Tuesday 3 December 2013

Sheria mpya kuirasimisha Dodoma kuwa makao makuu


Abdalah Mweri na Theodos Mgomba, Dodoma
SERIKALI imeandaa rasimu ya Waraka wa Baraza la Mawaziri kwa ajili ya uamuzi ya kutunga sheria mpya ya kuitambua Dodoma kuwa Makao Makuu ya Serikali.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi, alipokuwa akijibu swali la mbunge wa  Dodoma Mjini, Dk. David Malole (CCM), aliyetaka kujua lini serikali itahamia Dodoma.
Kwa mujibu wa Lukuvi, mara baada ya kukamilika kwa vikao husika vya Baraza la Mawaziri, serikali itatunga sheria hiyo itakayotamka rasmi kuwa Dodoma ni Makao Makuu ya Serikali.
Lukuvi alisema Ofisi ya Waziri Mkuu tayari imeshaitisha vikao viwili kwa ajili ya kupata maoni ya kuwezesha kutunga sheria hiyo mpya.
Alisema, pamoja na kupata maoni ya wadau, pia serikali inatarajia kupata maoni ya kamati husika ya Bunge.
Pia alisema katika kutimiza uhamiaji wa serikali mjini Dodoma,
Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) tayari imeshatengeneza ramani mpya ya mji wa Dodoma kuhakikisha mji huo unajengwa kwa  mipangilio.
Alisema ramani hiyo imetengenezwa kwa kushirikiana na Korea Kusini ambayo itahakikisha kuwa mji huo unafuata utaratibu  wa mipango miji katika ujenzi wake.
Akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti maalum, Diana Chilolo (CCM), Waziri Lukuvi alisema  CDA imeamua kuanza kutoa viwanja kwa mikopo kwa wahitaji.
CDA awali, alisema, ilikuwa na mpango wa kuwakopesha wananchi wa hali ya chini viwanja na kutakiwa kukamilisha malipo katika miezi  mitatu, lakini hivi sasa muda huo umeongezwa hadi mwaka mmoja.
Alisema hali hiyo imetokana na kuongezeka kwa bei ya viwanja kutokana na gharama za upimaji wa viwanja, kwani mara nyingine CDA hulazimika kutumia wapimaji binafsi wa kukodi.
"Kutokana na kukodi wapimaji na kulipa fidia ya viwanja tunavyovitwaa kutoka kwa wananchi  gharama zinaongezeka, hivyo  vinavyopimwa hulazimika kuuzwa kwa bei ya juu na wengine hushindwa  kumudu gharama hizo,íí alisema Lukuvi.
Katika swali lake, Diana alitaka kujua kwa nini viwanja
vinavyopimwa na CDA huuzwa kwa bei ya juu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru