Na Hamis Shimye
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimekunjua makucha yake dhidi ya wanachama wanaotangaza nia ya kugombea uongozi kabla ya wakati na kwamba wataitwa kwenye kamati Kuu na kuhojiwa.
Mbali na kuwaita na kuwahoji, kimesema wale watakaobainika kuwa wamekiuka taratibu watachukuliwa hatua za kinidhamu bila kujali umaarufu au nafasi zao.
Alisema wanachama hao ambao mbali na kuonyesha kila dalili za kutangaza nia hasa nafasi ya urais, wamekuwa wakifanya mambo ambayo ni kinyume cha utaratibu na kwamba hali hiyo inaleta nyufa ambazo zinaweza kukisambaratisha Chama.
Alionya kuwa wanachama hao wanaopita sehemu mbalimbali kujaribu kushawishi watu ili kukubalika juu ya azma yao, wanaopasa kuacha mara moja vitendo hivyo.
“Wanachama hao wasipoacha tabia hiyo wasitarajie kuteuliwa kuwa wagombea wa CCM, labda wawakilishe vyama vyao vya kijiweni na si Chama Cha Mapinduzi,” alisema.Mangula alisema kila mwanasiasa anapasa kutii kanuni na maadili ya Chama, ambapo viongozi nao wanapasa kusimamia hilo.
“Ikiwa hauzingatii kanuni na taratibu za Chama basi wewe hufai kuwa kiongozi wa CCM labda ukateuliwa na chama chako cha kijiweni ndiyo ukiongoze na si chama hiki,” alisisitiza.Alisema viongozi wa CCM kuanzia ngazi ya Shina hadi Mkoa, wanapasa kutumia vikao vya Kamati za Siasa kuwaita, kuwahoji, kuwaonya na hata kuwachukulia hatua viongozi na wanachama wanaojipitisha na kutangaza nia za kugombea.
Mangula alisema huu si wakati wa uchaguzi bali ni kipindi cha utekelezaji wa ilani ya uchaguzi kwa viongozi walioko madarakani, ambao walichaguliwa 2010.
“Chama hakina ajenda ya uchaguzi mkuu. Anayejitokeza na kusema yeye anafaa, huyo ana ajenda binafsi na hajatumwa na Chama. Na wale wanaojifanya wasafi wajiulize mikono yao hainuki damu ya rushwa?,”alisema.Alisema kila kiongozi anapasa kuheshimu kanuni za uongozi na maadili kwa kuwa ndizo nguzo za uwajibikaji kwa viongozi wote wa CCM.
Mangula alisema kanuni hiyo, imeelekeza kila kuhusiana na mambo yasiyoruhusu na anapojitokeza mtu anapokwenda kinyume cha mambo hayo anaonyesha udhaifu mkubwa.
Kutokana na msimamo huo, aliziagiza Kamati za Siasa za Matawi hadi Mikoa kulitazama jambo hilo na kuwapa taarifa wote wanaojipitisha pamoja na kuwasilisha taarifa zao Makao Makuu ya Chama.
Katika hatua nyingine, Mangula aliipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kutoa rasimu ya pili ya Katiba Mpya na kusisitiza kuwa huu ni wakati wa Chama kujipanga kwa kuelimisha wanachama wake, hasa baada ya Tume kukusanya na kuchambua maoni.
“Nayaagiza matawi yetu kuanzia chini kutoa elimu ya kutosha kuhusiana na rasimu hiyo, ili kuwaelemisha wananchi wakubali au kukataa,”’alisema.
Pia, alisema ajenda muhimu kwa CCM kwa mwaka 2014 ni Katiba Mpya na uchaguzi wa serikali za mitaa, hivyo ni wakati wa kuwaelimisha wanachama na wananchi juu ya mambo hayo na si vinginevyo.
Vinara wa makundi kuitwa
Kuhusu uchaguzi mkuu wa Chama mwaka 2012, alisema kilipokea malalamiko 94 ambapo na kamati ya Maadili ya Chama.
Mangula alisema baadhi ya malalamiko yameshafanyiwa kazi kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa na jumuia za Chama, ambapo malalamiko mengine hayakufanyiwa kazi baaada ya kuchambuliwa na kuonekana hayana msingi.
“Malalamiko yaliyofuatiliwa na kufanyiwa kazi ni 33, ambapo idadi hiyo imepungua kutokana na baadhi ya nafasi moja kulalamikiwa na zaidi ya mtu mmoja. Kamati Kuu imeshafanya uamuzi juu ya malalamiko matatu,’’alisema.Mangula alisema malalamiko hayo ni kwa wilaya za Momba, Longido kurudia uchaguzi wa nafasi za Mwenyekiti wa Wilaya na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa(NEC) huku Wilaya ya Lindi nafasi ya mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Wilaya.
Alisema baada ya mchakato huo kumalizika Kamati Kuu imeongeza miezi sita kushughulikia malalamiko yaliyobakia huku Tume ya Udhibiti na Nidhamu ikibaini chanzo kikubwa cha matatizo ni makundi, ambapo imepanga kuwaita baadhi ya watu ambao wanaonekana wanaweza kukivuruga Chama.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru