Tuesday 10 December 2013

Dunia yazizima


JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI
WAKUU wa nchi na viongozi mashuhuri duniani, wamefurika mjini hapa katika uwanja wa michezo wa FNB, kwa ajili ya mazishi na kumbukumbu ya kitaifa ya Rais wa kwanza mzalendo, Mzee Nelson Mandela (95), aliyefariki dunia wiki iliyopita.
Miongoni mwa viongozi hao ni  Rais Jakaya Kikwete, Barack Obama wa Marekani, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, Rais wa Ufaransa Francois Hollande na Rais wa Iran, Hassan Rouhan.
Kumbukumbu hiyo iliyofanyika jana ilihudhuriwa na watu zaidi ya 100,000, huku mvua kubwa ikinyesha, jambo lililotafsiriwa na viongozi hao kuwa baraka na makaribisho mema kwa maisha mapya ya Mzee Mandela.
“Siku ya mazishi yako inaponyesha mvua ni dalili kwamba Mungu anakupokea kwa heri na makazi yako ni mema,” alisema Makamu wa Rais wa Chama tawala cha Afrika Kusini ANC, Cyril Ramaphosa.
Viongozi hao wakuu na wawakilishi wa zaidi ya nchi 90 duniani walianza kuingia kwenye uwanja huo ili kushuhudia tukio hilo la kihistoria, ikiwa ni mfululizo wa shughuli kadhaa kabla ya maziko ya mzee Mandela, aliyekuwa mtetezi wa haki za binadamu.
Uwanja wa FNB ulioko katika kitongoji cha Soweto, ulijaa maelfu ya watu waliopanga foleni kuanzia alfajiri kwa ajili ya kuwahi nafasi ya kushuhudia tukio hilo.
Kumbukumbu hiyo ya kihistoria ilishuhudiwa na viongozi mbalimbali, baadhi wakipata fursa ya kutoa rambirambi, ambao walimuelezea mzee Mandela kuwa alikuwa mtu wa kipekee, asiye na mfano katika kutetea haki za binadamu katika karne ya 20.
Akitoa salamu, Obama aliyeambata na mkewe Michelle, aliwashukuru wananchi wa Afrika Kusini kwa kutokuwa wachoyo na kuwashirikisha wengine kunufaika na mchango wa Mandela.
Obama aliyeingia uwanjani saa moja baada ya shughuli kuanza, alipokewa kwa shangwe na vifijo na waombolezaji waliokuwa wakifuatilia tukio hilo.
OBAMA AVUNJA MWIKO
Katika kumbukumbu hiyo, Obama alivunja mwiko uliodumu kwa zaidi ya miaka 60, baada ya kupeana mkono na Rais wa Cuba, Raul Castro.
Wakati akielekea katika sehemu iliyoandaliwa kwa ajili ya kutoa rambirambi, Rais Obama aliwapa mikono viongozi mbalimbali waliokuwa karibu na eneo hilo, akiwemo Castro.
BAN KI-MOON ALONGA
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, alisema Mandela alikuwa kiongozi wa kupigiwa mfano duniani, anayepaswa kuigwa na watu wote.
Alisema Mandela alitumia muda mwingi wa uhai wake kupigania haki za binadamu bila kutanguliza maslahi binafsi.
Ban alisema kiongozi huyo anapaswa kukumbukwa milele na kuenzi mazuri aliyotenda ili iwe sehemu ya kuendeleza amani, utulivu na maendeleo ya binadamu.
NEEMA YA MVUA
Umati wa wananchi walioshindwa kuingia katika uwanja huo walinyeshewa mvua kutwa, wakiwa nje ili kuwa jirani na eneo ilikokuwa ikifanyika shughuli hiyo.
Misururu ya wananchi ilianza asubuhi kuingia kwenye uwanja huo na ilipofika mchana  hapakuwa na nafasi.
Huku wakinyeshewa mvua, wananchi hao walikuwa wakiimba nyimbo za kumsifu mzee Mandela kwa kazi kubwa aliyoifanyia nchi hiyo.
KUZIKWA JUMAPILI
Kwa mujibu wa ratiba, Mandela anatarajiwa kuzikwa kijijini kwao Qunu, Jumapili, ikiwa ni baada ya kukamilika kwa utaratibu wa kitaifa na kimila.
Ratiba hiyo inaonyesha mwili wa Mandela utapitishwa katika mitaa mbalimbali ya Afrika Kusini ili kuwapa nafasi wananchi kutoa heshima za mwisho kwa kiongozi huyo.
Mwili wa Mandela utalazwa Ikulu kwa siku tatu kuanzia jana kabla ya kuzikwa Qunu.
Viongozi wengine waliohudhuria kumbukumbu hiyo ni Rais wa Uganda, Yoweri Museveni,  Uhuru Kenyatta (Kenya) Nicolaus Madulo (Venezuela).
Goodluck Jonathan (Nigeria), Hifekepunye Pohamba (Namibia), Joyce Banda (Malawi).
Pia marais wastaafu wa Marekani, Bill Clinton na George W. Bush, walikuwa sehemu ya viongozi walPage one

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru