NA MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imekiri kukamata kontena la meno ya tembo katika Bandari ya Dar es Salaam.
Hata hivyo, imegoma kulizungumzia suala hilo kwa madai kwamba atafutwe Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, na Wizara ya Maliasilia na Utalii kwa kuwa ndio wenye mamlaka ya kufanya hivyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TPA, Profesa Joseph Msambichaka, alisema hayo jana wakati waandishi wa habari walipotaka kupata taarifa kamili kuhusu kukamatwa kwa kontena hilo bandarini.
Profesa Msambichaka alisema hawezi kusema kitu chochote kuhusiana na suala hilo na kushauri atafutwe Dk. Mwakyembe na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwa ndio wahusika wakuu.
Alisema suala hilo liko katika hatua ya juu ya utendaji wa kiusalama na kwamba watakapowaletea ripoti wataweza kulizungumzia.
“Sijaletewa taarifa kamili kama mwenyekiti lakini taarifa kama Mtanzania ninazo, muda muafaka ukifika mtapewa taarifa,”alisema.Mwenyekiti huyo aliwataka waandishi wa habari wawe na subiri katika suala hilo kwani linashughulikiwa na vyombo mbalimbali vya dola.
Hata hivyo, waandishi wa habari hawakuridhika na majibu ya mwenyekiti huyo ambapo walimuomba waitiwe Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Madeni Kipande, ili aweze kutoa taarifa kamili na ikiwezekana wapate picha ya kontena hilo.
Mwenyekiti huyo aliendelea na msimamo wake wa kuwataka wasiwe na subira wakati suala hilo linashughulikiwa.
Kontena hilo linadaiwa kukamatwa juzi bandari hapo na maofisa wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Matukio ya kuuawa kwa tembo yamekithiri nchini na hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete alisema sense ya ndovu katika Pori la Hifadhi ya Selous imekamilika, lakini taarifa yake inatisha kwani kuna ndovu 13,084 mwaka 1976 walikuwa na tembo 109,419.
Alisema watu 1,030 walikamatwa pamoja na silaha za kijeshi 18, za kiraia 1579 na shehena kubwa ya meno ya tembo na nyara nyingine na watuhumiwa walishafikishwa mahakamani.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru