Tuesday 10 December 2013

Wenyeviti CCM ‘wampa tano’ Kinana


NA FURAHA OMARY
WENYEVITI wa CCM wa mikoa yote nchini, wamemuunga mkono Katibu Mkuu wa Chama, Abdulrahman Kinana na sekretarieti, kwa kuitaka serikali kuwachukulia hatua viongozi na watendaji walioonyesha udhaifu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mwenyekiti wa wenyeviti hao, Mgana Msindai, alisema hayo jana alipotoa tamko lao kwa waandishi wa habari, katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam.
“Tunaitaka serikali ichukue hatua za haraka kurekebisha udhaifu huo. Viongozi na watendaji wote wa serikali walioonyesha udhaifu mkubwa katika kutekeleza majukumu yao, na ambao walipewa wito na wengine wanatakiwa kupewa wito wa kuhudhuria mbele ya Kamati Kuu ya CCM wachukuliwe hatua zinazostahili,” alisema.
Kwa mujibu wa Msindai, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida, wana-CCM wako mstari wa mbele kuisimamia serikali kwa mujibu wa Ilani ya uchaguzi ya Chama ya mwaka 2010 -2015.
“Kwa niaba ya wana-CCM tunamuunga mkono Katibu Mkuu Kinana na sekretarieti ya CCM kwa kuwa tangu alipopewa wadhifa wa ukatibu mkuu ameonyesha uwajibikaji mkubwa uliokiwezesha Chama kupata uhai mpya na kuamsha ari na matumaini zaidi ya Watanzania kwa Chama,” alisema.
Alisema Kinana amekuwa akikemea kwa nguvu zote udhaifu, hivyo wanamuunga mkono na kuitaka serikali kuchukua hatua.
Msindai alisema udhaifu huo ni ubadhirifu unaofanywa katika serikali za mitaa, hivyo kuzifanya halmashauri kujirudia kupata hati chafu, utendaji duni wa baadhi ya miradi ya maendeleo, jambo linalosababisha kuwepo kwa huduma duni na zisizokidhi thamani ya fedha.
Mwingine ni ucheleweshwaji wa maslahi na stahili za watumishi wa umma, jambo linalosababisha washindwe kufanya majukumu yao na kufanya migomo ya mara kwa mara.
Pia gharama kubwa ya uendeshaji wa shughuli za serikali na taasisi zake, ikilinganishwa na gharama zinazotumika kwenye miradi ya maendeleo.
Matatizo mengine ni usimamizi mbovu wa operesheni za serikali zenye nia njema, zikiwemo za kuhamisha wafugaji na kutokomeza ujangili, kushindwa na kuchelewa kutatua baadhi ya kero sugu kwa wananchi, yakiwemo malalamiko ya wakulima na rushwa zilizokithiri katika sehemu za utoaji huduma.
“Tunaitaka serikali ichukue hatua za haraka kurekebisha udhaifu huo,” alisema.
Wenyeviti hao pia waliwakumbusha viongozi kuwa wanapaswa kuiga mfano wa Kinana, kwa kuhakikisha wanaanza kufanya kazi kuanzia ngazi ya chini ya Chama.
Hivi karibuni Kinana na ujumbe wake walifanya ziara katika mikoa ya Ruvuma na Mbeya, ambako licha ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama, pia walitaja baadhi ya mawaziri wanaoonekana kushindwa kuwajibika ipasavyo.
Katika ziara hiyo Kinana na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, walisema mawaziri hao wataitwa mbele ya Kamati Kuu ya Chama ili wajieleze kutokana na utendaji usioridhisha wa wizara zao.
Ziara hizo ambazo pia zilihusisha mikoa ya Njombe na Mtwara, zililenga kufuatilia kero za wananchi ambazo kwa muda mrefu hazijaweza kupatiwa majawabu, ikiwemo soko la korosho, ambalo kwa muda mrefu wakulima wamekuwa wakilanguliwa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru