NA FURAHA OMARY
JAJI John Utamwa wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, leo atatoa uamuzi wa ama kutoa au la zuio la muda kwa Kamati Kuu ya CHADEMA, kutojadili au kutoa uamuzi kuhusu uanachama wa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe.
Uamuzi huo unaosubiriwa kwa hamu na CHADEMA na Zitto, utatolewa saa nne, asubuhi, mahakamani hapo, baada ya Ijumaa, Jaji Utamwa kusikiliza maombi ya Zitto, aliyoyawasilisha chini ya hati ya kiapo.
Kwa upande wake, Dk. Kitilla Mkumbo, amesema hajutii kufukuzwa CHADEMA, kwa kuwa huo si mwisho wa harakati zake kisiasa.
Zitto kupitia wakili Albert Msando, diwani wa CHADEMA, kata ya Mabogini, Moshi, Januari 2, mwaka huu, alifungua kesi namba moja ya mwaka 2014 na kuwasilisha maombi chini ya hati ya kiapo.
Kesi hiyo iliyofunguliwa dhidi ya bodi ya wadhamini ya chama hicho na Katibu Mkuu wa CHADEMA, ipo mbele ya Jaji Utamwa na imepangwa kutajwa Februari 13, mwaka huu.
Anaiomba mahakama iiamuru Kamati Kuu ya chama hicho na chombo chochote cha chama hicho, kutojadili na kuchukua uamuzi kuhusu uanachama wake hadi rufani yake itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi na baraza kuu la chama hicho.
Zitto, ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini, anaiomba mahakama imuamuru Katibu Mkuu wa chama hicho, ambaye ni mdaiwa wa pili katika kesi hiyo, ampatie mwenendo wa kikao cha Novemba 22, mwaka jana, cha baraza kuu ambacho kilifikia uamuzi wa kumvua nyadhifa zake zote za kichama.
Maombi ya Zitto yalisikilizwa Ijumaa, iliyopita, mahakamani hapo, ambako kulitokea vurugu kati ya wafuasi wa CHADEMA na wanaodaiwa kumuunga mkono Zitto, kabla na baada ya Jaji Utamwa, kusikiliza hoja za wakili Msando na mawakili wa CHADEMA, Tundu Lissu na Peter Kibatala.
Akiwasilisha maombi hayo katika ukumbi namba moja uliokuwa umefurika wafuasi wa chama hicho, Msando aliiomba mahakama kutoa zuio la muda kwa kamati kuu ya CHADEMA, isimjadili Zitto kwenye vikao vyake kuhusu uanachama.
Msando mbele ya Jaji Utamwa alidai wanaomba amri ya zuio kwa sababu Zitto ni mbunge wa Kigoma Kaskazini na kwa mujibu wa Katiba, mtu atakuwa mbunge kutokana na chama cha siasa.
Alidai endapo kamati kuu ya chama hicho itakaa na kufikia uamuzi ambao utasababisha apoteze uanachama, matokeo ya uamuzi huo, hayataweza kufidiwa kwa sababu muombaji atapoteza nafasi ya ubunge na hataweza kuwawakilisha wananchi waliomchagua kwa kura ambao si wa chama hicho pekee.
Msando alidai Zitto pia atapoteza nafasi ya uenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali na iwapo mahakama haitatoa zuio hilo, ataathirika zaidi kuliko wajibu maombi kutokana na mazingira ya kesi na nafasi ya uongozi.
Aliiomba mahakama katika kutoa amri ya zuio la muda iangalie maslahi ya wengi na si faida ya wachache na madai ya CHADEMA kwamba taarifa za kikao kilichomvua nyadhifa za kichama Zitto zimechelewa kwa sababu zitakamilika baada ya kikao cha kamati kuu cha Ijumaa iliyopita, ni kinyume cha katiba ya chama hicho.
Lissu kwa upande wake alidai Zitto hakuwa na haja ya kwenda mahakamani kwa kuwa hakuna ushahidi unaoonyesha kikao cha kamati kuu kilikuwa kinataka kumvua uanachama.
Alidai katika nyaraka za Zitto alizowasilisha mahakamani alisema: “Wana CHADEMA na wapenda demokrasia watambue mimi ni mwaminifu, nitakuwa wa mwisho kutoka katika chama, nitafuata utaratibu ndani ya chama katika kuhitimisha jambo hili.”Lissu alidai utaratibu wa chama hicho ambao Zitto anasema ataufuata ni kukata rufani na ameshaandika taarifa ya kusudio la kukata rufani na ameandika maombi ya kupatiwa mwenendo wa uamuzi.
“Kama amekubali atafuata utaratibu hadi kuhitimisha mgogoro huu, ugomvi wa kuja mahakamani ni upi?” alihoji.Alidai akifukuzwa uanachama hakuna madhara yoyote yatakayopatikana kwa sababu Katiba inasema jimbo likibaki wazi, uchaguzi utaitishwa ndani ya siku 90. Alidai Zitto anapaswa kuheshimu chama kilichompa ubunge, akiwa na mgogoro akae ajadiliwe.
Kwa upande wake, Dk. Kitilla alisema umaarufu iliyopata CHADEMA kutoka kwa wananchi unailevya na kuwapofua jambo ambalo litawagharimu.
Alisema anashindwa kuelewa kazi ya chama hicho, kwani chama cha siasa kina wajibu wa kuongeza wanachama jambo ambalo wanakwenda kinyume chake kwa kuita vyombo vya habari na kutangaza kufukuza wanachama kila mara.
“Siasa si kazi ambayo inanipatia ajira, hivyo kufukuzwa CHADEMA si jambo ambalo litanishughulisha, kwani kuondoka huko si mwisho wa kufanya harakati zangu za kisiasa.
Nawashangaa CHADEMA wakati wenzao CCM wanazunguka mikoani kukiiimarisha Chama, wao wapo katika vikao vya kufukuzana,” alisema.Aliongeza: “Kwa sasa tayari katika baadhi ya maeneo wanashusha bendera na kuchana kadi kutokana na kutoridhishwa na fukuza-fukuza isiyokuwa na tija.”
Alisema hawezi kuomba msamaha, kwani hajaona kosa alilofanya, pia kitendo cha kumfukuza hakitamuathiri, kwani ana ajira na alikuwa hakitegemei katika kumuendeshea maisha.
Dk. Kitilla alisema kwa sasa hana mpango wa kujiunga na chama chochote cha siasa.
Alisema dhambi ya kufukuza watu ndani ya chama hicho bado itaendelea kukitafuna, kwani tangu Freeman Mbowe (Mwenyekiti wa CHADEMA) aingie madarakani, Zitto ni kiongozi wa tano kuondolewa madarakani.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru