Tuesday 3 December 2013

Sh. bilioni 100 kuanzisha benki ya kilimo


NA MOHAMMED ISSA
SERIKALI  inatarajia kutoa mtaji wa sh. bilioni 100 kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), na kwamba itaendelea kutenga kiasi hicho kila mwaka ili kukuza mtaji wa benki hiyo.
Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, alisema hayo jana mjini Dar es Salaam, katika uzinduzi wa benki hiyo.
Alisema kwa sasa serikali ndiyo yenye hisa katika benki hiyo, hivyo inawajibika kutoa mtaji wa kuanzishwa kwake.
Saada alisema lengo la serikali ni kuhakikisha benki hiyo inapata mtaji na kwamba utatokana na fedha zitakazotengwa kwenye bajeti na misaada.
Alisema hali hiyo itasaidia benki hiyo kutoa mikopo ya kilimo kwa masharti nafuu kama azma ya kilimo kwanza inavyosema.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, kuanzisha benki hiyo serikali inatarajia kupata majibu ya haraka yakiwemo ya upatikanaji wa mikopo nafuu ya muda wa kati na mrefu kwa sekta ya kilimo.
Alisema serikali iliamua kuanzisha benki hiyo kwa lengo la kutoa mikopo kupitia SACCOS, MFI, na benki zingine, ambazo zitakopesha wakulima  katika sehemu mbalimbali nchini.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru