Thursday 29 January 2015

Mnyukano bungeni



  • Serikali yaipa rungu polisi kudhibiti uhalifu
  • usinde apongeza vinara wa vurugu kupigwa
  • Sadifa achafua hali ya hewa, Shekifu ang’aka

NA THEODOS MGOMBA, DODOMA
MVUTANO kuhusiana na sakata la Mwenyekiti wa Chama cha CUF, Profesa  Ibrahim Lipumba, kukamatwa na kufunguliwa mashitaka, umeendelea kutikisa bungeni.
Jana, wabunge walipata fursa ya kujadili suala hilo, ambapo wengi waliwashutumu wenzao wa upinzani kutokana na kuchochea vurugu na kulipaka matope jeshi la polisi pindi linapochukua hatua.
Wamesema iwapo wanasiasa wataheshimu amri halali za mamlaka, likiwemo jeshi la polisi, matukio ya kutiwa mbaroni na wakati mwingine kupigwa yatakuwa ni ndoto kutokea.
Hata hivyo, serikali imesema Jeshi la Polisi litaendelea kuchukua hatua kali kwa wote wanaokiuka sheria bila kujali cheo, dini wala elimu yake.
Akitoa kauli ya serikali bungeni jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, alisema ni muhimu kwa Watanzania kufuata sheria na kujaribu kuvuraga amani ni kosa, hivyo hakuna atayefumbiwa macho.
Alisema matukio ya watu kuvunja sheria kwa makusudi yamezidi kuongezeka huku wengi wakiwemo wanasiasa wakifanya hivyo kwa lengo la kutafuta umaarufu wa kisiasa.
Kutokana na hilo, Chikawe alisema serikali itaendelea kuchukua hatua kali ili kuhakikisha raia na mali za wananchi zinaendelea kulindwa.
Akizungumzia tukio la kukamatwa kwa Profesa Lipumba, Chikawe alisema Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ilipokea barua kutoka CUF ikiomba kufanya maandamano na mkutano wa hadhara.
Alisema barua hiyo yenye kumbukumbu namba CUF/OK/DSM/PF/0027/2A/F2015/1, iliyoandikwa Januari 21, mwaka huu, ilioomba kufanya maandamano kuanzia Temeke kupitia Sudan, Kichangani na kuishia Mbagala Zakhem, ambako mkutano ungefanyika.
“Profesa Lipumba pamoja na viongozi wenzake akiwemo Naibu Mkurugenzi wa Habari, Abdul Kambaya, walikutana na Kamishna wa Polisi, Simon Sirro na kujadiliana kuhusu suala hilo,” alisema.
Alisema Jeshi la Polisi lilibaini mambo matatu, ambayo ni maandamano hayo yaliyokuwa yafanyike siku hiyo, si halali na yangesababisha chuki miongoni mwa wananchi, kuwepo kwa dalili za vurugu na tishio la ugaidi kwenye baadhi ya maeneo.
Hata hivyo, alisema siku ya tukio, polisi walipata taarifa za kuwepo kwa mkusanyiko wa wafuasi wa CUF maeneo ya Temeke waliokuwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali yakisomeka  ‘Polisi acheni kutumika na CCM’.
Chikawe alisema baada ya polisi kufika eneo la tukio huku Profesa Lipumba akiwepo hapo, walitakiwa kuacha kufanya maandamano, lakini walikaidi amri hiyo.
Alizitaja baadhi ya namba za magari hayo kuwa ni T823 CJM na T237 ARR, ambayo yalionekana yakifanya msafara kuelekea eneo ambalo chama hicho kilipanga kufanya mkutano wa hadhara.
Alisema kuwa baada ya Kaimu Kamanda wa Temeke kupata taarifa hizo, alitoa agizo la kuwataka waache, lakini waliendelea.
Baada ya kutotii amri hiyo, amri ya kumkamata Profesa Lipumba na wafuasi wake ilitolewa na hatimaye kufikishwa mahakamani.
Serikali ilitoa taarifa hiyo baada ya James Mbatia (mbunge wa kuteuliwa), kutoa hoja bungeni ya kutaka tukio hilo lijadiliwe.

Kibajaji afyatuka
Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, alisema kazi ya polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao na kuwapongeza kwa kazi hiyo.
Alisema katika kudhibiti maandamano hayo askari wamefanya kazi yao kwa weledi mkubwa, ikiwa ni pamoja na kumwadabisha na kumtia mbaroni mhamasishaji.
Alisema miaka ya nyuma polisi walikuwa wakiwashikisha adabu na kuwatia mbaroni wafuasi, lakini sasa hivi wamemlenga mhusika mkuu na huo ndio utaratibu.
Aidha, aliwataka wabunge wenzake kuhakikisha wanaishi kwa kuheshimiana kwa kuwa kila mmoja anaweza kufanya vurugu ama kuzomea bungeni pindi wengine wanapozungumza.
Hata hivyo, alisema sababu kubwa ya kushamiri kwa zomea zomea na vurugu zisizo na msingi bungeni chanzo ni kiti cha Spika kwani, hakitoi adhabu kali kwa wanaokiuka kanuni.
“Mheshimiwa Spika kiti chako kinayumba kwa sababu akizungumza mbunge wa CCM, upinzani wanazomea na wewe umekaa kimya tu, kwani sisi hatuna midomo ya kuzomea?
“Mbunge mwenzako akiwa anazungumza wewe unakaa kimya sio kuzomea, mbona humu kuna watu nawajua hawajawahi kuzomea Mbowe , Zitto Cheyo, sasa nyinyi wengine ndo mnajua sana kuzomea au nini? Kwani nyinyi maneno yenu yanatufurahisha?” Aling’aka Lusinde 
kuhusu sakata la kupigwa kwa Profesa Lipumba, Lusinde alisema kuanzia sasa ni vyema polisi wakawapiga wahusika wenyewe na si wafuasia wao.
Alisema kila nchi ina utaratibu, hivyo anayepinga utaratibu huo kwa makusudi anapaswa kuchukuliwa hatua.
“Hata huko kwenye vyama vyao kuna katiba na taratibu zao, ukienda kinyume unafukuzwa kama kina Zitto na Kafulila, huo ni utaratibu na ukipenda kachumbali ujue ina pilipili nayo uipende,” alisema.
Alisema wapo wanachama waliotaka kugombea uenyekiti katika vyama hivyo, lakini matokeo yake walifukuzwa uanachama kama adhabu, hivyo hakuna sababu kwa wanaokiuka sheria kulaumu polisi.

Nkumba: Maslahi ya taifa kwanza
Akichangia taarifa na hoja hiyo, Said Nkumba (Sikonge-CCM), alisema ni vyema wabunge wakawa wamoja katika masuala yenye maslahi kwa taifa.
Alisema ni kweli kuwa CCM ndicho chenye kushika dola, lakini si mambo yote yanayofanyika hapa nchini ni ya CCM.
“Mbunge akiinuka cha kwanza ni kuilaumu CCM, huko ni kukosa ajenda, ni vyema wote tukawa kitu kimoja na kuangalia namna bora ya kutatua tatizo hili,” alisema.
Alisema haiwezekani kila mwanasiasa afanye analotaka, hiyo ni sawa na kambare ndani ya mto kila mmoja anasharubu.
Alisema nchi yeyote inaendeshwa kwa sheria hivyo ni lazima kuwepo kwa utii wa sheria.

Sadifa achafua hali ya hewa
Naye Sadifa Sadifa akichangia hoja hiyo, nusura achafue hali ya hewa na wapinzani wasuse tena kikao baada ya kusema kuwa CUF haina tofauti na Saccos.
Kauli hiyo iliamsha hasira miongoni mwa wabunge wa CUF na kumtaka kuifuta huku wengine wakiwa wamehamaki na kusimama.
Hata hivyo, mbunge huyo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, alisema hafuti kauli hiyo hadi hapo wabunge wa upinzani watakapofuta kauli kuwa CCM ni mafashisti.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, alilazimika kuingilia kati na kumtaka Sadifa kufuta kauli hiyo, ambapo naye aliridhia na kuifuta.
Hata hivyo, alisema hakuna haki isiyokuwa na mipaka, hivyo wanasiasa wasitumie vibaya haki hiyo.
Aliwataka wanasiasa kuacha kutumia hoja hiyo ya kupigwa kwa Mwenyekiti wa CUF kisiasa na kwamba, kiongozi huyo hakupigwa kisawasawa bali aligusgwa guswa tu.
Naye Yahya Kasim Issa (Chwaka-CCM), alisema inashangaza kuona vyama viwili tu nchini ndiyo vinalalamika kila mara juu ya utendaji kazi wa jeshi la polisi pamoja na mambo mengine .
Alisema Tanzania kuna vyama 24 vya siasa , lakini ni Chadema na CUF, ndivyo vinavyolalamika kila kukicha hivyo kuashiria kuna mambo maovu wanafanya.

Dola iheshimiwe-Shekifu
Henry Shekifu (Lushoto- CCM), akichangia hoja hiyo, aliwashukuru wabunge wa CCM kwa utulivu na ukomavu wa kutoonyesha hamaki.
Alisema  nchi  inataka amani, Watanzania wanahangaikia amani na CCM ndiyo imeifikisha nchi ilipo sasa.
“Mimi sitaki kutetea maovu, lakini nitatea yale yaliyo na haki na ambayo yanasimamia ukweli, hakuna nchi isiyo na polisi duniani, hakuna nchi isiyo na jeshi duniani,” alisema.
Alisema mara nyingi vurugu zinatokana na kuvunja kanuni na sheria za nchi,duniani kote matatizo yanatokea kwa sababu ya watu kukiuka sheria na kutotii utawala wa sheria.
Alisema  binafsi alishawahi kuwa mkuu wa mkoa na alisimamia amani.
“Mama Kamili ananifahamu vizuri sana, kwa nia njema tulifanya kazi vizuri na alikuwa mtiifu kwa sababu  ukimuambia usifanye anaacha.
“Hakuna uongozi wowote duniani ambao ukiambiwa usifanye jambo kwa mujibu wa sheria na wewe unaendelea kufanya,  hakuna serikali itakayokuvumilia,” alisema .
Alisema bunge linataka kutumika kama chombo cha kubadilisha serikali kila siku na kusisitiza kuwa hilo  haliwezekani.
Alisema  dhamana ya nchi imepewa CCM, hivyo haiwezekani kuona amani inavunjika au wananchi wanapata matatizo iangalie tu.
“Waziri nakuomba usiogope, tafuta ukweli kama ulivyosema  kuwa tume ya haki za binadamu inafanya kazi na wewe umeagiza kitengo cha malalamiko kipokee,  kifanyie kazi,” alisema.
“Ulivyoahidi kama yapo malalamiko, utaratibu utumike ukweli, ufahamike, wanaohusika wachukuliwe hatua, ndio hekima za utawala. Waziri katika hili, tunamwambia awajibike kwa lipi? Alikuwa Dar es Salaam wakati fujo  zinatokea, awajibike kwa lipi?” Alihoji.
Alisema kwa mtindo huo, bunge litawajibisha wangapi kwani, hakuna serikali ya namna hiyo duniani.
Alisema wabunge wamepewa kazi ya kuwaletea maendeeo wananchi, na sio kuwa chanzo cha vurugu na matukio ya kuvunja amani .
“Hatuwezi kukubaliana kupambana na vurugu bila kusimamia vyombo vinavyostahili,mimi napendekeza juhudi zinazofanywa kujua haki na tume ya haki ya binadamu iliyoamua kuchunguza iendelee na kazi na sisi tupewe taarifa na wananchi wajue,” alisema
Mbunge huyo alisema endapo wabunge wa CCM wasingependa kusimamia haki, wabunge wa upinzani wasingeshinda jambo kwa kuwa ni wachache ndani ya bunge
Alisema CCM ndiyo iliyoshika dola na kama ingetaka kufanya mabaya, ingeweza, lakini ni lazima kuwepo na utawala wa sheria.
Akihitimisha hoja yake, Mbatia alisema kunahitajika mabadiliko ya haraka katika jeshi hilo.
Alisema kitendo kilichofanywa cha kupiga hadi watoto, kinaonyesha kuwa hakuna weledi ndani ya jeshi hilo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru