NA FURAHA OMARY
WAFUASI 30 wa Chama cha CUF, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka matatu, likiwemo la kufanya mgomo baada ya kukatazwa kukusanyika na kuandamana.
Washitakiwa hao walisomewa mashitaka hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Emmilius Mchauru na kupelekwa rumande katika gereza la Segerea, kutokana na barua za wadhamini kutakiwa kuhakikiwa.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washitakiwa hao ni Shabani Ngurangwa (56), Shabani Tano au Kasakwa (29), Shabani Polomo (40), Juma Mattar (54), Mohammed Kirungi (40), Athumani Ngumwai (40), Shaweji Mohamed (39) na Abdul Juma (40).
Wengine ni Hassan Saidi (37), Hemed Joho (46), Mohamed Mbarucu (31), Issa Hassani (53), Allan Ally (53), Kaisi Kaisi (51), Abdina Abdina (47), Allawi Msenga (53), Mohamed Mtutuma (33) na Salehe Ally (43).
Pia wamo Abdi Hatibu (34), Bakari Malija (43), Abdallah Ally (32), Said Mohamed (40), Salimu Mwafisi, Saleh Rashid (29), Abdallah Said (45), Rehema Kawambwa (47), Salma Ndewa (42), Athumani Said (39), Dickson Leason (37) na Nurdin Msati (37).
Wakili wa Serikali, Joseph Maugo aliwasomea washitakiwa hao mashitaka ya kula njama za kufanya uhalifu, kufanya mkusanyiko usio halali na kufanya mgomo baada ya makatazo halali ya Polisi.
Maugo alidai Januari 27, mwaka huu, maeneo ya wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, washitakiwa wote walikuja njama ya kufanya uhalifu.
Shitaka la pili na tatu yanawakabili mshitakiwa wa kwanza hadi wa 28, ambapo wanadaiwa siku hiyo katika ofisi za CUF, karibu na Hospitali ya Temeke, bila halali walifanya mkusanyiko kwa nia ya kufanya maandamano yasiyo halali kwenda viwanja vya Mbagala Zakhem.
Katika shitaka la tatu, washitakiwa hao wanadaiwa siku hiyo maeneo ya mzunguko wa Mtoni Mtongani, Temeke, waligoma bila kujali tangazo halali lililotolewa na Polisi kuhusu kukusanyika na kuandamana isivyo halali.
Washitaka walikana mashitaka, ambapo Wakili Maugo alidai upelelezi haujakamilika na kwamba hawana pingamizi na dhamana kwa washitakiwa.
Maugo aliomba kabla ya washitakiwa kupatiwa dhamana, waweze kufanyia uhakiki barua za wadhamini kwa lengo la kuhakikisha wanafika mahakamani.
Upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Kibatala uliomba washitakiwa kupatiwa masharti nafuu ya dhamana.
Hakimu Mchauru alitoa masharti ya dhamana kwa kuwataka kila mshitakiwa kujidhamini kwa dhamana ya sh. 100,000 na kuwa na mdhamini mmoja atakayetia saini dhamana ya kiasi hicho.
Hata hivyo, Hakimu Mchauru aliahirisha shauri hilo hadi leo na kuamuru washitakiwa kurudishwa rumande kutokana na muda kuwa umeisha wa kuweza kuzifanyia uhakiki barua hizo.
Washitakiwa hao waliondolewa mahakamani hapo kupelekwa mahabusu katika gereza la Keko na basi kubwa la Magereza huku wakisindikizwa na gari la Polisi.
Thursday, 29 January 2015
Wafuasi 30 wa CUF wapandishwa kizimbani
06:37
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru