Thursday 2 January 2014

Familia ya Dk. Mgimwa yacharuka

NA WAANDISHI WETU

MWILI wa aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, aliyefariki dunia juzi, mjini Pretoria, Afrika Kusini, unatarajiwa kuwasili nchini kesho.
Kwa mujibu wa taarifa, mwili wa Dk. Mgimwa utarejeshwa nchini saa saba mchana, kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam. Alifariki dunia katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic, alikokuwa akipatiwa matibabu.

Serikali kwa upande wake imeunda kamati ya kitaifa ya kuratibu mazishi ya Dk. Mgimwa, inayoongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
Wakati hayo yakiendelea, familia ya Dk. Mgimwa imesema haifahamu lolote kuhusu uvumi kuwa kifo chake kimetokana na kulishwa sumu.
Familia hiyo imesema itatoa tamko baada ya kupata taarifa ya serikali na madaktari waliokuwa wakimtibu.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Lukuvi alisema kamati hiyo na nyingine ndogo inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, zimeundwa ili kuratibu mazishi ya Dk. Mgimwa.
Lukuvi alisema mwili wa marehemu unatarajiwa kuwasili kesho, saa saba mchana na ndege ya Shirika la Afrika Kusini na utapelekwa nyumbani kwake Mikocheni B, kabla ya kupelekwa Hospitali Kuu ya Jeshi ya Lugalo.
Alisema Jumapili mwili wa Dk. Mgimwa utapelekwa kwenye viwanja vya Karimjee kwa ajili ya ibada na utoaji heshima za mwisho kabla ya kusafirishwa kwa ndege kwenda Iringa kwa maziko.
Lukuvi alisema utoaji heshima za mwisho, utatanguliwa na rambirambi na ndipo umma utafahamishwa ugonjwa uliosababisha kifo cha Dk. Mgimwa.
Kuhusu kamati inayoongozwa na Dk. Christine, alisema inaratibu mazishi mkoani Iringa ambako yatafanyika maziko.
Alisema Jumapili mwili wa Dk. Mgimwa utapokewa katika Uwanja wa Ndege wa Nduli saa 10 jioni na utapelekwa ukumbi wa Siasa na Kilimo, mjini Iringa, ambapo wananchi na viongozi watoa heshima za mwisho.
Lukuvi alisema baadaye utasafirishwa kwenda nyumbani kwao kijiji cha Magunga na maziko yatafanyika Jumatatu, saa sita mchana.
Katika hatua nyingine, familia ya Dk. Mgimwa imewaonya wanaosambaza uvumi kuwa ndugu yao amefariki dunia kutokana na kulishwa sumu.
Familia hiyo imesema itatoa taarifa kuhusu kifo chake baada ya kupokea taarifa ya serikali na madaktari.
Msemaji wa familia hiyo, Charles Nyato, alisema hawajui chochote kuhusu sumu, bali wanatambua alikuwa anaumwa na alikuwa akitibiwa Afrika Kusini.
Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Sheni, amemtumia rambirambi Rais Jakaya Kikwete, kuhusu kifo cha Dk. Mgimwa.
Dk. Sheni alisema atakumbukwa kutokana na utumishi uliotukuka kwa serikali na wananchi wa Tanzania.
“Tanzania imempoteza kiongozi shupavu, mpendakazi, mzalendo, mwenye busara na upendo kwa wenzake,” alisema.
Rais Sheni pia amewapa pole wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Dk. Mgimwa.
Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa (CCM), alisema Dk. Mgimwa alikuwa mtu wa pekee, asiyekuwa na majivuno licha ya kuwa  waziri na kwamba, alizoea kumtania kwa kumuita mbunge wa mtaa wao wa Ruvu, ulioko Mikocheni, Dar es Salaam.
Alisema Dk. Mgimwa, aliyekuwa akishiriki kazi nyingi mtaani kwao kabla hajawa mbunge wa Kalenga na baadaye waziri, hakubadilika kwani aliendelea kuishi maisha yale yale, ikiwemo kushiriki kazi za kusafisha mitaro mtaani hapo.
“Nyumbani kwake ndiko nilikuwa nikihifadhi vitu vyangu vya ujenzi. Alikuwa mtu wa kawaida, nilipokuwa mbunge na yeye bado, alikuwa ananieleza mambo mengi na hata kunidadisi vitu kuhusu siasa. Sikujua naye alipenda siasa,’’ alisema.
Dk. Mgimwa aliyezaliwa Januari 20, 1950, ameacha mjane Jane na watoto sita. Aliwahi kufanya kazi katika taasisi mbalimbali za fedha na baadaye kufundisha katika Chuo cha Benki mkoani Mwanza.
Mwaka 2010 aliingia rasmi kwenye ulingo wa siasa na kuibuka na ubunge katika jimbo la Kalenga. Mwaka juzi aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha kuchukua nafasi ya Mustafa Mkulo, aliyeachwa katika uteuzi wa Rais.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru