Friday, 3 January 2014

Kipande apigiwa chapuo TPA

NA NJUMAI NGOTA

BODI ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imeshauri Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Mhandisi Madeni Kipande, aendelee na ikiwezekana aongezewe muda.
Kutokana na hali hiyo, bodi imeomba Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kusitisha mchakato wa kumpata mtendaji mkuu mpya ili apate fursa ya kuleta maendeleo makubwa ya uongozi chini yake na asimamie malengo ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kwa kasi.
Mwenyekiti wa bodi ya TPA, Profesa Joseph Msambichaka, alisema hayo jana wakati akitangaza uteuzi wa viongozi waandamizi wa mamlaka hiyo katika ofisi za TPA  makao makuu, Dar es Salaam.
Profesa Msambichaka alisema wamemshauri Dk. Mwakyembe asitishe mchakato huo kwa kuwashindanisha waombaji kutoka ndani na nje ya nchi, angalau kwa mwaka mmoja.
Alisema Kipande kwa ufanisi na nguvu ile aliyoanza nayo mwaka jana imeiletea tija TPA na kwamba ushauri huo Waziri alipokea na kuwaarifu kuwa ataufanyia kazi.
“Hii ni kwa kuzingatia ongezeko kubwa la ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam kwa kipindi cha mwaka mmoja ambapo TPA imeweza kudhibiti kwa kiasi kikubwa wizi na upotevu wa shehena zikiwemo kontena ndani ya bandari,”alisema.
Profesa Msambichaka alisema wameongeza ufanisi wa kuhudumia makontena na meli zinazotia nanga bandarini, kurejesha imani kwa  wateja wa nje kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia na Malawi.
Alisema TPA walipata hati safi kwa mwaka 2012/2013 na kuvuka malengo ya BRN kwa kuhudumia shehena zaidi ya tani milioni 13 mwaka jana ikilinganishwa na tani milioni 12.05 mwaka 2012 na tani takriban milioni 10.4 mwaka 2011.
Mwenyekiti huyo alisema bodi imefanya uteuzi katika nafasi zilizokuwa zimeachwa wazi baada ya hatua zilizochukuliwa na bodi za kuwaachisha kazi viongozi waliopatikana na makosa mbalimbali katika uendeshaji wa bandari.
Mbali na uteuzi, alisema wameanzisha utaratibu mpya katika ngazi ya wakurugenzi ambapo ajira zao zitakuwa za mikataba ya miaka mitano  na si wa kudumu kama ilivyokuwa awali na kwamba ikiwa utendaji wao utakuwa wa ufanisi wataongezewa muda.
Aliwataja walioteuliwa na nafasi zao kwenye mabano ni Mhandisi Alios Matei (Naibu Mkurugenzi Mkuu-Miundombinu), Awadh Massawe (Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam), Peter Gawile (Mkurugenzi wa Rasilimali Watu) na Mhandisi William Shilla (Mkurugenzi wa Uhandisi).
Wengine ni Mkurugenzi wa Tehama, Phares Magesa; Mkurugenzi wa Utekelezaji, Hebel Mhanga;  Mkuu wa Ulinzi, Lazaro Twange; Meneja wa Gati la Mafuta, Kapteni Andullah Mwingamno, Mameneja Ununuzi na Ugavi, Mashaka Kisanta na Michael Simba.
Profesa Msambichaka alisema wamemuongezea muda wa miezi sita Naibu Mkurugenzi Mkuu, Clemence Kiloyavaha ili kupata muda zaidi na kumtafuta mrithi wa nafasi hiyo mwenye sifa zinazostahili.
Nafasi zingine ambazo mchakato wa kuwatafuta wenye sifa ni za  Mkurugenzi wa Sheria na Meneja Mawasiliano.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru