Tuesday 24 December 2013

Pinda akabidhiwa msaada pikipiki 44


Na mwandishi wetu
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amepokea pikipiki 44 za msaada kutoka Ubalozi wa China na Kampuni ya Fu-Tang ya nchini humo.
Alikabidhiwa msaada huo jana, mbele ya viongozi wa Wilaya ya Mlele, katika hafla iliyofanyika kijiji kwao Kibaoni, wilayani Mlele, mkoani Katavi.
Balozi wa China nchini, Dk. Lu Youqing, akizungumza na viongozi wa wilaya hiyo na wakazi wa kijiji cha Kibaoni, kabla ya kukabidhi msaada huo, alisema anaamini pikipiki hizo zitasaidia kuleta maendeleo.
“Tunatarajia matumizi ya pikipiki hizi yatasaidia kuleta maendeleo ya haraka na hatimaye kuongeza kipato cha wakazi wa wilaya hii,” alisema. Ofisi ya balozi huyo imekabidhi msaada wa pikipiki 20.
Alisema China ina wakazi takriban bilioni 1.3 na anatamani kuona walau kila raia wa nchi hiyo ananunua kilo moja ya chakula kutoka Tanzania.
Naye Meneja Mkuu wa kiwanda cha kutengeneza pikipiki cha FEKON, ambacho ni kampuni tanzu ya Fu-Tang, Zheng Bing, alisema utaratibu utakapokamilika, watajenga kiwanda cha kutengeneza pikipiki na kompyuta nchini ili kuongeza ajira kwa Watanzania. Kampuni hiyo ilikabidhi pikipiki 24.
Waziri Mkuu Pinda kwa upande wake, alimshukuru Balozi Lu na kampuni ya Fu-Tang kwa msaada huo, na kuahidi kuzigawa ili ziwasaidie watendaji kusimamia kazi, hivyo kuharakisha maendeleo kwa wakazi wa wilaya hiyo.
“Tuna kata 24, kwa hiyo kila kata itapewa moja. Hiyo pikipiki si ya katibu kata binafsi, bali ya kata, kwa hiyo katibu kata atakuwa ndiye msimamizi,” alisema.
Waziri mkuu ambaye yuko Kibaoni kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka, alisema pikipiki saba zitapelekwa kwenye vituo vitano vya afya vya Mamba, Usevya, Inyonga, Katumba na Kanoge, na zahanati za Nsimbo na Kasansa.
Alisema pikipiki zingine nane zitapelekwa katika shule za sekondari za Sitalike, Machimboni, Magamba, Nsimbo, Mtapenda, Utende, Inyonga na Kasokola.
Pinda alisema wengine watakaofaidika na mgawo huo ni watendaji wa CCM wa wilaya ya Mlele, ambao watapatiwa moja, jumuia za Chama katika wilaya hiyo zitapatiwa tatu na moja itagawiwa kwa CCM mkoa wa Katavi.
Kuhusu uzalishaji wa chakula cha kutosha wakazi bilioni 1.3 wa China, alisema itabidi Tanzania izalishe magunia milioni 13 ya nafaka ili kufikisha lengo hilo.
Waziri Mkuu Pinda alikwishapokea msaada wa pikipiki 23 kutoka kwa wafadhili wengine na kuzigawa sita kwa Jeshi la Polisi, 13 kwa vikundi vya vijana na nne kwa shule za sekondari.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru