Tuesday 17 December 2013

Kimewaka bungeni


Na Hamis Shimye
SAKATA la baadhi ya wabunge kuchukua posho ya safari na kushindwa kusafiri limechukua sura mpya, baada ya suala hilo kufikishwa ofisi ya Spika wa Bunge.
Miongoni mwa wabunge wanaohusishwa na kashfa hiyo ya ufisadi wa fedha za umma, ni kiongozi wa chama cha upinzani, anayedaiwa kufanya hivyo akishirikiana na hawara yake, ambaye naye ni mbunge.
Mbunge huyo (jina linahifadhiwa), anayedaiwa kuwa na fedha nyingi nje ya nchi, inadaiwa alisafiri kwenda Dubai alikokutana na hawara yake na kutumia siku tatu kuponda starehe kwa fedha za umma, huku akikacha kwenda safari ya kikazi aliyopangiwa.
Habari zinasema mbunge huyo amekuwa na tabia ya kukacha safari na kutafuna fedha za posho anazopewa.
Akichangia taarifa ya kamati ya Bunge katika mkutano wa 14 unaoendelea mjini Dodoma, Ally Keissy (Nkasi Kaskazini – CCM), alisema kuna baadhi ya wabunge, akiwemo kiongozi mkubwa wa chama cha siasa cha upinzani ambao wanachukua posho ya safari, lakini hawasafiri.
Keissy alisema wabunge hao wamekuwa wakifanya vitendo hivyo kwa muda mrefu, huku akivifananisha na wizi ambao kwa muda mrefu unawatesa Watanzania.
Akizungumzia suala hilo jana, Keissy alisema wote wanaofanya vitendo hivyo wanajulikana na ameamua kulikomesha jambo hilo alilodai limeota mizizi.
Kwa mujibu wa Keissy, tangu alipoingia bungeni amekuta tabia hiyo, ambayo anaamini ni ya muda mrefu na kwa sasa imeota mizizi kwa baadhi ya wabunge.
“Wananchi ni masikini, hawana hata fedha za kujikimu sasa kwa nini mbunge upewe fedha zinazotokana na kodi za wananchi ili ufanye kazi ya mwananchi, lakini  hufanyi na unatumia kwa mambo mengine,” alihoji.
Keissy alisema ameamua kulifikisha suala hilo katika ofisi ya spika, ambayo imemuahidi itachukua hatua ili kuhakikisha kunakuwepo nidhamu ya matumizi ya fedha.
“Nimekutana na spika na kumwambia suala hili, na ameniahidi atachukua hatua kwa kuwaandikia barua wabunge waliofanya mchezo huo ili warudishe fedha,’’ alisema.
Alisema wabunge wanaofanya hivyo, wanajulikana na anashangaa kwa nini hawaandikwi kwenye vyombo vya habari. Alisema wengi wa wabunge hao wanatoka kambi ya upinzani.
“Hata wewe mwandishi ukipewa fedha na gazeti lako kwenda kuandika habari Mwanza na huendi huko, wewe ni mwizi, tena jambazi mkubwa kwa kuwa hukuwatendea haki mabosi wako,’’ alisema.
Mbunge huyo alisema anatarajia ofisi ya spika italifuatilia suala hilo kwa umakini, baada ya kulifikisha na hata ahadi ya kuwaandikia barua wabunge warudishe fedha hizo itakamilika.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru