Wednesday 11 December 2013

Sheria mpya ya mihadarati yaja


Na  Theodos Mgomba, Dodoma
SERIKALI ipo mbioni kutunga sheria mpya ya kudhibiti biashara ya dawa za kulevya,  itakayowataka wauzaji wadogo wawataje waagizaji wakubwa wa dawa hizo.
Pamoja na sheria hiyo, pia wanatarajia kuweka kitengo maalumu kitakachoshughulikia kesi za dawa za kulevya ili kuharakisha hukumu za kesi hiyo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa ya hali ya dawa za kulevya kwa mwaka 2012.
Waziri Lukuvi, alisema bado biashara hiyo ipo nchini licha ya juhudi mbalimbali kufanyika katika kuidhibiti.
Alisema kutokana na kuongezeka kwa biashara hiyo, serikali inaangalia uwezekano wa kutunga sheria kali zaidi ikiwemo ya kumuomba Jaji Mkuu kuunda kitengo maalumu cha kushughulikia kesi hizo.
Alisema katika nchi mbalimbali kumekuwa na sehemu maalumu ya kushughulikia wanaokamatwa na dawa hizo.
Alitolea mfano nchi ya Bangladeshi ambayo wana mahakama na mahakimu katika viwanja vyake vya ndege wanaoshughulikia kesi za dawa hizo.
“Hapa nchini tumegundua bado kuna mianya ya kuwafanya watu wanaokamatwa kutoroka, hivyo tunataka kuweka sheria kali zaidi, manake hata kama ukimkamata mtu lazima mkemia mkuu athibitishe,’’ alisema Lukuvi.
Alisema mpaka sasa imeonyesha kuwa biashara hiyo haifanyiki kwa kiasi kikubwa nchini, bali Tanzania imekuwa njia ya kupitisha dawa hizo kwenda nchi zingine.
Akizungumzia ukamataji wa dawa za kulevya, Lukuvi alisema kiasi cha hekari 214 za mashamba ya bangi ziliteketezwa katika kipindi cha mwaka 2012 ukilinganisha na hekari 23, mwaka 2011.
Alisema katika kipindi cha mwaka jana, jumla ya kilo 211 za dawa aina ya Heroin zilikamatwa mkoani Lindi ikiwa ni kiasi kikubwa kuliko chote kilichowahi kukamtwa kwa mkupuo.
Waziri huyo, alisema serikali pia iliendelea na jitihada za kuziharibu dawa za kulevya zilizokamatwa nchini, kilo 96.8 za heroin na Cocaine ziliteketezwa baada ya kesi husika kutolewa hukumu.
Kesi hizo zilitolewa hukumu katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Mtwara na Lindi na uteketezaji huo ulifanywa kwa ushirikiano wa vyombo vya dola.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru