Sunday, 5 January 2014

Kikwete awashukia vigogo wapotoshaji

Na Mwandishi wetu, Zanzibar

MWENYEKITI wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, amewashukia baadhi ya viongozi na kuwataka kuacha kupotosha mchakato wa Rasimu ya Katiba Mpya kwa maslahi binafsi.
Pia amewahakikishia wananchi kuwa maoni zaidi yataendelea kupokewa kwa ajili ya kupata katiba mpya itakayokidhi mahitaji ya wengi kupitia wabunge wa Bunge la Katiba.
Rais Kikwete alisema hayo jana, alipopokea matembezi ya vijana wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kuyaenzi Mapinduzi katika Uwanja wa Maisara, mjini hapa. Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Sheni pia  alihudhuria.
Alisema katika Bunge Maalumu la Katiba, wananchi watakaotaka serikali tatu au mbili wanayo nafasi ya kutoa maoni, hivyo kuwaonya wanasiasa kuacha kuwapotosha wananchi kuhusu mchakato mzima wa Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa kwake na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete aliwakumbusha vijana kuwa, Mapinduzi ya Januari 12, 1964 ndiyo yaliyowakomboa wazalendo wa Zanzibar na si uhuru wa Desemba 10 uliotolewa na Uingereza, kwani ulikuwa wa bandia.
Kutokana na hilo, aliwataka vijana kuyaenzi kwa nguvu zote Mapinduzi na kwamba, vijana wa CCM wanapaswa kuwa mstari wa mbele kukabiliana na watu wanaojaribu kupotosha ukweli.

“Vijana mtambue vizuri kuwa Mapinduzi yaliyofanywa na wazee wetu ndiyo halisi yaliyotuweka huru na kukomesha unyama na udhalilishaji, yale ya Mwingereza yalikuwa feki. Tunapaswa kuyalinda na kukabiliana na wote wanaotaka kupotosha kwa maslahi yao,’’ alisema.
Alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa kuyaendeleza Mapinduzi, ambayo misingi yake inaendelea kutekelezwa, ikiwemo wananchi kupewa ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo.
Rais Kikwete alisema malengo ya Mapinduzi ni kuwapatia wananchi elimu kuanzia ya msingi hadi  sekondari, ambayo katika utawala wa kikoloni yalikuwa hayatekelezwi.
Aliwataka vijana na wananchi kwa jumla kujitayarisha kujitokeza kwa wingi kusherehekea miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambao ni wa kupigiwa mfano barani Afrika.
UVCCM WAMVAA WARIOBA
Kwa upande wake, UVCCM imemvaa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, kuhusu mapendekezo ya muundo wa serikali tatu.
Umoja huo umesema mapendekezo yake ni kinyume cha misingi ya waasi wa taifa, ambayo ni ya serikali mbili kwa lengo la kuhakikisha Muungano unadumu na kupunguza gharama.
Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM (Zanzibar), Shaka Hamdu Shaka, alisema wameshitushwa na Rasimu ya Katiba, kwani ina dalili za kuleta mpasuko wa taifa iwapo serikali tatu zitapitishwa.
Alisema rasimu imekosa mashiko ya makubaliano ya waasisi wa taifa la Tanganyika na Zanzibar, wakati wakiunganisha mataifa hayo na kuzaliwa Tanzania.
Naye Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda, alisema wameshangazwa na rasimu kupendekeza muundo wa serikali tatu.
“Vijana tunawaheshimu viongozi wakiongozwa na Jaji Warioba, lakini tunasema warudi tena, kwani serikali tatu zinatishia umoja na mshikamano wa taifa,’’ alisema.
Awali, Mapunda alisema matembezi hayo yaliyoanza Desemba 22, mwaka jana, yaliwahusisha vijana 1,200 yakilenga kuamsha shamrashamra za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuwaweka tayari vijana kushiriki maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao mwakani.
Mapunda alisema CCM imejizatiti kushinda uchaguzi huo kuanzia nafasi ya rais, wabunge, wawakilishi na madiwani.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru