Thursday 29 January 2015

Maadhimisho miaka 38 ya CCM yapamba moto


NA  DUSTAN   NDUNGURU,   SONGEA
MAANDALIZI ya sherehe za maadhimisho ya miaka 38 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), yameanza kushika kasi mkoani Ruvuma, baada ya kuanza kuwasili kwa viongozi wa Chama kwa ajili ya sherehe hizo, zitakazofanyika Februari Mosi, mwaka huu, katika viwanja vya Majimaji.
Miongoni mwa viongozi walioanza kuwasili ni pamoja na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi Taifa,  Abdallah Bulembo na Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya, ambaye pia ni mbunge wa viti maalum mkoani humo.
Wageni hao wamewasili huku kukiwa na shamrashamra za kila aina, ambapo katika makao makuu ya ofisi za CCM mkoa, vipo vikundi mbalimbali vya ngoma, ambavyo hutumika kuburudisha viongozi wanaowasili ofisini hapo.
Akizungumzia sherehe hizo, Nape alisema CCM ndicho chama pekee chenye dhamira ya kweli ya kuwatumikia Watanzania, na kwamba ushahidi upo wazi kwenye utekelezaji wa Ilani yake ya uchaguzi baada ya kuitekeleza kwa vitendo.
Alisema kutokana na utekelezaji huo, Watanzania wameendelea kukipenda Chama, hali iliyokiwezesha kuibuka kidedea katika uchaguzi uliopita wa serikali za mitaa.
Nape alisema licha ya wapinzani kubeza  mafanikio yaliyofikiwa, bado Watanzania wamekuwa wakikipa ushirikiano Chama  kwa kukichagua, ambapo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu, CCM kitaibuka kidedea dhidi ya vyama vya upinzani.
Aidha, aliwataka Watanzania kuwa makini na viongozi wa vyama pinzani pindi wanapotoa kauli za kashfa kwa chama kilichopo madarakani, kwa sababu hawana dhamira ya kweli ya kuwatumikia.
Nape alisema wapinzani wanashindwa kuwasaidia wananchi kutokana na kutokuwa na  sera zinazolenga kuwakomboa, ikilinganishwa na CCM.
Kwa upande wake, Bulembo alisema  wazazi kote nchini wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha wanawaelekeza vijana wao juu ya umuhimu wa kudumisha amani na utulivu uliodumu tangu nchi ilipopata uhuru.
Alisema jumuia hiyo ni moja kati ya kiungo muhimu katika kufanikisha ushindi wa CCM, hivyo kwa kuwa wazazi ndio wenye jukumu la kuwaelimisha vijana wao, wanapaswa kufanya hivyo ili wasirubuniwe na viongozi wa upinzani.
«Wazazi wenzangu kamwe tusikubali vijana wetu kurubuniwa na viongozi kutoka kambi ya upinzani. Tuwaelekeze juu ya umuhimu wa kuunga mkono jitihada za CCM, ambazo zimewaletea maendeleo, lakini pia wahamasisheni wajiunge na Chama chenye nia ya kweli ya kuwainua vijana,» alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru