Thursday, 29 January 2015

Wanaowanyanyasa wafanyabiashara wadogo kukiona


NA THEODOS MGOMBA, DODOMA.
SERIKALI imesema itawashughulikia wale wote wanaowanyanyasa wafanyabiashara wadowadogo, akiwemo afisa tarafa wa Kariakoo kwa kisingizio cha kusafisha miji.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu.
Pinda alisema kumekuwa na unyanyasaji huo, ikiwemo unyang’anyaji wa mali katika maeneo mbalimbali kwa kisingizio hicho cha kuweka miji safi.


“Hata mimi nimerushiwa picha moja ikionyesha waswahili hawa wakigawana vitu, hii siyo sahihi.
“Picha hiyo nami nitawatumia watu wa TAMISEMI ili wawachukulie hatua hao waliopo kwenye picha na huyu afisa tarafa tutashughulika naye,” alisema Pinda.
Alisema ni vyema mamlaka za miji kukaa pamoja na wadau hao ili kuangalia njia sahihi ya kuweka miji safi badala ya kuwanyanyasa.
Pinda alisema kwa Ilala, jambo hilo lina sura tofauti na linahitaji utaratibu maalumu.
Alisema hata Ulaya wafanyabiashara hao wapo, lakini wamepewa maeneo maalumu kufanya biashara zao na kwa siku maalumu.
“Wabunge wa Dar-es-salaam tukae pamoja na mamlaka husika tuone tunafanyaje ili kuboresha  suala hilo,» alisema.
Awali katika swali lake, Zungu alisema hakuna mbunge asiyetaka mji kuwa msafi na mpangilio mzuri. Alisema kinachofanyika Kariakoo ni kuwanyang’anya mali zao wafanyabiashara wadogo wadogo na kina mama lishe.
«Mheshimiwa Waziri Mkuu, kinachofanyika Jijini Dar es Salaam ni dhuluma na unyanyasaji mkubwa na hasa huyu afisa tarafa mtoe kabisa,» alisema.
Mbunge huyo alisema katika nchi zingine, sekta isiyo rasmi imekuwa na mchango mkubwa katika pato la taifa.
Alitolea mfano nchi ya Kenya kuwa, sekta hiyo inachangia katika pato la taifa zaidi ya sh. Trilioni moja.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru