Tuesday 10 December 2013

Ajeruhiwa kwa bomu akilima shambani


NA MARCO KANANI,GEITA
YUSUFU Nteminyanda (71), mkazi wa Nyankumbu Kata ya Kalangalala, amelazwa katika Hospitali ya Wilaya Geita, baada ya kujeruhiwa na bomu wakati akilima.
Bomu hilo ni miongoni mwa matatu aliyoyakuta shambani kwake.
Akielezea tukio hilo, Nteminyanda, alisema lilitokea jana saa 1:45 asubuhi.
Kwa mujibu wa Nteminyanda, wakati akilima jembe liligusa vitu vitatu kama mawe na kulazimika kuvitoa ardhini na kuanza kuvichunguza.
Hatahivyo alisema alishangaa kuviona vitu hivyo huku kimoja kikiwa na mfuniko, ndipo alipomwita mtu aliyekuwa karibu wakaanza kuvichunguza kwa pamoja.
Nteminyanda, alisema aliamua kuchukua kile kilichokuwa na mfuniko na kujaribu kuufungua, ndipo kililipuka na kutoa sauti kubwa huku kikiwa kimemjeruhi kwenye paja la mguu wa kulia, kifuani na kwenye  bega la mkono wa kulia.
Mzee huyo huyo aliyelazwa wodi namba nane akiendelea na matibabu, alisema anasikia maumivu makali kwenye jeraha la pajani na kifuani.
Hata hivyo, mzee huyo amelalamikia huduma duni za hospitali hiyo na kudaiwa fedha za matibabu wakati umri wake anapaswa kutibiwa bure.
Naye mtoto wa Nteminyanda, Shaibu Yusufu, alisema jana waliombwa fedha za malipo ya damu sh.6,000, licha ya wao kumtolea damu baba yao.
Uhuru lilipohoji suala hilo kwa uongozi wa hospitali hiyo, haukutaka kulizungumzia.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Leonald Paul, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo wameomba wataalamu kwa ajili ya kuyafanyia uchunguzi, huku akiwaomba wakazi wa eneo hilo kuwa makini na kuijulisha Polisi wanapookota vitu wanavyovitilia shaka.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru