama huo baada ya kuwadhulumu wafanyabiashara wenzake wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.
Habari zinadai kuwa, mfanyabiashara huyo alifanyiwa unyama huo, Afrika Kusini baada ya kubainika kuficha dawa hizo.
Mfanyabiashara huyo anadaiwa kuficha mzigo aliopewa kutoka Afrika Kusini kuuleta Tanzania na kwamba baada ya kufika nchini, aliwaeleza wenzake kuwa mzigo huo umepotea.
Maelezo hayo yalionekana kuwaudhi waliompa mzigo huo, ndipo walipomuita Afrika Kusini, ambako baada ya kufika, waliamua kumfanyia unyama huo.
Picha mbalimbali zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, zinamuonyesha Tevez, akiwa na jeraha mgongoni, tumboni na jicho lake la mkono wa kushoto.
Mfanyabiashara huyo alijipatia umaarufu mkubwa jijini Dar es Salaam,baada ya kufunga ndoa na msanii maarufu wa muziki wa taarab, Isha Ramadhani ‘Mashauzi’ ama jike la Simba.
Katika nyimbo mbalimbali alizokuwa akiimba, Isha anasikika akimtaja mwenza wake huyo wa zamani waliyetengana.
Akizungumza kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini, mmoja wa marafiki wa Tevez, alisema amepata taarifa hizo kupitia mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, alisema baada ya kusoma habari hizo na kuona picha, alimpigia simu rafiki mwingine wa karibu wa mfanyabiashara huyo, ambaye naye alikuwa hajapata taarifa kamili.
“Ninachoweza kukueleza ni kwamba habari hizi nimeziona pamoja na picha kwenye mitandao ya kijamii, nimejaribu kufuatilia kwa rafiki yake mwingine, ambaye yupo karibu naye sana, lakini hakunieleza ipasavyo mkasa huo.
“Hadi sasa kwa kweli tupo njia panda, inawezekana ni kweli, lakini bado hizi taarifa rasmi kutoka kwa familia wanazificha sasa subiri tuone. Cha kusikitisha zaidi baadhi ya watu wanasema amevuta (kufariki dunia), lakini yote hayo hatujathibitishiwa,” alisema.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ilisema haijapata taarifa za kuteswa kwa mfanyabiashara huyo.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa wizara hiyo, Mkumbwa Ally, alisema wizara haina taarifa hiyo na kwamba wataendelea kuzifuatilia kupitia ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini.
Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya cha Jeshi la Polisi, Godfrey Nzoa, hakuweza kupatika kuzungumzia suala hilo kwani simu yake ya mkononi ilikuwa haipo hewani muda wote.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru