Tuesday 17 December 2013

Kinana bado gumzo CCM


BASHIR NKOROMO NA LATIFA GANZEL, MOROGORO
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro, kimepongeza ziara za Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman  Kinana, kutokana na kukiimarisha Chama na kukiongezea heshima.
Katibu wa Uenezi mkoani hapa, Dorothy Mwamsiku, alisema hayo jana, alipofungua semina ya viongozi wa Jumuia ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam. Semina hiyo inafanyika mjini hapa.
Aliwataka wanachama wa CCM kumuunga mkono Kinana na Sekretarieti ya Chama kwa kusimamia na kutekeleza maagizo aliyotoa katika ziara hizo.
Miongoni mwa maagizo hayo ni kusimamia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM, kusikiliza kero za wananchi na kujadiliana nao njia ya kuzitatua.
Alisema kuna kila sababu ya viongozi wa CCM kutokubali kuwafumbia macho watendaji wanaoshindwa kutekeleza Ilani kwa makusudi ili kukikwamisha Chama.
Dorothy alisema wapo watendaji ambao hawakitendei haki Chama kwa kufuja fedha za miradi.
‘’Unakuta baadhi ya watendaji hawatekelezi Ilani ya CCM ipasavyo, hivyo kusababisha Chama kusemwa vibaya. Tusikubali, tuwe wa kwanza kuwashughulikia kabla ya sisi  kunyoshewa vidole,’’ alisema.
Alisema kuna kila sababu kwa viongozi wa CCM na wanachama kwa jumla kutambua miradi yote ya maendeleo iliyoko katika maeneo yao.
Kwa mujibu wa Dorothy, licha ya kuwepo changamoto za baadhi ya watendaji wanaokwamisha utekelezaji Ilani, kwa kiasi kikubwa imetekelezwa.
“Licha ya utekelezaji huo, bado wapo watu wanaosema CCM haijafanya kitu, kazi ya wapinzani kukosoa na CCM kazi yetu kutenda, tusikate tamaa tusonge mbele,” alisema.
Aliitaka jumuia hiyo kuwa mstari wa mbele katika malezi ya watoto, kwa kuwa ndiyo moja ya malengo ya kuanzishwa kwake.
Katibu huyo wa uenezi alisema jumuia haipaswi kuwaacha vijana waharibike na kutumbukia katika vitendo viovu vinavyosababisha wapate maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Kwa upende wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Salum Madenge, ambaye ni mwenyekiti wa semina hiyo, alisema ina lengo la kuwajengea uelewa wa kutosha wa namna ya kutekeleza majukumu na wajibu wao kwa Chama.
Awali, Mwenyekiti wa Wazazi Wilaya ya Kinondoni, Charles Mgonja, alisema mada mbalimbali zitatolewa, ikiwemo umuhimu wa mchango wa jumuia katika kuimarisha Chama.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru