Monday 16 December 2013

Lema aweweseka na maandamano


na mwandishi wetu
MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ambaye jimbo lake limekuwa kinara wa maandamano, jana alipinga hatua ya Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama kuitaka serikali kuweka Sheria Maalum kudhibiti watu wanaofanya maandamano bila mpangilio.
Lema, ambaye muda wote alikuwa akijaribu kujenga hoja za kukataa ushauri huo wa Kamati ya Bunge, alisema maandamano si tukio la ghafla na kwamba, haliwezi kupangiwa siku wala muda wa kufanyika.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, maandamano ni kitendo cha ghafla, hivyo kukipangia siku na sehemu ya kupitia hayatakuwa maandamano bali ni mazoezi ya kupiga vita kisukari,’’ alisema Lema.
Awali, Mjumbe wa Kamati hiyo, Vita Kawawa, akiwasilisha taarifa hiyo bungeni, alisema umefika wakati kwa serikali kuwasilisha Muswada utakaoweka utaratibu wa watu ama vikundi kuandamana tofauti na ilivyo sasa, ambapo kila kukicha watu hupanga maandamano bila kujali athari za usalama na kiuchumi.
Kawawa, ambaye alisoma taarifa hiyo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo Edward Lowassa, alisema kwa sasa kuna vyama vya siasa vimekuwa vikiandama bila kuzingatia muda wala siku, hivyo kuleta usumbufu kwa watu wengine.
Naye Leticia Nyerere (Viti Maalum-CHADEMA), alisema ni vyema serikali ikaweka utaratibu maalumu wa kutumia majina ya waasisi wa taifa na si kila mtu kulitumia hata katika dhihaka.
Alisema hivi sasa baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakitumia majina hayo kwa manufaa yao na wengine hata kuyatumia vibaya ikiwemo kuyafanyia dhihaka.
“Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakitumia vibaya majina ya viongozi wetu na hata kuyafanyia dhihaka, lazima tuhakikishe suala hilo linakoma.
“Mimi ni mkwe wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, lakini inasikitisha unapoona baadhi ya watu wanatumia jina la kiongozi huyo kwa dhihaka, ni muhimu sasa kukawekwa sheria ya kuyalinda majina hayo,’’ alisema Leticia.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru