Thursday 2 January 2014

Mume amuua mkewe baada ya kumfumania


NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA
MKAZI wa Inyala, Huruma Layton, ameuawa kwa kipigo na mumewe, akimtuhumu kumfumania akifanya mapenzi na mwanaume mwingine.
Huruma (20), alifumaniwa na mumewe Ezekiel Mwakabenga (21), akiwa anafanya mapenzi na mwanaume mwingine kwenye nyumba wanayoishi na mumewe huyo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, alisema tukio hilo lilitokea juzi, saa 10:00 alfajiri.
Alisema hali hiyo ilimfanya Mwakabenga kukosa uvumilivu na kuanza kumshambulia mkewe kwa kumpiga sehemu mbalimbali za  mwili.
“Mwanaume aliyekuwa anafanya mapenzi na Huruma alifanikiwa kukimbia, ndipo Mwakabenga alipoanza kumshambulia mkewe huyo sehemu mbalimbali za mwili wake kwa ngumi, mateke na fimbo, na hivyo kumjeruhi vibaya, hali iliyofanya awahishwe hospitalini,” alisema Kamanda Msangi.
Alisema Huruma alifikishwa Hospitali ya Rufani Mbeya na alifariki dunia saa 5:00 asubuhi, alipokuwa akiendelea kupatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa Msangi, Mwakabenga ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Inyala, tayari ametiwa mbaroni na uchunguzi zaidi kuhusiana na mauaji hayo unaendelea kufanywa na polisi.
Utakapokamiliki, mtuhumiwa atafikishwa Mahakani kwa ajili ya kujibu tuhuma zinazomkabiri.
Katika tukio lingine; fundi ujenzi na mkazi wa Nsalaga jijini Mbeya, ameuawa kwa kuchomwa kisu shingoni.
Kamanda Msangi alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 1:00 usiku, maeneo ya Itezi mashariki, Tarafa ya Iyunga, mjini Mbeya.
Msangi alimtaja marehemu kuwa ni Christopher Mnyamba (20), ambaye alichomwa kisu na mtu aliyejulikana kwa jina moja la Ndele.
“Marehemu Mnyamba alikuwa na mwenzake aliyekuwa amempakia kwenye baiskeli na walipofika eneo la tukio, walikutana na vijana wawili waliokuwa wamekaa barabarani, waliwaomba njia ili wapiti, lakini kukatokea kutoelewana baina yao, hali iliyosababisha kuibuka kwa ugomvi baina yao,” alisema Msangi.
Alisema katika ugomvi huo, Ndele alitoa kisu na kumchoma Mnyamba shingoni kisha kukimbia.
Marehemu alikufa alipokuwa akipatiwa  matibabu katika Hospitali ya Rufani Mbeya.
Kamanda Msangi, alisema upelelezi zaidi kuhusiana na tukio hilo unaendelea pamoja na kumsaka mtuhumiwa ambaye mpaka sasa haijajulikana amekimbilia wapi.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru