Thursday, 29 January 2015

TWB kufungua vituo vidogo vijijini


BENKI ya Wanawake Tanzania (TWB), itaendelea kufungua vituo vidogo  vya kutunzia fedha katika maeneo ya vijijini ili kuwawezesha wanawake kuondokana na kuacha kutunza fedha kizamani.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Pindi Chana wakati akijibu swali la nyongeza la Roman Selasini (Rombo-Chadema).
Selasini aliitaka serikali kuzungumza na benki ili zifungue vituo vidogo vya kutunzia fedha katika maeneo ya vijijini na hatimaye wanawake waondokane na utaratibu wa kizamani wa kutunza fedha.
Katika swali la msingi, Mariamu Kasembe (Masasi- CCM), alitaka kujua ni watu wangapi wamenufaika na TWB na ni kutoka mkoa gani.
Pia, alihoji ni vikao vingapi vya wanahisa vimefanyika tangu mwaka 2007 ilipoanzishwa benki hiyo.
Naibu Waziri alisema benki hiyo ilianzishwa mwaka 2009, na hadi kufikia  mwaka 2014, ilishatoa mikopo kwa wateja takribani 12,992, (wanawake 11,350 na wanaume 1,642), yenye thamani ya sh. 24,868,782,000.
Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Njombe, Iringa na Ruvuma.
Pindi alisema tangu kuanzishwa kwa benki hiyo mwaka 2009 na kusajiliwa rasmi Julai, 2013, benki hiyo imeshafanya vikao vitano vya wanahisa kuanzia 2011  hadi 2014.
Alisema kikao cha kwanza cha wanahisa kilifanyika Aprili Mosi, 2011 na kikao cha pili kilifanyika Aprili 14, 2012.
Alivitaja vikao vingine kuwa ni kikao cha tatu kilichofanyika Mei 2013, kikao cha nne kilichofanyika Desemba 13, 2013 na kikao cha tano kilichofanyika Desemba 13, 2014.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru